Kifo Cha Mwandishi wa Habari

Vurugu kubwa zilizuka jana katika eneo la Nyororo wilayani Mufindi
kati ya polisi na wafuasi wa Chadema, baada ya askari hao
kusambaratisha mkutano wa chama hicho nakusababisha kifo cha mwandishi
wa habari na watu kadhaa kujeruhiwa.
Mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi
anadaiwa kuuawa kwa bomu lililorushwa na polisi katika vurugu hizo.
Awali, inadaiwa kuwa mwandishi huyo alishambuliwa kwa marungu na
Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kabla ya bomu hilo
kumjeruhi vibaya tumboni na kusababisha kifo chake.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio, alisema wakati mwandishi huyo
akishambuliwa na polisi, mmoja wa askari wa jeshi hilo aliwazuia
wenzake kuendelea kumpiga akiwaeleza kuwa anamfahamu kuwa ni mwandishi
wa habari, huku akimkumbatia.
Shuhuda huyo alidai kwamba jitihada za askari huyo hazikusaidia, kwani
baada ya kutupwa kwa bomu hilo lililosababisha utumbo wa mwandishi
huyo kutoka nje, polisi huyo naye alijeruhiwa mguu.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alikana polisi
kumuua mwandishi huyo akidai kwamba kilichosababish a kifo chake
nikitu kilichorushwa na wananchi ambapo alisema polisi inakichunguza.
Vurugu hizo ziliibuka baada ya polisi kufika Nyororo na kuwataka
viongozi wa Chadema pamoja na wafuasi wao kutawanyika kwa kuwa
walikuwa hawaruhusiwi kufanya mkusanyiko wowote kutokana na amri
iliyotolewa na jeshi hilo awali.
Polisi mkoani Iringa jana asubuhi walilipiga marufuku kufanyika kwa
maandamano na mikutano yote ya halaiki ya kisiasa mpaka hapo Sensa ya
Watu na Makazi itakapokamilika baada ya kuongezwa wiki zaidi.
Hata hivyo, pamoja na amri hiyo Chadema kilifanya mkutano wilayani
Mufindi kitendo ambacho polisi walisema ni kinyume cha sheria.

Source: Star Tv