BAJETI AFRIKA MASHARIKI ZASOMWA

Serikali za Afrika mashariki zimetumia kodi kuvitahadharisha viwanda vyake kwa upande mmoja na kuwapa motisha wananuzi wa bidhaa kutoka nje wanaosaidia sekta muhimu kama vile miundo mbinu, kawi mbali na utekelezwaji wa itifaki ya soko la pamoja.

Katika mapendekezo ya bajeti yaliosomwa siku ya alhamisi Kenya, Uganda Rwanda na Tanzania zimepunguza kodi za bidhaa zinaozoagizwa kutoka nje kwa sekta muhimu kama vile kawi,mawasiliano na miundo mbinu.

Kulingana na gazeti la the east African nchini Kenya, shinikizo la kuimarisha miundo mbinu, kupunguza gharama ya kufanya biashara na kuongeza mtiririko wa mapato kutoka kwa mafuta na gesi iliogunduliwa katika eneo la Afrika mashariki umeyafanya mataifa manne ya eneo hili kushusha masharti ya sera za kodi ili kurahisisha biashara na majirani zao pamoja na mataifa ya kigeni.

Rwanda imepunguza kodi katika magari yanayoagizwa kutoka nje hususan matinga tinga, malori pamoja na mabasi ya uchukuzi.

Tanzania kwa upande wake imechukua mkondo kama huo na kupunguza kodi ya kuagiza bidhaa kutoka nje kutoka asilimia 25 hadi 10 miongoni mwa mabasi yanayobeba abiria 25 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uwiano wa kikanda unalenga kurahisisha biashara na kuzuia hasara inayokumba kampuni zinazofanya biashara katika eneo hili.

Hatahivyo, wafanyibiashara katika mataifa kama vile Rwanda na Uganda wanalazimika kulipia hasara inayotokana na masharti ya kibiashara yaliowekwa na wasanifu.

Ili kuondoa matatizo hayo Kenya imetangaza kuwa inapunguza masharti kadhaa ya kibiashara kupitia kuondoa forodha ya usalama katika uagizaji wa sukari ya viwanda na unga na ngano.

Uganda nayo imechukua mkondo huo kwa kuondoa forodha yake ya usalama kwa bidhaa na kuanzisha mtindo wa kulipa unaojulikana ambao unalenga kuleta uwiano.