Wakenya Watakiwa kuwa watulivu

Wakati Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ikiwataka wananchi wa Kenya kuwa na subira wakati ikiendelea kukusanya na kuhesabu kura, mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyata anaendelea kuongoza kwa kura dhidi ya mgombea wa Muungano wa Cord, Raila Odinga.
Tangu kura zianze kuhesabiwa juzi jioni, Kenyatta amekuwa akiongoza wagombea wengine wa urais katika uchaguzi huo.
Tamko la Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan jana asubuhi lilitokana na malalamiko yaliyoanza kutolewa na wananchi na vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo kuwa matokeo yanacheleweshwa.
IEBC ilikuwa imeahidi kutangaza matokeo ya urais ndani ya saa 48 baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura juzi saa 11 jioni hakukuwa na matokeo hayo.
Kwa siku nzima jana, matokeo ya awali yaliendelea kutolewa lakini kwa kasi ndogo ikilinganishwa na juzi, huku mgombea urais kupitia Jubilee, Uhuru Kenyatta akiongoza akiwa na kura 2,735,353 (53.49%) dhidi ya Raila Odinga wa Cord aliyekuwa na 2,145,721 (41.96%) hadi kufikia saa 1 jioni jana.
Hassan alisema matokeo hayo yalichelewa kutokana na matatizo yaliyojitokeza ya baadhi ya mashine za utambuzi wa wapigakura kukwama na kusuasua kwa mtandao (network down) juzi usiku.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu wakati wakiendelea kupokea matokeo ya awali, kwa kuwa matokeo rasmi yangesubiri wasimamizi kuwasili Nairobi kutoka mikoani, wakiwa na karatasi rasmi za matokeo kwa ajili ya kulinganisha, hatua ambayo alisema isingewezekana ndani ya saa 48.
Alisema wasimamizi kutoka katika majimbo 290 na kaunti 47 walikuwa safarini kutoka mikoani kwenda Nairobi, hatua ambayo ingesaidia tangazo rasmi la matokeo.
“Tunatarajia wafike mchana wa leo (jana),” alisema Hassan alipozungumza na waandishi wa habari katika kituo cha kujumlishia kura, Bomas.
Hassan alitupilia mbali madai ya Muungano wa Cord kuwa matokeo hayo yanacheleweshwa akisema hayana msingi kwa kuwa sheria ya uchaguzi inaruhusu matokeo kutangazwa ndani ya siku saba, hivyo alikuwa bado na siku sita mkononi kisheria.
Alitumia nafasi hiyo kuzima furaha ya baadhi ya watu: “Hadi sasa tumepata matokeo kutoka vituo 23,000 kwa nchi nzima.
Hakuna anayestahili kushangilia, hakuna anayestahili kulalamika. Huu siyo muda wa kushangilia wala kuhuzunika,” alisema Hassan. Katika uchaguzi huo kulikuwa na vituo 31,981.
Alisema hawawezi kurudia makosa yaliyofanywa na iliyokuwa Tume ya Uchaguzi (ECK), mwaka 2007 yaliyoharibu uchaguzi na kusababisha machafuko.
“Tuko makini sana na suala hilo na ndiyo maana tumetumia gharama kubwa kuandaa mtandao huu. Hatuna nia ya kubadili matokeo yaliyotoka vituoni wala maeneo ya kuhesabia kura. Kila kura iliyopigwa itahesabiwa na itatangazwa,” alisema.
Polisi na msimamizi
Msimamizi mmoja wa uchaguzi aliripotiwa kuuawa kwa bahati mbaya na polisi juzi usiku wakati wakisafirisha masanduku ya kura kwenye kituo cha kujumlishia kura cha Kangema, Muranga, Mkoa wa Kati.
Askari na msimamizi huyo walikuwa wanasafiri kwenye gari moja, ndipo bunduki ikamponyoka na risasi kufyatuka ikielekea kwa msimamizi huyo.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Muranga Mashariki, Chris Mushimba alisema aliyeuawa alikuwa Msimamizi wa Kituo cha Ichichi na uchunguzi wa awali unaeleza ilikuwa ni bahati mbaya.
Waangalizi wapongeza
Timu za waangalizi wa uchaguzi wa kutoka Afrika Mashariki (EAC), Comesa na IGAD wameipongeza IEBC kwa kuendesha uchaguzi huru na haki kwa kufuata kanuni sheria na taratibu, licha ya kasoro za kiufundi zilizojitokeza.
Akisoma taarifa ya awali jana, Mwakilishi wa EAC, Abdulrahman Kinana alisema kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, wana imani kuwa matokeo yatakuwa ndiyo matakwa halisi ya Wakenya.
Kinana ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CCM, aliwataka wadau wa uchaguzi, Serikali na wengine, kuendelea kulinda amani, licha ya changamoto za kiusalama zilizojitokeza katika maeneo ya Garisa, Kilifi, Mombasa na Wajir.
Alivipongeza vyombo vya habari kwa kutimiza wajibu wao kuelimisha umma na kuwa makini dhidi ya habari ambazo zingeweza kuhatarisha amani.
Kwa upande wa polisi, alisema walifanya kazi yao vizuri, hawakutisha watu na walionekana wakiwasaidia wapigakura.
Alishauri IEBC kuendelea kupitia daftari la wapigakura mara kwa mara, msajili wa vyama vya siasa apewe mamlaka kisheria kusimamia chaguzi za awali ndani ya vyama na elimu ya uraia itolewe ili kupunguza matukio kadhaa yaliyojitokeza kama vile kuharibu kura.