WATUPWA JELA KWA WIZI WA MAFUTA YA TAA

Mahakama ya Wilaya ya Ilala leo imewahukumu watu watatu kwenda jela miaka mitatu baada ya kuwakuta na hatia ya wizi wa mafuta ya kupikia ndoo 900 yenye thamani ya Sh80m, mali ya mfanyabiashara Benard Kimoso.

Waliohukumiwa ni Habibu Aboubakar (46), Yahaya Salum(29) na James Limelia (30) ambao wanadaiwa kuiba ndoo ndogo 150 na ndoo kubwa 750 za mafuta ya kupikia aina ya Safi ambayo walikuwa wanayasafirisha kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha.

Pia mahakama hiyo imemwachia huru Makame Chande (54) baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Juma Hassan amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi watatu waliotoa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa hao.

“Nimeridhika na upande wa mashitaka pasi na kuacha shaka yoyote na ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hivyo nawatia hatiani kwa makosa yote mawili likiwemo la kula njama na kuiba,’’ amesema.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, wakili wa Serikali, Florida Wenceslaus aliomba mahakama itoe adhabu stahiki dhidi yao ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Hata hivyo, mshitakiwa wa kwanza Aboubakar aliomba mahakama impunguzie adhabu kwamba ana wadogo zake 27 wanamtegemea, wajane wanne, wake wawili, watoto pia alivunjika mkono na anasumbuliwa na presha.

Mshitakiwa wa pili aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ni mgonjwa huku mshtakiwa wa tatu akiomba apunguziwe adhabu kwa sababu amefiwa na mtoto wake, mke wake ni mgonjwa na yeye anasumbuliwa na presha.

Hakimu Hassan alisema katika kosa la kula njama anawahukumu miaka miwili na wizi wa mafuta ya kupikia  miaka mitatu ambapo adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Akisoma hati ya mashtaka, wakili Wenceslaus alidai washitakiwa walitenda kosa hilo Juni 21, mwaka 2014 eneo la Tabata, wilayani Ilala.

Ilidaiwa washitakiwa kwa pamoja waliiba mafuta ya kupikia ambayo yalikuwa yanasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha.


Chanzo: Mwananchi