NALIFUMBUA JICHO LANGU KUANGALIA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

UCHUMI
Kufumbua macho inawezekana ikawa kazi ngumu sana kwa Binadamu aliefumba macho. Binafsi sio mwanauchumi maana sina sifa hata moja ya kuingia kwenye Bodi ya wana uchumi Ila nataka nifumbue macho kidogo ingawa ntaumia sana Kufumbua macho yangu tena kwa wakati huu ambao wengi tumeamua kufumba macho huku tukifikiria Jamii nzuri ya kufikirika iliyowahi kupita ambayo pia tulikua tunaiota.

Wakati wa Ari Mpya Nguvu mpya kasi mpya chini ya Jakaya mrisho kikwete ndio wakati kwa sasa unaozungumzwa kama wakati bora ambao kila Mtanzania aliefumba macho huku akiukumbuka huo wakati mzuri ambao binafsi baada ya kutumia nguvu Kufumbua macho yangu tena kwa kutumia wembe wenye makali niliona wakati tunaoukumbuka ulikua wakati wa mambo kama mawili au matatu ambayo yalitufanya tena tukumbuke wakati wa uwazi na uwajibikaji chini ya Benjamin mkapa.

Kuna mambo machache ambayo sitaki kuyazungumza juu ya wakati wa Mkapa ila acha nianze na haya mambo ya wakati ambao tunasema tunaukumbuka ule wakati ulikua na EPA, RICHMOND na TEGETA Escrow iliyosababisha Bodi ya maendeleo ya milenia (MCC) kusitisha msaada kiasi cha shilingi 992.8 bilioni.

Hebu tujikumbushe kidogo wakati Benjamin Mkapa anatoka madarakani aliacha deni la taifa kiasi cha shilingi 9.3 trilioni ila ilimchukua miaka kumi Jakaya mrisho kikwete mpaka anatoka madarakani aliacha deni la shilingi 30.6 trilioni.

Kiuchumi serikali ya awamu ya nne ilijiendesha kwa kuziba mashimo ya matatizo kwenye kila wizara zake ila mtaani pesa ilikua ya kutosha kiasi kwamba kile kiasi kilichokua kinapita bila utaratibu kilikua kinatufikia mpaka walalahoi wa chini kabisa na huu ndio wakati ambao sote tunaukumbuka maana tumefumba macho na kwetu ni ngumu kuyafumbua macho yetu.

Nyerere alitengeneza uchumi vizuri kabla ya vita ya Uganda ila baada ya vita nchi ilikua hoi nakumbuka alianzisha kauli ya tufunge mikanda kwa miezi kumi na nane (18) hali ilizidi kua mbaya kiasi kwamba akaongeza miaka mitatu zaidi mbele ila bado haikutosha.

Mwinyi deni lilimshinda ila Mkapa akajitahidi kulipa jambo ambalo alishindana sana na Nyerere kwa wakati ule ila bado mkapa akatoka na deni.

Macho yetu tumeyafumba kwakua tunataka tuwe na Pesa nyingi mfukoni ambazo zitakuja kwa njia zisizo halali,  rushwa, ufisadi na njia zote zisizojenga uchumi wa muda mrefu zaidi kumaliza matatizo kwa muda mchache.

Sina shaka na jinsi tunavyopenda raha ila kama roho ya kichina ingeingia moyoni mwetu uchumi wetu ukajengwa na sisi wenyewe kwa kufanya kazi kwa bidii ingesaidia sana kulikomboa hili taifa kiuchumi.

Matatizo ya Muda mrefu kwenye uchumi wa Tanzania yanaweza yakawa kwenye makundi mbalimbali ila kwa kipindi kirefu yamesababishwa na sisi wenyewe yaani mimi na wewe.

RUSHWA
Rushwa miongoni mwetu imekua kwa kiwango kikubwa leo hata huduma ambayo ni haki yako unatoa pesa kuipata. Kupitia rushwa na namna Nchi inavyokwenda sasa uhalisi ni kwamba mtoaji rushwa bado anatamani kutoa rushwa na mpokeaji anaogopa kupokea rushwa.

UFISADI
Macho bado yamefumba ndio maana bado tunaikumbuka awamu ya nne ya vijisenti na pesa ya mboga. Hivi pesa zote za ufisadi kama zingeingizwa kwenye miradi ya Maendeleo au zingejenga madawati leo nani angekaa chini. Kuna muda ule wakati wa CHADEMA wa kupinga ufisadi ulikua moja ya wakati wangu bora sana ila leo zile harakati zote za kupinga ufisadi zimegeuka na kua harakati za kukumbuka ufisadi kuna shida naipata hapa naipata kwenye kufikiri kwangu kama kweli kukomboa uchumi ni kukumbuka tawala zilizopita au kujenga uchumi na kutoa ushauri mzuri kwa utawala uliopo au tunasubiri na huu ukitoka tuseme bora utawala wa Magufuli.
Ufisadi umeliathiri taifa hili kwa kiwango kikubwa na umepelekea hata mawazo yetu yamejaa ufisadi badala ya uzalendo.

SERIKALI ILIVYOKUA INAJIENDESHA
Kwa kipindi kirefu watumishi wa uma walikua wanaendesha serikali kwa mazoea ilikua kwenye Halmashauri zetu ndio sehemu ya kukutana na kupiga soga. Halmashauri zetu zilikua zinaizinisha matumizi ya pesa yasiyo kua na uhalisia huku watumishi wa serikali wakijinufaisha, Hii inanifanya nikumbuke ile kauli ya Shamba la bibi, ni kweli tulikua Shamba la bibi na naona kwasababu tumefumba macho tunachokumbuka ni jinsi tulivyokua tunafaidika na Shamba la bibi.

WAFANYABIASHARA KUKWEPA KODI
Watanzania wengi hasa wafanyabiashara waliingia kwenye siasa ili iwasaidie wao urahisi wa kukwepa kodi. Sote inabidi tutambue hakuna mfanyabiashara anaependa hasara hata siku moja ili uhalisia wafanyabiashara wametukwamisha kwenye kodi kuliko kawaida kodi ambazo zingeenda kwenye maendeleo ya jamii. Ili Nchi ijiendeshe ni kosa wafanyabiashara wakatawala siasa na uchumi matokeo ya hili ni wao kukwepa kodi.
Leo tutaongea maneno yote ila uhalisia kuna muda tumefumba macho na hatutaki kujiuliza kwanini wafanyabiashara wanalalamika au tumesahau uozo wote uliokuwepo kati ya wafanyabiashara na wanasiasa kutuhujumu leo ni kampuni ngapi zilitangaza kufilisika au haya yote hatukuyaona.

Binafsi napingana na kauli za kivivu za kukumbuka utawala wa awamu ya nne Kwamba ulikua una nafuu ila kama njia tunazozichukua kwa sasa kuboresha uchumi ni nzuri basi tukazie hapo hapo na sio tuongee kwa sababu tumeamua kufumba macho hivi deni la Taifa aliloacha Jakaya kikwete hatukuliona au tumesahau kutoka 9.3 trilioni mpaka 30.6 trilioni.

Mawazo yakukumbuka utawala wa awamu ya nne binafsi nayaita mawazo ya kifisadi maana ndio wakati uliokua na ufisadi wa kutosha kwa kila kada za serikali, Halmashauri nyingi zilifuja pesa wanasiasa walipiga dili za kutosha binafsi nimeshindwa kufungamana na safari ya awamu ya nne kama ya kuikumbuka ila nataka nifumbue macho kwa hii safari ya tano.
Ila nataka Rais Magufuli afanye haya mambo kadhaa.

KUPAMBANA NA UFISADI
Magufuli endelea kupambana na mafisadi maana imani yangu inaniambia kama utaendelea kupambana na mafisadi utasaidia kutuondolea wafanyabiashara wanasiasa ambao wanaingia kwenye siasa ili wakwepe kodi, lakini pia utakua umetusaidia vijana kwa wakati ujao zile mbinu za kutoa rushwa kwa wanasiasa ili kupata uongozi zitakua zimepungua na nafasi za kisiasa zitapata watu makini ambao katika kila kura za maoni za vyama vyetu hua wanakosa nafasi kwa kushindwa kushindana na wanasiasa wafanyabiashara ambao wanaenda kufanya biashara bungeni kuliko kutakua shida za wananchi.

KUENDELEA KUKUSANYA KODI
Nataka serikali iendelee kukusanya kodi kwa kasi zaidi lakini pia serikali iangalie ni kodi zipi ambazo zinapotea au kuna biashara zipi ambazo hazijarasimishwa ili nazo zirasimishwe ili serikali isipoteze tena kodi. Lakini pia serikali iangalie ule mchezo wa kampuni za uwekezaji ambazo hua zinabadili majina kila inapofikia hatua ya wao kuanza kulipa kodi.

SERIKALI KUWA NA VIPAUMBELE
Tumeshuhudia serikali kwa kipindi kirefu imekua ikijiendesha kwa kuziba mashimo na kukosa vipaumbele vya kitaifa ni muda sasa serikali iwe na vipaumbele ili kusaidia kupunguza ya malalamiko ya kila mwaka ya watanzania. Mfano serikali iweke mkazo kwa sekta zinazosaidia kwenye bajeti zetu ili Nchi iweze kujiendesha kwa kuangalia njia za kurekebisha sekta hiyo ili izidi kuzalisha zaidi na kusaidia uchumi wetu mfano serikali kwa sasa inabidi kuangalia kama mizigo imepungua bandarini ni kipi inapaswa kufanya lakini pia kuna sekta kama kilimo kwa kiwango kikubwa kama Nchi itaenda kuchagua zao la kitaifa basi ni rahisi sana zao likasaidia kwenye uchumi wetu ili uzidi kukua zaidi kufikia uchumi wa kati.

NCHI KUCHAGUA WAWEKEZAJI
Huu ni Muda pia wa taifa kuchagua wawekezaji wenye tija kwa kuangalia wawekezaji wanaotoka kwenye Nchi ambazo zinaendana na aina ya utawala wewe unaoutaka au wawekezaji watakaoendana na mipango au mikakati tuliyojiwekea kuelekea Tanzania ya viwanda.

Macho yangu yamefunguka ila nimetumia wembe mkali kuyafumbua ila damu nyingi ilinitoka nilipofumbua macho yangu na Damu yangu iliyomwagika itapinga milele ufisadi, ukwepaji kodi na rushwa kubwa iliyokua imekithiri machoni mwetu.

ZIMEBAKI WIKI TATU MBOWE ATIMULIWE BILICANAS

ZIMEBAKI wiki tatu kabla Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuchukua jengo la Bilicanas lililokodiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuendesha biashara ya ukumbi wa starehe, ilielezwa jijini jana.

Jengo hilo lipo eneo la Posta jijini Dar es Salaam.

Awali, NHC ilikuwa imetoa notisi ya siku 60 kwa wadaiwa sugu ambao wamepanga katika majengo yake akiwamo Mbowe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai taasisi za umma, binafsi nawatu binafsi jumla ya Sh. bilioni 15.

Notisi ya siku 60 ya kuondoka Bilicanas pamoja na majengo ya wadaiwa wengine ilishatolewa, Mchechu alisema na kwamba sasa zimesalia wiki tatu.

Alisema baada ya muda huo kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo hayo utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za kisheria.

Mchechu alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa (Sh. milioni 631).

Wadaiwa wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sh. bilionimbili), Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.

Mchechu alisema ukusanyaji wa madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo kukusanya fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia Dodoma.

Alipoulizwa iwapo mkakati huo una uhusiano wowote na masuala ya kisiasa kutokana na kumtaja Mbowe kuwa ni kati ya wadaiwa sugu, Mchechu alisisitiza hakuna uhusiano wa siasa na zoezi hilo kwani wateja wote wanachukuliwa sawa."Mwaka huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema Mchechu, hivyo fedha tunazodai zitatusaidia kukamilisha uwekezaji mjini humo."

"Ndiyo maana tumetoa kwa tunaowadai notisi ya miezi miwili, vinginevyo wataondolewa katika majengo ya shirika kama kanuni zinavyotaka.

"Hakuna uhusiano wowote kati ya shirika kukusanya fedha linazodai na watu binafsi akiwamo Mbowe, taasisi za umma na binafsi.

"Lengo ni kukusanya madeni ambayo baadhi yake yalisimama kutokana na mengine kuwa na kesi mahakamani."

Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.

Alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja na utachukua miezi 12.Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.

Alisema shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi na Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia Dodoma.

Alisema fedha nyingine zitapatikana baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.

Aidha, Mchechu alisema kitendo cha Serikali kuhamia Dodoma kitatoa fursa kwa Jiji la Dar es Salaam kujiimarisha kibiashara tofauti na ilivyo sasa ambapo linakwamishwa na foleni kubwa za magari kutokana na shughuli nyingi za serikali kufanyika.

"Dar es Salaam kuna bandari, uwanja wa ndege," alisema na kuongeza: "Hivyo suala la kiuchumi litaimarika zaidi kutokana na shughuli nyingi za Serikali kuhamia Dodoma. Hii itasaidia uchumi wa nchi kusambaa katika maeneo tofauti nchini."

Uwekezaji wa NHC jijini Dar es Salaam upo kwa asilimia 70, alisema na kwamba ufanisi wa Jiji utaongezeka hususani katika usafiri na sekta nyingine kiuchumi.

Chanzo: Nipashe

KITWANGA APONDA NDEGE ZA ATCL

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, jana aliponda aina ya ndege mpya zilizonunuliwa na serikali kutoka Canada kwa ajili ya kufufua Shirikala Ndege Tanzania (ATCL).

Kitwanga alisema ndege hizo si tu hazina mwendo, lakini pia ilikuwa niajabu kununuliwa kwa fedha taslim wakati duniani kote ndege hununuliwa kwa kulipa kidogo kidogo wakati mteja akiendelea kuzitumia.

Serikali imelipa kwa Bombardier Aerospace fedha za ndege mbili za Q400 zinazotumia injini za pangaboi; zenye uwezo wa kubeba abiria 70.

Kitwanga ambaye ni Mbunge wa Misungwi (CCM), alieleza kushangazwa na kitendo cha Serikali kununua ndege hizo ambazo amesema zinatoka kwenye kampuni ndogo ya mtu binafsi, na kuhoji ubora wake.

BWANA HARUSI AFARIKI KWA KUUMWA NA SIAFU

WAKAZI  wa Kijiji  cha  Nditu,  Kata  ya Suma, Wilaya ya Rungwe  mkoani Mbeya, wamegoma  kuzika mwili wa marehemu Shabani  Yusufu (27),  baada kushambuliwa na kundi la siafu nyumbani kwake  na kusababisha apoteze uhai.

Yusufu, amefariki dunia ikiwa ni siku moja tu baada ya kufunga ndoa na kuzua gumzo kubwa kijijini hapo.

Alikutwa na mauti hayo akiwa amejipumzisha ndani usiku wa kuamkia jana, jambo ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

Akisimulia mkasa huo, baba mzazi wa marehemu, Ebron Mwaipaja, alisema mwanawe  alitoka kufunga ndoa  juzi na alikutwa na mauti hayo akiwa amejipumzisha chini ya mti nyumbani kwake, ambako ghafla alivamiwa na siafu.

Alisema kulikuwa na maneno ya hapa na pale wakati wa maandalizi ya harusi hiyo kutoka kwa baadhi ya watu, ambayo yamesababisha tukio hilo kuhusishwa na imani za kishirikina.

Baba huyo alisema baada ya tukio hilo, wananchi na uongozi wa Serikali ya kijiji walifika eneo hilo, huku wakimtaja mmoja wa wanakijiji kuwa ndiye “aliyetuma” siafu hao.

“Wananchi waligoma kuandaa taratibu za mazishi wakishinikiza aletwe mganga wa jadi apige ramli ili kumbaini mtu anayeendesha matukio ya ushirikina yanayoendelea kijijini hapa,” alisema.

Alisema baada ya wananchi kugoma kuzika, Serikali ya kijiji nayo iligoma kutoa kibali, ikisema siku zote Serikali haiamini uchawi, jambo ambalo lilisababisha wananchi waliokujwa na silaha za jadi, kufanya maandamano na kufunga barabara.

Baada ya hali ya usalama kuzidi kuwa mbaya, polisi walifika eneo la tukio na kutuliza ghasia, huku familia ikifanya maandlizi ya maziko bila wanakijiji kuhusika.

“Kijana wangu ndiyo kwanza alitoka kufunga ndoa akifurahia maisha ya kuwa na mke, amekutwa na umauti tena kwa kuvamiwa na siafu wakati kijiji hiki hakijawahi kuwa na wadudu hawa, yote namwachia Mungu,” alisema Mwaipaja.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Joseph Kajura, alisema wanafahamu fika tukio hilo ni la kishirikina na ndiyo maana walimtafuta mganga wa kienyeji ili apige ramli kwa ajili ya kubaini mhusika.

Source: MTANZANIA

MWALIMU KORTINI KWA KUMLAWITI MWANAFUNZI

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Usevya wilayani ya Mlele, Makonda Ng-onga amefikishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kujibu tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake anayesoma kidato cha tano.

Mtuhumiwa  alifikishwa kizimbani hapo juzi na kusomewa mashtaka hayo na mwanasheria wa Serikali, Gregory Mhangwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga  Ntengwa.

Mhangwa alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti katika kipindi cha Novemba  mwaka jana hadi Aprili mwaka huu katika maeneo ya shule hiyo.

Alidai mtuhumiwa alitenda kosa  hilo kwa kutumia nafasi yake ya mkuu wa shule msaidizi, jambo ambalo ni kosa kinyume na kifungu  cha  sheria Na. 154 kifungu kidogo sura ya 16 ya sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mwalimu huyo anadaiwa kutenda  kosa hilo baada ya kuwa mwanafunzi anapokuwa  amefanya kosa shuleni hapo, humlazimisha kumwingilia kinyume cha maumbile kama adhabu, na endapo  mwanafunzi   atakataa amekuwa akimtishia kumfukuza shule .
Mwalimu huyo ambaye alikana mashtaka hayo, yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyomtaka kulipa Sh 3milioni mahakamani.

Hakimu  Chiganga aliharisha  kesi  hiyo  hadi Juni 27, mwaka huu itakapotajwa tena.

WATUPWA JELA KWA WIZI WA MAFUTA YA TAA

Mahakama ya Wilaya ya Ilala leo imewahukumu watu watatu kwenda jela miaka mitatu baada ya kuwakuta na hatia ya wizi wa mafuta ya kupikia ndoo 900 yenye thamani ya Sh80m, mali ya mfanyabiashara Benard Kimoso.

Waliohukumiwa ni Habibu Aboubakar (46), Yahaya Salum(29) na James Limelia (30) ambao wanadaiwa kuiba ndoo ndogo 150 na ndoo kubwa 750 za mafuta ya kupikia aina ya Safi ambayo walikuwa wanayasafirisha kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha.

Pia mahakama hiyo imemwachia huru Makame Chande (54) baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Hassan amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi watatu waliotoa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa hao.

“Nimeridhika na upande wa mashitaka pasi na kuacha shaka yoyote na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hivyo nawatia hatiani kwa makosa yote mawili likiwemo la kula njama na kuiba,’’ amesema.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, wakili wa Serikali, Florida Wenceslaus aliomba mahakama itoe adhabu stahiki dhidi yao ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Hata hivyo, mshitakiwa wa kwanza Aboubakar aliomba mahakama impunguzie adhabu kwamba ana wadogo zake 27 wanamtegemea, wajane wanne, wake wawili, watoto pia alivunjika mkono na anasumbuliwa na presha.

Mshitakiwa wa pili aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ni mgonjwa huku mshtakiwa wa tatu akiomba apunguziwe adhabu kwa sababu amefiwa na mtoto wake, mke wake ni mgonjwa na yeye anasumbuliwa na presha.

Hakimu Hassan alisema katika kosa la kula njama anawahukumu miaka miwili na wizi wa mafuta ya kupikia  miaka mitatu ambapo adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili Wenceslaus alidai washitakiwa walitenda kosa hilo Juni 21, mwaka 2014 eneo la Tabata, wilayani Ilala.

Ilidaiwa washitakiwa kwa pamoja waliiba mafuta ya kupikia ambayo yalikuwa yanasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha.


Chanzo: Mwananchi

WATU WATATU WAKAMATWA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU

Watanzania watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Tanga wakituhumiwa kuendesha biashara ya kuwasafirisha kwa kutumia gari aina ya hiace wahamiaji haramu 10 kutoka nchini Ethiopia.

Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ,Leonard Paulo amesema leo kuwa watanzania hao pamoja nawahabeshi wamekamatwa jana saa 2.30 usiku katika eneo la Misajini barabara kuu ya Hedaru- Mombo.

Amesema kuwa wahamiaji hao walimatwa wakati askari wakiwa doria waliokuwa wakisafirishwa kwenye gari aina Toyota Hiace iliyokuwa ikiendeshwa na Ally Juma (24) mkazi wa Dar es Salaam wakiingia mkoani hapa.

Amewataja watanzania wengine wawili ambao wamekamatwa wakituhumiwa kuwakisafirisha wahamiaji haramu hao kuwa ni Joseph John (42) mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Iddi Juma(38) mkazi wa mkoani Iringa.

Ametaja majina ya Wahabeshi waliokuwa wakisafirishwa kuwa ni
Tarfa Wolder (21),Aramei Yonas (21),Gazae Edson(20),Yohanes Abakar (27),Anemo Tamire (16),Indira Yaiso(18),Wasifimu Paresa (15),Dedacho Gadam (20),Tamelata Abala (17) na Mlatu Shugute (32).

RAIS NKURUNZINZA AMTUMIA RAIS DK. MAGUFULI UJUMBE

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amemuomba Rais John Magufuli kuwasihi wananchi wake waliokimbia nchini humo, kurejea akimhakikishia kuwa hali ni shwari.

Baadhi ya Warundi waliikimbia nchi hiyo wakihofia maisha yao kutokana na vurugu za kisiasa zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu baada ya kupinga kiongozi huyo kugombea tena.

Katika ujumbe uliowasilishwa Ikulu, jana na Mnadhimu wa Jeshi la Burundi, Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye ambaye ni mjumbe maalumu wa Rais Nkurunziza, kiongozi huyo alimuomba Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuwasihi wananchi wa Burundi waliokimbia nchi yao warejee nyumbani.

Meja Jenerali Ndayishimiye alimueleza Rais Magufuli kwamba ametumwa kuleta barua hiyo pamoja na shukrani za dhati kwa Tanzania ambayo ni rafiki, jirani na ndugu wa kweli wa Burundi kwa ushirikiano mzuri inaoupata.

Dk Magufuli alimshukuru Rais Nkurunziza kwa ujumbe huo na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki na ndugu wa dhati wa Burundi.

Kuhusu hali ya Burundi, Rais Magufuli alisema anaamini kuwa wasuluhishi mgogoro wa nchi hiyo; Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa watafanikiwa kuusuluhisha.


Chanzo:Mwananchi

RAIS MAGUFULI AWATUNIKU KAMISHENI MAAFISA 205

RAIS, Dk .John Magufuli leo amewatunuku Kamisheni kwa Cheo cha Luteni Usu, Maafisa Wanafunzi Wapya 205 pamoja na kutoa Nishanikwa Maafisa watano waliofanya vizuri kwenye masomo yao.

Rais alitoa Kamisheni hiyo kwa Cheocha Luteni Usu leo, katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu akiwa Rais.

Miongoni mwa Maafisa hao wapya watano waliotunukiwa nishani zao niwanawake wawili ambao ni Efrasia Bundala kutoka Tanzania na Winnie Indumuli kutoka nchini (Kenya) huku wanaume wakiwa watatu ambao ni Phinias Kiganga aliyefanya vyema darasani.

Wengine ni Frank Kitalekwa aliyefanya vyema upande wa medani na Ahmed Mmang'anda aliyefanya vyema darasani.

Baada ya kuwavisha nishani askari hao watano ambao ni miongoni mwa maafisa wapya 205, Rais Magufuli aliwatunuku Kamisheni kwa cheo cha Luteni Usu maafisa hao wapya ambao miongoni mwao wanawake ni 16 na wanaume wakiwa 189.

Aidha miongoni mwa wahitimu hao wawili wanatoka nchini Burundi, 4 nchini Kenya na 4 wanatoka nchini Uganda ambao ni nchi marafiki.

Mara baada ya kutoa kamisheni kwa maafisa hao, Rais Magufuli alipata burudani kutoka kwa Kikundi cha Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Oljoro ambao walipokuwa wakiimba walimpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi na kumuomba kusafisha wabadhirifu wote wakwepa kodi pia asafishe taasisi mbalimbali ili Tanzania iwe safi.

Nayo bendi ya Jeshi la Watanzania(JWTZ) iitwayo Chacharika Bendi ilikonga nyoyo za wananchi waliofurika kushuhudia ndugu zao waliotunukiwa Kamishenizao huku wakimpongeza kwa utoaji wa elimu bure.

Pia alipiga picha na maafisa hao wapya, viongozi mbalimbali.

Awali akiingia uwanjani kwa ajili ya ukaguzi wa gwaride Rais Magufuli alishangiliwa na wananchi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo lakini pia viongozi wa serikali pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria katika sherehe hiyo.