BODI YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU YAONGEZA MUDA WA MAOMBI HADI JULY 31

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza muda wa waombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 kuwasilisha maombi yao hadi mwishoni mwa mwezi huu (31 Julai, 2015).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumatano, Julai 15, 2015) na Mkurugenzi Mtendaji wa (HESLB) Bw. George Nyatega, hatua hiyo imechukuliwa ilikuwapa fursa wombaji ambao hawajakamilisha kufanya hivyo.

"Hatua hii imechukuliwa ili kuwapa fursa wale ambao kwa sababu mbalimbali hawakuweza kufanya maombi ya mikopo katika muda uliopangwa," amesema Bw. Nyatega katika taarifa yake iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari.

Itakumbukwa kuwa awali Bodi ilianza kupokea maombi kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) tarehe 4 Mei, 2015 na mwisho wa kuwasilisha maombi ulipangwa kuwa tarehe 30 Juni, 2015.

Kupitia taarifa yake, HESLB imewataka waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ambao hawajakamilisha maombi yao kukamilisha na kuwasilisha maombi yao ya mikopo ndani ya muda ulioongezwa na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda mwingine wa nyongeza baada ya tarehe 31 Julai, 2015.

HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu.