Mashua Yazama Nigeria

Mashua iliyokuwa imebeba watu 160 imezama umbali wa kilometa 74 toka
pwani ya Nigeria, wanaosimamia shughuli za uokoaji wamesema.
Mashua hiyo, iliyoundwa kwa mbao, ilianzia safari yake huko
kusini-mashariki mwa Nigeria Ijumaa, ikielekea Gabon, safari kati ya
Afrika Magharibi na Kati inayopendwa na wafanyibiasahara wengi.
Tomi Oladipo wa BCC, akiwa mjini Lagos, anasema kwamba safari hizi
huchukua siku kadhaa, na huwa si salama sana. Kwa ajili hiyo ajali
hutokea mara kwa mara.
Mashua hiyo ilianzia safari mjini Oron, jimboni Cross River, na
ilikuwa inasafiri katika Ghuba la Guinea ilipozama, duru rasmi
zimesema.
Waokoaji waliokuwa karibu na mji mkuu wa Jimbo la Cross River,
Calabar, walisema wameokoa makumi ya maiti ya wasafiri waliokufa maji.
Wawili wa walionusurika, mvulana mdogo na mwanamke, walishikilia
silinda ya gesi kabla ya kuokolewa na wavuvi, afisadharura wa Jimbo la
Cross River, David Akate, aliliambia shirika la habari la Reuters.