Xi Jinping Kutua Dar

Dar es Salaam. Rais wa China, Xi Jinping anatarajiwa kuwasili nchini
kesho kwa ziara ya siku moja, ambapo pamoja na mambo mengine atasaini
mikataba 17, katiya nchi hiyo na Tanzania, ukiwamo wa ujenzi wa
Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Ujenzi huo utakaofanywa na Kampuni ya Merchants Holding ya China,
utakwenda sambamba na ujenzi wabarabara inayounganisha bandari hiyo na
Reli ya Kati na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema ujio wa rais huyo
aliyechaguliwa wiki mbili zilizopita, utakuwa wa manufaa makubwa kwa
Tanzania.
"Mbali na mkataba huo pia tutasaini mikataba wa kidiplomasia.
Vilevile, China imefungua soko la Watanzania kuuza tumbaku nchini humo
na mkataba wa kuliendeleza Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC),"alisema Membe.
Waziri huyo alisema kiongozi huyo wa China pia atafungua jengo la
kisasa la mikutano la Mwalimu Nyerere.
"Kwa kuwa anakuja Afrika kwa mara ya kwanza huku Tanzania ikiwa nchi
ya kwanza, Jinping pia atatoa hotuba yake juu ya msimamo wa China kwa
Tanzania na Afrika kwa jumla," alisena Membe.