BUNGE linatarajia kufuta utaratibu wa kurusha matangazo ya moja
kwamoja kupitia televisheni kwa madai ya kukomesha vitendo vya baadhi
ya wabunge kukiuka kanuniza bunge na kuleta vurugu kwa kutafuta
umaarufu bila kujua kwamba tabia hiyo inaleta picha mbaya katika
jamii.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Bunge Dk.Thomas Kashilila jijini Dar es
salaam wakati akitoa taarifa ya mapendekezo yakuanzisha kamati ya
bajeti na kuvunjwa kwa baadhi ya kamati za bunge.
Amesema kuwa ili kuleta maadili kwa baadhi ya wabunge ambao wamekuwa
wanashindwa kufuata kanuni za bunge na kutumia nafasi hiyo kwa
kutafuta umaarufu kwa sasa wameomba kufutwa utaratibu wa kurusha
matangazo ya bunge ya moja kwa moja badala yake watarekodi ili kuondoa
hoja zisizokuwa za msingi.
Ameongeza kuwa kuna idadi kubwa ya wabunge wamekuwa wakikiuka kanuni
za bunge makusudi na kusababisha kuleta vurugu bungeni wakati jamii
ikiendelea kutazama mabishano yasiyokuwa na hoja za msingi.
Dk Kashilila amesema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya kamatiza bunge
ambazo zimevunjwa kutokana na baadhi ya kamati hizo kuingilia katika
utendaji jambo ambalo limekuwa likipoteza maana ya kamati hizo.
Hivi karibuni baadhi ya kamati ikiwemo ile ya Mashirika ya umma POAC
zimefutwa na kuacha maswali mengi kwa baadhi ya wananchi juu ya hatua
hiyo.