Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amekuwa kada wa 31, kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais, huku akijigamba kwa mafanikio ya serikali iliyopo madarakani.
Pinda maarufu kama "mtoto wa mkulima" alisema hawezi kusema atafanya nini bali atakachokiangalia ni ilani ya CCM, na hataanzisha jambo jipya bali kuendeleza pale serikali ya awamu ya nne ilipoishia.
Akitangaza nia baada ya kuchukua fomu katika ofisi za Makao Mkuu ya CCM, mjini Dodoma, alisema anafanya mambo kimya kimya na hatangazi kama wengine wanavyofanya na kwamba kwa upande wa miundombinu ambayo inafanya vizuri ni kwa sababu yeye ni kiranja wa mawaziri husika. Kaulimbiu yake ni "Wanyonge sasa tuwainue" na kusisitiza amesema hivyo kwa kuwa mpango wa pili wa maendeleo utayagusa makundi hayo.
"Uchungu wa mwana aujuaye mzazi, nimesema hivi makusudi, mimi ndiyo nipo serikalini hivi sasa, kamani uchungu wa mwana mimi naujua zaidi," alisema.
ILANI YA CCM
Pinda ambaye alijitapa kuwa ni mtoto wa serikali za mitaa, alisema CCM ina utaratibu mzuri kwani hakuna anayeweza kusimama na kusema lolote bali wanaongozwa naIlani na kwamba haijatoka hivyo hawezi kusema atakayofanya.
"Ndani ya Ilani kuna maelekezo yote, sera, mikakati na maelekezo ikiwamo kuahidi Watanzania nini atawafanyia kwa miaka mitano, kwa sababu haijatoka sina la kusema, nachoweza kuahidi ikikamilika na kupitishwa na mkutano mkuu na Mungu kunitambua, sitashindwa kutekeleza ilani hata kidogo," alibainisha.
"Nalisema kwa kujiamini kwani nimekuwapo serikanili kwa muda mrefu, nimefanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi kwa miaka kumi, Benjamini Mkapa kama Naibu Waziri na sasa nipo na Jakaya Kikwete kwa miaka nane, hawa pia ni viongozi wa chama hiki na wanasimamia ilani itekelezwe, nimejifunza mengi, pia mimi ndiyo msimamizi wa ilani."Alisema mambo makubwa ni usimamizi ni uwajibikaji, kupambana na rushwa, kilimo.
DIRA YA MAENDELEO
Alisema katika utelekezaji wa Ilani ya chama chake ni lazima kutelekeza Dira ya Maendeleo ya 2000 -2025, mwaka 2005.
Pinda ambaye ametajwa kwenye kinyang'anyiro hicho kwa muda mrefu, alisema Rais Kikwete alionekana kuongeza nguvu kwenye eneo hilo, na Kikwete alianzisha Mpango wa Maendeleo ili kuitekeleza Dira ipasavyo ambayo inataka ikifika mwisho Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati.
Alisema ndani ya Dira siyo rahisi kuona mambo yote kwa kuwa ni sera ya jumla na ndipo ulipozaliwa mpango wa maendeleo uliogawanyika katika miaka mitano mitano, na wa kwanza utakamilika mwaka huu.
NINI KIMEFANYIKA
Alisema ndani ya miaka mitano ilikuwa ya kufufua na kujenga mambo muhimu ambayo ni miundombinu ya barabara, reli na bandari.
"Mkapa alianza Kikwete akaendeleza ndani kuna program ya ujenzi wa barabara inayotakiwa kumalizika 2018, kuwe na mtandao wa barabranchi nzima kuunganisha makao makuu ya kila mkoa kwa barabara za lami."
"Anachokifanya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ni utekelezaji wampango wa miaka mitano na jingineni mkakati wa kupunguza umaskini ni program ndani ya mpango na hivi karibuni wataanza kuandaa mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano utalipeleka taifa hadi 2021 ili ikifika 2025/26 ili kutekeleza Dira."Alisema kinachotarajiwa kufanyika kwa miaka mitano ijayo ni kujenga uwezo wa kiuchumi kwa kujenga viwanda na msisitizo ni viwanda vyausindikaji wa mazao yanayotokana na wakulima, wafugaji na wavuvi.
MAADUI
Alisema maadui wakubwa wakati wa Mwalimu Nyerere ni umaskini, ujinga na maradhi, lakini kwa marais watatu waliopita walibainisha maadui wakubwa wengine uharibifu wa mazingira na utawala bora.
Alisema uchumi imara utawezesha kumaliza maadui ujinga, maradhi naumaskini, huku uharibifu wa mazingira utafanikiwa kwa kuelimisha umma kwa kujenga fikra mpya namna ya kuhifadhi misitu navyanzo vya maji.
UTAWALA BORA
Alisema unawataka Watanzania wote kutambua tuna wajibu kuhakikisha nchi iendeshe mambo yake kwa uwazi, viongozi waadilifu watakaolivusha taifa, kiongozi ambaye kila akikaa anajua watu wake ni maskini anatakiwa kuwainua.
"Wanatueleza mmnefanya vizuri lakini umaskini umepungua kwa kiasi kidogo sana asilimia 28, tunataka mshuke zaidi…wanasema tatizo lenu ukuaji wa uchumi umetegemea sekta ya ujenzi, maliasili, uchukuzi, mchangowake ni mkubwa lakini haugusi jamii kubwa moja kwa moja.
"Alisema wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kupeleka jitihada hizo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji kwa kutumia malighafi kutoka kwa makundi hayo na hivyo kupunguza umaskini kwa kasi kubwa.
KILIMO
Alisema kinachokimbiza watu kwenye kilimo ni jembe la mkono na kinachotakiwa ni vifaa vya kisasa,na hivyo ndani ya miaka mitano ijayo hali za maisha ya watu wa chini zitainuka.
"Kama Mwenyezi Mungu itampendeza nikawa mmoja wa waliochaguliwa, ni eneo piga geuza, kufa na kupona nitalisimamia kwa nguvu zangu zote," alisisitiza na kuongeza: "Wapo ambao hawataki kusikia hata na kusema ni mambo ya Kikwete, kinachotakiwa ni kuyabeba na kuyasukuma kwa kuwa msingi upo, tukienda hivi ndani ya miaka kumi Tanzania itabadilika."Aidha, aliwataka viongozi na Watanzania kutobeza juhudi za Kikwete.
RUSHWA
Pinda ambaye pia ni Mbunge wa Katavi, alisema lazima serikali izingatie utawala bora kwa kupambana na rushwa na uovu wowote wenye kulirudisha nyuma taifa kimaendeleo.
SERIKALI ZA MITAA
Alisema amekuwapo serikali za mitaa tangu aingie serikalini na kwamba hati chafu zimepungua kutokana na usimamizi wa karibu alioufanya.
Alisema yeye (Pinda) ndiye mtu sahihi kwani mtu mpya atahitaji muda wa kujifunza, kuelewa na kuuliza na wakati mwingine ataboronga.
MASHANGINGI
Pinda alisema serikali imepunguza magari ya kifahari aina ya VX8, ambayo gari moja ni zaidi ya Sh milioni 300, ambayo inawezesha upatikanaji wa magari mawili au matatu.
Waziri Mkuu aliambatana na wabunge na viongozi wengine ambao ni Dk. Cyril Chami, Martha Mlata, Dk. Orudencia Kikwembe, Dk. Peter Kafumu, Meya wa Jiji la dar es Salaam, Didas Masaburi, aliyewahi kuwa mbunge, Dk. Christan Mzindakaya, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Berbadetta Kinabo.