Kesi hiyo ilikuwa ikiwakabili raia wa Kenya, Said Abeid na wa Burundi, Garuka Haruna na Watanzania walioachiwa huru ni mfanyabiashara Bundala Kapela, Juma Kasago na Rashidi Juma.
Walihusishwa na wizi wa petroli ya thamani ya Sh milioni 100 na gari lenye thamani ya Sh milioni 200. Walitiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Igunga mjini Tabora nchini.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu mkazi Wilaya, Ajali Milanzi alisema mahakama imewatia hatiani washitakiwa namba tatu, Abeid na Haruna kutokana na kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Mahakama hiyo imewahukumu kwenda jela mwaka moja kila mmoja huku ikizingatia kuwa watuhumiwa hao walikaa mahabusu zaidi ya miezi minane.
Hakimu Milanzi alisema washitakiwa Kapela, Juma na Kasago wameachiwa huru baada ya mahakama kutowakuta na hatia dhidi ya tuhuma hizo za wizi wa mafuta na gari.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, Elimajidi Kweyamba, aliiambia mahakama hiyo kuwa Septemba mwaka 2014 saa 8:00 mchana katika kijiji cha Ziba, watuhumiwa hao waliiba gari lenye namba za usajili RAC 3542 likiwa na tela yake namba RL 0635 lenye thamani ya Sh milioni 200.
Gari hilo lilikuwa na mafuta lita 43,000 yenye thamani ya Sh milioni100, vyote vikiwa na jumla ya thamani ya Sh milioni 300 mali ya kampuni ya Merries ya Kigali, Rwanda.