MAKAMBA: NISIPOTEULIWA SITAKUWA NA KINYONGO

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye anawania uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea urais, ameahidi kuwa asipoteuliwa hatakuwa na kinyongo na atarejea kukijenga chama.

Aidha, ameahidi kuwa atalirudisha Jimbo la Iringa Mjini mikononi mwaCCM.

Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kadhalika, Makamba amemwaga ahadi lukuki kwa wakazi wa mji wa Iringa ikiwamo kuwasaidia vijana wabodaboda, kupanua uwanja wa ndege mkoani humo, kujenga barabara ya lami kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na kufufua viwanda.

Ahadi nyingine ni pamoja na kuhakikisha vijana wanaojiunga na vyuo vikuu, wanapata mikopo bila usumbufu wowote kwa kuwa kupata elimu ni haki yao.

Aliyasema hayo jana alipozungumzana makada wa CCM, kutoka wilaya zote za mkoa wa Iringa, alipokuwa akitafuta wanachama wa kumdhamini.

Makamba alipata zaidi ya wadhamini 600 ambao ni zaidi ya idadi inayotakiwa na chama ambayoni wanachama 30 kwa kila mkoa.

Aliongeza kuwa mchakato wa kumpata mgombea, hauna uhasamana kwamba hata kama kushinda ama kushindwa atakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga chama upya ili kurudisha mshikamano.

"Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuanza kukijenga chama baada ya uchaguzi mkuu, wanachama wote wanatakiwa kukaa kama familia moja ili kujenga mshikamo pamoja na kujadili makovu ya uchaguzi," alisema.

Makamba alisema ana imani kwamba CCM kitapitisha mgombea kwa kujiamini bila kuogopa kusambaratika na wala wanachama wasisikilize watu wanaojipitisha mitaani na kusema kwamba chama kitasambaratika baada ya uchaguzi.

Kabla ya kukutana na wanachama wa CCM katika ofisi za wilaya, Makamba alisema Iringa ni kama nyumbani kwao kwa kuwa aliwahi kuishi hapo wakati baba yake akifanya kazi mkoani humo.

Wakati wa mapokezi yake, vijana waendesha bodaboada waliongoza msafara wake, huku wakiimba nyimbo hadi katika ofisi za wilaya ambako alikabidhiwa majina ya makada waliomdhamini.

Kutokana na wingi wa wananchi wakiwamo makada wa CCM, uongoziwa wilaya wa CCM, ulilazimika kuwaomba watu watoke nje ya ukumbi ili wakutane na Makamba eneo la wazi azungumze nao.