Mahakama Kuu yaitisha mafaili kesi ya Lwakatare
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeiamuru Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu iwasilishe majalada ya kesi ya ugaidiinayomuhusu
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na
mwenzake katika kesi hiyo, Ludovick Joseph.
Hati ya kuitisha majalada hayo ilitolewa jana alasiri na Msajili wa
Mahakama Kuu, baada ya mawakili wanaomtetea Lwakatarekuwasilisha
maombi ya marejeo ya mwenendo wa kesi hiyo, iliyofunguliwa katika
Mahakama ya Kisutu.
Maombi hayo ya marejeo yaliwasilishwa mahakamani hapo jana chini ya
hati ya dharura yakiambatanishwa na hati kiapo yammoja wa mawakili
wanaomtetea Lwakatare, Peter Kibatala. Wengine ni Mabere Marando,
Profesa Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na Tundu Lissu.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata kisha baadaye kuthibitishwa na
mmoja wa mawakili wanaomtetea Lwakatare zilisema kuwa jana Msajili wa
Mahakama Kuu alisaini na kutoa hati hiyo kwenda Mahakama ya Kisutu.
Mapema jana mawakili wanaomtetea Lwakatare waliwasilisha maombi hayo
ambayo yalipokewa na kupewa usajili wa namba 14 ya 2013.
Mawakili hao wanaiomba Mahakama Kuu, iitishe majalada yote mawili ya
kesi hiyo, jalada namba 37 ya mwaka 2013 na namba 6 ya mwaka 2013 kwa
ajili ya uchunguzi ili iweze kujiridhisha usahihi na uhalali wa
mwenendo wake.
Pia wanaiomba Mahakama Kuu ifanye marejeo au kutengeua hati ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyowafutia mashtaka watoa maombi (Nolle
Prosequi) kabla ya kuwakamata na kuwafungulia tena mashtaka hayohayo.
Maombi yao mengine ni kutaka Mahakamaya Kisutu iamriwe kutoa uamuzi wa
maombi ya dhamana, uliokuwa umepangwa kutolewa na Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Emillius Mchauru, Machi 20, 2013, katika kesi namba 37.
Mawakili hao wanadai kuwa uamuzi huo ambao ulihusu dhamana ya
watuhumiwa, ulitenguliwa na hati ya DPP ya kuwafutia mashtaka
washtakiwa hao, isivyo halali.
Maombi mengine ni kurejea au kutengua mwenendo wa kesi namba 6
iliyofunguliwabaada ya hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi hao na
badala yake iendelee kesi namba 37.
Wanaiomba pia Mahakama Kuu iamue kwamba utaratibu uliotumiwa na wajibu
maombi (Jamhuri) kutoa hati ya kuwafutia mashtaka watoa maombi katika
kesi namba 37 ilikuwa kinyume cha sheria au haukuwa sahihi.
Wanadai kuwa utaratibu huo ulisababisha matumizi mabaya ya taratibu za
kimahakama na matumizi mabaya ya mamlaka ya kiuendeshaji mashtaka na
kushusha hadhi na uhuru wa mahakama.
Chanzo: Mwananchi