WATUPWA SIKU 1 JELA KWA KUKOJOA HADHARANI

Watu 109 wamehukumiwa kifungo cha siku moja jela kwa kukojoa hadharani huko India.

Polisi waliwakamata takriban watu 109 kwa kukojoa katika vituo vya usafiri wa umma na reli.

Wale wote waliokamatwa wanatuhumiwa kwa kupatikana na hatia ya kukojoa nje ama ndani ya vituo vya reli mjini Agra Kaskazini mwa India.

Waliokamatwa watahukumiwa kifungo cha saa 24 korokoroni ama walipe faini ya kati ya dola mbili na kumi au vyote.

Maafisa wa afya ya umma wanasema walifanya operesheni hiyo kwa ghafla ilikukabili uvundowa mkojo unaoathiri afya ya mamilioni ya watu wanaotumia huduma hiyo ya reli nchini India.

Mkuu wa polisi katika eneo hilo GRP, Gopeshnath Khanna aliyeongoza operesheni hiyo anasema kuwa itaendelea hadi wahindi wanaolaumiwa kwa kuharibu mazingira kwa kutema mate ukutani baada ya kutafuna thambuu na tumbako iliyowekwa rangi na kukojoa katika maeneo ya umma watakapo badili tabia zao.

Aidha wasafiri wa reli wanasemekana kupigwa na harafu mbaya ya mkojo pindi wanapoingia ndani ya vituo hivyo.

Operesheni hiyo ni sehemu ya kampeini ya waziri mkuu mpya wa India Narendra Modi ya kuimarisha afya ya umma al maarufu 'Swachh Bharat.

Waandishi wa habari katika eneo hilo la Agra wanasema hii ndio mara ya kwanza kwa maafisa wa kulinda afya ya umma kwa ushirikiano na serikali ya majimbo kuwakamata vikojozi.

Takwimu za afya nchini humo zinaonesha kuwa takriban watu milioni mia sita 600 m ama nusu ya raia wa India hawana vyoo.