MKULIMA WA DARASA LA SABA AUTAKA URAIS

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, Eldoforce Bilohe (43) jana alitinga makao makuu ya Chama Cha Mapindizi (CCM) kuchukua fomu ya kuomba ridhaa kuteuliwa kuwa mgombea urais, bila kuwa na ada huku akiwa amebeba maji ya chupa kwapani.

Bilohe ambaye alisema elimu yake ni ya darasa la Saba, aliwasili makaomakuu ya CCM muda wa saa 5:40 asubuhi na kuelekea Ofisi ya kupokea wagombea ndani ya ofisi baada ya kuwapita waandishi wa habari wakiwemo wapiga picha, waliokuwa wamejipanga kumsubiria, lakini aliwapita waandishi bila kumtambua kuwa ni mgombea,

Akiwa amevaa suruali ya kaki na fulani yenye rangi ya kijani na njano, alionekana kuduwaza watu wengi, ambao walikuwa wakiwasuburi wagombea, ambao walikuwa wakichukua fomu jana.

Akiwa kati ya watu waliokuwa kwenye orodha ya kuchukua fomu, Bilohe alikuwa amebeba chupa ya maji kwapani baada ya kufika na kupokelewa na maafisa, ambao walimtambua kuwa ni mgombea na ndipo wapiga picha waligutuka na kuanza kupiga picha.

Kisha aliingia ndani ya ofisi ya kuchukua fomu na alitoka baada ya muda mfupi na kuanza kuhojiwa na waandishi wa habari.

Alisema amefika Dodoma kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuteuliwa kuwa mgombea urais, lakini kwa sababu ambazo hazijafahamika, aliambiwa akachukue fedha.

"Nilipigiwa simu wakati niko benki ya CRDB nikiwa kwenye foleni, nikisubiri kuchukua fedha, ndiyo nikakimbia kuja hapa," alisema.

Alisema amekuwa mwanachama haiwa CCM tangu mwaka 2003 na elimu yake ni ya msingi na ana uzoefu kutokana na kuwa katika chama kwa muda mrefu.

"Nimekuja kama nilivyo kwa sababu sijawahi kuwa na makundi unayoyaona wewe, mimi ni mwanachama wa kawaida kama wanachama wengine," alisema.

Mmoja wa maofisa wa chama, ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema Bilohe amerudisha si kwa sababu hana hela, bali kuna vigezo ambavyo havijafikiwa, ikiwemo barua ya utambulisho kutoka kwa Katibu wa CCM Wilaya aliyotoka.

"Hajakamilisha taratibu za kumwezesha kuhukua fomu," alisema.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zilisema kuwa tayari mkulima huyo ameshalipia ada ya fomu ya Sh 1,000,000 na atachukua fomu yake leo saa 10 jioni.