NALIFUMBUA JICHO LANGU KUANGALIA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

UCHUMI
Kufumbua macho inawezekana ikawa kazi ngumu sana kwa Binadamu aliefumba macho. Binafsi sio mwanauchumi maana sina sifa hata moja ya kuingia kwenye Bodi ya wana uchumi Ila nataka nifumbue macho kidogo ingawa ntaumia sana Kufumbua macho yangu tena kwa wakati huu ambao wengi tumeamua kufumba macho huku tukifikiria Jamii nzuri ya kufikirika iliyowahi kupita ambayo pia tulikua tunaiota.

Wakati wa Ari Mpya Nguvu mpya kasi mpya chini ya Jakaya mrisho kikwete ndio wakati kwa sasa unaozungumzwa kama wakati bora ambao kila Mtanzania aliefumba macho huku akiukumbuka huo wakati mzuri ambao binafsi baada ya kutumia nguvu Kufumbua macho yangu tena kwa kutumia wembe wenye makali niliona wakati tunaoukumbuka ulikua wakati wa mambo kama mawili au matatu ambayo yalitufanya tena tukumbuke wakati wa uwazi na uwajibikaji chini ya Benjamin mkapa.

Kuna mambo machache ambayo sitaki kuyazungumza juu ya wakati wa Mkapa ila acha nianze na haya mambo ya wakati ambao tunasema tunaukumbuka ule wakati ulikua na EPA, RICHMOND na TEGETA Escrow iliyosababisha Bodi ya maendeleo ya milenia (MCC) kusitisha msaada kiasi cha shilingi 992.8 bilioni.

Hebu tujikumbushe kidogo wakati Benjamin Mkapa anatoka madarakani aliacha deni la taifa kiasi cha shilingi 9.3 trilioni ila ilimchukua miaka kumi Jakaya mrisho kikwete mpaka anatoka madarakani aliacha deni la shilingi 30.6 trilioni.

Kiuchumi serikali ya awamu ya nne ilijiendesha kwa kuziba mashimo ya matatizo kwenye kila wizara zake ila mtaani pesa ilikua ya kutosha kiasi kwamba kile kiasi kilichokua kinapita bila utaratibu kilikua kinatufikia mpaka walalahoi wa chini kabisa na huu ndio wakati ambao sote tunaukumbuka maana tumefumba macho na kwetu ni ngumu kuyafumbua macho yetu.

Nyerere alitengeneza uchumi vizuri kabla ya vita ya Uganda ila baada ya vita nchi ilikua hoi nakumbuka alianzisha kauli ya tufunge mikanda kwa miezi kumi na nane (18) hali ilizidi kua mbaya kiasi kwamba akaongeza miaka mitatu zaidi mbele ila bado haikutosha.

Mwinyi deni lilimshinda ila Mkapa akajitahidi kulipa jambo ambalo alishindana sana na Nyerere kwa wakati ule ila bado mkapa akatoka na deni.

Macho yetu tumeyafumba kwakua tunataka tuwe na Pesa nyingi mfukoni ambazo zitakuja kwa njia zisizo halali,  rushwa, ufisadi na njia zote zisizojenga uchumi wa muda mrefu zaidi kumaliza matatizo kwa muda mchache.

Sina shaka na jinsi tunavyopenda raha ila kama roho ya kichina ingeingia moyoni mwetu uchumi wetu ukajengwa na sisi wenyewe kwa kufanya kazi kwa bidii ingesaidia sana kulikomboa hili taifa kiuchumi.

Matatizo ya Muda mrefu kwenye uchumi wa Tanzania yanaweza yakawa kwenye makundi mbalimbali ila kwa kipindi kirefu yamesababishwa na sisi wenyewe yaani mimi na wewe.

RUSHWA
Rushwa miongoni mwetu imekua kwa kiwango kikubwa leo hata huduma ambayo ni haki yako unatoa pesa kuipata. Kupitia rushwa na namna Nchi inavyokwenda sasa uhalisi ni kwamba mtoaji rushwa bado anatamani kutoa rushwa na mpokeaji anaogopa kupokea rushwa.

UFISADI
Macho bado yamefumba ndio maana bado tunaikumbuka awamu ya nne ya vijisenti na pesa ya mboga. Hivi pesa zote za ufisadi kama zingeingizwa kwenye miradi ya Maendeleo au zingejenga madawati leo nani angekaa chini. Kuna muda ule wakati wa CHADEMA wa kupinga ufisadi ulikua moja ya wakati wangu bora sana ila leo zile harakati zote za kupinga ufisadi zimegeuka na kua harakati za kukumbuka ufisadi kuna shida naipata hapa naipata kwenye kufikiri kwangu kama kweli kukomboa uchumi ni kukumbuka tawala zilizopita au kujenga uchumi na kutoa ushauri mzuri kwa utawala uliopo au tunasubiri na huu ukitoka tuseme bora utawala wa Magufuli.
Ufisadi umeliathiri taifa hili kwa kiwango kikubwa na umepelekea hata mawazo yetu yamejaa ufisadi badala ya uzalendo.

SERIKALI ILIVYOKUA INAJIENDESHA
Kwa kipindi kirefu watumishi wa uma walikua wanaendesha serikali kwa mazoea ilikua kwenye Halmashauri zetu ndio sehemu ya kukutana na kupiga soga. Halmashauri zetu zilikua zinaizinisha matumizi ya pesa yasiyo kua na uhalisia huku watumishi wa serikali wakijinufaisha, Hii inanifanya nikumbuke ile kauli ya Shamba la bibi, ni kweli tulikua Shamba la bibi na naona kwasababu tumefumba macho tunachokumbuka ni jinsi tulivyokua tunafaidika na Shamba la bibi.

WAFANYABIASHARA KUKWEPA KODI
Watanzania wengi hasa wafanyabiashara waliingia kwenye siasa ili iwasaidie wao urahisi wa kukwepa kodi. Sote inabidi tutambue hakuna mfanyabiashara anaependa hasara hata siku moja ili uhalisia wafanyabiashara wametukwamisha kwenye kodi kuliko kawaida kodi ambazo zingeenda kwenye maendeleo ya jamii. Ili Nchi ijiendeshe ni kosa wafanyabiashara wakatawala siasa na uchumi matokeo ya hili ni wao kukwepa kodi.
Leo tutaongea maneno yote ila uhalisia kuna muda tumefumba macho na hatutaki kujiuliza kwanini wafanyabiashara wanalalamika au tumesahau uozo wote uliokuwepo kati ya wafanyabiashara na wanasiasa kutuhujumu leo ni kampuni ngapi zilitangaza kufilisika au haya yote hatukuyaona.

Binafsi napingana na kauli za kivivu za kukumbuka utawala wa awamu ya nne Kwamba ulikua una nafuu ila kama njia tunazozichukua kwa sasa kuboresha uchumi ni nzuri basi tukazie hapo hapo na sio tuongee kwa sababu tumeamua kufumba macho hivi deni la Taifa aliloacha Jakaya kikwete hatukuliona au tumesahau kutoka 9.3 trilioni mpaka 30.6 trilioni.

Mawazo yakukumbuka utawala wa awamu ya nne binafsi nayaita mawazo ya kifisadi maana ndio wakati uliokua na ufisadi wa kutosha kwa kila kada za serikali, Halmashauri nyingi zilifuja pesa wanasiasa walipiga dili za kutosha binafsi nimeshindwa kufungamana na safari ya awamu ya nne kama ya kuikumbuka ila nataka nifumbue macho kwa hii safari ya tano.
Ila nataka Rais Magufuli afanye haya mambo kadhaa.

KUPAMBANA NA UFISADI
Magufuli endelea kupambana na mafisadi maana imani yangu inaniambia kama utaendelea kupambana na mafisadi utasaidia kutuondolea wafanyabiashara wanasiasa ambao wanaingia kwenye siasa ili wakwepe kodi, lakini pia utakua umetusaidia vijana kwa wakati ujao zile mbinu za kutoa rushwa kwa wanasiasa ili kupata uongozi zitakua zimepungua na nafasi za kisiasa zitapata watu makini ambao katika kila kura za maoni za vyama vyetu hua wanakosa nafasi kwa kushindwa kushindana na wanasiasa wafanyabiashara ambao wanaenda kufanya biashara bungeni kuliko kutakua shida za wananchi.

KUENDELEA KUKUSANYA KODI
Nataka serikali iendelee kukusanya kodi kwa kasi zaidi lakini pia serikali iangalie ni kodi zipi ambazo zinapotea au kuna biashara zipi ambazo hazijarasimishwa ili nazo zirasimishwe ili serikali isipoteze tena kodi. Lakini pia serikali iangalie ule mchezo wa kampuni za uwekezaji ambazo hua zinabadili majina kila inapofikia hatua ya wao kuanza kulipa kodi.

SERIKALI KUWA NA VIPAUMBELE
Tumeshuhudia serikali kwa kipindi kirefu imekua ikijiendesha kwa kuziba mashimo na kukosa vipaumbele vya kitaifa ni muda sasa serikali iwe na vipaumbele ili kusaidia kupunguza ya malalamiko ya kila mwaka ya watanzania. Mfano serikali iweke mkazo kwa sekta zinazosaidia kwenye bajeti zetu ili Nchi iweze kujiendesha kwa kuangalia njia za kurekebisha sekta hiyo ili izidi kuzalisha zaidi na kusaidia uchumi wetu mfano serikali kwa sasa inabidi kuangalia kama mizigo imepungua bandarini ni kipi inapaswa kufanya lakini pia kuna sekta kama kilimo kwa kiwango kikubwa kama Nchi itaenda kuchagua zao la kitaifa basi ni rahisi sana zao likasaidia kwenye uchumi wetu ili uzidi kukua zaidi kufikia uchumi wa kati.

NCHI KUCHAGUA WAWEKEZAJI
Huu ni Muda pia wa taifa kuchagua wawekezaji wenye tija kwa kuangalia wawekezaji wanaotoka kwenye Nchi ambazo zinaendana na aina ya utawala wewe unaoutaka au wawekezaji watakaoendana na mipango au mikakati tuliyojiwekea kuelekea Tanzania ya viwanda.

Macho yangu yamefunguka ila nimetumia wembe mkali kuyafumbua ila damu nyingi ilinitoka nilipofumbua macho yangu na Damu yangu iliyomwagika itapinga milele ufisadi, ukwepaji kodi na rushwa kubwa iliyokua imekithiri machoni mwetu.