Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Usevya wilayani ya Mlele, Makonda Ng-onga amefikishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kujibu tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake anayesoma kidato cha tano.
Mtuhumiwa alifikishwa kizimbani hapo juzi na kusomewa mashtaka hayo na mwanasheria wa Serikali, Gregory Mhangwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga Ntengwa.
Mhangwa alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti katika kipindi cha Novemba mwaka jana hadi Aprili mwaka huu katika maeneo ya shule hiyo.
Alidai mtuhumiwa alitenda kosa hilo kwa kutumia nafasi yake ya mkuu wa shule msaidizi, jambo ambalo ni kosa kinyume na kifungu cha sheria Na. 154 kifungu kidogo sura ya 16 ya sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mwalimu huyo anadaiwa kutenda kosa hilo baada ya kuwa mwanafunzi anapokuwa amefanya kosa shuleni hapo, humlazimisha kumwingilia kinyume cha maumbile kama adhabu, na endapo mwanafunzi atakataa amekuwa akimtishia kumfukuza shule .
Mwalimu huyo ambaye alikana mashtaka hayo, yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyomtaka kulipa Sh 3milioni mahakamani.
Hakimu Chiganga aliharisha kesi hiyo hadi Juni 27, mwaka huu itakapotajwa tena.