WAZEE WOTE SASA KULIPWA PENSHENI ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuanzia mwaka huu wa fedha itawalipa pensheni wazee wote bila kujali kama waliajiriwa ama hapana.

Watakaonufaika na pensheni hiyo niwazee waliofikisha miaka 70 na kuendelea lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha kujikimu kimaisha.

Waziri wa Uwezeshaji Ustawi wa Jamii vijana Wanawake na Watoto Zainab Omar Mohamed akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo alisema mchakato wa kufahamu idadi ya wazee wote Unguja na Pemba wanaostahiki kulipwa pensheni hiyo umekamilika.

Alisema SMZ imechukuwa uamuzi huo ukiwa na lengo la kupambana na hali ngumu ya maisha inayowakabili wazee ambao baadhi yao hawakuajiriwa serikalini au na taasisi zake.

"Mheshimiwa Spika napenda kuwajulisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BWW)kwamba kwa mwaka wa fedha tutaanza kulipa pensheni kwa wote."alisema.

Aidha Waziri huyo aliwaambia wajumbe wa BWW kwamba juhudi za kupambana na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto zinaendelea ikiwamo kazi ya uzinduzi wa kampeni hizo iliyofanywa na Rais waZanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.

Alisema kampeni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba udhalilishaji unatokomezwa kwa kuzishirikisha taasisi mbali mbali pamoja na vyombo vya kusimamia haki na sheria.

Alieleza kuwa imebainika kwamba mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia yanahitaji ushirikiano baina ya wizara ikiwamoya Katiba na Sheria, Elimu pamoja na Wanawake na Watoto.

Aidha alizitaka mahakama za Ungujana Pemba kuchukuwa juhudi ya kuharakisha hukumu kwa kesi za ubakaji kwani wananchi wameanza kuvunjika moyo kutokana na kesi hizo kuchukuwa muda mrefu hadi kutolewa kwa hukumu zake kwa kuwepo visingizio mbali mbali ikiwemo kukosekana kwa ushahidi.

"Tabia ya nenda rudi kesho imeanza kuwakatisha tamaa wananchi ambao wengine wanatoka vijijini kuja mjini kwa ajili ya kusikiliza kesiyake ambapo bila ya kupewa taarifaza uhakika kesi inaahirishwa"alisema.

Alisema baadhi ya kesi zinalazimika kufutwa na nyingine majalada yake kufungwa moja kwa moja kwa sababu zinakosa ushahidi muhimu ambao ndiyo utakaoweza kuwatia hatiani watuhumiwa wa makosa ukiwamo ubakaji.