RAIS NKURUNZINZA AMTUMIA RAIS DK. MAGUFULI UJUMBE

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amemuomba Rais John Magufuli kuwasihi wananchi wake waliokimbia nchini humo, kurejea akimhakikishia kuwa hali ni shwari.

Baadhi ya Warundi waliikimbia nchi hiyo wakihofia maisha yao kutokana na vurugu za kisiasa zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu baada ya kupinga kiongozi huyo kugombea tena.

Katika ujumbe uliowasilishwa Ikulu, jana na Mnadhimu wa Jeshi la Burundi, Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye ambaye ni mjumbe maalumu wa Rais Nkurunziza, kiongozi huyo alimuomba Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kuwasihi wananchi wa Burundi waliokimbia nchi yao warejee nyumbani.

Meja Jenerali Ndayishimiye alimueleza Rais Magufuli kwamba ametumwa kuleta barua hiyo pamoja na shukrani za dhati kwa Tanzania ambayo ni rafiki, jirani na ndugu wa kweli wa Burundi kwa ushirikiano mzuri inaoupata.

Dk Magufuli alimshukuru Rais Nkurunziza kwa ujumbe huo na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki na ndugu wa dhati wa Burundi.

Kuhusu hali ya Burundi, Rais Magufuli alisema anaamini kuwa wasuluhishi mgogoro wa nchi hiyo; Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa watafanikiwa kuusuluhisha.


Chanzo:Mwananchi