*Asema anadaiwa kuhusika na Al-Shabaab, vurugu za Zanzibar
*Polisi yawaonya Waislamu wanaotaka kuandamana kesho
MKURUGENZI wa Mashitaka Nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amesema hatumii madaraka yake vibaya kumnyima dhamana Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na mwenzake.
Amesema kwamba, amezuia dhamana dhidi ya Sheikh Ponda kutokana na taarifa, kwamba watuhumiwa hao wanahusishwa katika vurugu mbalimbali zilizotokea nchini na nje ya nchi.
Mawakili wanaomtetea Sheikh Ponda na mwenzake walikutana na DPP Feleshi mwezi huu, kujadili ni kwa nini haondoi zuio la dhamana kwa wateja wao. Katika mazungumzo yao, DPP aliwaambia kwamba hatumii madaraka vibaya, bali kuna sababu za msingi.
Waliokutana na DPP ni Wakili Juma Nassoro na Yahaya Njama, ambao jana waliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwamba wamezungumza na DPP ofisini kwake ili kupata sababu zilizomfanya uzuie dhamana ya Sheikh Ponda na mwenzake.
“DPP alituita tukajadili suala la dhamana ya akina Ponda, alituambia kwamba, barua tuliyomwandikia kuomba aondoe zuio la dhamana haijamfikia, hivyo tumwandikie nyingine.
“Alikataa kwamba, hatumii madaraka yake vibaya kwa kuzuia dhamana ya washitakiwa hao, isipokuwa alifanya hivyo kwa ajili ya usalama kutokana na taarifa zilizomfikia kutoka Jeshi la Polisi.
“Katika maelezo yake, DPP hakueleza moja kwa moja sababu za kuzuia dhamana ya akina Ponda, lakini alieleza viashiria kwamba, kuna taarifa za Sheikh Ponda kuhusishwa na vurugu zilizotokea Markaz Chang’ombe, Dar es Salaam, vurugu za Zanzibar, vurugu zilizotokea Kenya, tetesi za kuhusika na kuingia kwa kundi la Al-Shabaab nchini na pia kulikuwa na taarifa za kuhusika na mauaji ya sheikh mmoja kule Mombasa, Kenya na suala jingine ni malalamiko kwamba Ponda siyo raia.
“Alitueleza kwamba, kuwapo ndani kwa Sheikh Ponda siyo kwa maslahi ya nchi peke yake, bali hata kwa usalama wake, pia endapo kuna watu wanataka kumdhuru au la,” aliongeza Wakili Njama. Alisema pamoja na kumpa barua hiyo DPP, kwa mara nyingine, hadi jana walikuwa hawajapata majibu kama maombi yao yamekubaliwa au la.
DPP akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, alikiri kukutana na mawakili hao kujadili suala la dhamana ya Sheikh Ponda. Pamoja na hayo, alisema amepanga kukutana na Wanazuoni wa Dini ya Kiislamu nchini Februari 28, mwaka huu, kwa lengo la kujadili suala la dhamana ya washitakiwa hao. Katika uamuzi huo, alisema Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu liliwaandikia barua mawakili wa Sheikh Ponda wakiomba wakutane naye kuzungumzia hatima ya dhamana ya washtakiwa hao.
“Barua waliyoandika nimeiona Februari 11 na mimi nimepanga kukutana nao niwasikilize na tuelimishane pia, kwa sababu hii ni ofisi ya umma ambayo mtu yeyote yuko huru kufika.”
Kutokana na amri ya DPP kuzuia dhamana ya Sheikh Ponda, Waislamu walifanya kongamano Februari 3, mwaka huu maeneo ya Mwembe Yanga, Temeke, wakihamasishana kufanya maandamano makubwa kesho kuelekea kwa DPP endapo washitakiwa hao hawatadhaminiwa.
Katika kusisitiza maandamano hayo, Shura ya Maimam na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, walimwandikia barua Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, wakimtaarifu juu ya maandamano hayo.
“Tunakutaarifu kwamba Februari 15, mwaka 2013, kutakuwa na maandamano ya amani ya waumini wa Kiislamu baada ya swala ya Ijumaa kutoka misikiti mbalimbali kuelekea Ofisi ya DPP.
“Madhumuni ya maandamano hayo ni kutaka kujua sababu inayopelekea DPP kuzuia haki ya dhamana kwa viongozi wa dini ya Kiislamu, akiwemo Ponda, katika kesi ya kiwanja iliyopo mahakamani takribani miezi minne,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo kwa Kamanda Kova.
Sheikh Ponda na Salehe Mukadam wako rumande tangu kesi hiyo ilipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza, Oktoba mwaka jana, kwa kuwa DPP aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana zao.
Sheikh Ponda na wenzake 49, wanakabiliwa na mashitaka matano, yakiwamo ya kuingia isivyo halali katika uwanja wa Markaz Chang’ombe na kujimilikisha uwanja huo ambao ni mali ya Agritanza Limited. Pia, wanakabiliwa na mashitaka ya kuwachochea wananchi hadi wakakusanyika katika uwanja huo, kuvunja na kuiba vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani zaidi ya Sh milioni 59, mali ya Agritanza Limited.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa. Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania, Sheikh Said Mwaipopo, ametoa tamko kwa waumini wa Dini ya Kiislamu, akiwataka wasishiriki maandamano yaliyopangwa kufanyika kesho kupinga Sheikh Ponda kunyimwa dhamana. Sheikh Mwaipopo liyasema hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Sisi sote tunajua kuwa, maandamano ni haki ya kila mwananchi, lakini lazima yaratibiwe na yakubalike na kutolewa kibali na polisi. Katika hili, sisi tumeshawasiliana na Kamanda Kova na amekanusha hilo,” alisema Mwaipopo.
“Watakaoandamana wajue watazidi kumweka Ponda katika mazingira mabaya, kwani hatatolewa kwa dhamana kirahisi kama wanavyotaka na hawataitendea haki Serikali na Waislamu kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Peace Foundation, Sadiq Godi, alisema wananchi wanatakiwa kujua ni kwanini DDP amefunga dhamana ya Sheikh Ponda.
Katika hatua nyingine, Kaimu Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, aliiambia MTANZANIA kwa simu, kwamba Waislamu wanaotaka kuandamana wanaligawa taifa.
“Hawa Waislamu wasitake kuligawa taifa kwa udini, huku wakiweka kisingizio cha kudai haki zao. Tunawaomba waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari wasiwaunge mkono kwa kuandika habari zao, badala yake tuungane kupinga vitendo hivyo.
“Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani, tumejipanga kudhibiti hali hiyo, maana tumesikia kwamba baada ya kutoka misikitini siku ya Ijumaa, wataandamana kwenda kwa DPP, nawaambia wasijaribu,” alisema.
“Katika zuio hili kuna sababu tano zinazotufanya tusiruhusu maandamano hayo, ya kwanza ni hatuna polisi wa kutosha kulinda misikiti yote jijini Dar es Salaam na ya pili ni kwamba ofisi ya DPP iko katikati ya jiji.
“Sababu ya tatu ni kwamba suala wanalolalamikia liko mahakamani, nne ni kwamba wapo wanazuoni walioomba kukutana na DPP na wamekubaliwa na sababu ya tano kuna taarifa za uvunjifu wa amani wakati wa maandamano hayo.
“Kutokana na sababu hizi, hatuko tayari kuruhusu maandamano yafanyike na nazidi kuwaambia wasithubutu kuandamana,” alisema Msangi.