BVR YABAINI 152 KUJIANDIKISHA ZAIDI YA MARA MOJA

Watu 152 wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters registration (BVR) katika mikoa mitano iliyokamilisha uandikishaji huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiahirisha uandikishaji wapigakura kwa wiki moja kuanzia jana katika mikoa minne.

Mikoa ambayo uandikishaji umeahirishwa kuanzia jana hadi Juni16, mwaka huu ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana na waandishi wa habari kuhusiana na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura unavyoendelea, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Dk. Sisti Cariah, alisema watu hao waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja watachukuliwa hatua.

"Kwa mujibu wa sheria, hilo ni kosa la jinai na kwa hiyo tutawachukulia hatua za kisheria mara moja na kwahali hiyo ninawaasa wananchi kuachana na udanganyifu huo, kwani mfumo wetu tulionao utawatambua mara moja," alisema.


KUAHIRISHA MIKOA MINNE

Kuhusiana na kusogezwa mbele kwawiki moja uandikishaji wa wapiga kura katika mikoa hiyo minne, Dk. Cariah alisema imetokana na mabadiliko ambayo yanaendelea kufanywa ya mipaka ya kiutawala yakata, vijiji, vitongoji na mitaa.

Alisema mabadiliko hayo yanatakiwa kufanyiwa kazi katika mfumo mzima wa Daftari la Wapigakura kwa mikoa hiyo minne na hasa ikitiliwa maanani kuwa katika mabadiliko hayo, kata 130 mpya zimeongezeka.

Alisema katika maeneo ambayo shughuli ya uandikishaji imeshafanyika, Nec itafanyia mabadiliko katika mfumo wake baadaye.


NEC YAFIKIA LENGO

Aidha, Dk. Cariah alizungumzia namna Nec ilivyofikia lengo lililotarajiwa la kuandikisha wapigakura katika mikoa mitano ilikomaliza kazi hiyo ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa na Njombe.

Alisema katika mkoa wa Lindi, idadiya watu walio na umri wa miaka 18 hadi kufikia siku ya kupiga kura iliyotarajiwa kuandikishwa kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa(NBS) ilikuwa ni 518,230, lakini Nec ilifanikiwa kuandikisha wapiga kura 529,224 sawa na asilimia 102.

Kwa upande wa Mkoa wa Mtwara, Nec ilitarajia kuandikisha wapiga kura 732,465, lakini iliandikisha wapiga kura 727,565 sawa na asilimia 99.

Alisema kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, Nec ilitarajia kuandikisha wapiga kura 783,296, lakini ikaandikisha wapiga kura 826,779 sawa na asilimia 106, na kwa Iringa, Tume ilitarajiwa kuandikisha wapiga kura 524,390 lakini ikaandikisha wapiga kura 526,006 sawa na asilimia 101.

Hata hivyo, alisema kwa Mkoa wa Njombe ambao ulikuwa wa kwanza kuboresha daftari hilo, bado mawasiliano yafanyika kupata takwimu sahihi.

"Hivyo utaona kuwa utendaji wetu karibu unavuka malengo pamoja na wasiwasi ulioonyeshwa kupitia kwenye vyombo vya habari," alisema.

Vile vile, Dk. Cariah alisema Nec imepata mashine zote 8,000 za BVRambazo serikali ilikuwa imeahidi hadi sasa na kwa hiyo shughuli hiyo itakamilika kama ilivyopangwa.

"Niwahakikishie wananchi kuwa shughuli ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura litakamilika kabisa kufikia mwishoni mwa mweziwa saba," alisisitiza.


CHANZO: NIPASHE