MAREKANI WADAI KUMUUA KIONGOZI WA AL SHABAAB

Taarifa kutoka idara ya ulinzi ya Marekani Pentagon zinasema kuwa mmoja wa wanzilishi wa kundi la Al Shabaab Ahmed Godane ameuawa.

Marekani imesema kuwa kuuawa kwa Godane ni hatua kubwa sana katika harakati dhidi ya wapiganaji hao wamekuwa msumari mkali kwa mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki na hata kwa serikali ya Somalia yenyewe.

Katibu wa Pentagon Nchini Rear Admiral John Kirby ametangaza kuwa Ahmed Godane ameuawakatika oparesheni iliyofanywa nchini Somalia Jumatatu wiki hii.

Kwa Mujibu wa Admiral Kirby, kuuawa kwa Godane ni pigo kubwa zaidi kwa kundi hilo la Al shabaab na itasaidia kukabiliana na ugaidi unaofanywa na kundi hilo eneo la Afrika Mashariki.

Marekani imekuwa ikishirikiana na washirika wake wakuu kukabili wapiganaji hao wa AL shabaab ambapo katika miaka ya hivi karibuni wamezidisha mashambulio sio tu nchini Somalia bali hadi nchi jirani.

Wiki iliyopita Kikosi cha kulinda amani chini ya mwavuli wa Muungano wa Afrika AMISOM kikishirikiana na majeshi ya serikali ya Somalia kilianzisha oparesheni kali kuwasaka wapiganaji hao wa AL shabaab. Na kufikia mwanzoni mwa wiki hii Marekani ikajiunga katika oparesheni hiyo ambapo walishambulia msafara ambao Ahmed Godane alishukiwa kuwa ndani.

Walioshuhudia waliambia BBC kuwa muda mfupi baada ya msafara huo kushambuliwa, ndege za kivita za helikopta zinazoaminiwa kuwa za Marekani zilishuka na kubeba maiti zote zilizo kuwepo. Kwa hiyo kwa muda hakukuwa na thibitisho lolote iwapo Godane mwenyewe aliuawa au la.

Upande wa AL shabaab nao walianza kukusanya watu katika kijiji karibu na eneo hilo la Shebeele ambako shambulio lilifanywa na kuwaua au kuwateka wengijne ambao hadi sasa hawajulikani waliko.

AL shabaab hawakuzungumzia iwapo Godane alikuwa miongoni mwa waliouawa.

Leo asubuhi kulikuwa na picha zilizo sambazwa katika mtandao ambazo hazikuthibitishwa zilizodai kuwa ni Ahmed Godane bado alikuwa hai.

Al shabaab hawajasema lolote baada ya tangazo la Pentagon kuthibitisha kifo cha Godane.

UAMSHO WAOMBA MSAADA KWA RAIS

Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed amemuomba Rais kuunda tume itakayowahusisha watu kutoka Tanzania Bara, Zanzibar, wanasheria na madaktari ili waweze kuchunguza afya zao.

Sheikh Farid aliyaeleza hayo jana muda mfupi baada ya mawakili wa Serikali Peter Njike na George Barasa kuiomba mahakama kubadilisha hati ya mashtaka ya ugaidi iliyokuwa ikiwakabili na kumuunganisha Sheikh Mselem Ali Mselem na mwenzake Abdallah Said Ali na kufanya idadi ya washtakiwa hao wa ugaidi kufikia 22.

Farid alimueleza hakimu kuwa anacho cha kusema na akapewa nafasi, kisha akadai kuwa Agosti 6 na 21, 2014 walifika mahakamani hapo na kueleza matatizo, madhila na unyama waliofanyiwa na polisi na siyo magereza.

Alidai kuwa gerezani wanaishi vizuri kwa kufuata sheria isipokuwasuala la matibabu ambapo aliongeza kuwa uwezo wa bajeti yake ni mdogo hivyo wanashindwa kuwatibia jambo ambalo linasababisha waagize dawa nje wakati ugonjwa huwa hausubiri.

"Watu wameingia gerezani wanaumwa wanavuja hadi usaa kutokana na kipigo walichopewa na polisi hivyo tunamuomba Rais aunde tume kutufanyia uchunguzi wa afya zetu,"

Alisema na kuongeza;"Sisi tunachodai siyo uchochezi ninayoeleza polisi wapo wameyasikia tumekamatwa na kushtakiwa Tanganyika kwani Zanzibar siyo nchi."

Hakimu Hellen Liwa alimueleza kuwa yeye anachojua wote ni Watanzania na suala la Muungano wengine wanauamini na wengine wanataka ukazikwe Butiama.

Hakimu alimtaka aandike kwa maandishi malalamiko yake ili waweze kuyapeleka sehemu husikana kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, 2014.

Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Hakimu Hellen Liwa alikubaliana naombi hilo na mawakili hao waliwaunganisha washtakiwa hao na kuwasomea mashtaka manne mapya.

Mawakili wa Serikali, Njike na Barasa jana walidai mbele ya Hakimu Liwa kuwa washtakiwa hao walijihusisha na mashtaka yakiwamo ya kula njama na kuwaingiza watu kushiriki vitendo vya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi yamwaka 2002.

Njike alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja waliwaingiza nchini Sadick Absaloum na Farah Omary ili kutenda makosa ya ugaidi.

Sheikh Farid na Mselem kwa makusudi wanadaiwa kutoa msaadakwa Absaloum na Omary ili waweze kushiriki katika vitendo vya kigaidi.

POLISI WATJA MAJAMBAZI WATANO

Polisi mkoani Kigoma, wamewaua watu watano wanaosadikiwa kuwa majambazi waliokuwa katika harakati za kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha kwa kuteka magari ya abiria mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed ilisema tukio hilo lilitokea Septemba 3, 2014 saa 11 alfajiri katika pori la Malagarasi Wilaya ya Kasulu.

Kamanda Mohamed alisema polisi imewaua majambazi hao baada ya msako mkali uliotokana na tukio la awali la kutekwa na kulipuliwa kwa bomu basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea Kata ya Kilelema.

Alisema Agosti 27, walipata taarifa za kuwapo majambazi kutoka nchi jirani ya Burundi wakijiandaa uhalifu.

"Baada ya kupata taarifa, tuliweka mtego katika eneo lililokusudiwa kufanyika uhalifu na muda uliokusudiwa majambazi hao, walifika eneo hilo na walipoona dalili za kukamatwa na askari, walianza kufyatua risasi ovyo na askari wakiwa katika harakati za mapambano waliyaua majambazi hayo," alisema.

Alisema majambazi hao walikutwa na mabomu matatu ya kutupwa kwa mkono.

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATANGAZO YA TIBA ASILI KATIKA VYOMBO VYA HABARI

Serikali imesitisha vibali vya kurusha matangazo ya tiba za asili na mbadala kwenye vyombo vyote vya habari baada ya kubaini kuwa yanapotosha jamii.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Tiba za Asili na Tiba Mbadala kwa vyombo vya habari jana, inaeleza kuwa katika siku za karibuni kumekuwapo na matangazo mbalimbali ya tiba hizo ambayo baadhi yake hayaisaidii jamii.

Kutokana na taarifa hiyo ya baraza, vyombo vya habari havipaswi kupokea kibali chochote cha kutangaza matangazo ya tiba hizo hivi sasa, kwa kuwa ni batili.

"Hivyo basi kituo chochote cha redio, luninga, mitandao na magazeti hayaruhusiwi kurusha tangazo lolote linalohusiana na mambo ya tiba asili na mbadala kwa kipindi hiki,"
ilisema taarifa iliyosainiwa na Lucy Mziray. Pia taarifa hiyo inaeleza kuwa, chombo chochote kitakachorusha tangazo au kipindi kitatozwa faini na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumzia uamuzi wa Serikali uliochukuliwa, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema kuwa matangazo ya tiba mbadala na asili kwa muda mrefu yamekuwa yakipotosha umma kwa kukiuka Sheria ya Waganga na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 inayowazuia kujiita madaktari na kujitangaza kwenye vyombo vya habari.

"Wanakwenda kinyume wanajiita madaktari, wengine maprofesa, halafu wanakwenda mbali zaidi na kuvaa vifaa vya udaktari kwenye televisheni ili kuwavutia watu,"alisema Dk Saidia.

Aliongeza:"Kuna watu wanatangaza kuwa wanatibu figo kwa siku saba jambo ambalo haliwezekani duniani kote, wanachofanya ni kuwachelewesha wagonjwa kwenda hospitali mapema."

Naye mtaalamu wa tiba za asili, John Kidua, alisema serikali imefanya kosa kuyazuia matangazo yote badala ya kuwaadhibu watu waliobainika kuipotosha jamii pekee yao. Alisema upo uthibitisho kuwa baadhi ya dawa za asili zinatibu vizuri kuliko dawa za hospitali jambo ambalo limekuwa kikiokoa fedha nyingi za kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.

"Ilitakiwa serikali itoe msaada kwetu ili tuongeze nguvu pale tunaposhindwa na siyo kutujumuisha wote kwenye kikapu kimoja,"alisema Kidua.

JOHN MNYIKA AKUSUDIA KUMSHITAKI WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA

Mh. John Mnyika anakusudia kumshtaki mahakamani Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda kwa kosa la ofisi yake kushindwa kutangaza tarehe pamoja na maadalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam huku akiwa ameambatana na mwanasheria wake, Mh. Mnyika amesema moja ya hoja zilizomo katika shauri watakalofungua kuwa ni kutaka mahakama imlazimishe waziri mkuu Mh. Pinda, atoe kanuni pamoja na kutangaza ni lini uchaguzi huo utafanyika baada ya kile alichodai kuwa ni kuwepo kwa kimya kirefu kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo.

Mh. Mnyika amesema kuwa kwa mujibu wa sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali zaMitaa inatakiwa itangaze pamoja na kutoa kanuni za uchaguzi huo miezi miwili kabla ya mwezi Oktoba na kwamba kitendo cha ofisi hiyo kukaa kimya hakileti tafsiri sahihi juu ya hatma ya uchaguzi huo.

Mbali ya kutaka waziri mkuu atangaze kanuni na siku ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, Mnyika amesema katika hoja zake ataiomba mahakama iitake serikali ibadilishe taratibu na sheria zinazosimamia uchaguzi huo ili uwe huru na wa haki.

AL-QAEDA WAFUNGUA TAWI JIPYA INDIA

Kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda, Ayman al-Zawahiri amesema kuwa wamefungua tawi jipya lamtandao huo wa kigaidi nchini India ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wanapandisha bendera za Jihad kusini mwa bara la Asia.

Taarifa zinasema kuwa picha za video za tangazo hilo zinasema kuwa hiyo ni hatua ya kuimarisha dola ya Kiislam ambao kwa sasa unashikilia eneo kubwa la Iraq na Syria.

Zawahiri amesema kuwa nguvu mpya ya mtandao inalenga kuvunja mipaka ya nchi na kuunganisha ukanda wa dola ya Kiislam kwa kuendesha mapigano kutoka India hadi Burma.

Hata jitihada za kundi hilo kutaka kuongeza himaya ya dola ya kiislam kusini mwa bara la Asia

JUMBA LA BIG BROTHER LATEKETEA KWA MOTO

Uzinduzi wa makala mapya ya kipindi maarufu cha Big Brother nchini Afrika Kusini umeahirishwa baada ya moto mkubwa kuteketeza studio za kipindi hicho mjini Johannesburg.

Kipindi hicho kilistahili kuanza Jumapili hii lakini waandaaji wa wa kipindi chenyewe wameamua kuahirisha uzinduzi huku wakitafuta sehemu nyingine ya kupeperushia kipindi hicho.

Hakuna aliyejeruhiwa kwenye mkasa huo wa moto na kilicho usababisha bado hakijajulikana kwani uchunguzi untarajiwa kufanywa.

Washiriki katika kipindi hicho kutoka nchi 14 Afrika watakuwa wanashiriki katika makalaya 9 ya kipindi hicho.

Kipindi chenyewe kinatarajiwa kupeperushwa kwa siku 99 kabla ya mshindi kutangazwa.

Mshindi wa mwaka huu anatarajiwa kupokea kitita cha dola 300,000 kima sawa na kile kilichotolewa kwa mshindi mwaka 2013.

Waandalizi wa kipindi hicho Endemol na M-Net walisema kuwa juhudi za kupata sehemu mbadala ya kuendeshea kipindi hicho itakuwa kazi ngumu kutokana na ukosefu wa teknolojia inayohitajika kuendeshea kipindi hicho kwani haipatikani kwa urahisi.

''Kila juhudi italenga kupata ufumbuzi haraka iwezekanavyo kuhakikisha kuwa kipindi hicho ambacho hutazamwa na watu wengi zaidi Afrika kitaendelea.''waliongeza kusema waandalizi.

Waandalizi pia walisema kuwa washiriki kutoka Ghana walipata tatizo la viza na hivyo wakaamua kuchua raia wa Ghana wanaoishi nchini Afrika Kusini kwenyewe.

Pia washiriki wapya walitarajiwa kutoka Rwanda na Sierra Leone kwa mara ya kwanza lakini kutokana na changamoto za hapa na pale hawataweza kushiriki.

Kipindi cha Big Brother nikipindi maarufu sana Afrika kutokana na kupendwa sana kwake, na kilianza kupeperushwa mwaka 2003.

Washiriki kutoka Tanzania, Angola, Nigeria, Namibia, Zimbabwe na Afrika Kusini wamewahi kushinda katika makala ya awali.

Mnamo mwaka 2010, kipindi hicho kiligonga vyombo vya habari baada ya mshiriki mmoja kutimuliwa kutoka katika nyumba hiyo baada ya kumpiga makonde mshindani mwanamke.

GARI LA ULINZI LA RAIS WA KENYA LILILOIBIWA LAPATIKANA UGANDA

Maafisa wakuu kutoka shirika la polisi wa kimataifa, Interpol amethibitisha kuwa gari la ulinzi wa rais Uhuru Kenyatta lililoibwa mjini Nairobi wiki jana limepatikana nchini Uganda.

Kwa sasa gari hilo limepelekwa mjini Kampala.

Gari hilo aina ya BMW liliibwa siku ya Jumatano usiku mjini Nairobi. Watu watatu wamekamatwa kuhusiana na wizi huo.

Mkurugenzi wa polisi wa kimataifa Interpol nchini Uganda Assab Kasingye aliambia BBC kuwa gari hilo litarudishwa Nairobi.

Gari hilo liliibwa na watu waliokuwa wamejihami Jumatano wiki jana.

Hata hivyo msemaji wa serikali Manoah Esipisu alikanusha habari hizo akisema kuwa gari lililoibwa halikuwa na ulinzi wa Rais Kenyatta bali lilikuwa gari kuu kuu la polisi.

Lakini lilikuwa linaendeshwa na afisa wapolisi aliyeripoti kuwa gari hilo ni mmoja ya magari ya ulinzi wa Rais.

Afisa huyo wa polisi pia alisemekana kuwa mmoja wa maafisa wa polisi wa ulinzi wa Rais.

Tukio la wizi wa gari hilo, lilisababisha taharuki miongoni mwa maafisa wa ulinzi kwa sababu magari ya ulinzi wa Rais yenyewe yanapaswa kuwa na ulinzi mkali.

Takwimu za polisi zinaonyesha kuwa visa vitatu vya wizi wa magari huripotiwa mjini Nairobi kila siku.

Hiki ni kisa kimoja kati yavingi vya wizi wa magari ambapo mtu yeyote anaweza kuathirika.

LUKUVI AZOMEWA MBELE YA RAIS

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amejikuta katika wakati mgumu mbele ya Rais Jakaya Kikwete baada ya kuzomewa hadi kukatisha hotuba yake akipingwa na wananchi pamoja na madiwani wa CCM wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma alipokuwa akitetea kuwapo kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).

Lukuvi alikumbana na mkasa huo wakati akijibu hoja za Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), David Malole ambaye alitaka CDA ivunjwe akiituhumu kuwavunjia wananchi nyumba bila kuwatafutia mahali pa kuishi.

Hoja ya Malole kutaka CDA ivunjwe iliibuka katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kikuyu, Manispaa ya Dodoma baada ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi wa Barabara ya Dodoma - Iringa.

Awali, mbunge huyo akitoa salamu kwa Rais Kikwete, alisema CDA imekuwa ni kero kwa wakazi wa mjihuu.

"Mheshimiwa Rais, ni bora CDA ikafutwa na ardhi ikarudishwa kwa halmashauri kwa kuwa hakuna kitu kinachofanyika. Ipo miji mingi ambayo haina CDA lakini imekuwa majiji. Leo hii zaidi ya miaka 40 CDA imeshindwa kuufanya Mji wa Dodoma kuwa jiji," alisema na kuongeza:

"Licha ya kuwa CDA jukumu lake ni kuhakikisha inapima viwanja na kupanga ustawi wa mji lakini imeshindwa kufanya hivyo, jambo ambalo linawakera wananchi wa Dodoma na kusababisha kukichukia Chama Cha Mapinduzi na Serikali yao," alisema.

Kutokana na hoja hiyo kushangiliwa na madiwani pamoja na wana CCM na wananchi wengine, Malole aliendelea kufafanua kuwa suala la kupigania wananchi wapate viwanja linamuweka katika hali ngumu kwa sababu anatishiwa kuwa hatapata nafasi ya kugombea ubunge tena.

"Mimi nasema, ikimpendeza Mungu kuwa mbunge nitaendelea kuwa mbunge na kama siyo mpango wa Mungu basi, kwani kunapropaganda nyingi juu yangu lakini hiyo yote ni kutokana na kupigania wananchi wapewe haki zao," alisema.

Kuzomewa

Baada Malole kutoa madai hayo, Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya CDA alilazimika kupanda jukwaani ili asawazishe kauli za mbunge huyo, jambo ambalo liliibua zogo na wananchi kuzomea.

Zomeazomea dhidi ya Lukuvi ilitawala katika kipindi chote alichokuwa jukwaani huku viongozi wa chama wakihaha kuwazuia wanachama na madiwani wa CCM wasizomee bila mafanikio.

Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Lukuvi pale aliposema, "Mimi ni mdau mkubwa wa CDA na ni kati yawatu ambao walishiriki kupeleka maendeleo katika Mji wa Dodoma."

Kauli hiyo ilisababisha madiwani pamoja na wananchi kuanza upya kumzomea huku wakimtaka ashuke jukwaani kwa madai kuwa hana cha kuwaeleza hadi wamwelewe.

Hali hiyo iliambatana na nyimbo zilizoanzishwa na madiwani, "CCM.. shuka chini, CCM shuka chini" hali iliyomfanya Lukuvi kushuka jukwaani.

Baadaye Rais Kikwete akizungumza na wakazi hao, alitoa siku saba kwa viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na mbunge kukaa na kutatua mgogoro huo na aliahidi kukutana nao Septemba 8, mwaka huu.

Alisema migogoro haiwezi kutatuliwa katika mikutano ya hadhara, bali vikao vya kazi. Aliwataka kukutana kuangalia ni jinsi gani watamaliza mgogoro huo bila kuwa na fujo wala lawama.

Chanzo: Mwananchi

UTAFIT: WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI WAATHIRIWA NA NGONO, WENGI WAFANYA KINYUME NA MAUMBILE

UTAFITI uliofanywa na mradi wa PREPARE uliokuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa vijana kupunguza ngono, umebainisha elimu ya afya ya uzazi bado inahitajika ili kuwakinga na tabia hatarishi.

Akitoa matokeo ya awali ya utafiti huo, mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, kitengo cha magonjwa na afya ya akili, Lusajo Kajula, alisema kuwa asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 14 ambao ni wanafunzi wa darasa la tano na sita wameshawahi kufanya ngono.

Alisema ngono hiyo kwa asilimia kubwa hufanywa na wanafunzi hao kinyume na maumbile.

Kajula alisema vijana wengi wamebainika kufanya ngono ya kawaida na ya mdomo, ikifuatiwa na ngono ya kinyume na maumbile.

Alisema kwa wale ambao wameshawahi kufanya ngono, asilimia 6.3 wamefanya kinyume na maumbile wakati asilimia 93.7 hawajawahi kufanya.

Alisema utumiaji wa kondomu umebainika kuwa mdogo kwa vijana wadogo ambao wameanza kufanya ngono.

"Asilimia 68 ya wale walioanza kufanya ngono hawajawahi kutumia kondomu kabisa, wakati asilimia 32 wamewahi kutumia," alisema.

Alisema hiyo ni sehemu ya utafiti wa miaka minne ulioshirikisha Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda, Cape Town na Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway, Maastricht cha Uholanzi na Sussex cha Uingereza.

Katika utekelezaji wa utafiti huo, wanafunzi 5,099 walichaguliwa mwanzoni mwa mradi kufanyiwa utafiti huo, ambapo 4,783 (asilimia 93.9) walifuatiliwa kwa miezi 6 na wengine 4,370(asilimia 85.8) kwa miezi 12.

Mradi huo wa PREPARE ulitekelezwa kwenye shule 38 kutoka Manispaaya Kinondoni zilizochaguliwa, kwa kutumia sampuli mtawanyiko, zilizopangwa katika makundi mawili yashule.

"Kimsingi tunataka kuwaambia wanahabari kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi wa PREPARE ni kuchelewesha kuanza ngono miongoni mwa wanafunzi wa kiume na wa kike wenye umri wa miaka 12-14 katika Mkoa wa Dar es Salaam," alisema Kajula.

Matokeo yaliyotathminiwa ni mabadiliko katika masuala ya ngono (kuanza ngono) na kutumia kondomu wakatiwa kujamiiana kwa wale waliokwisha anza vitendo hivyo.

Kajula alisema kwa wastani mradi wa PREPARE umefanikiwa kupunguza uwezekano wavijana wadogo hasa wavulana na wasichana kuanza ngono na kuongeza matumizi ya kondomu kwa wale walioanza.

Hata hivyo, katika utekelezaji wa mradi mabadiliko katika uchukuaji wa hatua yalionekana zaidi miongoni mwa wasichana waliopata mwingilio ukilinganisha na wale ambao hawakupata.

Alisema uchukuaji wa hatua ulisababisha kuwapo tabia ya kutumia kondomu kwa wanafunzi wa jinsia zote na taarifa za ongezeko la utumiaji wa kondomu miongoni mwa vijana wa kiume.

Kajula alisema ili kuweza kupata matokeo yaliyokusudiwa, mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watano wakufunziwa wakufunzi.

Alisema mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watekelezaji 76, na waelimishaji rika wanafunzi 132 na kuelekeza watoa huduma 8 wa afya katika kliniki za huduma rafiki kwa vijana ili kutekeleza mwingiliano.

Mradi huo umefadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya, ambapo programu ya utafiti wa afya imelenga kuangalia mwingilio ulio katika misingi ya utamaduni na jinsia, endelevu, kijamii ili kukuza ujinsia na afya ya uzazi miongoni mwa vijana wenye umri miaka 12-14 kwa kutumia shule kama njia ya kufundishia.

Mtathmini kiongozi wa mradi huo, Mrema Kilonzo, alisema utafiti umeonyesha haja ya kutolewa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wadogo ambao bado hawajaanza ngono ili kuchelewesha kuanza ngono kwa mfumo wa kisaikolojia kama njia ya kufanya wajitambue.


Chanzo: Habari 5

KUPATA URAIA MPAKA MIAKA 15 YA NDOA

KAMATI Namba Tatu ya Bunge Maalumu la Katiba imependekeza mtuyeyote anayetaka uraia wa kuandikishwa baada ya kufunga ndoa na Mtanzania, asipewe uraia huo mpaka adumu katika ndoa husika kwa miaka 15.

Akisoma maoni ya wengi kutoka kwenye Kamati Namba Tatu bungeni jana, Dk Francis Michael alisema kamati hiyo imependekeza kuwa Ibara ya 58 inayozungumzia uraia wa kuandikishwa ni vyema mmoja wa wanandoa awe na sifa ya kuomba uraia baada ya kukaa kwenye ndoa kwa muda huo.Dk Michael alisema Ibara ya 58 inayozungumzia uraia wa kuandikishwa, ni vyema mmoja wawanandoa kuwa na sifa ya kuomba uraia baada ya kukaa kwenye ndoa kwa muda huo.

Lengo la hatua hiyo ni kuondoa udanganyifu wa watu kutumia mwanya wa ndoa, kupata uraia na kisha kupata haki za kumiliki ardhi na rasilimali zingine.

Kamati Namba 10 pia ilitoa pendekezo katika ibara hiyo, ambapo Mwenyekiti wake Anna Abdallah, alisema kamati hiyo imependekeza haki ya mwanandoa kupewa uraia, itekelezwe baada ya kudumu katika ndoa miaka saba.

Rasimu ya Pili ya Katiba, iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitambua wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wenye sifa za kisheria kuomba uraia wa kuandikishwa, ikiwemo mtu aliyefunga ndoa awe amedumu katika ndoa kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Aidha, kamati nyingi zimeonesha kuunga mkono pendekezo kumpa hadhi maalumu, Mtanzania aliyekana uraia wake mara anaporejea nchini, ingawa zimepinga kuwepo kwa uraia pacha.

Rasimu inampa hadhi maalumu mtu wenye asili au na saba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwaraia wa Tanzania kwa kupata uraia wa nchi nyingine, wanapokuja Tanzania kwa masharti yatakayo ainishwa na sheria za nchi.

Licha ya kutoa maelezo kuwa kamati yake inatambua uraia pacha, Abdallah alisema wanapendekeza sheria inayoainisha sifa na masharti ya mtu huyo anaporejea nchini.

Masharti hayo ni suala zima la umiliki wa rasilimali, ambapo pia kamati hiyo imependekeza watu hao kutoshiriki mchakato wa uchaguzi kwa kuchagua au kuchaguliwa.

Akiwakilisha maoni ya wachache katika Kamati Namba 10, Said Arfi alisema wachache pia waliunga mkono kifungu hicho, ili kuimarisha umoja, amani, uzalendo na usuala zima la usalama wa nchi.

MWANDISHI MWINGINE ACHINJWA, OBAMA AONGEZA WANAJESHI

Wapiganaji wa dola ya Kiislam IS wamesambaza picha za video katika mitandao kwa lengo la kuonyesha kuchinjwa kwa mwandishi wa habari raia Marekani Steven Sotloff ambaye ni mmoja wa mateka wanaoshikiliwa na wapiganaji hao.

Mwandishi huyo Sotloff, mwenye umri wa miaka 31 ambaye alitekwa na wapiganaji hao mwezi August mwaka jana.

Mwezi uliopita Sotloff alionekana mwishoni katika picha za video zilizoonyeshwa kuhusiana na kuchinjwa kwa mwandishi mwingine wa Marekani James Foley.

Wapiganaji hao wa katika picha hizo pia wameonekana wakimtishia kumuua mateka mwingine anayedhaniwa kuwa ni raia wa Uingereza.

Baada ya mauaji ya mwandishi wa awali Foley, mama mzazi wa mwandishi wa Sotloff alitoa ombi maalumu kwa kiongozi wa wanajeshi hao Abu Bakr al-Baghdadi kutoa muua mtoto wake.

Msemaji wa Ikulu ya White House Josh Earnest amesema kuwa maofisa wa Marekani wanaendelea na uchunguzi wa ripoti hiyo.

Marekani hivi karibuni ilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya IS nchini Iraq.

Mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC Frank Gardner amesema hatua hiyo ya wapiganaji wa IS ni kulipa kisasi kwa Marekani.


OBAMA AIDHINISHA WANAJESHI KUONGEZWA

Rais Barack Obama wa Marekani ameidhinisha kupelekwa vikosi vya wanajeshi wapatao 350 kwa lengo la kuwalinda wanadiplomasia na wafanyakazi raia wa nchi hiyo waishio mji mkuu waIraq Baghdad.

Ikulu ya Marekani imesema wanajeshi hao watakaopelekwa baadhi yao ni wale wanaojihusisha na diplomasia ya ulinzi ya iraq ambao ni zaidi ya mia nane.

Hata hivyo Marekani inatarajia kuwatuma maofisa waandamizi akiwemo John kerry katibu mkuu wa marekani na Chuck Hagel katibu wa ulinzi ambao watakwenda mashariki yakati katika harakati za kuimarisha ushirikiano.

Hatua hiyo inafuatia vitendo vya mashambulizi na mauaji yanayoendelea Iraq ikiwani matokeo ya utofauti kati ya Marekani na makundi ya wapiganaji ambao wamekuwa wakiwalenga raia wa Marekani waliopo nchini humo.

NIGERIA KUISHITAKI SCHALKE 04 FIFA

Shirikisho la soka Nigeria limesesema litaishitaki klabu ya Schalke ya Ujerumani kwa Fifa baada ya klabu hiyo kukataa kumruhusu mshambulizi Chinedu Obasi kushirki michuano ya kufuzu kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2015.

Hata hivyo klabu ya Schalke imesema kuwa sababu ya kukosa kumruhusu mchezaji huyo kuondoka ni kwamba pasi yake ya usafiri iko katika ubalozi huku viza yake ikitayarishwa kabla ya kuanza kwa michunao ya klabu bingwa Ulaya.

Afisa wa habari wa Super Eagles Ben Alaiya ameambia BBC kwamba wana mechi mbili ambazo tayari zimeidhinishwa na Fifa.

"Nchi yetu ina haki ya kukabidhiwa mchezaji wake Chinedu Obasi kwa michuano ya kufuzu kwa kombe hilo. ''

Nigeria ambao ni mabingwa wa Afrika, watamenyana na Congo mnamo tarehe sita Septemba. Siku nne baadaye watatoana kijasho na Afrika Kusini. Nigeria imekasirishwa na Schalke kuhusu mchezaji wake Obasi.

Vilabu hushurutishwa kuwaruhusu wachezaji wa kigeni kuchezea nchi zao katika michunao ya kimataifa pindi wanapotakiwa na nchi zao kucheza.

Klabu hiyo ya Bundesliga inamtaka Obasi, kucheza dhidi ya Borussia Monchengladbach katika ligi hiyo na mechi itakayochezwa dhidi ya Chelsea katika michunao ya klabu bingwa Ulaya tarehe 13 na 17.

Alaiya aliongeza kusema kuwa mchezaji anapaswa kurejea kushirki majukumu ya kimataifa pindi anapohitajika.

"katibu wa timu amefanya awezalo na sasa tutachukua hatua kwa kushitaki Schalke kwa Fifa.''

Wakati huohuo Nahodha wa Nigeria amejiondoa katika mechi mbili za kufuzu kwa michuano ya taifa bingwa Afrika.

KIONGOZI WA AL SHABAAB ASHAMBULIWA

Wanajeshi wa Mreakani wamefanya mashambulizi ya angani dhidi ya msafara wa magari ya mmoja wa viongozi wa kundi la Al Shabaab nchini Somalia.

Haijulikani ikiwa kiongozi wa kundi hilo, Ahmed Abdi Godane aliuawa kwenye shambulizi hilo lililofanyika umbali wa kilomita 240 kusini ya mjini mkuu Mogadishu.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa wanajeshiwa Marekani walionekana wakishuka katika eneo hilo kwa helikopta na kuchukua miili ya wapiganaji waliouawa.

Msemaji wa idara ya ulinzi ya Marekani, (Rear Admiral John Kirby) alisema bado inadurusu matokeo ya shambulizi hilo.

Baadhi ya taarifa zinasema kuwa wapiganaji waliwakamata wakazi walioshukiwa kutoa taarifa kwa Marekani.

SHEKH PONDA AOMBA KESI ISIMAMISHWE

Wakili Nassoro Juma anayemtetea Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ameiomba Mahakama Kuu itumie busara kusimamisha kesi ya jinai inayomkabili mteja wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.

Ponda kupitia wakili huyo, aliwasilisha maombi akitaka mahakama iamuru kesi hiyo inayomkabili mkoani Morogoro isimame ili kusubiri kwanza uamuziwa rufaa yake aliyokata mahakamani hapo.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Ponda anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi katika maeneo mbalimbali mkoani humo,likiwamo la kukaidi amri ya Mahakama ya Kisutu.

Mahakama ya Kisutu katika hukumu yake Mei 9, 2013, ilimtaka Sheikh Ponda awe mhubiri amani katika jamii likiwa ni sharti la kifungo cha mwaka mmoja nje baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai mwaka 2012.

Katika kesi hiyo, Ponda na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtakaya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni na kuingia kijinai kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali eneo la ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd na uchochezi.

Hata hivyo, Sheikh Ponda kupitia kwa mawakili wake alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu.

Kutokana na rufaa hiyo, ndipo walipowasilisha maombi ya kusimamisha kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.

Jaji Lawrence Kaduri anayesikiliza maombi hayo alikubaliana na maombi ya Jamhuri na kuahirisha shauri hilo hadi Septemba 10.

MREMA AMSHITAKI MBATIA KWA RAIS KIKWETE

KATIKA hali ya kutapatapa kisiasa, Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP), amemshtaki kwa Rais Jakaya Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), akitaka ang'olewe ubunge.

Mrema, alitoa kituko hicho juzi mjini hapa, wakati Rais Kikwete alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye wabunge kujadiliana kuhusu maridhiano ya mchakato wa katiba mpya.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Mrema alimwomba Rais Kikwete awaonye Mbatia na John Mrema wa CHADEMA, akidai wanamsumbua jimboni wakitaka kumng'oa katika uchaguzi ujao.

Itakumbukwa kuwa Mbatia ndiye alikuwa mbunge wa kwanza kuongoza jimbo hilo mwaka 1995 katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na John Mrema aligombea mwaka 2010 akashindwa na Mrema.

Inaelezwa kuwa, katika hali ya kuchekesha, Mrema aliacha hoja ya msingi iliyowapeleka kwa Rais na kutumbukiza malalamiko yake binafsi, akidai Mbatia ni mtu hatari kisiasa na anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuwa ameanza kampeni kabla ya wakati.Chanzo hicho, kiliongeza kuwa Mrema alisema pamoja na kwamba Mbatia anafanya kampeni kabla ya wakati, lakini anamlaumu zaidi Rais Kikwete kwa sababu ndiye amempa jeuri baada ya kumteua kuwa mbunge.

"Alipokuwa akisema hayo, Rais alicheka kweli kweli maana ilikuwa kama Sinema,kwa sababu alikuwa akizungumza kwa msisitizo akionyesha kukerwa na Mbatia zaidi," kilisema chanzo hicho.

Kwamba, Rais Kikwete katika kumpooza, alimtaka Mrema asiwe na wasiwasi kwa sababu wananchi wa Vunjo wanamjua mbunge wao ni nani kati yake na Mbatia.

"Rais alimuuliza kuwa kama akimwondoa Mbatia halafu akaja mwingine akamteua tena itakuwaje, lakini Mrema alishinikiza akitaka amwondoe tu na kusisitiza kwamba asipomtoa atakuwa hamtendei haki," alisema mtoa taarifa.

Mbatia alikiri kushutumiwa na Mrema mbele ya Rais na kusema kuwa hiyo ni mara ya pili kufanya hivyo hadharani."

Ni kweli alilalamika kwa Kikwete, na hii si mara yake ya kwanza kwani hata Agosti 2 mwaka huu, alinilalamikia katika kikao cha TCD.

"Namheshimu sana Mrema, ila namuomba aendelee kuwatumikia wananchi wa Vunjo lakini kwa kuwa anazidi kunifuatafuata, Septemba 6 mwaka huu, nitahutubia mkutano wa hadhara huko Vunjo kueleza msimamo wangu," alisema Mbatia.

Naye Mrema, alisema alilazimika kumfikishia kilio chake Rais Kikwete kwa sababu ndiye alimteua Mbatia."

Mbati ni mtu hatari sana, yaani anakwenda jimboni na kuwaambia wananchi mimi ni mzee na kibaya zaidi anasema tumekubaliana nimwachie jimbo.

"Nilimsema kwa Rais kwa sababu ananifanyia rafu kule jimboni, ni hatari sana," alisema Mrema.

Hivi karibuni, Mbatia alitangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo huku John Mrema wa CHADEMA naye akiamini kwamba uchaguzi ujao atashinda kiti hicho.

NDEGE YAANGUKA SERENGETI

UCHUNGUZI wa awali kuhusu kupotea kwa ndege ya mizigo ya Shirika la Safari Express ya nchini Kenya, umeonesha kuwa ndege hiyo yenye usajili namba 5Y SXP, aina ya Fokker 27, imepata ajali.

Taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), iliyotumwa jana jioni katika vyombo vya habari, imeonesha kuwa ndege hiyo iliyopoteza mawasiliano juzi usiku, imeonekana ikiwa imeanguka katika eneo la Kongetende Serengeti mkoani Mara.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, haijathibitika kama watu watatu ambao ni wafanyakazi waliokuwa kwenye ndege hiyo, wamepoteza maisha au la.Awali, Meneja wa Usalama na Usafiri wa Anga wa TCAA, mkoani Mwanza, John Shushu alisema, ndege hiyo iliondoka kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Mwanza Agosti 31, saa 1.26 usiku.

Mawasiliano ya mwisho na ndege hiyo, inayomilikiwa na Kampuni ya Safari Express ya Nairobi Kenya, yalikuwa saa 2:05 usiku wakati ndege ipo umbali wa kilometa 40 kutoka mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo ndege hiyo ilikuwa angani futi 17,000 juu ya usawa wa bahari.

Ndege ilipaswa kuvuka eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya saa 2:11 usiku, lakini ilipoteza mawasiliano na Kituo Kikuu cha Kuongozea Ndege cha Dar es Salaam na rubani wa ndege hiyo, hakutoa taarifa kuonesha iwapo ndege yake ilikuwa na tatizo.

Baada ya kubainika kwa mabaki ya ndege hiyo, uchunguzi wa ajali hiyosasa umeanza ili kubaini sababu ya ajali hiyo. Uchunguzi huo unashirikisha wataalamu kutoka Mamlaka na Kitengo cha Uchunguzi wa Ajali.

MADARAKA NYERERE AWATETEA WANAOTAKA URAIS

MTOTO wa baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Madaraka Nyerere, amesema ni hatari kwa vyama vya siasa kuwazuia watu wenye nia ya kutaka kugombea urais mwaka 2015.

Amesema kitendo cha kuwazuia ni kuwanyima nafasi wananchi kupima uwezo, uadilifu na busara zao kama wanafaa kuongoza Taifa la Tanzania.

Akizungumza juzi, mjini Butiama alipotembelewa na viongozi wa Chama cha Siasa cha ACT-Tanzania, walipofika nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Madaraka alisema nimuhimu wa watu wanaotaka kuwania urais kujulikana mapema, huku akisisitiza kuwanyima nafasi ya kujitangaza sasa ni kuwanyima uhuru Watanzania wa kuwachambua na kuwatathmini.

"Miezi mitatu ya kuwafanya wananchi wamsikilize mtu atakayekabidhiwa madaraka ya nchi ni michache kwa ajili ya kumfanyia tathmini na kwamba, marufuku ya aina hiyo ndani ya vyama ingeachwa," alisema Madaraka.

Aliongeza, si sawa kwa viongozi wanaotaka kushika nafasi ya Urais wakakatazwa kujitangaza mapema.

Kuhusu upinzani, Madaraka alisema wanapaswa kujitofautisha na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Akizungumzia vyama kuungana ili kuiondoa CCM madarakani, alisema wakifanya hivyo wanaweza kufanikiwa, lakini alitahadharisha madhara yanayoweza kujitokeza.

Pia, alisema vyama hivyo vinatakiwa kuwa na malengo kwani bila hivyo, watakuwa wakiishia kwenye malumbano na tofauti ambazo hazitakuwa na tija kwao upinzani.

Pamoja na hayo, ACT-Tanzania walimwambia Madaraka kuwa, lengo la kufika nyumbani kwa Baba wa Taifa, ni kupata baraka zake na kujifunza maisha aliyoishi Mwalimu Nyerere, kabla na baada ya uongozi wake.

Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu alisema ni vema kujifunza historia ya Nyerere kwa viongozi wa Tanzania, kwa kuwa kiongozi huyo aliwaunganisha Watanzania wote.

WAPIGANAJI WATEKA MAJENGO NA OFISI ZA SERIKALI TRIPOLI

Wapiganaji nchini Libya wameteka ofisi na majengo ya wizara za serikali mjini Tripoli.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya nchi hiyo.

Watu waliokuwa wamejihami waliwazuia wafanyakazi kuingia katika ofisi za wizara hizo.

Mnamo siku ya Jumapili, wapiganaji hao waliteka makao ya ubalozi wa Marekani.

Libya imekumbwa na vurugu tangu kung'olewa mamlakani kwa hayati kanali Muammar Gaddafi aliyepinduliwa na wanajeshi wa Nato wakisaidiwa na wapiganaji wa kiisilamu mwaka 2011.

Wapiganaji hao wamekuwa wakipigana miongoni mwao wenyewe wakitaka mamlaka.

Maafisa wakuu wa serikali na wabunge walihamia katika mji wa Tobruk, Mashariki mwa nchi hiyo mwezi jana.

Marekani na mataifa mengine yalilazimika kuwaondoa wafanyakazi wao kutoka nchini humo mwezi Julai huku mapigano yakichacha mjini Tripoli.

Benki kuu ya Libya pamoja na kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ziko mjini humo.

Waziri mkuu Abdullah al-Thinni na baraza lake la mawaziri, walijiuzulu wiki jana ili bunge liweze kuteua serikali mpya.

Uchaguzi huo ulikuwa wa pili tangu kanali Gaddafi kuuawa katika mapinduzi ya mwaka 2011. Matumaini ya uchaguzi huu kurejesha uthabiti nchini Libya ni hafifu mno.

BABA AMNYONGA MPAKA KUFA BINTI WAKE WA MWAKA MOJA KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

MTOTO mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili, Regina Geofrey ameuawa kikatili kwa kunyongwa na baba yake mzazi Geofrey Kilingwa 'Simbaiwe" (27) kwa kuwa alizaliwa akiwa ametanguliza makalio yake.

Baba wabinti huyo ambaye pia mganga wa kienyeji anayeishi kitongoji cha Mwikang'ombe, kijijicha cha Katuma, wilayani Mpanda alitenda unyama huo kwa mdai kuwa mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza makalio yake ni mkosi na nuksi kubwa katika shughuli zake hizo za uganga wa kienyeji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari akizungumza leo na waandishi wa habari mjini hapa amedai kuwa mzazi huyo aliyetenda uhalifu huo Julai 20 mwaka huu ambapo alikamatwa na jeshi la Polisi Agosti 26, mwaka huu..

Inadaiwa siku hiyo ya tukio mtuhumiwa huyo baada ya kumnyonga hadi kufa binti yake huyo alimzika kwa siri katika kibanda chake anachofanyia shughuli zake za uganga wa kienyeji.

Akisimulia mkasa huo Kamanda Kidavashari alidai kuwa mtoto Regina alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao haukufahamika kwa zaidi ya mwezi mmoja.

"Ndipo baba mzazi wa binti huyo alipoalazimika kuanza kumuuguza kwa siri pasipo mama yake mzazi kufahamu kwani alimdanganya kuwa mtoto wao huyo amepelekwa kutibiwa na babu yake huko mkoani Mwanza " alieleza Kidavashari.

Inadaiwa kuwa kibanda ambacho mtuhumiwa alikuwa akifanyia shughuli zake za uganga kilikuwa mbali na makazi yake hivyo ilikuwa rahisi kumficha mtoto wake huyo kwa zaidi ya mwezi mzima akimtibu bila mama mzazi wa mtoto huyo kufahamu.

Kwa mujibu wa kamanda Kidavashari, wakazi wa kitongoji cha Mwikan'gombe wakiongozwa na Mwenyekiti wao walimtilia shaka mtuhumiwa kutokana na tetesi zilizozagaa eneo hilo kuwa mtoto Regina alikuwa ameuawa na baba yake mzazi na kuzikwa kwa siri.

Inadaiwa wakazi haona mwenyekiti wao waliamua kufika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuhoji alipo binti yake Regina ambapo alipinga vikali lakini alipopekuliwa katika kibandani kwake walibaini kuweko kwa tuta dogo lililkuwa limechimbwa siku za karibuni.

Kidavashari aliongeza kuwa wakazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wao waliamua kufukua tuta hilo na kukuta kichwa cha mtoto huyo kisha wakaitaarifu polisi.

Mama wa marehemu aitwae Maria Exavery (22) alidai kuwa hakuhusishwa wala kupewa taarifa kwamba binti yake huyo amekufa "Mie nilikuwa nafahamu kuwa Regina yuko kwa babu yake , Mwanza akitibiwa " alieleza.

Nae Regina Kaboni (40) mkazi wa Isamilo Mwanza ambaye alikuwa akitibiwa na mtuhumiwa anadai kuwa alishirikishwa katika maziko ya binti huyo "hata hivyo nilishtushwa sana kwa kitendo cha mtuhumiwa kumzika mwanae bila ya kumshirikisha mkewe , nilipomuuliza mtuhumiwa alidai kuwa kwa mila ya kwao mtoto aliyezaliwa kwa kutanguliza makalio yake mama mzazi wa mtotoni mwiko kushirikishwa katika maziko ya mtoto huyo ' anadai Kwa mujibu wa Kidavashari watu wanne wakiwemo wazazi wa marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi ambapo watafikishwa mahakamani mara tubaada ya upelelezi wa awali kukamilika ..

Wengine wanaoshikiliwa na Jeshi hilo ni pamoja na Regina Kabonina Msolwa Jacob (29) mkazi wakitongoji cha Mwikang'ombe.

Chanzo: Katavi Yetu

WAKRISTO WAKIMBIA KANISA

WAKRISTO nchini Ujerumani wanazidi kujiondoa katika makanisa yao wakiudhiwa na utoajiwa zaka (kodi ya kanisa) ambayo wanaona ni kubwa.

Imeelezwa kuwa katika majimbo ya Bavaria na Baden Wurttemberg sadaka (zaka) ni asilimia nane ya mapato halisi.

Maeneo mengine ya Ujerumani sadaka ni asilimia 9. Kwa mujibu wa taarifa zinazopatikana mtandaoni zinasema kwamba mwaka huu kumekuwepo na kundi kubwa linalojiondoa katika Ukristo (Ukatoliki na Uprotestanti) nchini humo.

Waumini elfu kumi wa Kiprotestanti wamejiondoa kutoka Kanisa la Berlin, idadi inayoelezwa kuwa kubwa kuliko waliojitoa mwaka 2011 na 2012 wakichanganywa pamoja.

Aidha ukanda wenye Ukatoliki mkubwa wa Bavaria,Wakatoliki 14,800 walijiondoa kati ya Januari na Juni mwaka huu ukilinganisha idadi ya waliojiondoa 2013 kwa mwaka mzima. Zaka ya kanisa nchini humo hukatwa moja kwa moja na Hazina ya Ujerumani.

Mpaka mwaka huu walipa kodi walitakiwa kujieleza kuhusiana na zaka lakini kuanzia mwaka ujao zaka hizo zitakatwa moja kwa moja na benki zao. Kutokana na mabadiliko hayo ya sheria, benki zitalazimika kujua madhehebu ya wateja wao.

Pamoja na masuala ya sadaka, masuala mengine yanayosababishawatu kujitoa ni ndoa ambapo imeelezwa wengi wa wanandoa walioachana wameenda kuoa au kuolewa kwingine, na wanajitoa wakihofia adhabu ya kufungiwa kiimani.

Pamoja na waumini kupungua makanisa hayo yamekuwa yakiingiza fedha nyingi za kanisa. Mwaka jana Kanisa Katoliki lilikusanya euro bilioni 5.5 (Sh trilioni 11.5) wakati makanisa ya Kiprotestanti yalikusanya euro bilioni 4.8 (Sh trilioni 10).

MAHAKAMA IMEWATIA HATIANI WALIOJARIBU KUMUUA JEN. NYAMWASA

Mahakama nchini Afrika ya Kusini imewatia hatiani watu wanne kwa kujaribu kumuua Jenerali Faustin Nyamwasa, aliyewahi kuwa mshirika wa karibu wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambaye alipigwa risasi nyumbani kwake jijini Johannesburg miezi michache baada ya kutorokea huko akitokea Rwanda.

Nyamwasa anasema utawala wa Kagame uliwakodi watu hao ili wamuue, madai ambayo Rwanda inayakanusha, ingawa serikali imekuwa ikituhumiwa kwa kuwafuatilia wakosoaji wake  wanaoishi nje.

Mkuu wa zamani wa usalama wa taifa wa Rwanda, Patrick Karegeya, aliuawa huko huko Afrika ya Kusini mwaka 2013 na uchunguzi wa kifo chake bado unaendelea.

YANGA WAMSHITAKI OKWI TFF

Klabu ya Young Africans imemshitaki mchezaji Emmanuel Okwi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuwasilisha nakala kwa shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) na shirikisho la soka duniani (FIFA) kwa kuingia mkataba na timu nyingine wakati akiwa bado ana mkataba wa miaka miwili.

Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Yanga mitaa ya Twiga/Jangwani, mwenyekiti wa Yanga Bw Yusuf Manji amesema wameshangazwa nakitendo hicho kilichofanywa na viongozi wa Simba , wakala wake na mchezaji mwenyewe.

"Emmanuel Okwi awali tulishapeleka malalamiko TFF na kuwapa nakala CAF na FIFA juu ya kufanya mazungumzo na timu ya Wadi Degla FC ya nchini Misri na kufikia klabu hiyo kutuma ofa ya kutaka kumnunua bila kuwasiliana na uongozi wetu" alisema Yusuf.

Ikiwa hilo tunasubiria majibu kutoka TFF jana mchezaji huyo amesaini mkataba mwingine, hii inaonyesha ni jinsi gani mchezaji huyu kuna watu walikua wanamrubuni,kwa kusaini mkataba mwingine kitu ambacho amekiuka sheria za FIFA za usajili.

Baada ya kuona jana amesaini mkataba na Simba, Yanga tulichokifanya leo ni kuandika barua nyingine TFF juu ya suala hilo na kuomba kulipwa fidia ya US Dollar 500,000 (sawa na TZS 800,000,000/=) kutoka kwa klabu yaSimba, wakala wake na mchezaji mwenyewe aliongeza "Manji"Aidha uongozi wa Yanga umeiomba TFF kuwa imelipatia ufumbuzi sualahilo ndani ya siku saba, na kama siku saba zikipita basi uongozi wa Yanga utakwenda moja kwa moja FIFA na ikishindakana mahakama ya soka CAS.

Lengo sio kuikomoa timu ya Simba,bali tunachotaka ni sheria ifuatwe, Okwi alikua ameitumikia klabu ya Yanga kwa kipindi cha miezi sita tu, na kuwa amebakiza mkataba wa miaka miwili mpaka msimu mwishoni mwa msimu wa 2015/2016.

Mchezaji anayekutwa na kosa la kusaini sehem mbili adhabu yake nikufungiwa kucheza soka kuanzia mwaka mmoja na kuendelea huku klabu husika ikifungiwa kusajili kuanzia miaka mwili na kuendela nakushushwa daraja au adhabu zote kwa pamoja.

WATU KUMI WAFARIKI PAPO HAPO NA WENGINE SABA WAJERUHIWA KATIKA AJALI JIJINI MBEYA

WATU kumi wakiwemo watoto wawili wamefariki dunia papo hapo na wengine saba wamejeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari mawili.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa nne asubuhi ikihusisha gari ndogo ya abiria maarufu daladala lenye namba za usajili T 237 BFB aina Toyota Hiace na gari kubwa aina ya Fuso lenye namba za usajili T 158 CSV.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo wamesema ajali hiyo ilitokea maeneo yaMbalizi baada ya Hiace iliyokuwa ikitokea Mbeya mjini kuelekea Mbalizi kulivaa Fuso ilikuwa ikiingia barabarani.

Walisema inasemekana dereva wa Hiace gari yake ilimshinda kutokana na kutelemka mlima mkali wa Mbalizi inagawa pia walimtupia lawama dereva wa Fuso ambaye alikuwa akiingia barabarani bila kuchukua tahadhari.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali teule ya Ifisi Mbalizi, Sikitu Mbilinyi, ambako Majeruhi na marehemu walikimbizwa hapo alithibitisha kupokea majeruhi 7 ambapo alisema kati yao ni wanawake 3 na wanaume 4.

Alisema kati ya majeruhi hao wawili wamepewa rufaa kwenda hospitali ya Rufaa Mbeya kutokana na kuhitaji msaada zaidi huklu wengine wakiendelea kupatiwa msaada wa haraka ili kunusuru hali zao.

Mbilinyi aliongeza kuwapia wamepokea miili ya marehemu 10 wakiwemo watoto wawili na Wanawake wanne na Wanaume wanne.

Hata hivyo majina ya majeruhi na marehemu hayajaweza kupatikana mara moja kutokana na kuwa katika hali mbaya ambapo Dereva wa Fuso akitokomea mara baada ya tukio.

Source: MBEYA YETU BLOG (http://mbeyayetu.blogspot.com/2014/08/breaking-news-tukio-katika-picha-watu.html?spref=fb&m=1)

GARI YA ULINZI WA RAIS YAIBIWA?

Taarifa za kutatanisha za kuibiwa kwa gari la ulinzi wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta zimeibuka nchini humo.

Taarifa hii ilitolewa na baadhi ya vyombo vya habari ingawa msemaji wa Rais Kenyatta ameikanusha taarifa hiyo akisema kuwa gari lililoibiwa lilikuwa la idara ya polisi likiendeshwa na inspekta mkuu wa polisi.

Gari hilo lililokuwa lisemekana kuwa na uwezo wa kuhimili risasi, liliibiwa usiku wa Jumatano na kwamba aliyekuwa analiendesha gari hilo alikuwa afisa wa polisi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Daily Nation ikimnukuu mtu anayesemekana kuwa dereva wa gari hilo la kifahari alilazimishwa kuvua nguo zake kabla ya kupokonywa gari hillo.

Gari lenyewe lilikuwa na nambari ya usajili ya kibinafsi.

Ni gari la polisi au la Rais?

Kwa mujibu wa msemaji wa Rais, gari hilo aina ya BMW 735 la mwaka 2000, lilikuwa linaendeshwa nainspekta wa polisi alipovamiwa na wanaume wanne waliokuwa wamejihami karibu na eneo la Ruai viungani mwa mji mkuu Nairobi.

Msemaji wa Rais Manoah Esipisu amekanusha madai kwamba gari hilo lilikuwa moja ya magari ya ulinzi wa Rais Uhuru Kenyatta kama ilivyokuwa imenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari

Bwana Manoah amesema kuwa Inspekta aliyekuwa anaendesha gari hilo aliporwa dola mia saba na simu yake gari hilo lilipoibiwa saa tatu usiku.

Alitekwa na majambazi hao kwa karibu saa tano kabla ya kumwachilia usiku wa manane.

Alisema kuwa wezi hao walitoweka na gari hilo ambalo alisema hutumiwa kwa shughuli za polisi na kwamba tayari msako umeanzishwa ingawa gari hilo bado halijapatikana.

Kadhalika alikanusha kuwa gari hilo lilikuwa la ulinzi wa Rais na kwamba lenyewe lilikuwa na uwezo wa kuhimili risasi.

Visa vya wizi wa magari na utekaji wa madereva sio jambo geni nchini Kenya ila kilichowashangaza wengi ni kwamba je vipi gari la ulinzi wa Rais liibiwe?

Bwana Manoah amesema takwimu zinaonyesha visa vya uhalifu vimepungua hasa katika jiji kuu Nairobi katika miezi ya hivi karibuni na kwamba ulinzi unaendelea kuimarishwa.

JAJI AHOJI WINGI WA KESI ZA SHEIKH PONDA

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemtaka katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda aeleze sababu za kuwa na kesi nyingi, huku akihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu nchini.

Pia mahakama hiyo imeamuru vyombo vya dola kuacha kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani kusikiliza kesi zake, na kushauri kama wana wasiwasi nao, waweke mashine za ukaguzi katika mlango wa kuingilia mahakamani hapo.

Mwenendo huo wa Sheikh Ponda ulihojiwa mahakamani hapo na Jaji Augustine Shangwa juzi kabla ya kuanza kusikiliza rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtia hatiani katika kesi ya jinai, mwaka 2012.

"Sheikh Ponda, sijui ni kwa nini unakesi nyingi kiasi hiki. Kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi (Kisutu) una kesi, Mahakama Kuu una kesi. Nani yuko nyuma ya kesi zako? Je! Serikali inakuchukia?" alihoji Jaji Shangwa.Licha kumhoji Sheikh Ponda maswali hayo, alimweleza kuwa kama atakuwa na jambo la kuzungumza, atampa nafasi siku nyingine rufaa yake itakapotajwa. Pia Jaji Shangwa alimshauri apunguze mapambano.

"Ikiwezekana uyapunguze (mapambano) maana dunia hii si yakupambana nayo," alisema Jaji Shangwa na kusisitiza kuwa lazima ajiulize kwa nini ana kesi nyingi.

Jaji Shangwa aliendelea kusema: "Jambo likitokea Zanzibar, wewe umo; likitokea Morogoro umo; likitokea Dar es Salaam umo. Bahati mbaya kuna kikundi cha Uamsho kinadaiwa kulipua mabomu na kuua watu, nasikia na wewe unatajwa kuhusishwa."Hata hivyo baadaye Jaji Shangwa alimuuliza Ponda kama ana la kueleza kuhusu wingi wa kesi zinazomkabili.

Sheikh Ponda alidai kuwa kesi hizo ni mzigo anaotwisha kutokana na kutetea kile alichokiita masilahi, huku akijitetea kuhusu hukumu ya kesi iliyomtia hatiani ambayo amekata rufaa kuipinga, akieleza kuwa eneo analodai kuvamia ni mali ya Waislamu.

Hata hivyo, Jaji Shangwa alimkata kauli akisema anayoyaeleza yanapaswa kusemwa na mawakili wake katika rufaa hiyo kama alikuwa na hatia au la. Alimtaka aeleze ni kwanini anakabiliwa na kesi nyingi.

Hata hivyo, wakili wake Juma Nassoro alisimama na kuieleza Mahakama kuwa si kwamba mteja wake ana kesi nyingi, bali anakabiliwa na kesi mbili tu moja iliyokuwa Mahakama ya Kisutu ambayo ndiyo wameikatia rufaa na ile iliyoko Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.

Awali, wakati akivipiga 'stop' vyombo vya dola kuwazuia wafuasi wake kuingia mahakamani, Jaji Shangwa alisema: "Huyu Sheikh Ponda ana wafuasi wengi, wanahitaji kuja kusikiliza kesi yake. Vyombo husika visiwazuie, waacheni waje wasikilize kesi ya Sheikh wao." Pia aliwaonya wafuasi hao kuacha mapambano na vyombo vya dola.

JWTZ KUWACHUNGUZA MAKOMANDO WA NEPAL

JESHI la Wananchi Tanzania(JWTZ), limeshtushwana taarifa za kuwepo kwa makomandoo wa kijeshi kutoka nchi ya Nepal ambao waliingia nchini kinyemela kwa madai ya kutafuta kazi.

Pia, JWTZ imesema taratibu za mwanajeshi kwenda kuajiriwa sehemu nyingine ya nchi haipo karibu duniani kote, hivyo suala hilo wanalifuatilia kwa karibuili kupata undani wake, ambapo hati za kusafiria za makomandoo hao zikiwa zinashikiliwa, huku Serikali ikibeba jukumu la kuwahudumia.

Akizungumza na gazetihili jana kwa njia ya simu,Mkurungenzi wa Idara ya Mawasiliano JWTZ, Luteni Kanali Erick Komba alisema kwa mujibu wa kanuni za jeshini kwamba, mwanajeshi kutoka nchi moja kwenda nyingine suala halipo.

Hata hivyo, Komba alisema inawezekana kukawa na makubaliano maalumu ya nchi au katika jumuia za kusaidia kijeshi, ndipo wanajeshi waliokubalika nchi na nchi hutolewa kwa lengo la kazi maalumu, kama ilivyo kwa vikosi vya kulinda amani ambavyo JWTZ hushiriki.

"Wanajeshi kwa kawaida haajiriwi kama wafanyakazi wengine, ila huteuliwa na jopo maalumu na baada ya kuridhishwa, hupewa nafasi ya kujiunga na jeshi, hivyoni mapema kulisemea na ningeomba uwasiliane na watu wa uhamiaji kwa maelezo zaidi,"alisema Luteni Kanali Komba.

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Dar es Salaam, Grace Hokororo alisema tayari wahamiaji 12 wa Nepal wametumiwa tiketi kutoka kwa ndugu zao na wanatarajiwa kusafirishwa kurejea kwao Septemba 2, mwaka huu.

Alisema wanawashikilia wahamiaji 50, ambapo 12 kati yao ndiyo walioletewa tiketi na waliobaki wanaendelea kuhifadhiwa kama walivyokutwa kwenye nyumba ya mzee mmoja ambaye hakumtaja jina lake.

"Tumefi kia hatua ya kumwomba mzee atusaidie kuwatunza kwenye nyumba hiyo walimokamatiwa, wakati taratibu nyingine zikifanyika, ikiwa pamoja na kuwatafut amawakala wawili waliowaleta nchini," alisema.

Hokororo alisema mawakala waliowaleta wahamiaji hao,walifahamika kwa majina ya Ali Hamidu Ali au kwa jina lingine anajulikana kama Ali Prosper Ngurigwa ambaye ni Mtanzania akishirikiana na raia wa Nepal, Devi Ram Dhamala akiwa na pasipoti 4277471.

Alisema kwa mujibu wataarifa zilizopatikana kutoka kwa wahamiaji hao, zinasema waliletwa nchini baada ya kurubuniwa kuwa, kuna kazi zenye ujira mzuri watakazo pata pindi wakifika Tanzania."

Kuna gharama walilipa, pia kulipa tiketi ya kwenda na kurudi, lakini cha ajabu walipofi kahapa nchini kupitia uwanja wandege, walipelekwa Kijitonyama na Tegeta kwa mafungu na kula yao ikawa ya shida hadi suala hilo lilipofahamika hadharani.

"Hatuwezi kuwaweka ndani kutokana na sheria zilizopo za ndani na nje ya nchi, kwa vile watu hao walidaganywa kwa lengo la kupata ajira, hivyo wanakuwa waathirika wa janga hilo," alisema na kuongeza kwa sasa Serikali imechukua hatua ya kuwahudumia hadi watakapo ondoka nchini.

Makomandoo hao walikamatwa juzi maeneo ya Tegeta jijini Dar es Salaam wakiwa wamehifadhiwa katika nyumba mbili tofauti, huku wakiwa na sare za kijeshi la Nepal.

Chanzo: Jambo Leo

MAJAJI WATATU KUAMUA HATMA YA BUNGE LA KATIBA

JOPO la Majaji watatu linatarajia kusikiliza ombi kwa Mahakama itoe amri ya kusimamisha Bunge Maalumu la Katiba lililofunguliwa na Mwandishi wa Habari, Said Kubenea katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Jopo litakalosikiliza ombi hilo linaongozwa na Jaji Augustine Mwarija. Wengine ni Jaji Dk Fauz Twaib na Jaji Aloysius Mujulizi lakini bado halijapangiwa tarehe yakusikilizwa.

Kubenea aliwasilisha ombi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala, akiomba Bunge hilo lisimamishwe hadi Mahakama itakapotoa tafsiri sahihi ya Bunge hilo kuhusu mamlaka iliyonayo na kama ni sahihi kwenda kinyume na Rasimu.

Katika ombi hilo, Kubenea anaiomba Mahakama itoe amri hiyo wakati wakisubiri uamuzi wa Mahakama kuhusu tafsiri sahihi kama Bunge hilo linaweza kwenda kinyume na Rasimu pia tafsiri kuhusu mamlaka ya Bunge hilo.

Aidha anaomba Mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 25(1) na (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi ambacho kinaeleza mamlaka ya Bunge hilo.

Ombi hilo lililowasilishwa chini ya hati ya dharura limeungwa mkono na hati ya kiapo ya Kubenea ambapo anaeleza, Desemba Mosi, mwaka 2011, Bunge la Tanzania lilipitisha mabadiliko ya Katiba na kuanza maandalizi ya kupata Katiba mpya.

Hati hiyo inadai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa ajili ya kusimamia mchakato huo, ambapo Rais alitoa maelekezo kwaTume hiyo kukusanya maoni kwa wananchi kwa ajili ya kuandaa Rasimu ya Katiba mpya.

Kwa mujibu wa hati hiyo, Tume ilianza kutekeleza kazi hiyo kwa kukusanya maoni kwa wananchi kupitia mikutano na njia nyingine ikiwemo Mabaraza ya Katiba katikawilaya zote ambapo wananchi 33,537 walitoa maoni.

Tume iliandaa Rasimu ya pili ya Katiba na Desemba 8, 2013, iliikabidhi kwa Rais ambapo Rais kwa mamlaka yake alielekeza Bunge Maalumu kujadili Rasimu hiyo.

Anadai baada ya kuanza kwa Bungehilo wajumbe walitofautiana kutokana na kuingizwa kwa hoja ambazo hazipo kwenye Rasimu ndipo wajumbe wengine ambao ni Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakatoka bungeni kwa madai Rasimu hiyo haiwezi kufanyiwa marekebisho kama wajumbe walivyokuwa wanadai.

Chanzo: Habari leo

POLISI WAMKAMATA MPIGA RISASI WANAWAKE ARUSHA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas amesema jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa wa matukio ya kuwapiga risasi wanawake jijini Arusha.

Mtu huyo ni Adam Mussa, mwenye umuri wa miaka 30, mkazi wa Majengo Jijini Arusha ambaye amekamatwa na bastola mbili zikiwa na risasi kumi.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda Liberatus Sabas amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti26 mwaka huu, majira ya usiku, nyumbani kwake Majengo Juu.

Kamanda Sabas amesema baada ya kumkamata mtuhumiwa na kumhojiambapo alikiri kuhusika katika matukio yanayoendelea jijini Arusha ya upigaji wanawake risasi na moja kati ya silaha hizo iliibiwa ndani ya gari la mfanyabiashara Seleman Bakari Msuya mkazi wa Sombetini, baada ya watu wasiojulikana kuvunja kioo cha gari na kuichukua.

Mtuhumiwa anatarakiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kumalizika.

Kamanda Sabas ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa siri za mtandao huo uliozuka ghafla mwezo Agosti mwaka huu na kujeruhi na kuua wanawake wenye magari mjini Arusha, ambapo hadi sasa tayari watu nane wanashikiliwa kwa kuhusiana na matukio hayo.

DROO YA LIGI YA MABINGWA ULAYA

Group A: Atlético, Juventus, Olympiacos, Malmö

Group B: Real, Basel, Liverpool, Ludogorets

Group C: Benfica, Zenit, Leverkusen, Monaco

Group D: Arsenal, Dortmund, Galatasaray, Anderlecht

Group E: Bayern, Man City, CSKA, Roma

Group F: Barcelona, PSG, Ajax, APOEL

Group G: Chelsea, Schalke, Sporting, Maribor

Group H: Porto, Shakhtar, Athletic Club, Bate Borisov

WANAMGAMBO KUCHUKULIWA HATUA LIBYA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotoa wito wa kusitisha mapigano nchini Libya haraka iwezekanavyo na kuweka vikwazo dhidi watu wanaohusika na ghasia zinazoendelea nchini humo kati ya makundi yawanamgambo wanaopingana.

Balozi wa Libya katika Umoja wa Mataifa ameliita azimio hilo kama"msingi", lakini ameonya kuwepo kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Orodha ya watakaokabiliwa na vikwazo vya uchumi bado haijaamuliwa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshtushwa na kuongezeka kwa mapigano katika ya makundi ya wanamgambo na vikundi vya kijeshi.

Mapigano ya karibuni yamejikita katika uwanja wa ndege wa kimataifa, Tripoli, ambao kwa sasa unadhibitiwa na wanamgambo kutoka Misrata na miji mingine yakiwa chini ya mwavuli wa "Mapambazuko ya Libya", ikiwa ni pamoja na makundi mengine ya kiislam.

Yameuchukua uwanja huo kutoka mikononi mwa kikundi cha wanamgambo wenye makaazi yao katika mji wa Zintan, licha ya tuhuma za mashambulio ya anga kufanywa na Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu wakililenga kundi lenye uhusiano na makundi ya wanamgambo wa Kiislam.

Pia Libya inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa, kwa viongozi wawili wanaopingana na mabunge ambayo yanaendesha shughuli zao katika sehemu mbili tofauti za nchi, kila bunge likiungwa mkono na makundi ya wanamgambo wenye silaha.

Uzuiaji wa silaha waimarishwa Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja walipitisha azimio ambalo linatishia kuwawekea vikwazo, kama vile utaifishaji wa mali, kuzuia safari dhidi ya viongozi wa makundi ya wanamgambo na wafuasi wao.

Marekani imeishutumu Misri na Muungano wa Falme za Kiarabu kwa kufanya mashambulio ya anga yakilenga vikundi vya wanamgambo vyenye uhusiano na wapiganaji wa Kiislam.

Azimio hilo limesema kuwa vikwazo vitawalenga watu binafsi na makundi yanayohatarisha usalama wa Libya au kupuuza mageuzi ya kisiasa nchini humo.

Pia azimio limeimarisha upigaji marufuku silaha, amri ambayo tayari imewekwa ambapo mtu au kundi anayetaka kuingiza silaha Libya atahitaji idhini ya mauzo yoyote ya silaha au kibali cha kusafirisha silaha kwenda nchini humo.

ARFI ATAMANI UKAWA WARUDI BUNGENI

MBUNGE wa Mpanda Mjini, ambaye ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Said Arfi (Chadema), ameelezea matamanio yake kuona wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurudi bungeni.

Amesema kwa hali inavyokwenda sasa, mapendekezo ya upande mmoja wa chama tawala ndiyo yanayopita na kuongeza: "Tungekuwepo wote ndani ya Bunge hili, lisingewezekana kwa sababu tungepinga kwa nguvu zaidina hata kuhakikisha Bunge haliendelei."

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Arfi alisema kuondoka kwa Ukawa ndani ya Bunge, ni sawa na nyani aliyekabidhiwa shamba la mahindi lisilo na mlinzi.

Alipoulizwa kama wajumbe wa kuteuliwa wa Kundi 201, wangeweza kusaidia kutetea baadhi ya hoja za Ukawa, alisema wajumbe wa kundi hilo wanaangalia maslahi ya makundi yao zaidi na ya wananchi kwa ujumla.

Pamoja na kutokuwepo nguvu ya ajenda za Ukawa, Arfi alikiri kuwepo kwa mabadiliko mazuri yaliyofanyika katika Rasimu ya Pili ya Katiba mpya, yatakayo nufaisha wananchi hasa wakulima, wafugaji na wavuni.

Arfi, ambaye amejitapa hajutii uamuzi wake wa kushiriki Bunge hilo, akipingana na wajumbe wenzake wa Ukawa, alitaja mazuri hayo kuwa ni pamoja na haki za wakulima, wafugaji na wavuvi kumiliki ardhi, haki ya hifadhi ya jamii, haki ya makazi na haki ya afya, chakula, maji safi na salama.

Hata hivyo, Arfi alidai amepanga kwenda mahakamani ili kupata ufafanuzi juu ya alichoita Bunge hilo kuachana na rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba.

Amedai kuwa kinachofanyika sasa ni kuandika rasimu nyingine ili iendane na muundo wa serikali mbili ambao ndio CCM wanaoutaka, kazi ambayo imekuwa rahisi kwa sababu hakuna upinzani wa kutosha kuzuia.

Hata hivyo, tayari Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alishatoa ufafanuzi kuwa msingi wamajadiliano yote tangu Bunge hilo limeanza, ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya na hakuna rasimu nyingine inayojadiliwa isipokuwa hiyo ya Tume."Maana ya rasimu ni andiko ambalo halijajitosheleza … anayekabidhiwa rasimu, anayo hakina mamlaka ya kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu.

"Itakuwa ni jambo la ajabu na lisilona mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka ya kujadili rasimu, ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa," alisema Sitta.

Hata hivyo, Arfi alisema kutokana na mwandishi wa habari Said Kubenea kupitia mwanasheria wake, Peter Kibatala kufungua kesi Mahakama Kuu kutaka mahakama kuzuia kuendelea kwa Bunge la Maalumu la Katiba, anasubiri ushauri wa wanasheria wake kuhusu azma yake ya kufungua kesi hiyo.

Kuhusu Muungano, Arfi alisema kwa sasa wajumbe wanajadili namna ya kuboresha Muungano kwa kupunguza kero zake, ikiwemo kuanzishwa kwa Makamu wa Rais watatu; wa kwanza ambaye atatokana na Mgombea Mwenza, wa pili Rais wa Zanzibar na wa tatu Waziri Mkuu.

Alitaja jambo jingine la kuboresha Muungano kwa kuondoa kero kuwani kuanzishwa kwa mabunge matatu ya Jamhuri, Zanzibar na Tanganyika.

Kwa sasa Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na vikao vya kamati yakupitia rasimu ya Katiba na kesho kutwa kamati hizo zinatarajiwa kukamilisha kazi zao kupisha kamati ya uandishi chini ya Mwenyekiti Andrew Chenge kuandaa maoni ya kamati zote na Septemba 2, mwaka huu majadiliano yataendelea ndani ya Bunge maalumu kwa ajili ya utungaji wa Katiba mpya.

Chanzo: Habari Leo

MIZENGO PINDA AUTAKA URAIS

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameingia rasmi katika mbio za kuwania urais kupitia Chama ChaMapinduzi (CCM), hatua ambayo imebadili mwelekeo wa kinyang'anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.

Gazeti hili limethibitisha kwamba Pinda tayari ameamua kujitosa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ambayo tayari inawaniwa na makada wa chama hicho wasiopungua 15 na baadhi yao wameishatangaza nia zao kwa nyakati tofauti.

Habari kutoka ndani ya CCM zinasema uamuzi wa Pinda kuwania urais mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwakani, umesababisha kiwewe miongoni mwa wagombea na kunakifanya kinyang'anyiro hicho kuchukua sura mpya.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM aliliambia gazeti hili siku chache zilizopita mjini Dodoma kuwa: "Na sisi tumesikia kwamba PM (Waziri Mkuu) amejitosa na kama ni kweli atawasumbua wagombea wengi kutokana na rekodi yake hasa katika uadilifu."

"Yeye (Pinda) ana faida tatu kubwa; kwanza hana kundi katika chama, anaelewana na watu wote, pili nafasi yake ya uwaziri mkuu inampa nafasi ya kufahamika kwa watu wengi na tatu rekodi yake ya uadilifu, hana kashfa za ovyoovyo, labda kama ataharibu dakika hizi zamwisho," alisema kiongozi huyo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania uraia kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wakekatika nafasi hiyo, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wegine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta.

Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba, Asha-Rose Migiro.

Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na aliyewahikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Balozi Ali Karume.


Wasomi

Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema wingi wa wanaojitokeza kutaka kuwania urais ni njia ya kuunda mtandao utakaomwezesha mtu fulani au mmoja kunyakua tiketi hiyo.

"Watu wanapiga kampeni katika harambee kwa njia ya kutengeneza mitandao, kwani ukifika wakati wa chama kumpitisha mgombea, asiposhinda ataibuka na kuwaeleza kuwa mnaoniunga mkono mimi muungeni fulani," alisema.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kujitokeza kwa idadi kubwaya wanaowania nafasi ya urais, kutatoa fursa ya wananchi kutambua udhaifu wa kila mmoja jambo litakalowezesha kupatikana kwa mtu sahihi wa kupeperusha bendera ya chama hicho.

"Wakiwa wengi, kila mmoja atataka kuonyesha umahiri wake na sisi ambao ni wananchi watawaliwa tutaweza kutambua upungufu wa kila mmoja, jambo litakalosaidia kupatikana kwa mtu sahihi," alisema Mbunda


Kambi ya Pinda

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa mjini Dodoma ambako vikao vya Bunge Maalumu vinaendelea umebaini kuwa kambi ya Pinda inaongozwa na Mwenyekitiwa Mamlaka za Mitaa Tanzania (ALAT) ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.

Inadhaniwa kuwa Dk Masaburi atatumia ushawishi wake kwa viongozi wa mamlaka za miji na wilaya zinazoongozwa na wenyeviti wa halmashauri na mameya wa miji, manispaa na majiji kumuunga mkono mgombea huyo ambaye piahivi sasa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziko chini ya ofisi yake.Wiki hii kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini Dodoma likijaribu kutafuta kuungwa mkono na makada viongozi wa CCM ambao walikuwa wakishiriki kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho pamojana wale walioko katika Bunge Maalumu. Habari zinasema mbali na Dodoma, tayari kambi hiyo imeshafanya vikao kadhaa jijini Dares Salaam na Visiwani Zanzibar lengo likiwa ni kutafuta kuungwa mkono na makada wa CCM katika sehemu hizo. Hivi sasa nguvu za Pinda zinaelekezwa katika mikoa mingine nchini kwa lengo hilohilo. Kutokana na kasi ya kambi yake, wafuasi wa baadhi ya wagombea wameanza kufuatilia mwenendo wao kwa lengo la kukusanya ushahidi wa kile wanachokiita 'rafu' zinazochezwa ili kupata ushahidi unaoweza kutumika dhidi ya mgombea huyo wakati mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM utakapoanza mapema mwakani.

Itakumbukwa kwamba makada watano wa chama hicho ambao ni Lowassa, Membe, Makamba, Wassira na Ngeleja wanatumikia adhabu na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema hivi sasa ni mapema mno kusema ni lini mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama hicho utaanza na kwamba wakati mwafaka ukiwadia wananchi watafahamishwa.


Uwezo, udhaifu wake

Hata hivyo wakosoaji wake wanasema Pinda akiwa Waziri Mkuuhana cha kujivunia na kwamba amekuwa mzito kufanya uamuzi mara kadhaa kiasi cha kusababisha baadhi ya mambo muhimu ya nchi kukwama na kwamba kwa maana hiyo hastahili kuwa rais.

"Ni kitu gani ambacho nchi inakikumbuka kuhusu huyu bwana ambacho alikifanya katika miaka yake ya uwaziri mkuu, kama alikuwa kwenye nafasi kubwa kiasi hicho na hakuna alichofanya, atawezaje kumudu madaraka ya mkuu wa nchi?" alihoji mmoja wa makada wakongwe wa CCM.

Waziri mmoja wa sasa (jina tumelihifadhi), alisema Pinda hana uwezo wa kuongoza nchi, kwani wao wakiwa mawaziri ameshindwa kuwasaidia katika kero mbalimbali walizokuwa wakimfikishia kama kiongozi wao.

"Muulize waziri yeyote kuhusu uwezo wa jamaa, kila kukicha tunampelekea mambo tunayokutana nayo, lakini hakuna kinachowezekana kwake, atakwambia subiri leo, subiri keshona hatimaye jambo linaishia hivyohivyo," alisema.

Kwa upande mwingine, watetezi wake wanasema Pinda wanayemnadi ni yule aliyepata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi) kiasi cha kuonekana anafaa kuwa Waziri Mkuu.

Wanasema kushindwa kwake kufanya kazi ipasavyo ni matokeo ya sababu zilizomfanya mtangulizi wake, Lowassa kung'oka katika nafasi yake.


Chanzo: Mwananchi

CLOUDS MEDIA WAADHIBIWA

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), imetoa onyo pamoja na kutoza faini ya takribani Sh milioni 5 kwa kituo cha redio na televisheni cha Clouds, kwa kukiuka kanuni za utangazaji za mwaka 2005.

Wakielezea uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, Kamati ya Maudhui ya mamlaka hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Margaret Munyagi ilisema kuwa ukiukwaji wakanuni hizo ulifanywa kwa nyakati tofauti na vituo hivyo.

Alisema kwa upande wa kituo cha redio cha Clouds, kupitia kipindi chake cha 'Njia Panda' kilichorushwa hewani Juni 15 mwaka huu kati ya saa 8.00 mchana na saa 10.00 jioni kilikuwa na mada iliyohusu safari ya kuzimu ambapo maudhui yake yalijaa simulizi za kufikirika, za kishirikina na kichawi.

Aidha alisema kosa lingine kituo hicho hakikufuata kanuni za Utangazaji(maudhui) za mwaka 2005 zinazowataka kuwasilisha ratiba ya vipindi vyao kwa TCRA ili viidhinishwe na vilevile kuvichapisha katika gazeti kabla ya kurushwa hewani ambapo kipindi cha Njia Panda hakikuwasilishwa kwa ajili ya kuidhinishwa.

Wakati huo huo, kituo cha televisheni cha Clouds kilirusha kipindi cha 'Bibi Bomba' Mei 16 na Juni 6 mwaka huu kati ya saa 3.00 na saa 4.00 usiku ambacho kilikiuka kanuni za Utangazaji (maudhui) za mwaka 2005.

Alisema kipindi hicho kilidhalilisha mabibi hao walioshiriki pamoja na wanawake kwa ujumla kutokana namaswali ya aibu waliyokuwa wakiulizwa na waamuzi wa shindano hilo ambayo ni kinyume na kanuni hizo.

Aidha alisema kituo hicho kinatozwa faini ya Sh milioni moja na kutakiwa kuwasilisha TCRA mwongozo wa kuchuja na kusimamia maudhui yasiyofaa kabla ya kutangazwa.

TCRA imesema kama Kanuni za Utangazaji zitaendelea kukiukwa hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI(HESLB) YATOA MAJINA YA WANAFUNZI AMBAO HAWAJAKAMILISHA BAADHI YA TAARIFA

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB) katika mchakato wa kuhakikisha taarifa za wanafunzi walioomba mikopo katika mwaka wa masomo 2014/2015 wamegundua baadhi ya makosa katika form za waombaji, Hivyo wametoa majina ya wanafunzi wote walioomba mikopo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 ambao hawaja kamilisha baadhi ya taarifa.

Wanafunzi ambao hawaja ambatanisha baadhi ya taarifa kama vyeti vya kuzaliwa, Picha(passport size), nakala za kitambulisho cha mpiga kura au pasi ya kusafiria wanatakiwa kutuma taarifa zao kwa The Executive Director, Higher Education Students' Loans Board, P. O. Box 76068,DAR ES SALAAM. Kwa kuambatanisha na barua ambayo itakuwa na Majina Kamili pamoja na Namba ya mtihani wa kidato cha nne(form four)

Kwa wale ambao hawajaweka sahihi ya muombaji (Applicant signature) na sahih ya mdhaming wanatakiwa kufika makao makuu ya bodi ya mikopo HESLB offices on Plot No. 8, Block No. 46 Sam Nujoma Road, Mwenge- Dar es Salaam wao wenyewe nasi mwakilishi wao.

Ili kuangalia majina ya waombaji ambao taarifa hii inawahusu watembelee link ifuatayo:-

http://www.heslb.go.tz/index.php/application-guidelines/168-call-for-loans-applicants-to-correct-their-loan-applications ??

AMCHANA MWANAE KWA WEMBE SEHEMU YA HAJA KUBWA ILI AWEZE KUJISAIDIA

Mkazi wa Kata ya Kitangiri katika Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, Anastazia Ngilitu, amemchana kwa wembe mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili na wiki mbili baada ya mtoto huyo kuzaliwa bila kuwa na sehemu ya haja kubwa

Aidha, amebainisha kuwa wakati wa kujifungua, mtoto huyo alifanyiwa upasuaji katika Hospitaliya Bugando na kuwa baada ya muda mchache hali hiyo ilijirudia na kuamua kumnasua kwa kumchana bila kujua madhara ya aina yeyote ambayo yangeweza kumpata mtoto wake ambapo kwa sasa afya ya mtoto hairidhishi baada ya kuchanwa.

Wakazi wa eneo hilo wamesema wamekuwa wakimpa msaada mama huyu mara kwa mara, huku wakithibitisha maisha ya mama huyo kuwa ni magumu kutokana nakufukuzwa na mume wake na kupata kipigo.

"Kwa sasa sina fedha za kununulia chakula na fedha za matibabu za kumtibu mwanangu na mimi pia kwamaana titi langu lina uvimbe, naomba wasamaria wema wanisaidie kunichangia kwa chochote walichonacho" Alisema BiAnastazia huku akilia

BOMU LATUPWA NDANI YA HIACE LAUA WATATU

Watu watatu wamekufa, akiwemo mtoto mchanga ambaye mashuhuda wanasema "alitupwa nje," baada ya basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace kurushiwa bomu na watu wasiojulikana huko Kasesema, Kigoma alfajiri ya leo.

Shambulizi hilo limefanyika jirani na Kambi ya Jeshi ya Migongo wilayani Buhigwe majira ya saa 11 alfajiri, wakati basi hilo likivusha abiria toka Kilelema kwenda Kasulu Mjini.

Watu wengine 6 wamejeruhiwa vibaya katika tukio hilo la kutisha, ameeleza kamanda wa polisi (OCD) wa wilaya ya Buhigwe, Samuel Utonga.

Mashuhuda wameiambia Mwananchi kwamba, wakati Hiace hiyo ilipokuwa ikipita eneo la Migongo, alijitokeza mtu mwenye bunduki, akasimama katikati ya barabara akiishinikiza isimame.

Alipoona dereva hapunguzi mwendo, haramia huyo alilipisha hilo basi, ambalo lilosonga mbele umbali mfupi tu kabla ya mtu mwingine kujitokeza toka kusikojulikana na kulirushia bomu.

Taarifa toka wilayani humo leo mchana zinasema hali ya wahanga hao wa bomu "imezidi kuwa mbaya," hivyo imebidi wahamishwe toka hospitali ya Muyama na kupelekwa Kasulu Mjini kwa tiba zaidi.

Chanzo: Mwananchi

MJUMBE WA CCM AJIUNGA 'UKAWA'

Jana ilikuwa kama sinemapale viongozi wa Kamati Namba Moja ya Bunge Maalumu walipojikuta wakibishana na mjumbe wao mbele ya waandishi wa habari, huku siri za mambo ya ndani ya vikao zikianikwa hadharani.

Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu),William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.

Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawiwa Jamii, Dk Seif Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.

Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.

Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya vikao kutotimia.


Sinema ilivyoanza

Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy alipewa fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza kuzungumzia masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisemayeye ni muumini wa serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na wengi kutoka katika chama chake.

Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.

"Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu, naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana," alisema Mwalimu.

Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza kwamba ni muumini wa Tanganyika.

Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia kati na kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele za kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.

Alipopewa nafasi ya kuzungumzia jambo hilo, Keissy alisema: "Jana (juzi), mimi nilihesabu mara mbili nikaona Zanzibar hawajatimia lakini kumbe mmoja nilimfanya akawa mtu wa Tanganyika, kwa hilo nilighafilika, lakini mle ndani mambo siyo mazuri," alisema Keissy.

Kabla hajaendelea Mwalimu alidakia na kumtaka anyamaze kimya kwa kuwa huo haukuwa mkutano wake, ili yeye (Mwalimu) aendelee kueleza mambo yaliyojirindani ya kamati.

"Jamani waandishi si mnaona amekanusha, huu ni mkutano wangu na yeye sitaki azungumze mambo ya mle ndani kwa kuwa msemaji ni mimi au makamu wangu au mtu yeyote atakayeteuliwa na mwenyekiti, sasa tunaendelea," alisema Mwalimu.

Mara baada ya Mwalimu kutoa taarifa ya kamati yake kwa waandishi wa habari na kumaliza kujibu maswali, alinong'ona na Profesa Mbarawa na hapo wakampa nafasi Keissy ili azungumze kwa ufupi mambo yake lakini palepale mbele yao.


Kauli za Keissy

Akitumia fursa hiyo, Keissy alisema: "Kuna mambo yanafanywamle ndani ambayo mimi na wenzangu wengine tunalazimishwa, hatukubaliani nayo likiwamo suala la kuizika Serikali ya Tanganyika wakati wa upande wa pili (Zanzibar)wanapewa nafasi na kunufaika na rasilimali za nchi hii, ndugu zangu huu ni uonevu."

Alisema uonevu huo umekuwa mkubwa kwa wabunge wa Tanzania Bara ukilinganisha na wenzao wa Zanzibar ambao alisema wanakula fedha nyingi za bure ilihali hawafanyi kazi za Tanganyika.

"Ndugu zangu, hapa tusidanganyane, we fikiria watu zaidi ya 50 wanatoka kule Zanzibar na kuja kutuamulia mambo yetu, hii si halali hata kidogo. Haiwezekani mtu wa Zanzibar akaja kuzungumzia masuala ya Nkasi wakati hayajui," alisema.

Alisema kuwa msimamo wake siku zote ni serikali tatu na kwamba hatayumbishwa na vitisho au jambola aina yoyote hata kukiwa na kulazimishwa.

Mbunge huyo alisema kuwa kutakuwa na urahisi wa kuongoza Serikali kama Tanganyika itapewa hadhi yake kuliko ilivyo sasa kwa serikali mbili zinazopigiwa upatu.

Kwa mapendekezo yake alisema ni vyema likawepo Bunge la Tanganyika, Bunge la Zanzibar na kisha miongoni mwa wabunge hao, wachaguliwe wachache kuunda Bunge la Muungano.

Aliendelea kusisitiza kuwa wabunge kutoka Zanzibar wanawanyonya wenzao wa Tanzania Bara kwa kila kitu kauli ambayo ilionekana kumkera Profesa Mbarawa na kuamua kumkatisha asiendelee kuzungumza.

Wakati akiendelea kuzungumza, viongozi hao walimkatisha tena na kumwambia akubali waondoke pamoja kuendelea na vikao vya kamati. Baada ya hapo, Mwalimu na Profesa Mbarawa walinyanyuka na kuanza kuondoka, lakini Keissy alisimama na kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari.

Baada ya kuona anaendelea, Profesa Mbarawa alirudi na kumshika mkono Kessy huku akisema; "Mheshimiwa Keissy twende bwana, maana ukimwacha huku huyu atazungumza mambo mengi."

Wakati akiondoka eneo hilo, Keissy alipaza sauti akiwaambia waandishi wa habari: "Angalieni tunavyodhibitiwa, lakini msimamo ni huo wala sitayumba ngoja tukaendelee lakini mimi ndiyo mtoa habari namba moja."

Msimamo wa serikali tatu ni wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) waliosusia Bunge.

BOKO HARAM WATEKA CHUO CHA POLISI

Kundi la wapiganaji la kiislam la Boko Haram, wamevamia shule moja ya mafunzo ya kipolisi.

Kituo hicho cha mafunzo kilichoko kwenye kitongoji cha Gwoza kiko karibu na mpaka wa nchi ya Cameroon ambacho hufundisha maofisa wa Polisi nchini Nigeria.

Kikundi hicho Boko Haram pia kinasemekana kuudhibiti mji wa jirani na Gwoza uitwao Buni Yadi.

Nalo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch wametoa takwimu ya vifo vilivyosababishwa na kundi hilo kua watu zaidi ya elfu kumi mpaka sasa tangu walipoanzisha harakati za kutaka upande wa kaskazini mwa Nigeria uwe chini ya utawala wa Kiislam.

MAREKANI WAENDELEA KUWASHAMBULIA IS HUKO IRAQ

Majeshi ya Marekani yameendelea kuwashambulia wapiganaji wa Islamic State huko Iraq licha ya vitisho kutoka kwa kundi hilo kuwa watawaua mateka wengine wamarekani iwapo Obama angeendelea kuishambulia himaya hiyo kaskazini mwa Iraq.

Majeshi ya Marekani kwaushirikiano na ndege zisizikuwa na marubani zilifanya mashambulizi 14 usiku wa kuamkia leo.

Mashambulizi kumi na manne ya angani yamefanyika katika eneo karibu na bwawa la Mosul na yalilenga kuwasaidia wanajeshi wa Iraq na wa kikurdi.

Maafisa wajeshi la Marekani wamesema kuwa walifaulu kulipua magari ya kijeshi na vitu vingine vilivyokuwa vikitumiwa na wapiganajiwa IS.

Tarifa kutoka kwa wakurdi zinasema kuwa ndege ambazo hazina rubani zilikuwa angani kuwalinda wanajeshi Wakurdi wakati wapiganaji wa Pesh Merga wakisukumwa katika milima, kusini mashariki mwa bwawa kubwa la Mosul, ambalo lilitwaliwa tena kutoka kwa wapiganaji wa kiislamu wiki hii.

Pentagon imethibitisha kuwa mashambulizi kumi na manne ya angani yalifanywa katika sehemu hiyo kuliko bwawa na kuyalenga magari kadhaaya kijeshi na vitu vingine.

Televisheni ya taifa ya Iraq imesema kuwa ndege hizo za vita za Marekani zilikuwa pia zimetekeleza mashambulizi katika kambi za magaidi mkoanial-Anbar hadi magharibi mwa Baghdad, na zilikuwa zimetoa ulinzi wa angani kwa vikosi vya serikali vilivyokuwa vikielekea kuwakabili waasi wa kisuni.

Awali makao kuu ya Jeshi la Marekani limesema kuwa wanajeshi la kitengo maalum walijaribu kumuokoa mwanahabari James Foley na waamerika wengine walioshikwa mateka nchini Syria.

Habari hii imetolewa baada ya video ya aliyetekwa nyara novemba 2012 nchini Syria kuonyeshwa akiuawa kikatili na wanamgambo wa Kiislamu kutokea jumapili.

Wanamgambo hao walisema mauaji yake ilikuwa kulipiza kisasi dhidi ya Marekani kwa sababu ya kuwashambulia wapiganaji wao hewani Iraq.

Rais wa Marekani Barack Obama alikashifu mauaji hayo na kuwalinganisha wanamgambo hao na ugonjwa wa saratani na kuwa itikadi zao hazikuwa na mwelekeo aliendelea kuwa kusema tendo hilo lilishtua ulimwengu mzimaUmoja wa kitaifa,uingereza na wengine pia wameeleza huzuni yao kutokana na video hiyo.

Mamake Bwana Foley Diane alisema kuwa mwanawe aliaga dunia kwa niaba ya watu wa Syria.

Kamati inayolinda wanahabari ilisema ina wasi wasi kwa wanahabari wote waliozuiliwa na wanamgambo hawa na kusema wanahabari wajiepushe na Syria.

BABA AWACHOMA WANAE MOTO KISA KUANGALIA TV KWA JIRANI

Salum Juma, fundi gereji wilayani Temeke, mkazi wa Mbagala Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam anadaiwa kuwachoma moto mikono watoto wake wawili kwa kutumia tambi za jiko kisa ni kuangalia TV kwa jirani.

Watoto hao, Agustino Said (7), mwanawe wa kufikia na NurdinSaid (5), wa kumzaa mwenyewe, walikutwa na mkasa huo baada ya kwenda kuangalia runinga kwa jirani na kurudi nyumbani saa 5:00 usiku

Kitendo hicho kilifanyika huku mama yao akiwa kwenye biashara zake za kukaanga mihogo.

MWANDISHI WA MAREKANI ACHINJWA NA ISLAMIC STATE

Kikosi cha kiislam cha kijeshi chenye msimamo mkali kimeachilia video inayoonesha mauaji ya mwandishi habari mwenye asili ya Marekani. James Foley alipotea tangu alipokamatwa mateka na kushikiliwa nchini Syria miaka miwili iliyopita na sasa ameuawa.

Ikulu ya Marekani imesema inaifanyia uchunguzi wa kina video hiyo na ikithibitika kwamba mwandishi huyo wa habari ni wa taifa hilo ,serikaliya Marekani itataka ufafanuziwa kina ilikuaje na kwanini James Foley auawe.

Katika mtandao wa kijamii waFacebook familia ya mwandishi huyo iliandika kuwa 'tunajua kwamba wengi wenu mnasubiri uthibitisho ama majibu ya maswali yenu,tafadhalini muwe watulivu mpaka nasi sote tupate taarifa tunazo tamia,na tunaomba muendelee kumbumbuka Foleys na kumwombea kila siku.''

Katika video hiyo iliyobeba ujumbe unaosomeka kua ujumbe kwa Marekani, mwandishi huyo pia alionekana akiwa chini ya ulinzi wa mtu aliyekua amevalia kinyago usoni, askari huyo alikua aku akizungumza ndani ya lafidhi yenye athari za Uingereza, akisema kua kifo cha mwandishi huyo ni matokeo ya mashambulizi ya magurunedi yalowalenga wa Iraq.

MWAFRIKA MWINGINE AUAWA MAREKANI

Mauaji mengine ya raia wa kiafrika yaliyofanywa na polisi katika eneo la St Louis yameongeza hali ya wasiwasi na vurugu katika eneo hilo ambalo kwa takriban siku 11 sasa kumekuwa na vurugu kutokana na mauaji yaliyotokea awali.

Jumanne wiki hii afisa mmoja wa polisi alimpiga risasi na kumuua raia wa kiafrika aliyedaiwa kuwatishia kwa kisu polisi.

Mkuu wa polisi wa St Louis Sam Dotson amesema mauaji hayo ya August 9 ya Michael Brown yameongeza hali ya machafuko katika eneo hilo.

Mwanasheria mkuu wa Marekani Eric Holder anatarajiwa kutembelea eneo la Ferguson jumatano wiki hii ili kujadili taarifa rasmi za uchunguzi wa mauaji hayo.

Mwendesha mashitaka katika kesi ya mauaji ya Michael Brown leo amewasilisha ushahidi dhidi ya afisa anayedaiwa kuhusika katika mauaji ya Michael Brown.

Vurugu zimeendelea katika mji huo huku waandamanaji wanaopinga mauaji hayo wakiwa wamepakaa maziwa usoni kujikinga na mabomu ya machozi kufuatia waandamaji wawili kuathirikana mabomu hayo.

PAPA AMRUHUSU PADRE KUOA

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amekubali kumuondolea sakramenti ya upadri, RaymondMosha wa Jimbo Katoliki la Moshi ikiwa ni miaka 20 tangu padri huyo aombe kuachana nadaraja hilo.

Barua ya uamuzi wa Papa Francis ilisomwa juzi katika parokia na vigango vyote vya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi katika ibada zilizofanyika katika makanisa ya jimbo hilo.

Miongoni mwa parokia ambazo barua hiyo ilisomwa ni Karanga ambako Paroko wake, John Matumaini alitoa tangazo hilo katika ibada zote. Uamuzi huo ambao ni nadra kutolewa na Papa, unamaanisha kuwa sasa padri huyo yuko huru kuoa na kuwa na familia.

Hata hivyo, wakati uamuzi huo ukitangazwa rasmi juzi, tayari Padri Mosha ambaye ni profesawa falsafa na maadili katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha, ana mke na watoto watatu ambao kwa sasa wako vyuo vikuu.

Padri Mosha alisema aliandika barua kuomba kuondolewa daraja hilo mwaka 1994 kabla ya uamuzi kutolewa juzi.

Katika orodha ya mapadre 185 wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi iliyopo katika tovuti ya jimbo hilo, jina la Padri Mosha linaonekana likiwa ni namba 23.

Akizungumzia hatua hiyo, Padri Mosha alisema: "Ninafurahi kufunguliwa kifugo hiki na hii itanifanya niishi kama Mkristo. Kwa vile hawajaniondolea sifa ya kutoa huduma kama vile ibada za mazishi, sakramenti yamwisho na ubatizo, nitaendeleakutoa kwa wahitaji kwa sababu ninaupenda ukristo."

Nashukuru sasa nimekuwa muumini wa kawaida nitaweza kufunga ndoa kanisani kwa kuwa nilikuwa nimefunga ndoa ya kisheria tu kwa DC.

"Kuhusu kwa nini aliamua kuacha upadri, Profesa Mosha alisema ni baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka 20 na akaona ipo haja ya kuwa na familia lakini kanisa lilikuwa haliruhusu."

Sasa kwa kuwa kanisa haliruhusu mapadri kuoa ndiyo maana nikaamua kuandika barua ambayo hata hivyo, imechukua muda mrefu kujibiwa na tayari nina watoto watatu wako chuo kikuu.

MABASI YAGONGANA USO KWA USO, YAUA NA KUJERUHI

Hali ni tete sana eneo la Mkolye, takribani km 4 toka Mjini Sikonge baada ya basi la Sabena toka Mbeya kwenda Mwanza na basi la A.M. toka Tabora kwenda Katavi kugongana uso kwa uso (head on collision).

Dereva wote wa mabasi hayo wamefariki hapo hapo, mmoja akiwa amekatika kichwa!
Nimeshuhudia abiria kadhaa wakiwa wamenasa katika mabasi hayo, baadhi wakiwa wamekatika mikono na miguu!

Abiria wapatao 18 wamefariki mpaka sasa na majeruhi zaidi ya 30 wamepelekwa katika Hospitali ya Mission ya wilayani Sikonge.

Chanzo cha ajari ni dereva wa basi la Sabena kutoka Mbeya kwenda Tabora kutaka kuovertake gari ambapo vumbi lililokuwa limetimka lilifanya ashindwe kuona na kusababisha kukumbana uso kwa uso na basi A.M kutoka Mwanza kuja Katavi

Neno langu: SUMATRA wanatakiwa kusimamia hii njia ya Mwanza-Tabora-Katavi kwa mwendo mabasi yanaoutumia ni wa hovyo na kasi sana. Mungu azilaze mahara pema peponi roho za marehemu na awatie nguvu wafiwa, Awaponye wale majeruhi wote

MWANAE JACKIE CHAN AKAMATWA NA BANGI

Mwanawe muigazaji nyota wa Hollywood Jackie Chan amekamatwa kwa madai alitumia mihadarati.

Jaycee Chan, 31, ambaye mwenyewe ni msanii pamoja na muigizaji kutoka Taiwanese Kai Ko, 23, walikamatwa alhamisi iliyopita kwa mujibu wa taarifa ya polisi mjini Beijing.

Polisi wanasema kuwa wawilihao walipatikana wamevuta bhangi huku mwanawe Chan akikabiliwa na kosa zaidi la kupatikana na dawa hiyo haramu.

Kukamatwa kwa wawili hao kunawadia wakati polisi wamekuwa wakifanya misako ya dharura na kuwakamata wasanii nyota kadhaa.

Gao Hu, 40, aliyeigiza katika filamu ya mwaka wa 2011 Zhang Yimou "The Flowers of War", alikuwa miongoni mwa wasanii wengine wakutajika waliokamatwa mapema mwezi huu.

HU alipatikana ametumia Bhangi pamoja na madawa aina ya methamphetamines.

Operesheni hizi zinafuatia agizo la rais wa China Xi Jinping mwezi juni kwa polisi la kuwataka kuimarisha juhudi za kukabiliana na matumizi ya mihadarati nchini humo.

Duru zinaarifu kuwa Kukamatwa kwa mwanawe msanii maarufu zaidi nchini humo maafisa wa polisi wanajaribu kuwadhibitishia umma kuwa hakuna atakayeepuka mtego wao.

Mwandishi wa BBC mjini Beijing Martin Patience anasema kuwa watu wenye sifa kubwa wanalengwa na maafisa wa polisi kutokana na ushawishi mkubwa walionao miongoni mwa jamii nchini humo.

Hata hivyo kiongozi wa idara ya baraza la umma la Beijing inayopambana na matumizi ya mihadarati bwana Jin Zhihai amekanusha kuwa idara yake imekuwa ikilenga wasanii na waigizaji nyota katika kampeini yao dhidi ya matumizi ya mihadarati.

"ikiwa tutaendelea na kampeini hii dhidi ya matumizi ya mihadarati ninahakika waigizaji wengi nyota watakamatwa ''Juma lililopita miungano 42 inayowakilisha wasanii walitia sahihi maagano ya kukataa kuwasajili wasanii waotumia mihadarati katika maonesho yao.

Kampuni inayomwakilisha bwana Chan iliomba msamaha kwa uma kwa niaba yake.

Kampuni hiyo ya M'Stones International iliahidi kumpeleka hospitalini ilikukomesha matumizi ya dawa hizo.

Babake Jackie Chan hajasema lolote kufikia sasa.

JAJI MAKAME AFARIKI DUNIA

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, amefariki dunia katika Hospitali ya Ami Trauma Centre iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Jaji Makame alifariki jana mchana katika hospitali hiyo, alikokuwa amelazwa ambapo pia Rais Jakaya Kikwete, alimtembelea kumjulia hali. Taratibu za mazishi zilikuwa zikiendelea jana nyumbani kwake Masaki.

Historia fupi iliyopatikana, inaonesha kuwa Jaji Makame alikuwa na Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza, ambapo baada ya kufanya mazoezi na kufanya kazi nchini humo, alirejea nchini Tanzania miaka ya 1960 na kutumikia Taifa mpaka alipofikia cheo cha Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Mbali na cheo hicho, Jaji Makame pia alitumikia Taifa katika nafasi yaMwenyekiti wa NEC na Mwenyekiti wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-ECF).

Wakati akiwa Mwenyekiti wa NEC kwa takribani miaka 19, Jaji Makame aliweka historia ya kusimamia uchaguzi kadhaa wa vyama vingi nchini.

Alistaafu wadhifa huo baada ya mkataba wake kuisha Julai mwaka 2011. Nafasi yake ilichukuliwa na Jaji mstaafu Damian Lubuva.

MAANDAMANO YA ALBINO YASAMBARATISHWA

MAANDAMANO ya walemavu wa ngozi kwenda Kituo cha Polisi Buguruni jijini Dar es Salaam jana, yalisambaratishwa kwa mabomu yamachozi na askari Polisi, baada ya waandamanaji hao kuzingira kituo hicho na kukaidi amri ya kutawanyika.

Waandamanaji hao walitokea Mahakama ya Mwanzo Buguruni kwenda katika kituo hicho, kulalamikia uamuzi wa Mahakama hiyo kutoa dhamana kwa mshitakiwa, Ombeni Swai, mkazi wa Tabata Matumbi, anayedaiwa kutishia kumuua mwenzao.

Kabla ya maandamano hayo, Swai alifikishwa mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Benjamini Mwakasona na kushitakiwa kwa kosa la kutishia kumuua mlemavu wa ngozi, Mwinyisi Issa.

Karani wa mahakama hiyo, Edwin Mwandawanda alidai mahakamani hapo kwamba Swai alitishia kwa maneno kumuua Issa Agosti 16 mwaka huu, saa 7 mchana katika eneo la Buguruni Wilaya ya Ilala.

Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo Hakimu Mwakasona aliahirisha kesihiyo mpaka Septemba 3, mwaka huu na kumwambia mshitakiwa kuwa dhamana ya kesi yake ipo wazi, ambapo alitakiwa kuwa wadhamini wawili waliotakiwa wote kuwa na barua zinazotambulika na serikali za mtaa.

Pamoja na dhamana hiyo kuwa wazi, mshitakiwa hakufanikiwa kutimiza masharti hayo kwa wakati, hivyo akaendelea kushikiliwa wakati akisubiri wadhamini wake kutekeleza masharti hayo.

Vurugu

Kitendo hicho cha mahakama kutangaza dhamana kwa mshitakiwa, kiliamsha hasira kwa walemavu wa ngozi waliokuwa wamekusanyika nje ya mahakama kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, iliyotajwa kwa mara ya kwanza.

Baadhi ya walemavu hao walifanikiwa kupenya mpaka alipokuwepo mshitakiwa na kuanzakumpiga. Kitendo hicho kilifanya Polisi kumpakia haraka kwenye gari na kumpeleka kituoni Buguruni, kwa nia ya kumnusuru.

Hatua hiyo haikuwaridhisha albino hao, ambao walijikusanya na kuandamana kwenda katika Kituo cha Polisi Buguruni, kwa lengo la kutaka kumdhuru mshitakiwa.

Mashuhuda waliozungumza na gazeti hili, walidai kuwa waandamanaji hao walipotakiwa kutawanyika, walikaidi, hatua iliyosababisha Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Walisema baadhi ya albino walidiriki kupanda ndani ya gari la polisi aina ya Land Rover 'Defender' na kuanza kumshambulia kwa mateke na ngumi mshitakiwa, jambo lililowalazimu polisi kuondoka eneo hilo hadi kituo cha polisi Buguruni.

Albino hao pia walifuata kwa nyuma huku wengine walipanda ndani ya gari hilo hadi mahali hapo. Wananchi waliokuwepo nje ya kituo cha polisi, walikumbwa kwa taharuki.

Albino hao waliendelea kumshambulia mshitakiwa huyo hadi walipofika nje ya kituo hicho, huku wakizuiliwa na polisi hao, ambao baadae walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya.

Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marry Nzuki, ambaye alikiri kutokea kwa vuruguhizo. Alisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa Polisi kwa kosa hilo.

"Baada ya kutawanywa pale kituo cha Buguruni, Mkuu wa Kituo aliwaambia waje katika ofisi zangu,lakini hadi hivi sasa sijamuona mtuyeyote wala kiongozi wao kuleta mashitaka yoyote," alisema Kamanda Nzuki.

Dau la Mengi

Wakati vurugu hizo zikitokea, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ametangaza kutoa Sh milioni 10 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa watu walioshiriki kumkata mkono mlemavu wa ngozi, Susan Mungi (35) na kumuua mumewe wilayani Igunga, Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mengi alisema pia IPP itasomesha watotowa mlemavu huyo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwapia na baadhi ya viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Mengi alisema anafanya hivyo kama mwananchi wa kawaida ambaye ameguswa na vitendo hivyo vya kinyama, vinavyofanywa dhidi ya watu hao wenye ulemavu.

Aliomba Polisi kuwasaka wote waliohusika, kuwakamata na kuwapeleka mahakamani haraka.

Alisema albino ni watu kama wengine hivyo vitendo vyovyote vya kinyama dhidi yao lazima vilaaniwe na watu wote.

"Hakuna albino ambaye amependa awe hivyo, hakuna aliyemwomba Mungu ampatie ulemavu huo, hawa ni binadamu kama sisi, jamii na serikali kuendelea kukaa kimya juu ya unyama huu ni jambo linalosikitisha," alisema Mengi.

Mengi alisema waliotumwa kumkata albino huyo wakamatwe. Susan, mkazi wa Kijiji cha Buhelelekati ya Nsimbo wilayani Igunga, alikatwa kiwiko cha mkono wake nawahusika kutoweka nacho.

Katika tukio hilo, mumewe Mapambo Mashili aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.

Mtoto huyo hadi sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo.

Katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa ametangaza dau la Sh 500, 000 kwa mwananchi atakayesaidia kukamatwa kwa watu wanaofanya vitendo hivyo.

Tukio hilo limekuwepo ikiwa ni wiki baada ya mtoto, Upendo Sengerema (15) mkazi wa Kijiji cha Usinge kata ya Uganza wilayani Kaliua mkoani Tabora, kukatwa mkono na watu waliokimbia nao.

Katibu Mkuu Chama cha Albino (TAS), Ziada Nsemo alisema kati yawatanzania milioni 45, Mengi ni mmoja wa watu waliojitokeza hadharani kukemea vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa.

Alisema licha ya polisi kuahidi kuwalinda, wameendelea kuuawa.

Alitoa mwito kwa albino nchini, kujilinda na kukaa karibu na makundi ya watu ili wanapovamiwa iwe rahisi kupata msaada kwa sababu ulinzi kwao ni wa shaka na wanawindwa kila kona.

Chanzo: Habari leo