Dar es Salaam. Moto mkubwa uliotokana na hitilafu ya umeme,
umeteketeza bidhaa za mabilioni zilizokuwa zimehifadhiwa katika maghala
ya Kampuni ya Sunda ya jijini Dar es Salaam.
Magari zaidi ya 20 ya vikosi vya zimamoto na
uokoaji vya taasisi mbalimbali vilishindwa kuzima moto huo, ulioanza saa
4:45 asubuhi na kuendelea hadi jana mchana.
Akizungumza katika eneo la tukio, Kaimu Kamanda wa
Zimamoto Kanda Maalumu, Bakari Mrisho, alisema walichelewa kupata
taarifa za moto huo uliokuwa unateketeza maghala hayo ya kuhifadhi vifaa
vya ujenzi na samani za ndani la ‘Ubungo Business Park’.
Mmoja wa wamiliki wa maghala hayo ambaye jina lale halikupatikana, alizimia baada ya kuona mali zake zikigeuka jivu.
Baadhi ya vifaa vilivyoelezwa kuwamo kwenye ghala
hilo ni pamoja na marumaru, mashine za kufyatulia matofali, jasi,
baiskeli, matoroli, mabomba ya plastiki na makasha mbalimbali yaliyokuwa
na vocha za simu.
Vifaa vingine ni matairi ya baiskeli, vifaa vya
maalumu vya ulinzi (CCTV, Smart Card ) na kontena zipatazo nne za vocha,
(Pampasi, chupa za chai, vikombe vya chai vyote vilitekelea kwa moto
huo).
Baadhi ya kampuni zilizokumbwa na janga hilo ni
Sandu (T) Limited, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel, Poly Machinery
na Brick Machinery.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Sunda (T) Limited,
Mashaka Zuberi alisema moto huo ulianza muda mfupi baada ya fundi umeme
wa ghala hilo kufanya matengenezo ya kuongeza nguvu ya nishati hiyo.
Alisema fundi wa umeme jana (juzi) alikuwa
anafanya matengenezo ya kuongeza nguvu ya umeme kwani umeme uliokuwapo
haukuwa na uwezo wa kuhudumia vifaa vilivyokuwapo.
Zuberi alisema leo (jana) saa 4.30 fundi huyo
alifika kumalizia kazi hiyo ambapo aliwataka kuzima vifaa vyote vya
umeme ili kuwezesha kuwasha baada ya kumaliza matengenezo.
Naye Kaimu Kamanda wa Zimamoto, Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Bakari Mrisho alisema kitendo cha baadhi ya watu kukaidi
kuzingatia sheriza zimamoto ndio chanzo cha maafa ya aina hiyo.
Alisema walifanya ukaguzi na kuwataka kuweka
kisima cha maji jambo ambalo hawakulitekeleza na kusababisha usumbufu wa
kupata maji ya kuzimia moto huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela
alisema kutokana na moto huo kuwa mkubwa aliamua kuomba msaada wa
magari ya zimamoto kutoka Bandari na Uwanja wa ndege.
Alisema chanzo cha moto huo hakijaweza kujulikana
ambapo vitu mbalimbali vimeweza kuteketea kwa moto na hakuna
aliyejeruhiwa katika tukio hilo.