RAIS KIKWETE AKANA NJAMA ZA KUMMALIZA DK.MENGI

RAIS Jakaya Kikwete ameshtushwa na taarifa za kuhusishwa na mikakati ya kummaliza Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi. Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya Dk. Mengi kudai kuwa kiongozi huyo wanchi ameapa kupambana naye kama ilivyoripotiwa na moja ya magazeti ya kila wiki nchini.

Kauli ya Rais Kikwete ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa waandishi wa habari.

Madai ya Dk. Mengi yalitokana na taarifa za gazeti hilo, zikidai kuwa Rais Kikwete aliyasema maneno hayo baada ya kukutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye alimweleza mkakati wa mfanyabiashara huyo wa kutaka kupambana naye baada ya kung'atuka madarakani.

Baada ya maelezo aliyotoa katika hotuba yake, waandishi walitaka kujua msimamo wa Ikulu juu ya madai ya Dk. Mengi, ambapo Rweyemamu alisema: "Wakati niko Jordan ndio tulipata habari kuwa mzee Mengi amesema hayo aliyosema, kila mtu akiwapo rais alishangazwa sana na kauli hiyo." Alisema kwa muda mrefu Rais Kikwete hajafanya kikao chochote na Zitto wala kuwasiliana naye kwa njia ya simu. "Hata wakati wa Escrow hakuwasiliana naye kwa sababu alikuwa nje ya nchi," alisema Rweyemamu.

Alisema Dk. Mengi ana mawasiliano ya Rais Kikwete na ni marafiki, hivyo ilitarajiwa baada ya kupata taarifa hizo angewasiliana naye.

Rweyemamu alisema hivi sasa kunauzushi mwingi nchini, hivyo siyo jambo jema mfanyabiashara huyo kusikiliza maneno ya watu kwani kufanya hivyo atakosana na watu wengi. Aprili 15, mwaka huu Dk. Mengi alituhumiwa kutaka kuiangusha Serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza uongozi wake Oktoba, mwaka huu.

Dk. Mengi alisema habari hiyo imempa hofu kubwa juu ya mustakabali wa maisha yake kutokana na kile kilichoandikwa kuwa Kikwete aliapa atapambana naye. "Hofu yangu kubwa inasababishwa na Ikulu na Maelezo kwa kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi. "Ikulu na Maelezo wako makini katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu Rais Kikwete, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa," alisema Dk. Mengi.

Aprili 18, mwaka huu naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema watu waliotajwa katika wizi wa fedha za Escrow wasitapetape kutafuta mchawi wakati wao ndio wezi wenyewe.

Kutokana na hali hiyo amesema suala la kumuhusisha mfanyabishara huyo kuwahonga wabunge ili kuishughulikia Serikali ni sawa na porojo. Kauli hiyo aliitoa mjini Shinyanga alipokuwa akihutubia ambapo alisema hatorudi nyuma katika kusimamia haki za Watanzania na kama kuna mtu ana chembe ya ushahidi wa jambo hilo apeleke kwenye vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.

JK kimya kimya Jordan Rweyemamu alisema pia kuwa Jumamosi ya juma lililopita Rais Kikwete alisafiri kwenda nchini Jordan bila kutoa taarifa kwa umma kutokana na jambo hilo kuwa nyeti hali iliyochangiwa na mazingira ya mkutano aliokwenda kuhudhuria.

Alisema Rais Kikwete alikwenda nchini humo kwenye mkutano ambao pamoja na mambo mengine walizungumzia masuala ya ugaidi ambayo kwa sasa yamekuwa tishio duniani. "Ule mkutano ulitakiwa uwe wa siri kutokana na uzoefu wa Jordan na mambo ya ugaidi na pia majirani zake ambao ni Syria, Israel, Iraq na mataifa mengine," alisema. Sheria ya mtandao Rweyemamu alisema Rais Kikwete ataisaini sheria ya makosa ya mtandao licha ya baadhi ya wadau kuipinga.

Alisema sheria hiyo ilipitia hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Lazima rais aisaini kwa sababu ilipitia hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na kupitishwa na Bunge," alisema Rweyemamu.

WAKIMBIZI 152,572 WAPATIWA VYETI VYA URAIA

Waliokuwa wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania zaidi ya 152,572 walioingia nchini humo tangu mwaka 1972, wamekabidhiwa vyeti vya uraia wa Tanzania na kuwa huru kuishi kama Watanzania wengine.

Wakimbizi hao walikuwa wameomba uraia wa Tanzania mwaka 2008 na kupewa na waziriwa mambo ya ndani mwaka 2010, sasa ni halali kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo za udiwani na ubunge.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa vyeti hivyo, mkuu wa makazi ya Mishamo, Frederick Nisajile alisema ugawaji wa vyeti hivyo ulianza Novemba 24 mwaka 2014 katika makazi ya Katumba mkoani Katavi magharibi mwa Tanzania ambako watu 56,554 walipewa vyeti vya uraia na baadaye kuhamia katika makazi ya Ulyankulu mkoani Tabora, magharibi mwa Tanzania ambako wakimbizi 43,453 tayari wamepewa vyeti hivyo.

Kwa upande wake msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Isaack Nantanga amesema hatua ya Tanzania kuwapa uraia wakimbizi hao ni kutokana na hiyari yao na kwamba serikali ya Tanzania ilishauriana na Burundi na hatimaye kukubaliana wapatiwe uraia wanaotaka wa kuwa Watanzania.

Hata hivyo si mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa uraia kwa wakimbizi wanaoishi Tanzania kwa muda mrefu.

Tanzania imefanya hivyo kwa wakimbizi waBurundi na Somalia ambao wameishi Tanzania kwa miaka mingi.

RAIS MORSI AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 20 JELA

Rais wa zamani wa Misri Mohamed Morsi amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa ya kusababisha kuuliwa waandamanaji mwaka 2012.

Rais wa Zamani wa Misri Mohamed MorsiKorti ya makosa ya jinai mjini Cairo imetoa hukmu hiyo wakati Morsi na watuhumiwa wengine katika kesi hiyo-wengi wao wakiwa viongozi wa chama cha Udugu wa kiislam-wakisimama ndani ya tundu la vigaendani ya ukumbi wa mahakama katika chuo cha mafunzo ya polisi mjini Cairo.

Kesi yao inahusu matumizi ya nguvu yaliyotokea nje ya kasri la rais mwezi decemba mwaka 2012.

Wafuasi wa Morsi waliwashambulia waandamanaji wa upande wa upinzani na kusababisha machafuko yaliyopelekea watu wasiopungua 10 kuuwawa.

Jaji Ahmed Youssouf ameachilia mbali madai ya kuchochea mauaji ya waandamanaji wawili na mwandishi habari mmoja machafuko hayo yaliporipuka mbele ya kasri la rais-madai ambayo wadadisi wengi walikuwa wakifikiriaa yangepeleka Morsi kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Mbali na Mohamed Morsi, wakuu wengine 12 wa chama cha Udugu wa kiislamu na wafuasi wa itikadi kali akiwemo Mohammed el Beltagy na Essam el Erian, nao pia kila mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Akitoa hukmu hiyo jaji Ahmed Youssouf ameyataja majina ya mtuhumiwa wote na kufafanua:
"Mohammed Mohamed Mursi, Mohammed el Baltagy na Essam el Erian wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa ushiriki wao wa kuchochea mauwaji ya umma wa wamisri na tuhuma za kulidhuru taifa la Misri."

Morsi na watuhumiwa wenzake walinyoosha vidole vinne-alama inayokumbusha malalamiko yaliyofanywa katika msikiti wa Rabaah al Adawiya ambako polisi waliingia kwa nguvu wakawauwa mamia ya waandamanaji wafuasi wa Morsi Agosti 14 mwaka 2013.


*Kesi zilisosalia dhidi ya Morsi hazitaharakishwa

Morsi anakabiliwa na kesi nyengine nne pamoja na wanachama wenzake wa udugu wa kiislamu, tangu alipopinduliwa na wanajeshi decemba mwaka 2013.

Morsi na wenzake wana nafasi ya kukata rufaa dhidi ya hukumu ya leo.

Wadadisi wanahisi viongozi wa Misri hawatofanya pupa kusikiliza kesi nyengine kwakua hakuna ghasia majiani na wafuasdi wa Udugu wa kiislamu hawakusayiki kwa wingi ili kuepusha wasikamatwe..

ETHIOPIA YAANZA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO

Ethiopia imeanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kwa heshima za raia wake waliouawa na wanamgambo wa kundi la Islamic State nchini Libya.

Bendera zitapepea nusu mlingoti wakati nalo bunge la nchi hiyo likikutana kujadili hatua ambazo litachukua kufuatia mauaji hayo ya raia wake zaidi ya ishirini.

Msemaji wa serikali Redwan Hussein, alisema kuwa waathiriwa hao wanaaminika kuwa wahamiaji waliojaribu kusafiri kwenda barani ulaya.

Mungano wa Afrika ambao una makao yake makuu nchini Ethiopia ulilaani mauaji hayo na kusema kuwa utafanya mikakati ya kuhakikisha kuwepo usalama nchini Libya.

Wanamgambo wa Islamic State walitoa kanda ya video ambayo inakisiwa kuonyesha mauaji hayo yanayoonyesha watu hao wakipigwa risasi na kukatwa vichwa.

DK. MENGI AHOFIA MAISHA YAKE

Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi amesema anahofia usalama wa maisha yake, kufuatia habari iliyoandikwa katika gazeti moja la kila wiki kwamba, Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye jambo ambalo limempa hofu kubwa.

Kadhalika, amelalamikia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari Maelezo kwa kukaa kimya nakuacha kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma hizo, huku taarifa hizo zikiendelea kusambazwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mengi alisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuwa yeye nikinara wa kuhujumu serikali ya Rais Kikwete siyo za kweli.

Dk.Mengi alisema amesoma kwa masikitiko makubwa habari iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na gazeti la Taifa Imara, yenye kichwa cha habari 'Zitto amchongea Mengi kwa JK' ambapo pamoja na mambo mengine inasema kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete kwamba ndiye kinara wa kuhujumu serikali yake.

Alisema habari hiyo ambayo chanzo chake kimeelezwa kwamba ni Ikulu,iliendelea kueleza kuwa Zitto alikutana na Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow ambayo Zitto alikuwa ni mwenyekiti wake.

"Habari hiyo inasema kwamba katika mazungumzo yake na Rais Kikwete Zitto amenukuliwa akimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara ni Mengi," alisema Dk. Mengi.

Dk. Mengi alisema habari hiyo ambayo nakala yake ameiambatanisha kwenye taarifa yake, inasema yeye Zitto , binafsi amekuwa akishawishiwa na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.

Hata hivyo, Dk. Mengi alisema katika habari hiyo Zitto alikwenda mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa Rais Kikwete akimaliza muda wake wa Urais atamshughulikia kwa nguvu zake zote.

Alisema habari hiyo imeeleza kwamba baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa taarifa hizo.

Mengi alisema tuhuma zilizotolewa kuhusu nia yake ya kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko la kwamba Rais Kikwete aliapa kuwa atapambana na yeye zimempa hofukuhusu mustakabali wa maisha yake.

Alisema kuwa hofu yake kubwa inasababishwa na Ikulu na Idara ya habari Maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote.

"Najua umakini wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya habari Maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu Rais, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,"alisema Dk. Mengi.

Aliongezea kusema kuwa," hofu yangu inazidi kuwa kubwa kwa sababu Rais ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama. Kauli yake kama ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba atapambana na mimi inawezekana kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola kuniangamiza," alisema.

Alitolea mfano mwaka 1170, AskofuMkuu wa Canterbury nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia mfalme akisema"hakuna anayeweza kuniondolea huyo mkorofi?". Walinzi wake wakadhani mfalme ameagiza wamuue Askofu huyo na wakamuua, alisema.

CHANZO: NIPASHE

MWANDISHI WA HABARI APIGWA RISASI UKRAINE

Mwandishi maarufu wa Ukraine ameuawa kwa kupigwa risasi mjini Kiev na watu waliokuwa wameficha nyuso zao.

Oles Buzyna alifahamika sana kwa maoni yake ya kuunga mkono Urusi na amefanya kazi yauchapishaji akishirikiana na serikali ya rais Viktor Yanukovych aliyeondolewa madarakani nchini Ukraine.

Kifo chake kimekuja siku moja baada ya mwanasiasa mwenye kupendelea Urusi, Oleh Kalashnikov kuuawa katika shambulio linalofanana.

Rais Poroshenko ametaka uchunguzi ufanyike haraka, amesema mauaji haya dhidi ya watu maarufu yamefanyika makusudi na maadui wa Ukraine.

KIJANA JELA MIAKA 30 KWA KUMLAWITI MWANAFUNZI

MAHAKAMA ya Wilaya ya Tabora imehukumu Masudi Nassor (20) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wa kike wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka tisa.

Akitoa hukumu hiyo jana Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Bahati Chitepo alisema kwamba ametoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia kama hiyo kama kijana huyo mdogo.

Alisema kitendo alichofanya kijana huyo mwenye nguvu ya kufanya kazi na kupata mwenzi wake wanayelingana umri inaonesha wazialifanya hivyo makusudi.

Hata hivyo Hakimu Chitepo alisema kwamba ushahidi uliotolewa mbele ya Mahakama hiyo kutoka kwa mganga aliyemhudumia mtoto huyo katika Hospitali ya Kitete unaonesha wazi kwamba mshtakiwa alimwingilia mtoto huyo kinyume na maumbile yake na kumsababishia maumivu makali.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Mwendesha Mashitaka wa Serikali aliiomba Mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshitakiwa huyo kwa kile alichoeleza kuwa hilo ni kosa lake la pili hivyo adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye nia mbaya.

Awali Mwendesha Mashitaka alieleza Mahakama hiyo kwamba mnamo Januari 22, mwaka huu majira ya asubuhi katika Kata ya Kiloleni, Manispaa ya Tabora, Nassor akiwa anaendesha baiskeli alikutana na mlalamikaji akiwa anakwenda shuleni na kuomba lifti.

Baada ya kumpandisha kwenye baiskeli Nassoro alikwenda naye kwenye pori la Kalunde ambapo alimlawiti mara tatu na kumtelekeza huko kisha kukimbia lakini alikamatwa na askari Jeshi aliyekuwa dori katika kambi hiyo nakumfikisha Polisi.

Hata hivyo mshitakiwa huyo aliiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu kwani anaishi na babu yake mlemavu wa mguu na wazazi wake wote wamefariki.

WATANZANIA KURUDISHWA TOKA YEMEN

Tanzania imetangaza kuwarejesha nchini raia wake wanaoishi Yemen, kufutia mapigano yanayoendelea nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitangaza uamuzi huo wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Yemen, Ali Ahmed Saleh, jana.

Waziri Membe alisema ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, wanarejea nyumbani salama.

Awamu ya kwanza ya kurudisha Watanzania ilianza siku chache zilizopita chini ya uratibu wa Ofisi zaUbalozi wa Tanzania mjini Mascut, Oman.

Kwenye awamu hiyo Watanzania 25 walirudishwa nyumbani huku jitihada za kuandikisha wengine zikiendelea.

"Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko ya Yemen wanarejeshwa salama nyumbani mara moja," alisema Membe.

RAIS ZUMA ASHTUSHWA NA GHASIA ZA NCHINI MWAKE

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ameshutumu ghasia zilizopo nchini humo hivi sasa ambapo wahamiaji wageni wameshambuliwa.

Ametaja ghasia hizo kama za kutisha na zisizokubalika.

Watu watano wameuawa tangu juma lililopita ambapo wamelaumiwa na wenyeji kwa kufanya kazi wanazostahili kufanya wao.

Akihutubia bunge leo alasiri, RaisZuma alisema mashambulizi hayo yalikiuka haki za kibinadamu kama vile haki ya kuwa hai na kuheshimiwa.

Awali maelfu ya raia wa Afrika Kusini wamefanya maandamano katika mji wa Durban kulalamikiakile walichotaja kama ukatili dhidi ya Waafrika wengine.

Katika maeneo yanayopakana na Johannesburg, wenye maduka wenye asili ya kutoka Ethiopia, Somalia na maeneo mengine ya Afrika walifunga biashara zao, wakiogopa kuwa mali yao itaporwa.

WATU 10 WATIWA MBARONI KWA KUHISIWA KUJIHUSISHA NA UGAIDI

POLISI mkoani hapa imewatia mbaroni watu zaidi ya tisa wanaojihusisha na uhalifu wakiwa na milipuko hatari na zana za milipuko, wakiwa wamefichwa ndani ya Msikiti wa Suni kata ya Kidatu, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.

Licha ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, mwingine ameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira baada ya kumshambulia na kumkata kwa jambia shingoni askari polisi mwenye namba F. 3323 Koplo Nassoro.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha jana na kusema watu hao walikamatwa juzi majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha Nyandeo, Kijiji cha Chicago, kata na tarafa ya Kidatu, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.

Hata hivyo, alisema Polisi walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa mashaka.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, waumini wote walitakiwa kutoka nje ya msikiti wakiwa na mabegi yao, nandipo katika ukaguzi na upekuzi huo walifanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na milipuko hatari.

Hata hivyo, alisema kukamatwa kwao ni baada ya Polisi kupokea taarifa za siri zinazohusu watu hao kujihusisha na vitendo vya uhalifu na pia alimtaja aliyefariki katika tukio hilo kuwa ni Hamad Makwendo mkazi wa Manyasini, Ruaha wilayani Kilombero ambaye ndiye anadaiwa kuwa mwenyeji wa watuhumiwa hao wengine.

Akielezea zaidi alisema, baada ya kupokea taarifa hizo, Polisi ilifuatilia na kwamba, katika ufuatiliaji huo waliona pikipiki mbiliza matairi matatu aina ya Bajaj zikielekea katika mji wa Mkamba eneo la wilaya ya Kilombero ambazo ziliwapotea na baada ya kitambo kidogo, Bajaj hizo zilirudi tena zikiwa na abiria mmoja.

Alisema, Polisi waliokuwepo eneo hilo walisimamisha bajaj moja na iliposimama, mtu mmoja akiwa na jambia mkononi aliruka kwenye bajaj na kuanza kukimbia ndipo askari walipoanza kumkimbiza.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mtuhuyo alipogeuka alimshambulia kwakumkata na jambia shingoni askari mwenye namba F. 3323 Koplo Nassoro na ndipo askari mwenye namba E. 9245 Koplo Chomola alipompiga risasi ya mguuni upandewa kulia mtuhumiwa huyo.

Alisema wananchi walifika eneo la tukio na baada ya kuona askari ameumizwa ndipo walipomchoma moto mtuhumiwa na kusababisha kifo chake.

Alisema baada ya tukio hilo, taarifa zilifikishwa mkoani na ndipo Polisi mkoa walikwenda eneo la tukio wakiwa na timu ya askari na kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo ndipo walipokamatwa watuhumiwa zaidi ya tisa waliokutwa ndani ya Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, vitu vilivyokutwa katika mabegi hayo ni pamoja na milipuko 30 aina ya 'Water Explosive Gel', bendera nyeusi yenye maandishi ya Kurani na Kiswahili yenye maneno Mungu Mmoja; nyaya, majambia, bisibisi, nguo za jeshi, misumeno yachuma, spana piperange, madaftari na vitabu mbalimbali vikiwemo vya risiti.

Vitu vingine walivyokutwa navyo ni vifaa vya kuficha uso 'mask' na kitambulisho kimoja chenye jina la Ramadhani Hamis kinachojieleza ni Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hata hivyo, alisema kwa mtuhumiwa aliyeuawa na wananchi alikutwa na risasi sita kati ya hizo tano zikiwa za bunduki aina ya SMG na risasi moja ya bunduki aina ya Mark IV, pamoja na nyaya mbili za umeme zikiwa kwenye mfuko mdogo wa kijeshi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa ambapo askari aliyekatwa na jambia shingoni amelazwa Hospitali ya Kiwanda cha Sukari Kilombero na hali yake inaendelea vizuri.

MGANGA WA JADI AKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linamshikilia mganga mmoja wa Jadi kwa tuhuma za kumkamata akiwa na ngozi mbili za chui na mkia wa nyumbu akiwa amehifadhi ndani ya chumba chake cha kulala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri alimtaja mtuhumiwa huyo aliyekamatwa na nyara hizo za Serikali kuwa ni Kabichi Nhulu (39)Mkazi wa Kijiji cha Kakese Tarafa ya Misunkumilo Wilaya ya Mpanda Mkoani hapa.

Alisema tukio la kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo lilitokea hapo majira ya saa kumi na mbili jioni nyumbani kwa mtuhumiwa katika Kijiji cha Kakese.

Alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa kufuatia taarifa za kilizotolewa kwa jeshi la polisi kutoka kwa raia wema kuwa mtuhumiwa huyo anamiliki nyara za Serikali visivyoalali.

Alieleza baada ya taarifa hizo kulifikia jeshi la polisi lilifika kijijini hapo kwa lengo la kufanya upekuzi kwenye nyumba ambayo anaishi mtuhumiwa huyo.

Kidavashari alisema baada ya polisi kufanya upekuzi ndani ya nyumba ya mtuhumiwa Kabichi Nhulu alikamatwa akiwa na ngozi mbili za chui na mkia wa nyumbu akiwa amehifadhi ndani ya chumba chake cha kulala akiwa ameficha chini ya uvungu wa kitanda.

Mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika ili aweze kujibu tuhuma inayomkabili.

Chanzo: KATAVI YETU

AJARI ZAUA WATU 866 KATIKA MIEZI MITATU

JESHI la Polisi nchini, limesema Watanzania 866 wamefariki dunia katika kipindi cha miezi mitatu, kutokana na ajali za barabarani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga alisema kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, ajali 2,116 zimetokea katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema katika ajali hizo, watu 866 wamepoteza maisha na wengine 2,363 kujeruhiwa, ambao baadhi yao wamepata ulemavu.

Hata hivyo nje na kipindi hicho, ajali nyingine zilizotokea kuanzia Machi 11 hadi April 12, mwaka huu zimesababisha vifo vya watu wengine 103 na hivyo kufanya idadi ya watu walipoteza maisha katika kipindi cha miezi mine kuwa 969.

Akizungumzia sababu za ajali hizo, Kamanda Mpinga alisema ni mwendo kasi usiozingatia alama za barabarani na kufutika kwa baadhi ya michoro barabarani.

Alisema sababu nyingine, ni baadhi ya wamiliki wa vyombo vya moto kuhamasisha mwendo kasi kwa madereva wao, abiria kushabikia nabaadhi ya wadau wa usalama barabarani kutowajibika ipasavyo.

Kamanda Mpinga, alisema uzembe wa madereva, ubovu wa barabara na uoni hafifu kwa baadhi ya madereva ni miongoni mwa sababu zinazochangia ajali nyingi kutokea.

Alisema kuwapo kwa tatizo la utelezi, ulevu na uchovu, unaosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha nako kumeongeza idadi ya ajali.

"Utumiaji wa dawa za kulevya ni sababu nyingine ambayo inasababisha ajali nyingi," alisema.

Huku akionekana kusikitishwa na matukio hayo, Kamanda Mpinga alisema tatizo jingine ni ubabe wa madereva wanaoendesha magari makubwa ya mizigo kutothamini magari ndogo, waenda kwa miguu, bajaj pamoja na pikipiki wawapo barabarani.


HATUA KALI

Kuhusu hatua, Kamanda Mpinga, alisema madereva wote waliosababisha ajali za hivi karibuni watachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kunyang'anywa leseni zao.

Alisema ajali nyingine zitakazo tokea baada ya hizo, wamiliki wa vyombo husika watafungiwa kampuni zao.

Alitoa wito kwa watumiaji wa barabara kuchukua hadhari, madereva kuwa makini msimu huu wa mvua.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wamiliki wa mabasi yanayokwenda safari za mbali kuajiri madereva wawili watakao safiri ili kumpunguzia dereva uchovu.

Aliomba Bunge Ili kukomesha au kupunguza wimbi la ajali hizo, Kamanda Mpinga ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubadilisha sheria zilizopo za usalama barabarani ambazo zinatoa adhabu ndogo kwa watu wanaosababisha ajali.

Alisema uchunguzi uliofanywa na kikosi hicho, umebaini wamiliki wa mabasi wamekuwa wakihamasisha madereva wao kwenda mwendo kasi kwa kujali maslahi yao kibiashara zaidi.

Miongoni mwa ajali zilizogusa mioyo ya watu ni ile iliyotokea Machi 11, mwaka huu katika Kijiji cha Changarawe Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ambapo watu 50 walipoteza maisha, huku 20 wakijeruhiwa kutokana na basi la Majinja kugongana na lori.

Katika ajali nyingine iliyotokea maeneo ya Mikumi Mbugani mkoani Morogoro Machi 17, mwaka huu na kuhusisha basi la Fm Safari na lori aina ya Scania, watu wawi walipoteza maisha na nane kujeruhiwa.

Ajali nyingine ilitokea Machi 19, mwaka huu eneo hilo hilo la Mikumi na kuhusisha basi dogo aina ya Tata linalojulikana kwa jina la Msanga Line lililogongana na basi la Luvinzo na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi 17.

Ajali nyingine ni ile iliyotokea Aprili3, mwaka huu iliyokuwa imebeba mashabiki wa timu ya soka ya Simba ambao walikuwa wakielekea mkoani Shinyanga, ambapo iliua watu saba na kujeruhi 22.

Mbali na ajali hizo, ajali nyingine iliyotokea mkoani Tanga eneo la Mkata ilihusisha basi la Ratco, Ngorika na gari dogo aina ya Paso ambapo watu 10 walipoteza maisha pamoja na kujeruhi wa 12.

Pia Aprili 12, mwaka huu mkoani Morogoro kulitokea ajali katika milima ya Hiyovi ambapo basi la Nganga Express lililogongana na Fuso na baadaye kuwaka moto na kusababisha watu 19 kupoteza maisha, huku wengine 10 wakijeruhiwa.

17 WAUAWA SHAMBULIO LA AL SHABAAB

Watu 17 wameripotiwa kuuawa na wengine 20 kujeruhiwa vibaya wakati wanamgambo wa Kiislamuwa Al Shaabab waliposhambulia majengo ya wizara ya elimu mjini Mogadishu, Somalia.

Mwandishi wa BBC Mohammed Moalimu, amesema kuwa wavamizi hao walilipua bomu lililotegwa ndani ya gari kwenye ukuta wa jengo hilo Kulingana na msemaji wa idara ya usalama wa ndani Mohammed Yusuf watu 8 waliuawa na wavamizi hao huku wanajeshi wawili wakipoteza maisha yao.

Askari mmoja ni wa muungano wa majeshi ya umoja wa Afrika.

Msemaji huyo anasema kuwa wavamizi hao walikuwa ni 7 wawili waliojilipua langoni huku wengine watano wakikabiliwa na maafisa wa usalama.

Walioshuhudia wanasema wavamizi hao walitumia bomu lililotegwa ndani ya gari kabla ya wavamizi kadhaa kuingia ndani yajengo wakiwa wamejihami kwa bunduki za rashasha.

Msemaji wa wa kitengo cha mashambulizi cha kundi la wapiganaji wa Al Shabaab Sheikh Abdiasis Abu Musab, amethibitisha kuwa ni wao waliotekeleza shambulizi hilo na kuwa ''wapiganaji wetu wamekwisha ingia ndani ya jengo hilo lenye wizara ya elimu''

Mapigano yanaendelea hadi sasa ndani ya jengo hilo baina ya majeshi ya serikali na wapiganaji hao kulingana na mwakilishi wa polisi.

Wapiganaji wa Al shabaab wametekeleza mashambulizi kama haya katika siku za hivi punde.

Mwezi uliopita wapiganaji wa Al Shabaab walishambulia hoteli moja mjini Mogadishu uvamizi huo ulikamilika siku mbili zilizofwatia.

Waandishi wa habari walioshuhudia matukio kabla ya uvamizi huo wanadai kuwa kulikuwa na milipuko miwili mikubwa kabla ya milio ya risasi kuanza kusikika kutoka jengo hilo.

Hakuna kundi lililothibitisha kutekeleza shambulizi hilo lakini Al shabaan imekuwa ikitumia mbinu kama zilizotumika leo.

Kundi hilo la waislamu linapinga serikali iliyoko sasa ambayo inaungwa mkono na majeshi ya Umoja wa Afrika.

OBAMA KUIONDOA CUBA KATIKA ORODHA YA UGAIDI

Rais Barack Obama amesema ataiondoa Cuba kutoka orodha ya Marekani ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani.

Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani imesema hatua hiyo inakuja huku kukiwa na jitihada za kujenga uhusiano kati ya Marekani na Cuba.

Uwepo wa Cuba katika orodha hiyo pamoja na nchi za Syria, Iran na Sudan kilikuwa kigezo cha Cuba katika mazungumzo yake na Marekani ya kufungua ofisi za balozi kati ya nchi hizo.

Seneta wa chama cha Republican Marco Rubio ameishutumu Ikulu ya Marekani kwa uamuzi huo, akisema kuwa Cuba bado ni taifa linalofadhili ugaidi.

"Wanawahifadhi Wamarekani ambao wanakimbia mkono wa sheria, akiwemo mtu aliyemuua afisa wa polisi huko New Jersey zaidi ya miaka 30 iliyopita," amesema Bwana Rubio, Mmarekani mwenye asili ya Cuba ambaye alizindua kampeni yake ya uchaguzi wa rais wa Marekani 2016.

"Ni nchi ambayo pia inaisaidia Korea Kaskazini kukwepa vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa."

Bwana Obama alitangaza tukio la kihistoria la kurejesha uhuasiano kati ya Marekani na Cuba mwezi Desemba 2015 lakini vikwazo vya kibiashara vya Marekani dhidi ya Cuba vinabakia, na vinaweza kuondolewa tu na baraza la Congress.

ASASI ZISIZO ZA KISERIKALI 53 ZAMUANDIKIA BARUA RAIS ASISAINI MUSWADA

Asasi zisizo za kiserikali 53 zimemwandikia Rais Jakaya Kikwete,barua ya kumuomba asisaini Sheria ya Takwimu ya 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni ili kuruhusu kufanyiwa marekebisho kwanza.

Kwa majibu wa barua hiyo iliyosainiwa na asasi 53 na mtandao wa asasi za kiraia ambayo NIPASHE imeona nakala yake, zinataka sheriahizo zirudishwe bungeni kuondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na haki za binadamu kwa ujumla.

"Tunashauri kabla ya kutia saini sheria hizi upate muda wa kusikilizakilio cha jamii juu ya ubaya wa sheria hizi kwa mustakabali wa taifa. Sheria hizi zikipitishwa katika utawala wako zitatia doa dhamira yako nzuri ya kuongeza wigo na uhuru wa habari na ushiriki wa wadau katika maendeleo ya kitaifa,"alisema.

Barua hiyo imeeleza sababu za kumtaka Rais kutosaini sheria hizo kuwa ni, malengo ya Sheria ya Takwimu siyo tu kuratibu takwimu za kitaifa, bali umetoa madaraka makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kama kitovu cha utoaji wa takwimu nchini.

"Maana yake ni kwamba taasisi zote za serikali, mashirika binafsi, taasisiza elimu ya juu, vyuo vikuu na taasisi za utafiti hazitakuwa na uhuru wa kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa ya NBS" ilisema barua hiyo.

Imesema pia sheria hiyo imeweka adhabu kali kwa vyombo vya habari,asasi za kiraia, taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu vitakavyotenda makosa yaliyoainishwa katika sehemu ya tatu ya sheria.

Kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao, barua hiyo imesema itaminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa wananchi kuwasiliana na kupashana habari endapo itasainiwa bila marekebisho.

"Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa uhuru wa mawasilianona matumizi ya mitandao ya kijamiikama Facebook, WhatsApp, Jamii Forums, Twitter, blog… Kupitishwa kwa sheria hii bila kufanyiwa marekebisho kutasababisha Watanzania wengi kutiwa hatiani bila sababu, lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari nchini" iliongeza kusema.

CHANZO: NIPASHE

RADI YAUA 6 YAJERUHI WENGINE 15

Wanafunzi sita wa shule ya msingi, wamefariki dunia kwa kupigwa na radi na wengine 15 wamejeruhiwa miongoni mwao vibaya kufuatia mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi kunyesha katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana.

Tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi katika Shule ya Msingi Kibirizi iliyopo kwenye manispaa hiyo.


KAULI YA MGANGA

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni, Dk. Fadhili Kibaya, alisema alipokea maiti za watu wanane zikiwamo za wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Kibirizi na moja ya mwalimu wao jana saa 6:00 mchana.

Alisema maiti nyingine ni ya mwanaume mkazi wa Bangwe katika manispaa hiyo. Alisema mbali ya maiti, pia alipokea majeruhi 15.

Dk. Kibaya aliyataja majina ya wanafunzi waliofariki dunia kuwa ni Yusuf Athumani (8), Hassani Ally (9),Fatuma Silei (7), Zamuda Seif (8), Warupe Kakupa (10) na Shukurani Yohana (7) ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Kibirizi.

Alisema wengine waliofariki dunia katika tukio hilo la kusikitisha ni mwalimu wa shule hiyo, Elieza Mbwambo (25) na Focus Ntahaba (35), mkazi wa Bangwe katika manispaa hiyo.

Dk. Kibaya alitaja wanafunzi waliojeruhiwa katika tukio hilo na ambao wamelazwa wodi namba nane hospitalini hapo kuwa ni Mahamoud Sijafiki (10), Najimu Rajabu (9) na Khatibu Amani (9).Aidha, alisema wengine watano wako kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU) na wengine walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwao.


MWALIMU ANENA

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kibirizi, Emmanuel Wilbert, alisema mwalimu aliyefariki dunia alitoka darasa la tatu na kuingia ofisi ya walimu na kukaa akiendelea na shughuli zake kama kawaida.

Wilbert alisema baada ya muda mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali na radi huku walimu wengine wakiwa madarasani wakiendelea na vipindi, ilipiga radi iliyosababisha kifo cha mwalimu na wanafunzi hao waliokuwa madarasani.

Alisema baada ya tukio hilo, wanafunzi na walimu walikimbia ovyo na mwalimu mwingine Merina Serilo, alipigwa na radi na kujeruhiwa. Hata hivyo, alisema hali yake inaendelea vizuri.


KAULI YA KAMANDA

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alithibitisha kutokea kwa tukiohilo na kueleza kuwa masuala ya radi hayazungumziki.

WANAFUNZI KIU WAGOMA

Wanafunzi wa vitivo vya Sayansi ya Afya wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Kampala-tawi la Dar es Salaam (KIU), wamegoma kuendelea na masomo baada ya kubaini kuwa kozi wanazosoma katika chuo hicho hazijasajiliwa katika ya bodi mbalimbali kama taratibu na sheria zinazoelekeza.

Walianza mgomo huo tangu Ijumaa iliyopita baada ya kugundua kuwa kozi wanazofundishwa hazijasajiliwa katika Bodi ya Mafamasia, Bodi ya Maabara na Baraza na Madaktari.

Walisema jana chuoni hapo kuwa wamekuwa wakiendelea na masomo bila kugundua kama kozi wanazochukua hazijasajiliwa katika bodi hiyo huku uongozi wa chuo ukikaa kimya.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Wanafunzi (KIUSO), Kenedy Murunya, alisema walibaini kuwa kozi wanazosoma hazijasajiliwa baada ya kwenda katika ofisi za bodina kuelezwa kuwa hazijasajiliwa. Wanafunzi waliokumbwa na tatizo hilo ni wale wanaochukua Shahada za maabara, udaktari na upasuaji.

"Wanafunzi walipokwenda Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) waliambiwa kuwa tume imeshafanya asilimia 50 ya usajili wa chuo hicho na asilimia 50 nyingine zilizobaki zinatakiwa zishughulikiwe na bodi husika za usajili," alisema.

Mwakilishi wa Kitivo cha udaktari (SUGA)), Martin Augustine, alisema 2013 wakati wanaanza masomo waliambiwa na uongozi wa chuo kuwa kozi zao zimesajiliwa bila kujua walikuwa wanadanganywa na uongozi wa chuo hicho.

Alisema mwaka huu walikwenda Bodi ya Madaktari Tanganyika wakaambiwa kuwa bado kozi yao haijasajaliwa kutokana na uongozi wa KIU kuzembea kutuma nakala muhimu zitakazofanikisha usajili.

Alisema Ijumaa baada ya mgomo wawakilishi wa vitivo vya sayansi wangazi zote za masomo walifanya kikao na uongozi wa chuo chini ya OCD wa Ilala kujadili matatizo ya usajili na uongozi na kuwa cha ajabu wawakilishi hao hawakupewa majibu yanayoridhisha hali iliyosababisha mgomo huo kuendelea.

Alisema tangu mgomo uanze Jeshi la Polisi limeweka kambi likiangalia hali ya usalama wa chuo.

Alisema Septemba, 2014 walikwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa lengo la kumuona Waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, lakini hawakumuona hivyo kumwandikia barua ili awape majibu ambayo hadi sasa hawajapatiwa.

Alisema wanaendelea kulipa ada kubwa japokuwa serikali ilikiagiza chuo hicho kushusha ada cha kushangaza Baraza la KIU ambalo lipo Uganda lilikataa maagizo ya serikali.

Alisema wanafunzi wa udaktari mwaka wa pili wanalipa Sh. milioni 8 wakati wa mwaka kwanza wanatozwa Sh. milioni 6.7, maabarash. milioni 4.8, Famasia milioni 5.4 huku wa mwaka wakilipa sh. milioni3.8.Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa KIUSO, Elisha Mushi, mgomo huo unajumuisha wanafunzi wa vitivo vya sayansi pekee wakati vitivo vya biashara na sharia vinaendelea na masomo.

Jitihada za kumpata Rais wa KIUSO, Elias Mbogo pamoja na Waziri wa Elimu, Answari hazikufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa wote wamekwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata ufumbuzi wa matatizo ya wanafunzi.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu wa Kiuso, Fadhilina Kassim, alisema anachofahamu yeye kuwa chuoni hapo kuna mgomo wa wanafunzi, lakini mwenye dhamana ya kuzungumzia suala hilo ni Waziri wa Elimu au Waziri Mkuu.

Afisa Masoko na Uhusiano wa KIU, Keneth Uki, alithibitisha kuwapo kwa mgomo wa wanafunzi hao huku akisisitiza kuwa vitivo vingine vya sayansi vimeshakamilika usajili ingawa kitivo cha wanafunzi wanaochukua Famasia tu ndio kozi zao hazijakamilisha usajili katika Baraza la Famasia Tanzania.

Wanafunzi hao wanaiomba wizara husika iwapatie ufafanuzi kuhusiana na suala hilo pamoja na uhalali wao KIU kwa kuwa walijiunga na chuo hicho kupitia TCU na NACTE.

NEC YASEMA BVR 1600 KUWASILI MUDA WOWOTE

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema vifaa BVR Kts 1,600 vinatarajiwa kuwasili wakati wowotekuanzia leo.

Kadhalika, Nec imesema itatoa ratiba ya uandikishaji kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR), kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Iringa na Ruvuma.

Mikoa hiyo ni yenye watu 4,809,428kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na kati yao watu 2, 599,205 ndiyo wenye sifa ya kupiga kura hadi kufika siku ya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva (pichani), alisema aliliambia NIPASHE kuwa baada ya vifaa hivyo, 248 vilivyowasili hivi karibuni na 250 vilivyokuwa vinatumika mkoani Njombe, vitatumika kwenye mikoa hiyo kwa pamoja.

Aidha, alisema ratiba ya uandikishaji kwenye mikoa hiyo itatolewa wakati wowote wiki hii ili kuwafanya wananchi wa maeneo husika kujitokeza kwa wingi kushiriki.

Jaji Lubuva alisema Nec ina uhakika wa kuandikisha Watanzania wenye sifa ya kupiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura hadi Julai, mwaka huu na kwamba uchaguzi mkuu ni lazima ufanyike.

Akizungumzia uwezekano wa kugawanywa kwa majimbo na kata za uchaguzi, alisema utaratibu huo ni wa kawaida na unafanyika kila mwaka wa uchaguzi mkuu.

"Kwa sasa tunaangalia maeneo ya utawala wa serikali, mipaka na kujua kama kuna ongezeko la mgawanyo wa maeneo ndipo tuweze kutangaza maeneo mapya ya uchaguzi," alisema.

Alisema kwa sasa wako kwenye mchakato na wakati wowote baada ya kukamilisha watatangaza kama kuna ongezeko la maeneo ya uchaguzi kwa ngazi ya kata na majimbo.

CHANZO: NIPASHE

TANZANIA KUMENYANA NA UGANDA MICHUANO YA CHAN

Tanzania itachuana na Uganda wakati Kenya itakipiga na Ethiopia katika michuano ya kufuzu ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kufuatia ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika, (CAF), Mechi hiyo ya awali itachezwa kati ya Juni 19-21 wakati ile ya marudiano itachezwa kati ya July 3-5 mwaka huu.

Fainali za CHAN zitafanyika nchini Rwanda kuanzia January 16 mpaka February 7, 2016.

Michuano hiyo, kwa mujibu wa ratiba ya CAF, itashirikisha timu 42, ambazo zitashindana katika kanda 6 na fainali zake zitachezwa na nchi 16 tu wakiwemo timu mwenyeji.

Uganda kwa sasa ipo nafasi katika nafasi ya 84 ya viwango vya FIFA, wakati Tanzania ipo nafasi ya 100.

Ratiba ya kufuzu ya CHAN ni kama ifuatavyo

Kanda ya Magharibi A.

Guinea Bissau vs Mali

Mauritania vs Sierra Leone

Guinea vs Liberia

Senegal vs Gambia


Kanda ya Magharibi B

Ghana vs Ivory Coast

Nigeria vs Burkina Faso

Niger vs Togo


*Kanda ya kati

DR Congo vs Jamhri ya Kati (CAR)

Cameroon vs Congo

Chad vs Gabon


*Kanda ya Kati Mashariki Hatua ya awali

Tanzania vs Uganda

Djibouti vs Burundi

Ethiopia vs Kenya


*Kanda ya Kusini

Zimbabwe vs Visiwa vya Comoro

Lesotho vs Botswana

Namibia vs Zambia

Msumbiji vs Seychelles

Afrika ya Kusini vs Mauritius

Swaziland vs Angola


*Kanda ya Kaskazini

Libya vs Tunisia

Morocco vs Libya

MARUBANI WAZIKUNJA KWENYE CHUMBA CHA KUONGOZEA NDEGE

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati dunia bado ikiwa na kumbukumbu mbaya ya ndege yashirika la ndege la Ujerumani na vifo vya abiria 150 ndaniye,kituko kingine kimegubika tasnia ya urubani baada ya marubani wawili kuondolewa kwenye zamu ya urushaji ndege kufuatia madai yawawili hao kuzikunja katika chumba cha kuongozea ndege.

Marubani hao hurusha ndege za shirika la ndege la India, Air India walishushwa katika ndege yao baada ya rubani msaidizi kumshambulia captain wake ama nimwite rubani kiongozi.

Hata hivyo ili kulinda hadhi ya shirika la ndege la India, maafisa wa juu wa shirika hilo walidai kuwa marubani hao wawili walirushiana maneno na hawakuingiana mwilini.

Msemaji wa shirika hilo la ndege amedai kwamba marubani hao wawili wote waliondolewa kwenye zamu zao na maswali tele yaligubika msuguano wa marubani hao,na kitengo cha nidhamu cha shirika hilo la ndege kilipewa jukumu mara moja kuwaketisha marubani hao kujua chanzo cha sintofahamu hiyo na hatimaye kuyamaliza.

Lakini askari wa ngazi za juu nchini India wamedai kwamba chanzo cha mzozo huo kilianzia pale Rubani kiongozi alipomtaka rubani msaidizi kurekodi mwenendo wa ndege hiyo ikiwemo idadi ya abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo kabla haijaanza safari yake.

Ndege hiyo inadaiwa ilikuwa ifanye safari kutoka Delhi kuelekea Jaipur na baada ya kutua salama wafanyakazi wa ndege hiyo waliarifiwa juu ya tukio hilo.

Tukio hili limekuja siku chache tubaada ya rubani wa shirikisho la ndege za kukodi nchini India kumuandikia waraka mkurugenzi kuu wa mamlaka ya anga nchini humo akielezea msongo wa mawazo unavyowatesa marubani.

Katika barua hiyo rubani huyo alielezea namna marubani wanavyozongwa na mambo na chanzo ni mishahara midogo, masuala ya kifamilia, hayo ndo baadhi aya vyanzo vya matatizo yanayozonga vyumba vya marubani.

Kwa taratibu za mamla za anga rubani anapaswa kuwa mtulivu kwa namna yoyote,na inawezekanaje rubani wa shirika la ndege la India afanye kazi wakati akiwa amevurugwa?

RADI YAPIGA KANISANI, YAUA WATANO

Watu watano wamefariki dunia papo hapo katika kijiji cha Shilabela, kata ya Bwanga, wilayani Chato, mkoa wa Geita, baada ya kupigwa na radi wakati wakiendelea na ibadaya Sikukuu ya Pasaka.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni kwenye Kanisa la Assemblies of God Tanzania (AGT) na kujeruhi watu wengine 18 wakati wakiwa kwenye maadhimisho ya sikukuu ya kufufuka kwa Yesu Kristo, Pasaka. Kati ya majeruhi hao, wanne wamelazwa katika Zahanati ya Bwanga, wilayani Chato.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, akizungumza na NIPASHE jana, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliofariki ni Daud Merdad (20), Daud Lazaro (20), Saimon Marco (15), Haile Shija (20) na Monica Sumuni (19).

Kamanda Konyo aliwataja majeruhi watatu waliolazwa Zahanati ya Bwanga ni Mabula Mathias (8), Fabian Ezekiel (10) na Edina Leonard (21).

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Deogratias John, alisema majeruhi 18 walipokelewa katika zahanati hiyo, lakini 14 walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kutengemaa.

Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa kata hiyo, Mahobe Chiza, alisema nikubwa na la aina yake lililotokea wakati wananchi hao wakisherehekea sikukuu ya Pasaka.

"Walikuwa katika sikukuu ya Pasaka, lakini bahati mbaya mvua iliyokuwa ikinyesha ilisababisha radi kupiga nakuwadhuru waumini hao," alisema Chiza.

Naye Mchungaji wa kanisa hilo, Deus Mhangwa, alisema kanisa lake limepata msiba mkubwa wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka, ambayo ni siku ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo baada ya kusulubiwa msalabani.

"Kila nafsi itaonja mauti, lakini tukio hili limewaachia simanzi kubwa waumini wa kanisa pamoja na wananchi kutokana na kupotea kwa nguvu kazi ya kanisa na taifa kwa ujumla," alisema Mchungaji Mhangwa.

CHANZO: NIPASHE

SHAMBULIZI LAFANYIKA CHUONI NCHINI KENYA

Takriban watu sita wameuawa baada ya watu watano wanaodaiwa kufinika nyuso zao kushambulia chuo kikuu cha Garrissa Kaskazini mashariki mwa Kenya.

Watu hao wanadaiwa kuingia katika taasisi hiyo mwendo wa saa kumi asubuhi wakati ambapo waislamu walikuwa wakifanya sala yao ya alfajiri.
Hatahivyo maafisa wa polisi wanasema kuwa shambulizi hilo lilifanyika mwendo wa saa kumi na moja unusu.

Mwandishi wa BBC mjini humo anasema kuwa walinzi wawili waliuawa katika lango la chuo hicho huku maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda chuo hicho pamoja na wanafunzi wakijeruhiwa.

Walioshuhudia wanasema kuwa kumekuwa na majeruhi mengi ndani ya chuo hicho.

Mwandishi wetu anasema kuwa wapiganaji hao bado wako ndani ya chuo hicho na wamewateka nyara watu kadhaa.

Jeshi la Kenya KDF ,maafisa wa polisi na magari ya ambulance yamewasili katika eneo la tukio ambapo kumekuwa na ufyatulianaji wa risasi.

Jeshi la Kenya KDF ,maafisa wa polisi na amabulansi wamefika katika eneo la tukio na sasa wameingia ndani ya majengo ya chuo hicho ambapo kumekuwa na ufyatulianaji wa risasi kati ya washambuliaji na maafisa wa jeshi.

Wanafunzi 27 wamefanikiwa kutoroka na sasa wako katika kituo kimoja cha kijeshi.

Kufikia sasa hakuna kundi ambalo limekiri kutekeleza shambulizi hilo ijapokuwa kundi la wapiganaji wa Somalia Al Shabaab limeshukiwa kutekeleza shambulizi hilo.

Chuo hicho ndio taasisi ya kipekee ya masomo ya juu katika eneo hilo kilichofunguliwa mwaka 2011 na kiko takriban kilomita 350 kutoka mji mkuu wa Nairobi.