WAGOMBEA URAIS WAINGIA MITINI KWENYE MDAHALO

WAGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), juzi walikimbia mdahalo wa kupambana kwa hoja ulioandaliwa na wenyeviti wa sekta binafsi na kujulikana kama 'CEO round table of Tanzania'.Mdahalo huo ulikuwa na lengo la kujadili mambo makuu mawili, ikiwa ni sekta ya uchumi na utawala bora na kwa jinsi gani wagombea hao wakipata ridhaa ya kuliongoza taifa, wangetekeleza vipaumbele hivyo katika kuliletea taifa maendeleo.

Akizungumza mara baada ya kuahirisha mdahalo huo, Mwenyekiti wa Mdahalo, Ally Mfuruki alisema amesikitishwa sanana wagombea hao kwa kushindwa kuhudhuria kwenye mdahalo huo, kwani hadi muda unakaribia wa kuanza majadiliano, walitoa taarifa za kuhudhuria.

"Nashindwa hata kuelewa ni sababu zipi zimewafanya hawa wagombea wasifike kwani muda mfupi tu uliopita niliwasiliana nao na wakasema wanakuja, lakini baada yakuona muda unaenda na hakuna aliyefika, nikapata taarifa kuwa hawatafika na sijapewa ni sababu zipi zimewakwamisha," alisema Mfuruki.

Waliotarajiwa kuhudhuria mdahalo huo ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mawasiliano January Makamba, Balozi Amina Ally, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Alisema anashangaa kutojitokeza kwao na kuwa aliyejitokeza ni mgombea mmoja tu, mwanamke pekee katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania kiti cha urais, ambaye ni Balozi Amina Ally.

Lakini, alithibitisha kupokea taarifa za kutohudhuria kwa Waziri Nyalandu na kusema kuwa alipata dharura ya kikazi na hivyo alitoa taarifa ya kutohudhuria mapema na Sumaye pia alipata dharura na kutoa taarifa ya kutokuwepo kwenye mdahalo.

Kwa upande wake, Balozi Amina Ally alisema anasikitishwa na wagombea wenzake kwa kutoitika wito wa kuhudhuria, kwani wananchi wanachokitaka ni kuwafahamu kwa undani wagombea kwa kupitia midahalo na kuweza kutambua ni yupi atakayewaletea maendeleo na kuwatatulia changamoto zinazowakabili.