KANISA LANUSURIKA KUTEKETEA KWA MOTO

KANISA la Tanzania Assemblies of God lililopo Chanika, Dar es Salaam, limenusulika kuungua moto baada ya watu wasiofahamika kutaka kulichoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 8:30 usiku.

Alisema watu wasiofahamika walifika kanisani hapo na kidumu cha mafuta ya petroli pamoja na mpira uliotumika kuingizia mafuta ndani ya kanisa hilo ambapo katika tukio hilo viti 20 vya plastiki vimeteketea kwa moto.

Kamanda Minangi alisema mpaka sasa wamekamata watu wanaowatilia shaka kuhusika na tukio hilo.

Mchungaji wa kanisa hilo, Fidelisi Kalinga, alisema hawana uhasama na majirani zao na wanashirikiana vizuri, ila alikiri kuwapo kwa uhasama wa kiimani na kupokea vitisho vinavyoashiria uvunjifu wa amani.

DAKTARI AKAMATWA AKITAKA KUMTOA MIMBA BINTI

Polisi mkoani Kilimanjaro, imemtia mbaroni daktari mstaafu wa Hospitali ya Serikali ya Mkoa ya Mawenzi kwa tuhuma za kumtoa mimba msichana wa miaka 17.

Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi, ambapo Dk huyo anayedaiwa kuwa na umri wa miaka 50 (jina tunalo), alikamatwa saa 10:45 alasiri katika nyumba ya mjomba wake iliyopo eneo la Kiboriloni mjini hapa akiwakatika harakati za kufanya tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz aliwaambia wanahabari jana kuwa, uchunguzi umebaini msichana aliyekuwa akitolewa mimba ni mhitimu wa Chuo cha Ualimu Masama Suni.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, msichana huyo amelazwa katika Hospitali ya Mawenzi akiendelea kupatiwa matibabu baada ya jaribio hilo la kumtoa mimba kuzimwa na polisi kabla halijakamilika.

Katika tukio kama hilo, daktari mmoja aliwahi kumsahau mwanafunzi aliyekuwa akimtoa mimba na kwenda kunywa pombe na baadaye mwanafunzi huyo alipoteza maisha.

Desemba 20,2012 Polisi lilimtia mbaroni daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama pia.

JK ASEMA TANZANIA HAITOKI, NA HAITOTOKA EAC

RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania imo, itaendelea kuwemo na haina mpango wa kujiondoa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, licha ya vitimbi vinavyofanywa na viongozi wa nchi za Kenya, Uganda na Rwanda. Katika hotuba yake kwa Bunge jana, Rais Kikwete alisema wazi kuwa nchi hizo zimekiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika mambo manne kati ya mambo manane ambayo wameyajadili katika vikao vyao vya utatu.

"Tanzania hatuna mpango wa kutoka katika jumuiya ya Afrika Mashariki, tumo na tutaendelea kuwemo," alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa hatuwezi kujiondoakwani Tanzania haijafanya jambo lolote baya dhidi ya jumuiya hiyo au dhidi ya nchi yoyote mwanachama.


Badala yake Rais Kikwete alisema Tanzania imekuwa mwanachama mwaminifu, mvumilivu na mtiifu kwa jumuiya hiyo ndio maana vitendo vinavyofanywa na viongozi wa nchi tatu wanachama, Uhuru Kenyata (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame (Rwanda),vinazua maswali mengi ambayo hayana majibu.

"Tunajiuliza maswali mengi hadi tunakosa majibu, wanachukia nchi yetu, wanataka kuunda jumuiya yao au wananichukia mimi mwenyewe?"Alihoji Rais Kikwete hasa akielezea mshangao wake kwa viongozi hao kukaa katika vikao vitatu bila kushirikisha viongozi wa Tanzania na Burundi.

Alisema madai ya viongozi hao kwamba huo ushirikiano wa utatu huo ni wa nchi ambazo ziko tayari kuharakisha maendeleo ya Jumuiya hiyo, ni uwongo kwani haiwezekani hawaaliki baadhi ya viongozi wa ndani ya Jumuiya halafu wadai nchi ambazo hazikualikwa hawana utayari.

Rais Kikwete pia alitumia hotuba hiyo kukanusha madai kwamba Tanzania imekuwa kikwazo kuchelewesha maendeleo ya jumuiya hiyo, na akasema maadai hayo hayana ukweli wowote kwani Tanzania inachopigania ni kwa nchi wanachama kuheshimu mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo.

Alisema Tanzania haiwezi kuhangaika kwa kutumia muda na fedha zake katika kuijenga jumuiyahiyo, halafu iwe nchi ya kwanza kuidhoofisha "Haiwezekani tutumie dola za marekani milioni 12 kila mwaka kuchangia jumuiya hii halafu tuidhoofishe."

Kikwete hakumng'unya maneno, aliposema kinachoonekana kuwakera viongozi wa nchi zingine ndani ya Jumuiya hiyo, ni msimamo wa Tanzania katika kupinga kuharakisha kuundwa kwa shirikisho, hasa katika eneo la umiliki wa ardhi, uhamiaji na ajira.


Rais Kikwete alisema anapata taabu kuamini kutofautiaa katika misimamo ya nchi, ndio kuwe chanzo cha nchi hizo tatu kukataa kushirikiana na Tanzania, hata katika mambo ambayo haina mvutano nayo.

Alisisitiza kuwa msimamo wa Tanzania ni kuona jumuiya hiyo inajengwa hatua kwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye mkataba na sio kuruka baadhi ya hatua. "Hatuna tatizo na kuundwa kwa shirikisho, tatizo letu ni kuruka hatua zilizoanishwa.

"Hatua hizo ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na baadaye ndipo kuundwa kwa Shirikisho la Kisiasa ambako, kutafikiwa baada ya kura ya maoni itakayopigwa na wananchi wa nchi wanachama.


Rais alisema Tanzania haikuunga mkono kuharakisha shirikisho kabla ya hatua zingine kutekelezwa, kwa vile inaamini shirikisho hilo la kisiasa ni lazima lijengwe katika msingi imara wa kiuchumi na ndio maana wanaona kuna ulazima wa kuimarisha hizo hatua zingine.

"Kwa msimamo wetu shirikisho ni hatua ya mwisho, huo ndio msimamo wa Watanzania," alisema Rais Kikwete.

Alionya kuwa suala hio likiharakishwa kuna hatari ya jumuiya hiyo kuvunjika kwani mambo yanayozua mvutano siku zote ni ya uchumi na wala sio ya kisiasa.

"Kwa kweli kama hawata badilika sijui mambo yatakuwaje huko mbele? alionya Rais Kikwete na kusisitiza kuwa jumuiya hiyo itakuwa ya makundi kati ya Tanzania na Burundi na kundi lingine litakalohusisha nchi hizo tatu.

Aliongeza kuwa Tanzania haitaki yaliyotokea 1977 yatokee tena na akasisitiza kuwa itaendelea kushiriki katika Jumuiya hiyo na kutekeleza itifaki zote zilizoanishwa kwenye Mkataba.

Alisema Tanzania itahakikisha haidhoofishi Jumuiya wala kuwa chanzo cha kufa kwake.


"Hata kamaikidhoofika au kufa hatutaki Tanzania inyoshewe kidole kuwa ndio chanzo cha kufa kwake. Ndio maana hatutachoka kuzungumza nao, nimeshazungumza na baadhi yao na nitaendelea kuzungumza nao."

Utatu ulivyoanza Nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zimeshafanya vikao vitatu huko Mombasa, Kampala na juzi kimefanyika mjini Kigali Rwanda. Katika vikao hivyo viongozi wa nchiwaliamua mambo manane ya msingi kwa kile walichoita ni kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa EAC.

Mambo hayo ni kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura, ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini, kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, kuanzisha Himaya Moja yaUshuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote.

Mengine ni kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki ambapo wameunda kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho, kuharakisha uanzishwaji wa hati ya pamoja ya kuishi ndai ya nchi hizo tatu (visa) ya pamoja ya utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kuwa hati yakusafiria katika nchi zao; na kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.


Rais Kikwete alisema orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya.

Alisema mambo manne kati ya hayo manane, hayamo kwenye mashartiya kutokufanyika bila ya kuihusishaau kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mambo hayo ni uzalishaji na usambazaji wa umeme, ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda, ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda na ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura ambalo pia alisema Tanzania haina tatizo nalo kwa vile sio mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais alisema katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hana maneno nayo.

Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati yakusafiria na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani waliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari waanze.

Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha na kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki, Rais Kikwete alisema nchi hizo zimekiuka uamuzi wa pamoja. Hata hivyo RaisKikwete alikiri kushangazwa na kuuliza: "Kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi.

Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na wao baadae Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla."


-Habari leo

AUWAWA KWA KUKATWA NA SHOKA KICHWANI MKOANI KATAVI

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ruswetura Mahongo (40) mkazi wa Kijiji Kambuzi Halt Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi ameuwawa kwa kukatwa na shoka kichwani na shingoni na sehemu ya bega la kulia na watu wawili waliokuwa wanafanya kazi ya kibarua nyumbani kwake ya kujenga uzio wa zizi la ng'ombe.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo la mauwaji ya kutisha lilitokea hapo jana majira ya saa kumi na moja jioni nyumbani kwa marehemu.

Alisema siku moja kabla ya mauwaji hayo alifika mtu mmoja nyumbani kwa marehemu na kuomba kibarua cha kutengeneza zizi la Ng'ombe na ndipo alipokubaliwa na kuanza kazi ambayo hakuimaliza siku hiyo.

Kidavashari alieleza siku iliyofuata kibarua huyo alifika nyumbani kwa marehemu akiwa na kijana mwingine ambae alionekana kumsaidia kazi hiyo hata marehemu alielewa hivyo.

Alisema ilipofika majira ya saa kumi na moja jioni marehemu akiwa amelala kwenye jamvi pembeni ya nyumba yake mke wake mdogo aitwaye Tatu Shiranga alimuaga marehemu kuwa anakwenda mtoni kuteka maji na alimuacha marehemu akiwa na vibarua hao pamoja na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka saba.

Baada ya mke wake kuondoka vibarua hao walimfuata mahari alipokuwa amelala marehemu na kuanza kumkatakata kwa shoka kichwani shingoni na kwenye bega hali ambayo ilipelekea mwanae huyo mdogo akimbie mbio na kujificha kichakani huku akiwa akishuhudia wanavyo mshambulia baba yake na alishindwa kuomba msaada kwa majirani kutokana na wao kuishi mbali na majirani.

Kamanda Kidavashari alieleza mke wa huyo wa marehemu alirejea kutoka mtoni kuteka maji ndipo alipokaribia kufika kwake mtoto wake alimkimbilia na kumweleza kuwa wale watu wawili waliokuwa wakifanya kazi ya kibarua wamemkata baba yake kwa shoka na kisha wamekimbilia porini.

Alisema mke wa marehemu alilazimika kwenda kuangalia pale ambapo alikuwa amemuacha mumewe amelala na ndipo alipomkuta akiwa amegalagala chini huku mwili wake ukiwa na majeraha makubwa na damu zikiwa zimetapakaa huku akiwa amefariki dunia.

Alifafanua kuwa uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi baada ya kumhoji mke mdogo wa marehemu na ndugu zake kifo hicho kimesababishwa na sababu mbambali zilizotokana na tabia ya ukorofi na ubabe wa marehemu kwa majirani na ndugu zake.

Marehemu wakati akiishi katika Kijiji cha Mtowisa mkoa wa Rukwa hapo mwaka 2012 aliwahi kuvamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa mapanga na kuponea chupuchupu na nyumba yake kuchomwa moto na ndipo baada ya hapo marehemu aliamua huhamia katika kijiji hicho mkoani Katavi.

Kamanda Kidavashari alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na jitihada za kuwatafuta zinaendelea kuwasaka watu waliohusika katika mauwaji ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

SULTANI MAKENGA NA WAASI WENGINE WA M23 WAJISALIMISHA UGANDA

Maafisa wa Serikali ya Uganda wanasema kuwa kamanda wa kijeshi wa wapiganaji walioshindwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, M23, amejisalimisha kwa utawala wa Uganda.

Ripoti kutoka Uganda zinasema kuwa mamia ya wapiganaji wamejisalimisha pamoja na kiongozi wao, Sultani Makenga.

Wapiganaji hao wamejisalimisha katika eneo la hifadhi ya Wanyama ya Pori ya Mgahinga, kwenye mpaka wa Uganda na DRC.

Mnamo Jumanne M23 walisema kuwa wamesitisha maasi yao ya miezi 20 Mashariki mwa Congo, baada ya kutimuliwa katika ngome zao Mashariki mwa Congo na wanajeshi wa Serikali wakishirikiana na askari wa kudumisha amani wa Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo serikali za Uganda na DRC hazijaweza kuthibitsha madai haya.

Mapema wiki hii, M23 ilisema kuwa inamaliza uasi wake wa miezi kumi na tisa masaa chache baada ya majeshi ya serikali kudai ushindi dhidi ya waasi hao.

Ripoti zinasema kuwa Sultani Makenga na waasi wengine 1,700, wamesalimisha silaha zao na wanazuiliwa na jeshi la Uganda katika kambi ya jeshi ya Mgahinga, karibu na mpaka na DRC.

Mapema wiki hii, maafisa wa DRC walisemaMakenga alitoroka na kuingia Uganda au Rwanda.

Uganda imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya waasi na serikali ya DRC , ingawa hakuna mkataba wa amani umefikiwa.

AU YAIKOSOA UN

Muungano wa Afrika AU umekosoa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kwa kupuuza sauti za Waafrika katika maamuzi yake.

Mkurugenzi wa Baraza la Amani na Usalama la AU El Ghasim Wane anasema wakati mwingi, baraza la usalama hutoa maamuzi bila kuzingatia maoni ya Muungano huo.

Wane ameonya kuwa huenda mapendekezo ya baraza hili yakapuuzwa, iwapo hali itaendelea kama ilivyo.

Wane alikuwa akizungumza kwenye mkutano uliandaliwa kuangazia suala la ufadhili wa mipango ya usalama na amani barani Afrika, lakini suala tata la uhusiano wa AU na baraza la Usalama la umoja wa mataifa, lilijitokeza.

Mkurugenzi wa baraza la amani na usalamala AU El Ghasim Wane, alisema wakati umefika kwa baraza la usalama la umoja wa Mataifa kusikiza kwa makini sauti ya Afrika.

Tetesi hizo zinajiri huku baadhi ya wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa wakiripotiwa kupuuza ombi la Umoja wa Afrika la kutaka kesi inayomkabili rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, kusimamishwa kwa muda.

Hata hivyo balozi wa Uingereza katika AU Greg Dorey alisema suala muhimu kuhakikisha kuwa uhusiano wa Umoja wa mataifa na AU unaimarishwa.

Huku akitaka muungano huo kuwa katika mstari wa mbele kutatua baadhi ya changamoto zinazokabili bara hili.

Walikuwa wakizungumza katika mkutano wa kujadili jinsi wafadhili wa kimataifa wanavyoweza kuboresha juhudi za AU kukabiliana na changamoto za kiusalama.

Katika mkutano huo, AU ilikiri kuwa inaweza kufanya vyema zaidi katika kukabiliana na vita kama vile nchini Mali nakatika Jamhuri ya Afrika ya kati.

WAFUGAJI NA WAKULIMA WAUWANA HUKO MVOMERO

MAPIGANO makali yakihusisha silaha za kisasa na jadi yamezuka kati ya wanakijiji wa Hembeti na wafugaji jamii ya Kimasai wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro na kusababisha vifo vya watu saba huku wengine 55 wakijeruhiwa vibaya.

Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, taarifa zilizolifikia gazeti hilijana jioni zilisema kuwa Kamanda wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Makao Makuu alilazimika kufika eneo hilo akiwa na kikosi cha askari kujaribu kutuliza fujo hizo licha ya awali jeshi hilo kudaiwa kutoonyesha ushirikiano.

Awali, kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Hembeti, Juma Malaja na Ofisa Mtendaji Kata, Charles Chikuni, waliokufa walikuwa wawili; Yusuph Hamad (30) mkazi wa Mkindo aliyefariki akipata matibabukatika Hospitali ya Bwagala-Turiani na mfugaji ambaye jina lake halikupatikana mara moja.

Majeruhi waliokuwa wametambuliwa ni Hamiss Hussen, Athuman Mtaalam, Kibuyo Nasoro, Mveda William, Francis Laulent na Juma Adam wakazi wa Mkindo, Muya Paulo (Hembeti), Francis William (Dihombo) na Yusuph Hamad aliyefariki akihudumiwa.

Lakini baadaye jioni, hali ilibadilika na watu watano wengine zaidi kuuawa kwa kuchinjwa huku majeruhi nao wakiongezeka kutoka 28 wa awali na kufikia 55.

Iilielezwa kuwa miili hiyo mitano ilihifadhiwa katika kituo cha afya Mvomero huku majeruhi 27 wapya nao wakapatiwa matibabu hapo. Kwamba waliouawa ni wanakijiji wanne na wafugaji wa Kimasai watatu.

Mapema, baadhi ya mashuhuda waliopiga kambi katika ofisi za tarafa na Kituo Kidogo cha Polisi Mvomero na familia zao kwa hofu ya mapigano hayo, walisema vurugu hizo zinachangiwa na rushwakukithiri kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya tarafa, wilaya na mkoa na kupuuza mawazo na mipango ya wananchi juu ya ulinzi wao na mali zao.

Zainabu Joseph na Seleman Williamambao wamelazwa hospitali ya Bwagala, walisema tukio hilo lilianza juzi saa 3:00 asubuhi katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji na Kata ya Hembeti wakati wafugaji hao wakiwa na silaha za kisasa zaidi ya saba kutaka kuwachukua kwa nguvu ng'ombe kwa kupiga risasi hovyo.

Walisema kuwa ng'ombe hao wapatao 300 walikamatwa jioni ya Oktoba 4 mwaka huu, wakiwa wameharibu chanzo cha maji Mto Dimamba, kingio la maji yanayotumika kwenye vijiji vya katahiyo na shamba la mahindi la mtu mmoja ambaye hakufahamika jina lake.

Waliongeza kuwa asubuhi ya Oktoba5, wafugaji hao walimwagiza mmojawao kuja kufanya mazungumzo ya suluhu, lakini akiwa kikaoni na viongozi wa kijiji na kata, aliwasiliana na wenzie kwa ujumbe mfupi wa simu, ambao walifika eneo hilo wakiwa na silaha hizo za kisasa.

"Tukiwa tunalinda wale ng'ombe, ghafla walikuja vijana wa Kimorani zaidi ya 15 wakiongozwa na Kafuna Kandulu na silaha za kijeshi kama saba, wakaanza kupachika magazini kwenye bunduki zao na kufyatua risasi nyingi hovyo zilizojeruhi baadhi ya watu na mimi," alisema William.

William ambaye amejeruhiwa kisogoni, shingoni, mkononi kushoto na tumboni ilikokwama risasi, alisema baada ya milio ile ya bunduki, wanakijiji walianza kutoka majumbani wakiwa na silaha za jadi zikiwemo pinde na mishale kisha kukusanyika katika eneo hilo.

Kufuatia hali hiyo, Wamasai hao walianza kuwalenga na kuwapiga risasi sehemu mbalimbali za miili yao, huku wanakijiji wakijibu kwa kuwarushia mishale iliyowasambaratisha wafugaji hao na kuanza kukimbilia porini huku wakiwarushia risasi.

Wakihusisha mgogoro huo na iliyopita, ukiwemo uliosababisha kufungwa barabara eneo la Dihombo, viongozi hao; Malaja na Chikuni kwa nyakati tofauti, walionyesha kusikitishwa na vyombo vya dola kuchelewa kuimarisha ulinzi eneo la tukio hadikufikia maafa hayo.

"Unajua wananchi walifanya kazi nzuri na kubwa sana, lakini wamekosa msaada kutoka vyombo vya dola, kwani baada ya taarifa ya kukamatwa ng'ombe wale, binafsi niliomba msaada wa nguvu ya ulinzikwa OCD na Mkuu wa Wilaya, lakini mpaka sasa hakuna hata polisi," alisema Malaja.

Kuhusu hali ya usalama katika vijiji vya kata hiyo, walisema mapigano hayo yamesababisha taharuki kubwa katika vijiji vya Hembeti, Msufini, Kwampepo, Dihombo na Mkindo ambako watu wameyakimbia makazi yao na kwenda kusikojulikana huku wengine kujihifadhi katika ofisi ya tarafa na kituo cha polisi Mvomero.

Kwa mujibu wa Dk. Mashaka Issa wahospitali ya Bwagala, hadi jana walikuwa na taarifa ya kifo cha Yusuph Hamadi (30) na juzi walipokelewa majeruhi wanane huku wengine 15 wakipokelewa jana mchana.

Alisema kuwa majeraha waliyonayoni ya kupigwa risasi na kukatwa na vitu vyenye ncha kali kama mapanga au sime.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Anthon Mtakana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustn Shilogile hawakupatikana kutoa ufafanuzi wa tukio hilo kutokana na simu zao kutokuwa hewani.


Chanzo: Tanzania daima

TANZANIA YAENDELEA KUCHANGIA ASKARI AFRIKA

TANZANIA ni miongoni mwa nchi tano za Afrika, zilizojitolea kutoa askari wa kuunda Kikosi cha Kukabiliana na Migogoro ya Kijeshi Haraka na Mahali Popote Barani Afrika (ACIRC), kitakachoundwa kwa mujibu wa uamuzi wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana kwavyombo vya habari, ilieleza kuwa Tanzania itatoa kikosi kimoja; na nchi nyingine zilizokubali kuchangia askari ama polisi katika kikosi hicho,ni Afrika Kusini, Uganda, Algeria na Chad.

Nchi hizo zilijitokeza kushiriki katikakikosi hicho wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Majeshi wa nchi hizo, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Uamuzi wa mkutano huo uliidhinishwa na kukubaliwa na wakuu wa nchi akiwamo Rais Jakaya Kikwete. Wakuu hao walikutana Jumanne iliyopita.

"Uamuzi wa kuanzisha kikosi hicho ulitolewa na wakuu wa nchi wanachama wa AU waliokutana katika kikao chao cha 22 cha kawaida Mei, mwaka huu, mjini Addis Ababa.Kikosi hicho kitakuwa cha muda wakati Afrika inaendelea na maandalizi yake ya kuunda Jeshi la Kudumu la Afrika (ASF) na lenye uwezo wa kukabiliana na migogoro haraka na popote.

Jeshi hili litakuwa na uwezo wa kuingia nchi yoyote, chini ya AU, na hivyo wakati mwingine litatumika kutuliza migogoro katika nchi yoyote ya Afrika hata kama nchi husika haijaomba msaada wa jeshi hilo.

Jeshi hilo litakalofanya kazi yake chini ya Mfumo wa Amani na Usalama Afrika, litawezesha AU kuwa na jeshi la askari na polisi wenye uwezo na nguvu kukabiliana na mizozo ya kijeshi barani Afrika na vifaa vyake vitatolewa nchi wanachama wa Umoja huo, ambao watakuwa tayari kushiriki katika mpango huo.

YASSER ARAFAT RIPORT YADAI HUENDA ALIUWAWA KWA SUMU KALI

Aliyekuwa kiongozi wa Palestina Yasser Arafat huenda aliuawa kwa sumu kali ya Polinium.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya kisayansi iliyofanywa na wanasayansi nchini Uswizi ambayo shirika la bahari la Al Jazeera limeweza kupata.

Hata hivyo ripoti za awali kulingana na rekodi za kimatatibu zake hayati Arafat zinasema kuwa alifariki kutokana na kiharusi , kilichosababishwa na ugonjwa wadamu.

Lakini mwili wake ulifukuliwa mwaka jana kwa uchunguzi zaidi kutokana na madai kuwa Arafat aliuawa.

Ripoti hiyo ya wanasayansi kutoka Uswizi, inasema kuwa mwili wa Arafat ulionyesha dalili za kuwa na kiwango kikubwa cha sumu ya Polonium, na hivyo kuunga mkono dhana ya kuuawa kwake kwa sumu.

Wapelestina wengi wameamini kwa miaka mingi kuwa Israel ndio ilimuua Aarafat kwasumu. Wengine wanadai kuwa alifariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi au Saratani.

Israel imekuwa ikikana madai ya kuhusika na mauaji ya hayati Arafat.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Israel, amesema kuwa uchunguzi uliofanywa na wanasayansi wa Uswizi ni kama mchezo wa kuigiza tu.

Wanasayansi hao walifanyia uchunguzi wa kina nyaraka za kimatibabu za Arafat, wakachunguza mabakai yake pamoja na vitu alivyokwenda navyo hospitalini mjini Paris kutafuta matibabu alipofariki mwaka 2004.

Walifanyia uchunguzi mifupa yake pamoja na mchanga katika sehemu alikozikwa Arafat.

Wanasayansi hao walisema kuwa matokeo ya utafiti wao yanawiana na madai ya Arafat kuuawa kwa sumu aina ya Polonium-210.

JK MGENI RASMI ZIARA YA KOMBE LA DUNIA

Kombe halisi la Dunia la Shirikisho la Soka la Dunia(FIFA) litawasili nchini Novemba 29 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika nchi 88 duniani kote.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutangaza ujio wa kombe hilo, Meneja Mkazi wa Coca-Cola Tanzania inayodhamini ziara hiyo, Yebeltal Getachew alisema, Novemba 30 maelfu ya mashabiki wa soka watapata fursa ya kulishuhudia kombe hilo katika tukio litakaofanyika kwenye Uwanjawa Taifa, Dar es Salaam.

Getachew alisema,mgeni rasmi wakati wa ziara ya kombe hilo hapanchini atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

"Wito wangu kwa mashabiki wa soka hususani wa Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi wakati wa ujiowa kombe hilo hasa kutambua kwamba hii ni fursa adimu,"alisemaGetachew na kuongeza:

"Mashabiki watapata fursa ya kupiga picha, kutazama video zinazoonyesha matukio mbalimbaliya kihistoria ya Kombe la Dunia la FIFA na kufurahia burudani za kusisimua.

"Alisema, ujio wa kombe hilo kwa mwaka huu 2013, umezingatia mafanikio ya ziara zingine za Kombe Halisi la FIFA zilizowahi kufanyika mwaka 2006 na 2009.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Michezo, Leonard Thadeo alisema, ziara hiyo itasaidia kuitangaza Tanzania katika medani ya kimataifa.

"Mkumbuke kwamba ujio wa Kombe la Dunia hapa nchini utaambata na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa hivyo ni wazi sisi kama nchi tutapata nafasi ya kujitangaza kimataifa,"alisema Thadeo.

SERIKALI YASEMA HAIJAFUTA ZERO

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema Serikali haijafuta daraja sifuri katika matokeo ya mitihani taifa ya shule za sekondari na kwamba ilichokifanya ni kuondoa mrundikano wa madaraja.

Mulugo aliyasema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).

Magige alitaka kufahamu kama kushusha madaraja ni suluhisho la kuwaokoa vijana waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.

Mapema katika swali lake la msingi,Magige, alitaka kufahamu kama Serikali ina mkakati wa kuanzisha mpango maalumu hasa wa ufundi kwa wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.

Akijibu swali hilo, Mulugo alisema hawajashusha madaraja wala kuweka viwango tofauti na ilivyokuwa awali. "Tumeongeza madaraja ili kuwatambua watoto, kulikuwa na mrundikano katika daraja moja. Serikali haijafuta division ziro na wala hakuna division V, ipo divisionI, II,III, IV na ziro kama kawaida," alisema.

Alisema uamuzi wa kushusha madaraja, hauna lengo la kuwaokoawanafunzi wanaofanya vibaya na badala yake, unalenga katika kuondoa mrundikano wa alama katika daraja moja.

Alitoa mfano wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kuwa lilikuwa linapanga daraja F kuanzia alama 0 hadi 34.

Alisema kulikuwa hakuna ufuatiliajiwa maendeleo ya mwanafunzi kama kanuni inavyosema kuwa lazima kuwe na ufuatiliaji wa asilimia 50 kwa 50.

Alisema kanuni hiyo inataka kutunzwa kwa alama 50 katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi na katika mtihani ya kumaliza shule asilimia 50.

Alisema wameanza kuyaweka madaraja kwa kutofautiana kwa alama 10 kila daraja.

Alisema bado daraja la ufaulu litaendelea kuwa 40 ama alama C.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kujibu swali hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliiagiza Serikali kupeleka bungeni kauli ya waziri kuhusiana na suala hilo.

"Naibu Waziri nenda mtuletee kauliya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kupata majibu yanayoridhisha," alisemaKuhusu wanafunzi waliofanya vibaya mwaka jana katika mitihani yao, Mulugo alisema Serikali haitaanzisha mpango maalumu wa ufundi kwa vijana hao.

Alisema badala yake, Serikali inawashauri wazazi kuwashawishi watoto kurudia mtihani wa kidato cha nne.Kwa mujibu wa Mulugo, kwa mwakahuu, jumla ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea wamejisajili kufanya mtihani wa kidato hicho.

VIONGOZI WA SADC WAFIKIA MAKUBALIANO

Viongozi wa mataifa ya kusini mwa afrika SADC na wenzao wa mataifa ya maziwa makuu wamekubaliana kuhusu maswala kumi na moja ambayo yalikuwa yakijadiliwa katika mkutano wa Kampala kati ya waasi wa M23 na serikali ya DRC.

Maamuzi hayo yaliyotokana na mkutano wa viongozi hao mjini Pretoria Afrika Kusini, yamesema kuwa wale wote walioshiriki katika mzozo huo wataingia katika makubaliano kwa masharti kwamba waasi wa M23 wasitishe mashambulizi.

Na baada ya kutanga kumaliza uasi wao, ina maana kwamba M23 wameafikia moja ya masharti ya kutangaza rasmi kwamba watafuata njia za kisiasa kuafikia malengo yao.

Kundi la M23 limekuwa likishambuliwa na vikosi vya umoja wa mataifa ambavyo vimewafurusha wapiganaji hao kutoka ngome yao ya mwisho mashariki mwa Congo.Hata hivyo Rais wa Rwanda Paul Kagame hakuhudhuria kikao hicho.

Kagame ni jirani mkuu wa DRC Congo na amekuwa akituhumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ingawa daima amekuwa akikana madai hayo.

WAASI WA M23 WASACHARAZWA NA KUWEKA SIRAHA CHINI

Waasi wa M23 katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametangaza kumaliza uasi wao ndani ya nchi hiyo muda mfupi baada ya kupigwa katika ngome yao ya mwisho na majeshi ya serikali ya Congo yakishirikiana na kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kilichopewa uwezo wa kupigana na waasi hao.

Katika taarifa walioitoa waasi hao wamesema badala ya kufanya uasi sasa wataendesha harakati zao kutumia njia ya kisiasa.

Muda mfupi uliopita Kiongozi wa waasi hao Bertrand Bisimwa ametangaza kuwaamuru mkuu wa wapiganaji wa M23 na makamanda wa vikosi vyote muhimu wa kundi hilo kuwaandaa wapiganaji wao kusalimisha silaha, kutawanyika kuondoka katika eneo la mapigano na kukubaliana namatakwa yatakayowekwa na serikali ya Congo.

Awali Msemaji wa Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Lambert Mende aliambia BBC kuwa majeshi ya nchi yameishambulia ngome ya mwisho ya waasi na wamekimbia na wengine huenda wakawa wamejisalimisha.

Majeshi ya serikali ya Kongo yakishirikana na kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kilichopewa uwezo wa kupambana na waasi hao walianza mapambano dhidi ya M23 Octoba mwaka huu na kufanikiwa kuwaondoa katika eneo la Bunagana kwenye mpaka wa Uganda ambayo ni ngome yao muhimu.

AMUUWA MJUKUU WAKE KWA KUMPIGA NA FIMBO KICHWANI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linamshikila Zenobi Lusale (65) Mkazi wa Kijiji cha Sibwesa Tarafa ya Karema Wilaya ya Mpanda kwa tuhuma za kumuuwa mjukuu wake kwa kumpiga na fimbo kichwani.

Baada ya kumtuhumu kumwibia debe moja la mahindi Kwa mujibu wa Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi Joseph Shilinde tukio hilo lilitokea majira ya saa kumi na moja jioni katika kitongoji cha senta Magogo Kijiji cha Simbwesa Tarafa ya Karema Wilayani hapa.

Kaimu kamanda Joseph Shilinde alimtaja aliyeuwawa kwa kupigwa na fimbo kichwani na babu yake kuwa ni Stansilaus Joseph (15) Mkazi wa kijiji hicho.

Siku hiyo ya tukio mtuhumiwa Zenobi alikwenda kwa jirani kunywa pombe ya kienyeji aina ya komoni mida ya mchana na kisha aliporejea nyumbani kwake aliko kuwa akiishi na mjuu kuu wake huyo na ndipo alipo mwita kwa lengo la maongezi.

Marehemu aliitika wito huo wa Babu yake kwa kujua wanataka kufanya mazungumzo kama ambavyo wamekuwa wakifanya yeye na Babu yake mara kwa mara.

Kaimu Kamanda alieleza kuwa ndipo mtuhumiwa alipoanza kumshutumu marehemu mjukuu wake kuwa kuna mahindi debe moja yameibiwa ndani na yeye marehemu ndiye aliyeiba mahindi hayo.

Marehemu baada ya kuambiwa tuhuma hizo alimkatalia katakata Babu yake kuwa yeye haja iba mahindi hayo labda aliuza mwenyewe na amesahau kama alimuuzia mtu kwani yeye hana tabia ya wizi.

Mtuhumiwa baada ya kujibiwa hivyo na marehemu alianza kumshambulia kwa fimbo kichwani huku mjukuu wake huyo akipiga mayowe na ya kuomba msaada na huku akimsihi babu yake asiendelee kumpiga lakini hakufanya hivyo aliendelea kumpa kichapo tuu.

Majirani walifika katika eneo hilo na kumkuta mtuhumiwa akiwa ameshika fimbo hiyo aliyotumia huku marehemu akiwa amegalagala chini na huku akiwa ameishafariki dunia kutokana na kipigo hicho na majirani hao walimkamata mtuhumiwa na kumweka chini ya ulinzi.

Polisi walifika kwenye eneo hilo na kumkuta mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi wa wanakijiji hicho na ndipo walipomchukua hadi katika kituo cha polisi cha Mpanda Mjini.

Shilinde alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospital ya Wilaya hii na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara uchunguziwa tukio hili utakapo kuwa umekamilika.


Chanzo:Katavi Yetu Blog

KIZIMBANI KWA KUKOJOLEA QURAN

Mtu mmoja Mkazi wa Nsemulwa Kichangani mjini Mpanda Mkoa wa Katavi Jafeti Nobeti (15) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mfawidhi mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Chiganga Ntengwe kwa tuhuma za kukojolea Quran Tukufu.

Mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo majira ya saa tano asubuhi katika eneo la msiki wa Kichangani uliopo katika mtaa wa Nsemlwa mjini hapa.

Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa wa Katavi Mwandolomi aliileza Mahakama kuwa siku hiyo ya tukio mtuhumiwa alikojolea Quran hiyo ambayo ilikuwa imewekwa na watoto wa kisramu ambao walikuwa wakisoma madrasa iliyoko katika msikiti huo.

Ilielezwa wakati watoto wa madrasa wakiendelea na mchezo wa mpira wa miguu wakati wa kipindi cha mapumziko ndipo mtuhumiwa Jafeti alipofika kwenye eneo hilo akitokea kwao ambapo ni jirani na msikiti huo.

Watoto wa Madrasa wakati wakiendelea na mchezo wa mpira ndipo walipo mwona mtuhumiwa akiwa anakojolea Quran hiyo hari ambayo iliwashitua na kumfuata mtuhumiwa na kuanza kumshambulia kwa kipigo.

Mtuhumiwa aliendelea kupokea kipigo hadi hapo alipokuja kuokolewa na mwalimu wa Madrasa hiyo Ustadh Khalfan Juma na Shekhe wa mtaa Shekhe Yusuph Mkumba ambao walilazimika kumuhifadhi kwenye nyumba ya mwalimu wa madrasa hiyo na baada ya hali kuwa tulivu walimpeleka kwenye nyumba ya mwalimu huyo na kisha hali ilipokuwa shwari walimpeleka kwenye kituo cha polisi cha mpanda mjini.

Mtuhumiwa baada ya kusomewa mashtaka alikiri kutenda kosa hilo lakini alieleza kuwa hakufanya kitendo hicho kwa maksudi bali wakati alipokua akikojolea hakujua kama ni Quran alidhani kuwa ni kashala kuhifadhia kanda za video hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya mpanda Chiganga Ntengwa baada ya mtuhumiwa kusomewa mashtaka na kukirikutenda kosa hilo bila kukusudia aliahirisha kesi hiyo hadi hapo Nov 14 hata hivyo mtuhumiwa aliweza kupata dhamana baada ya kutimiza masharti ambapo alitakiwa adhaminiwe na mtu mmoja kwa dhamana ya shilingi milioni moja na nusu kwani hakimu Chiganga kutokana na umri wa mtuhumiwa kuwa mdogo isingekuwa busara kwa mtuhumiwa kupelekwa mahabusu.


Chanzo: Katavi Yetu Blog

SHEHENA YA PEMBE ZA NDOVU YAKAMATWA

Siku moja baada ya wabunge kuwataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, pembe 706 za ndovu zimekamatwa jijini Dar es Salaam.

Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi za wanyama pori mbalimbali hapa nchini.

Tukio hilo lililotokea jana jioni katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni, liliongozwa na Waziri Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.

Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung.

Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba hiyo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza nchini vitunguu swaumu kutoka China na kusafirisha nje ya nchi makombe yanayopatikana baharini.

Alipoingia ndani ya nyumba hiyo, Kagasheki ambaye aliambatana na askari polisi na baadhi ya maofisa usalama alishuhudia shehena kubwa ya pembe za ndovu ikiwa imehifadhiwa kwenye viroba vyenye uzito wa kilo 50.

Mbali ya kushuhudia shehena ya pembe hizo, alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah ambalo watuhumiwa hao hulitumiakutoa pembe porini na kuyaingiza jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika eneo la tukio mara baada ya kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa na Serikali juzibaada ya wabunge kuilalamikia.

Waziri Kagasheki alisema kwamba katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa hao walitoa Sh30 milioni kwa ajili ya kujaribu kuwahonga askari.

"Walitaka kuwahonga askari ili wasikamatwe," alisema huku akionyesha noti za fedha hizo.

Alisema wabunge wanaomtaka ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete pekee.

"Sasa mimi nasema kunitoa haitakuwa rahisi anayeweza kunitoani yule aliyeniweka," alisema.

Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya
wabunge kutaka kuwang'oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.

"Itakuwa ni jambo la ajabu kwambakila mtu akiingia madarakani wanataka atoke, watatolewa wangapi?" alihoji na kuongeza kuwaoperesheni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kunusuru tembo wasiishe.

Alisema kwamba ni kweli kuna baadhi ya dosari zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo kuuawa kwa baadhi ya mifugo, lakini siyo kwamba zoezi zima halina manufaa.

Kagasheki alisema kama kasi hii ya kuuawa kwa tembo itaachiwa iendelee baada ya miaka 10 tembowote watakuwa wameisha nchini.

Alisema hataki kuona utawala wa Rais Kikwete ukiondoka madarakaniukiwa na lawama ya kuachia majangili wawamalize tembo.

Mmoja wa watuhumiwa hao, Huang Qin alisema shehena yote ya pembe za ndovu iliyokamatwa nyumbani kwake ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.

Akiongea kwa Kiswahili Qin alisema: "Mimi hii si yangu, kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii (pembe) kidogo kidogo.

"Januari mwaka huu, Gazeti La Daily Mail la Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata shehena ya vipande 638 vya pembe za ndovu ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.

Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa tani nne za pembe za ndovu zenye thamani ya Dola za Marekani 3.4 milioni sawa na takriban Sh5.4 bilioni zilikamatwa Hong Kong Oktoba 20, mwaka jana, huku ikielezwa kuwa meno hayo yalikamatwa yakisafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.

Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na pembe za ndovu yenye thamani ya Sh18.4 milioni yaliyotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi.

Chanzo:Mwananchi

MATOKEO YA DARASA LA SABA 2013 YATANGAZWA

Matokeo ya darasa la saba mwaka 2013 yametangazwa na mwaka huuufaulu umeongezeka toka asilimia 30.72 mwaka jana na kufikia asilimia 50.61 mwaka huu.

Kaimu katibu mtendaji wa baraza la mitihani, Charles Msonde amesema jumla ya watahiniwa 427,606 kati ya 844,938 wamefaulu mtihani kwa kupata alama zaidi ya 100 katika jumla ya alama 250.

Watahiniwa wamefaulu zaidi somo la kiswahili kwa asilimia 69.06 na somo ambalo wamefaulu kwa kiwango cha chini ni hisabati maana ufaulu wake ni asilimia 28.62

WIZARA YAFUTA DIVISION ZERO NA KUPACHIKA 5(FIVE)

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imefumua mfumo wa upangaji alama katika mitihani ya elimu ya sekondari, ambapo sasa mtihani wa mwisho utakuwa na asilimia 60 ya matokeo yote huku daraja sifuri likifutwa.

Kutokana na mabadiliko hayo, mfumo wa tathmini endelevu (CA),unaopima maendeleo ya mwanafunzi akiwa shuleni, ndio utatumika kumpa mwanafunzi asilimia 40 zilizobaki na atapaswa kujua alichopata katika alama hizo kabla ya kuingia kwenye mtihani wa mwisho.

Akitangaza mabadiliko hayo jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, alisema mabadiliko hayo yataanza na wanafunzi wanaoanza mtihani wa kidato cha nne Jumatatu.

Profesa Mchome alisema katika mabadiliko hayo, Wizara imeweka utaratibu wa jinsi mwanafunzi atakavyopata asilimia 40 ya mtihani wa mwisho, kutokana na kazi atakazokuwa amefanya tangu alipojiunga sekondari.

Kwa kidato cha nne, asilimia 15 kati ya 40, mwanafunzi atatakiwa azipate katika mtihani wa Taifa wa kidato cha pili; huku katika matokeo ya mtihani wa kidato cha tatu, kwa mihula yote miwili, atatakiwa awe na asilimia 10, kila muhula akipata alama tano.

Mtihani wa Majaribio (mock) kwa kidato cha nne, mwanafunzi atatakiwa apate asilimia 10 na kazi za mradi alama tano. Kwa mujibu wa Profesa Mchome, matokeo ya kidato cha sita kwa sasa yanafuata mfumo huo na utaendelea kama muundo wa sasa ulivyo.

Mfumo huo utatumika hadi kwa wanafunzi wa kujitegemea ambao alama zao zitatokana na matokeo ya mitihani ya awali.

Madaraja mapyaProfesa Mchome alisema kuanzia sasa kwa vidato vya nne na sita, alama za ufaulu katika masomo zitaanzia A, B+,B, C, D, E na F, ambapo mwachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana kwa kidato cha nne na cha sita.

Mfumo huo ni tofauti na zamani, ambapo alama za masomo ya kidato cha nne ilikuwa A, B, C, D naF, wakati kidato cha sita ilikuwa A, B, C, D, E, S na F.

"Katika alama hii ya B, kundi la kwanza la B litakuwa la wanafunzi waliopata alama kuanzia 50 hadi 59 na lingine la B+ litakuwa la waliovuka wigo wa B na kufikia wa 60 hadi 74," alisisitiza Mchome.

Alisema pamoja na kuwa na mwachano wa alama 26, alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia 75 hadi 100, ambapo waliofaulu kwa kiwango hicho walikuwa wachache na hivyo Serikali imeonahakuna haja ya kubadili alama hiyo, badala yake juhudi ziendelee kuongeza kiwango cha ufaulu, ili kupata wanafunzi wengi zaidi katika daraja hilo.

Alama C yenye maana ya ufaulu mzuri itaanzia 40 hadi 49, D ambayo ni ufaulu hafifu itaanzia 30hadi 39, E ufaulu hafifu sana itaanzia 20 hadi 29 na F ufaulu usioridhisha, itaanzia 0 hadi 19.

Muundo wa madarajaDaraja la kwanza kwa mujibu wa mfumo huo mpya, daraja la kwanza ambalo ni la kundi la wanafunzi walio na ufaulu, uliojipambanua na bora sana. Daraja la pili litakuwa kundi la ufaulu mzuri sana na daraja la tatu,kundi la ufaulu mzuri na wa wastani.


Daraja la nne litakuwa kundi la ufaulu hafifu na daraja tano litakuwa la ufaulu usioridhisha. Mtihani kidato cha 4 Wakati huo huo, jumla ya watahiniwa 427,906 ambao kati yao 367,399 ni watahiniwa wa shule na 60,507 wa kujitegemea wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kuanzia Novemba 4 hadi 21.

Mchome alisema idadi hiyo ya watahiniwa ni pungufu ya watahiniwa 53,508, sawa na asilimia 11.1 ikilinganishwa na 481,414 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana.

ASKARI WALA NJAMA NA KUPORA SH.220 MILIONI

Askari polisi wawili wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kula njama na kushiriki katika uporaji wa Sh220 milioni za Kampuni ya Dot Services ya mjini Moshi.

Habari za uhakika zilisema baada yakubanwa na makachero, askari hao walirejesha Sh60 milioni na watuhumiwa wengine wawili ambao ni raia, walirejesha Sh23 milioni.

Askari hao ni wale walioko katika Kikosi cha Polisi wa doria wanaotumia pikipiki na jana watuhumiwa wote walitawanywa katika vituo mbalimbali ili wahojiwe kwa nyakati tofauti tofauti.

Habari za kipolisi zilisema askari hao hawakwenda eneo la tukio lakini walifahamu mpango mzima kuhusu uporaji huo uliowawezesha kupata mgawo wa fedha hizo.

Waliotiwa mbaroni wana vyeo vya Constable (majina tunayo) na inaelezwa kuwa tukio hilo limewachukiza baadhi ya polisi wakidai ni kuwa mfululizo wa matukio yanayochafua sura ya jeshi hilo.

Habari hizo zimebainisha kuwa tukio hilo ni mpango mahususi uliowashirikisha watu wasiopungua 10 wakiwamo baadhi ya watumishi wa Kampuni ya Dot Services waliovujisha mpango wa kuhamishafedha hizo.Kulingana na vyanzo vya habari, idadi ya walioshiriki katika mpango wa kupora fedha hizo ni kati ya watu wanane na 10 na tayari polisi wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz alikaririwa akisema kuwa fedha hizo ziliporwa Jumanne asubuhi katika makutano ya Barabara za Arusha na Boma mjini Moshi.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya kufika katika makutano hayo, wafanyakazi wa Kampuni ya Dot Services waliokuwa na gari ainaya Toyota Hilux T.864 AZM walisimama kuruhusu pikipiki ipite.

Kamanda Boaz alisema wakati wakisubiri pikipiki ipite, ghafla walijitokeza watu wawili wakafungua milango na kuingia ndani ya gari na kuwateka wafanyakazi na kuwaamuru waelekee eneo la Shanty Town.

Hata hivyo mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo ya ujenzi yenye makao yake makuu nchini Uganda, Shuresh Bab alifanikiwa kuruka kwenye gari hilo na kutoa taarifa polisi.

Kamanda Boaz alifafanua kuwa msako wa kuwatafuta wahusika ulianza mara moja ambapo polisi walifanikiwa kulipata gari hilo na wafanyakazi wakiwa wametelekezwa mto Karanga mjini Moshi.


Chanzo: Mwananchi

ISRAEL YAFANYA SHAMBULIO SYRIA

Ndege za kivita za Israel zimefanya mashambulizi katika mji wa pwani wa Syria wa Latakia.

Hii ni kwa mujibu wa afisaa mkuu wa Marekani alisema kuwa shambulizi hilo lililenga makombora ya Urusi yaliyokuwa yananuiwa kupelekwa kundi la wapiganaji la Hezbollah.

Latakia ni ngome ya kisiasa ya Rais Bashar al-Assad, na pia kuwa mji muhimu ambako jamii yake ya Alawite inatoka.

Israel, inasemekana kufanya angalau mashambulizi matatu ya angani dhidi ya Syria mwaka huu pekee.

Taarifa hii inajiri huku kikundi cha wataalamu wa silaha za kemikali kutoka shirika la OPCW waliokuwa na jukumu la kuharibu vifaa vya silaha za kemikali vya Syria, kusema kuwa limekamilisha kazi yake siku moja kabla ya makataa iliyotolewa.

Hatua ya shirika hilo ilitokana na makubaliano yaliyofikiwa kufuatia madai yaliyokanushwa na serikali ya Syria kuwa majeshi yake yalitumia nguvu pamoja na silaha za kemikali katika maeneo ya raia, na pia baada ya Marekani na Ufaransa kutishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Serikali ya Syria.

Afisaa huyo alisema kuwa mashambulizi yalifanyika Jumatano na kuendelea hadi Alhamisi.

Hata hivyo Syria na Urisi zingali kutoa tamko lolote kuhusu madai hayo.

Israel imekuwa ikisema kuwa itachukua hatua ikihisi kuwa silaha za Syria, ziwe za kemikali au za kawaida zinapelekewa wapiganaji katika eneo hilo hasa kundi la wapiganaji la Hezbollah.

MUHONGO AAGIZA HALMASHAURI KUTOA TAARIFA ZA USHURU WA MADINI

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka Halmashauri zote Nchini ambazo maeneo yao yana migodi ya madini kuhakikisha wanatowa taarifa za fedha zinazopatikana kutokana na ushuru wa madini kwa wananchi wao.

Waziri Muhongo alitowa kauli hiyo wakati akiwahutubia viongozi wa Mkoawa Katavi na wachimbaji wa madini katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi Wa Idara ya maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ya Wizara hiyo.

Alieleza kuwa wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini wamekuwa wakipotosha kuwa Halmashauri zimekuwa hazipatiushuru kwenye maeneo yao unaotokana na ushuru unaotokana na madini kitu ambacho sio sahihi Alisema hakikisheni mnawasomea wananchi wenu mapato yote ambayo Halmashauri zenu zinapata kutoka kwenye makampuni yanayochimba madini badala ya kuwaficha wananchi na matokeo yake yamekuwa ni wananchi kujenga chuki kwa makampuni hayo wakijua kuwa Halmashauri zao hazipati chochote kutoka kwa makampuni ya uchimbaji wa madini Pia alizitaka Halmashauri kuhakikisha fedha wanazolipwa kutokana na ushuru wa madini zinatumika kwa ajiri ya shughuli za maendeleo kwenye maeneo yote.

Profesa Muhongo alieleza zipo baadhi ya Halshauri wamekuwa wakitumia pesa hizo kwa ajili ya watumishi wao kwenda kujifundisha namna ya kuzowa taka kwenye mikoa mingine hayo siyo matumizi mazuri ya fedha alisema Muhongo Aidha alieleza kuwa serikali imeshaweka utaratibu ambao hakuna mgodi ambao unaanzishwa hapa Nchini bila kuwa na ubia na Serikali ndio utaratibu ambao umeisha wekwa na wizara hiyo kwani kama tulikosea mwanzo hatutakiwi kukosea tena Pia aliwashauri wachimbaji wadogo wadogo waanzishe vyama vyao ili iwe rahisi kwao kukopeshwa mikopo ambayo itawasaidia kununua vifaa vya kisasa.

Viongozi wa wachimbaji wawe na utaratibu wa kuwasikiliza kero za wachimbaji vijijini kuliko ilivyo sasa ambapo wachimbaji wanapiga simu mojakwa moja kwa waziri Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi DR Rajabu Rutengwe alieleza kuwa mbali ya mkoa kuwa na madini mbalimbali kama vile Dhahabu Shaba bado wachimbaji wanakabiliwa na changamoto mbalimbali Rutengwe alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwani vifaa duni wanavyotumia kuchimbia na mitaji midogo kwa wachimbaji.

Nae Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Katavi Willy Mbogo alimweleza waziri Muhogo kuwa jumla ya leseni 1035 zimeisha tolewa kwa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Katavi.


Source: Katavi yetu

MWANAMKE MMOJA APIGWA RISASI BAADA YA KUKAIDI AMRI YA ASKARI

MWANAMKE mkazi wa PPF jijini hapa, Vailet Mathias, amepigwa risasi na polisi na kujeruhiwa eneo la Benki ya CRDB Mapato baada ya kukaidi amri halali ya Polisi na kumtishia silaha. Tukio hilo lilitokeajana saa 7 mchana katika benki hiyoya CRBD tawi la Mapato, mkabala naMamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha.

Vailet alifika eneo hilo akiwa na gariaina ya Toyota Cresta namba T 888 BWW na kutaka kuliegesha katika lango la kuingilia magari ya kuchukua na kupeleka fedha katika benki hiyo.

Askari Polisi aliyekuwa akilinda eneo hilo, alimwamuru Vailet ambaye umri wake haukupatikana mara moja, kutoegesha gari eneo hilo, lakini akapuuza na kukaidi kisha akaingia ndani ya benki na hivyo askari huyo kuamua kutoa upepo kwenye matairi.

"Vailet alifika eneo hilo na kuingia ndani ya benki baada ya kupuuza amri ya askari aliyekuwa lindoni aliyemtaka atafute maegesho sehemu nyingine, lakini hakujibu kitu na kuwatazama askari waliokuwa hapo kwa dharau," alisema Kamanda wa Polisi wa Mkoawa Arusha, Liberatus Sabas alipokuwa anawathibitishia waandishi wa habari tukio hilo.

Alisema baada ya muda mfupi, Vailet alitoka nje na kukuta gari lakehalina upepo naye kwa hasira akamkabili askari Polisi aliyekuwa lindoni huku akimtolea maneno ya "hata kama una bastola nami ninayo" na kuitoa na kukoki akitaka amshambulie askari.

"Hata hivyo, askari alimwahi kwa bastola na kumpiga begani na kumfanya aanguke chini na bastola yake kumtoka mkononi," alisema Kamanda Boas huku akitoa mwito kwa wananchi kutii sheria bila shuruti. Alisema alichokifanya mwanamke huyo ni ukiukaji mkubwa wa sheria na kosa la jinai.

"Tunaomba kila mtu atii sheria, huuni ukiukwaji wa sheria na alimtishia bastola askari wetu, naye askari akamwahi maana eneo hili ni muhimu na hatujui mhusika alikuwana lengo gani," aliongeza Kamanda.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Fatma Kikuyu alidai mwanamke huyo alifanya kosa kukaidi amri ya Polisi na kuonesha ubabe kwa polisi na ndiyo maana tukio hilo likamkuta. Vailet alikimbizwa katika hospitali ya Mount Meru kwa matibabu, lakini alipofikishwa hapo alitolewa na kukimbizwa katika hospitali ya Selian.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya hospitali hiyo kutoka kwa daktari, ambaye hakutaka kutaja jina lake, Vailet alifikishwa hapo na wakati huo alikuwa akisubiri kuingizwa katika chumba cha upasuaji ili kutolewa risasi iliyompata kwenye bega la kushoto.


Source:Habari leo

KIGWANGALLA KUKUSANYA SAINI ZA KUMNG'OA MAKINDA

Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza kukusanya saini za wabunge akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.

Dk Kigwangalla aliibua hoja ya kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha wabunge wote cha kuelezea shughuli zitakazofanywa na Bunge katika mkutano wa 13, kilichofanyika juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, jana alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika kikao cha wabunge, lakini hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala yake alisema kwamba leo ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kukamilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika Makinda.

Chanzo chetu kutoka katika kikao hicho cha wabunge kilibainisha kuwa Kigwangalla alihoji kuhusiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bungeya Bajeti, Andrew Chenge (CCM-Bariadi Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati katika kamati nyingine wenyeviti na makamu huchaguliwa na wajumbe wa kamatihusika.

Pia Dk Kigwangala alisema Spika Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya Sh430,000 kwa siku wajumbe wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati wajumbe wa kamati nyingine wamekuwa wakipewa Sh130,000.


"Anachokifanya Spika ni matumizi mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye kazi hata bila posho lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya Sh430,000 kwa siku?" chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji. Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti hili jana alisema mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada tofauti na viwango vya kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika unapoomba kwa Spika.

"Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo.

Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya Spika kuridhia basi nao wanapewa," alisema Dk Kashililah.

Katibu huyo wa Bunge alieleza kuwa zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo ya ziada kwa maana ya kutaka posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata chakula, ikiwazinakabiliwa na majukumu ya ziada pia katika mazingira tofauti nje ya utaratibu wa kawaida.


"Kimsingi, kamati nyingi zinapewa malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka saa saba au nane usiku, au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida, taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhikana maelezo ya kazi husika, basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo," alisema Dk Kashililah.

Kuhusu Serukamba Aidha, Dk Kigwangalla alinukuliwa akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), kuwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.

"Hakuna mbunge yeyote aliyepo katika kamati mbili lakini hata kungekuwa na sababu maalumu basi wa kuteuliwa angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini-CCM) ambaye TRA (Mamlaka ya Mapato Nchini) ipo chini ya kamati yake," kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema Dk Kigwangalla alisema badala ya kumweka karibu katika ushiriki, Mgimwa alipokwenda katika kamatihiyo aliambulia kufukuzwa.

Akizungumzia suala hilo, Dk Kashililah alisema Serukamba pamoja na wabunge wengine kadhaa waliteuliwa na Spika kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kamati hiyo wakati wa kipindi cha Bajeti Kuu ya Serikali.

Aliwataja wabunge wengine walioteuliwa kushiriki katika Kamatiya Bunge ya Bajeti kuwa ni John Cheyo (Bariadi Mashariki-UDP), Salahe Pamba (Pangani - CCM) na Hamadi Rashid Mohamed (Wawi - CUF).

Kanuni za BungeKwa mujibu wa kanuni za Bunge katika toleo la mwaka 2007, kifungu cha 137(1), ili kumwondoa Spika madarakani, mbunge anayetaka kuwasilisha hoja hiyo atatakiwa kuwasilisha taarifa ya maandishi ya kusudio hilo kwa Katibu, akieleza sababu kamili ya kutaka kuleta hoja hiyo.

Kifungu kidogo cha pili kinasema baada ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la kumwondoa Spika kwenye madaraka, Katibu atapeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.

Kifungu cha tatu kinabainisha kuwa endapo kamati hiyo itaridhika kuwazipo tuhuma mahususi dhidi ya Spika zinazohusu uvunjaji wa masharti ya ibara husika za Katiba, sheria au kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi kamati hiyoitaidhinisha hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.

Kanuni zinasema Naibu Spika, atakalia Kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka kumwondoa Spika madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa mjadala na kwamba ili kumwondoa zinahitajika kura zisizopungua theluthi mbili ya idadi ya wabunge wote.

Source:Mwananchi

M23 WAFULUMUSHWA TOKA KWENYE NGOME YAO

Wanajeshi wa DRC wamefanikiwa kuwatimua waasi wa M23 kutoka katika ngome yao kuu katika eneo la Bunagana.

Wanajeshi hao wamekomboa mji wa Bunagana kufuatia makabiliano makali adhuhuri ya leo ambapo baadhi ya waasi walilazimika kuimbilia msituni huku baadhiwakidai waliingia Uganda baada ya kuvalia mavazi ya kiraia.

Msemaji wa serikali alisema kuwa mji wa Bunagana ulio katika mpaka wa Uganda na DRC, sasa uko chini ya wanajeshi wa serikali.

Wenyeji wa mji huo walithibitishia BBC kuwa mji huo ulikombolewa na kuwa waasiwamekuwa wakitoroka mapambano makali dhidi yao.

Hatua hii ya wanajeshi ni sehemu ya ushindi mkubwa ambao wanajeshi wamekuwa wakiupata dhidi ya waasi hao wa M23 walianza harakati zao dhidi ya serikali ya Congo mwaka jana wakidaiwa kusaidiwa na serikali ya Rwanda.

Mnamo siku ya Jumatatu mjumbe maalum wa M23 hawana tena nguvu za kijeshi kwani sio tesho tena.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa wakimbizi elfu tano wamelazimika kutoroka Bunagana na kuingia Uganda kwausalama wao.

HUKUMU YA BABU SEYA NA PAPII KOCHA YAANZA KUSIKILIZWA MAHAKAMA YA RUFAA

Hukumu ya Nguza Viking maarufu kama babu Seya imeanza kupitiwa.

Mahakama ya rufaa imeanza kupitia hukumu ya mwanamuziki maarufu nchini mwenye asili ya jamhuri ya kidemokrasia ya congo DRC Nguza Viking maarufu kama Babu seya na mwanawe Johnson Nguza maarufu kama Papii kocha.

Mapitio hayo yanafanywa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Mh Nathali Kimaro amboa ndio waliotoa hukumu Februari 2010 kwa upande wa waleta maombi wakiongozwa na wakili Mabetre Marando wamewasilisha mahakamani hapo mambo sita ambayo wangepedwa mahakama hiyo iyaangaliye kwa makini,ambapo moja ya mambo hayo ni pamoja na kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi mashahidu muhimu hawakuitwa kutoa ushaidi wao.


Aidha wanataka ushaidi wa watoto uliotolewe katika kesi hiyo uondolewe katika kumbukumbu kwa sababu haukufuta taratibu na vigezo vya matwakwa ya sheria ya ushaidi pia wamesema kuwa katika ushaidi uliotolewa ulionyesha kuwa katika nyumba ya babu seya kulikuwa na mlango wa siri lakini mahakama ilipokwenda hapo mlango huo haukuonekana.

Kwa upande wa serikali kupitia wakili wake mwandamizi jackson burashi wameiomba mahakma hiyo kutupilia mbali shauri hilo kutokana na ukweli kuwa yapo hapo kinyume na sheria na yameletwa kama rufaa na siyo mapitio.


Aidha akaongeza kuwa maombi hayo hayajakidhi viwango vya sababu za mapitio kwa kuwa maombi hayo yalipaswa kuonyesha kuwa kosa limetendeka na haki ya mleta rufaa imepotea. Baada ya maelezo ya pande zote mbili mahakama ikasema itatoa maamuazi baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili.

Babu Seya na mwanaye papii kocha wanaendelea kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hati ya makosa ya kunajisi na kulawiti watoto wadogo kupitia huku iliyotolewa na mahakama ya hakimu mkazi kisutu mwaka 2004 ambapo walihkumiwa kifungo cha maisha.

TANZANIA YAFIKILIA KUJITOA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Serikali ya Tanzania imesema inatafakari ushiriki wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na inaweza kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo itaendelea kutengwa katika baadhi ya vikao.

Aidha imesema Tanzania haitambui vikao vinavyofanywa na nchi tatu zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikizitenga Tanzania na Burundi.

Waziri anayehusika na masuala ya Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta ameliambia Bunge la Tanzania kuwa makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na nchi za Kenya, Rwanda na Uganda yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao hivyo kwa sababu vinafanyika nje ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo.

Katika mikutano iliyofanyika hivi karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa kwenye vikao hivyo.

Kwa mujibu wa Waziri Sitta mikutano ya wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambayo ilianza kwa kuitenga Tanzania ilifanyika Entebbe nchini Uganda mwezi Juni mwaka huu na kufuatiwana mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka huu huko Mombasa nchini Kenya ambapo nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania walizungumzia uanzishaji wa himayamoja ya forodha.

Mambo mengine waliyozungumza wakuu hao ilikuwa uanzishaji wa visa moja ya utalii kwa nchi zao na matumizi ya vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika kama hati za kusafiria miongoni mwa nchi hizo.

Aidha Waziri Sitta amesema ndani ya mikutano hiyo pia walizungumziakuanzisha mchakato wa kuanzisha shirikisho la nchi hizo.

Tayari Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuangalia ni kwa namna gani zitaanzisha ushirikiano nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama zinavyofanya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya.

VIJANA MILIONI 2.6 WANAISHI NA VVU NCHI

Vijana milioni 2.6 wenye umri wa miaka kati 15 na 24 nchini, wanaishi na virusi vya Ukimwi.


Takwimu hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Abdoul Coulibaly, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya elimu ya jinsia na afya ya uzazi kwa vijana katika nchi 21 za Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema karibu vijana 50 katika nchi hizo huambukizwa virusi vya Ukimwi kila saa moja, huku idadi ya wasichana wakiongoza kwa maambukizi hayo.

Coulibaly alisema idadi hiyo ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana kwa Tanzania, inachangiwa na kutokuwapo kwa elimu ya kutosha ya jinsia pamoja na VVU na Ukimwi, afya ya uzazi na ukuaji wa binadamu.


Alisema asilimia kubwa ya vijana hawana uelewa wa masuala ya afya ya uzazi na jinsia, jambo ambalo husababisha kujiingiza kwenye mapenzi katika umri mdogo na kusababisha kuongezeka kwa mimba za utotoni.

Pia aliiomba serikali kuweka mikakati madhubuti ya kutoa elimu ya afya na jinsia kwa vijana kwa ajili ya kusaidia kupunguza idadi ya maambukizi kwao pamoja na mimba za utotoni zinazosababishwa na ukosefu wa elimu hiyo.

Kaimu Mkurugenzi, kitengo cha masuala mtambuka kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Laetitia Sayi, alisema changamoto ya maambukizi ya VVU kwa vijana ni kubwa na kwamba serikali kwa upande wake inafanya jitihada mbalimbali za kutatua tatizo hilo.

WATU WATATU WAKAMATWA NA MKONO WA BINADAMU

Watu 3 wamekamatwa na kiganja cha mkono wa binadamu mkoani Mwanza.

Watu watatu wakiwemo waganga wawili wa jadi wamekamatwa na polisi katika eneo la Igombe Tx, jijini Mwanza wakiwa na kiganja cha mkono wa kulia unaoaminika kuwa wa binadamu.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, kamishna msaidizi wa polisi Joseph Konyo amesema tukio hilo limetokea eneo la kati ya ziwani na nyuma ya uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya raia wema kuwapa taarifa za siri.


Source:ITV

TANZANIA YAPUUZIA MIKUTANO INAYOITISHWA NA RWANDA, UGANDA NA KENYA

Jumuiya ya Afrika Mashariki imekumbwa na msukosuko bada ya TZ kupuuza mikutano inayofanya ikisema inakiuka utaratibu wa jumuiya.

Wakuu wa nchi za Kenya,Uganda na Rwanda baadaye leo wanatarajia kusaini makubaliano ya kuanzisha kituo kimoja cha kukusanya ushuru kinachotarajiwa kurahisisha uchukuzi wa bidhaa kutoka Mombasa Kenya -- Uganda hadi Rwanda.

Kuundwa kwa Kituo hicho pia kunatazamiwa kurahisisha shughuli nzima za uchukuzi katika maeneo hayo ya Afrika Mashariki.

Taifa la Sudan Kusini pia linataraji kuidhinishwa kama mshirika katika kikao cha wakuu wa mataifa hayo.

Mkutano huu unalenga kuimarisha maendeleo ya kikanda kupitia kwa miundo msingi bora , uchumi na biashara.

Shughuli hii inakuja baada ya mkutano uliofanyika mjini Kampala Uganda, mnamo mwezi Juni na mwengine uliofanyika mjini Mombasa mnamo mwezi Agosti ambako viongozi walipendekeza kupanuliwa kwa bandari ya Mombasa ili kuwezesha uharaka wa bidhaa kupitishiwa bandarini humo katika kuhudumia kanda nzima.

Tanzania awali ilipuuza mikutano ya Kenya ,Uganda na Rwanda ikisema kuwa ni kinyume na utaratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kando na hayo mkutano mwengine wa marais wa nchi nane utafanyika Kesho ambapo watakutana kwenye kongamano la siku nne mjini Kigali ambalo linatarajiwa kuweka kipaombele kwa uimarishwaji wa huduma za internet katika mataifa hayo.

Mkutano huo unaofanyika miaka sita baada ya Kigali kuwa mwenyeji wa kongamano la Connect Africa, mwenyeji wake atakuwa Rais Paul Kagame na Dr Hamadoun I. Toure, katibu mkuu wa muungano wa kimataifa wa mawasiliano ya kiteknolojia (ITU).

Marais hao ni pamoja na Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Salva Kiir wa Sudan Kusini Ali Bongo Ondimba waGabon, Thomas Boni Yayi wa Benin na Rais Blaise Compaore wa Burkina Faso.

Mkutano huo unaanza rasmi Kesho.Nchi zengine 15 za Afrika zitashiriki kwenye mkutano huo ambao kwa mujibu wa waandalizi, zaidi ya wajumbe 1,500 watahudhuria.

WASHUKIWA WAWILI WA UGAIDI WAUWAWA TANGA

Watu wawili wanaodaiwa kuhusishwa na vitendo vya kigaidi wameuawa kwa kupigwa risasi wakati kundi hilo lilipokuwa msikitini huku wafuasi wake wakiwa na silaha za moto na baridi walipokuwa wakijibizana kwa kutumia silaha mbali mbali ndipo askari walipowahi kuwashambulia viongozi wa kundi hilo kisha kuwanyang'anya silaha zao ili kuepuka madhara makubwa zaidi.

Mkuu wa mkoa wa Tanga luteni mstaafu Chiku Gallawa amesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Kimamba kilichopo kata ya Negero wilayani Kilindi wakati kundi hilo lilipokuwa limejiandaa kujibu mashambulizi ya askari msikitini kwa kuwa na silaha aina ya bunduki na mapanga ndipo viongozi hao waliposhambuliwa ambapo mmoja alifariki papo hapo huku mwingine akifariki hospitali ya wilaya.


Chanzo:ITV

CHADEMA WATUPIANA MAKONDE

Viongozi Chadema wazipiga kavukavu kwenye mkutano
Mkutano wa Baraza la Uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka ukumbi wa ngumi, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha,

Samson Mwigamba kushushiwa kipigo.
Mwigamba alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya viongozi wenzake wa chama kwa madai ya usaliti na tayari amesimamishwa uongozi kwa muda usiojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema kufikishana polisi.

Alikutwa na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu wa Chadema Taifa, Mwenyekiti, Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei katika Hoteli ya Coridal Spring.


Viongozi hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo nchi nzima, kuimarisha chama na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.

Habari kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa hatua hiyo ilifuatia tuhuma kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.


Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wote wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili mustakabali wa chama hicho, mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu wote wa Chadema wa kanda hiyo.

Hata hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema walimtuhumu Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo, uliokuwa ukizungumzia ufisadi ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti Mbowe kukubali kuchunguzwa.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba alisema kuwa baada ya Lema kutoa tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi wengine na vijana waliokuwa wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza kumpiga pamoja na kumnyang'anya kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa nayo, kisha kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.

"Wamenipiga sana na kuniweka ndani, ila nashukuru Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OCCID), alikuja na kunitoa saa 5:00 asubuhi,"alisema Mwigamba.


Alisema kuwa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ataeleza yote yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa yeye ni kiongozi wa juu wa chama.

Hata hivyo, alieleza kwamba bado anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua waliompinga.


Kauli ya polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi wameona hakuna kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana na malalamiko yaliyofikishwa kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama kwenye mitandao.

"Hili suala la mitandao ni kubwa na lina taratibu zake sasa kusema tu umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi unahitajika kwao, sisi tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo sababu tulimwachia, Mwigamba,"alisema Sabas.

Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba

Akizungumzia sakata hilo jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba Mwigamba alibainika kutuma ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums uliokichafua chama hicho, akieleza haikuwa mara yake ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu.

"Kilichotokea ni hicho, vijana wa Red Brigade ndio waliomtoa ukumbini, baada ya kumbaini kukichafua chama, kwani laptop yake baada ya kuchunguzwa na wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye aliyetuma ujumbe huo,"alisema Lema.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii ya Jamii Forums.

Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.

Golugwa alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye kikao, Mwigamba alikiri kuandika na kurusha taarifa hizo kwenye mitandao, lakini alipotakiwa kukabidhi kompyuta yake ili ichunguzwe na wataalamu wa mawasiliano wa chama hicho aligoma, hali iliyozua tafrani kati yake na walinzi wa chama hicho (Red Brigade), waliolazimika kutumia nguvu kumdhibiti.

Purukushani zilivyotokea
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za kutaka kumnyang'anya Mwigamba kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema mkoani Arusha alianza kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, kabla ya kufanikiwa kumdhibiti.
Zinaeleza kuwa katika tukio hilo kulitokea pia kurushiana maneno na matusi ya nguoni kati yake na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo Lema.

Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.

Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, alisema kikao chao kiliendelea jana bila ya vurugu zozote na kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka 2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo ujao.
Adhabu kwa Mwigamba
Katika hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha uongozi Mwigamba kwa tuhuma za kukisaliti, kukihujumu chama hicho na viongozi wake.

Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse alibainisha kuwa uamuzi wa kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda ya Kaskazini kilichokutana juzi.


Alisema kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo tuhuma zitathibitishwa, hatua nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana na kanuni na katiba ya Chadema.

"Kwa sasa Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya kumi, kifungu cha 10.1 kifungu kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema inayozungumzia maadili ya uongozi,"alisema Natse.

Akifafanua zaidi alisema kuwa sura na vifungu hivyo vinakataza kiongozi wa chama hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wenzake bila kufuata vikao halali vya kikanuni na kikatiba.

MASHABIKI WA DORTMUND WAVUNJA VITI EMIRATES

Kama ulizani tatizo lipo kwa watanzania tu kung'oa viti uwanja wa taifa basi ondoa mawazo hayo.

Mashabiki wa Borussia Dortmund kutoka Ujerumani wamevunja na kung'oa viti(Pichani) katika uwanja wa Emirates unaomilikiwa na klabu ya Arsenal kutoka Uingereza.

Tukio lilitokea siku ya jumanne wakati timu hizo zilipokutana katika mchuano wa ligi ya klabu bingwa ulaya ambapo Dortmund waliondoka na ushindi wa goli 2 kwa 1.

Magoli katika mchezo huo yalifungwa na H. Mkhitaryan wa Borussia Dortmund katika dakika ya 18 ya michezo kabla ya mfungaji wa Arsenal Olivier Giroud kusawazisha katika dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza.

Alikuwa ni Roberto Lewandowski aliyepigilia msumari wa mwisho katika dakika ya 85 na kufanya ubao wa matangazo kusomeka Arsenal 1-2 B. Dortmund na kuharibu furaha ya kocha Arsene Wenger ambae ilikuwa siku yake ya kuzaliwa na kufikisha miaka 64.

Arsenal bado wanashikilia usukani wa kundi huku wakiwa pointi sawa na Dortmund pointi 6 tofauti ya magoli imeibeba Arsenal. Baada ya Dortmund wanafuata Napol kutoka Italy wakiwa na pointi 6 kisha Marseille ya Ufaransa ikiwa haina kitu.

MALAWI YACHUKIZWA NA MATAMSHI YA ZUMA

Serikali ya Malawi imeghadhabishwa na matamshi ya Rais wa Afrika Kusini Jacob Kusini yaliyoonekana kudharau miundo msingi nchini Malawi.

Malawi sasa imemtaka balozi mkuu wa Afrika Kusini nchini humo kuelezea matamshi ya kusikitisha yaliyotolewa na Rais Jacob Zuma kuhusu nchi hiyo.

Balozi huyo, Cassandra Makone alitakiwa na serikali ya Malawi kufafanua matamashi ya Zuma yaliyotafsiriwa na wengi kumaanisha kuwa Malawi bado iko nyuma sana alipokuwa anazungumzia miundo msingi ya Afrika Kusini.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Quent Kalichero aliambia shirika la habari la AFP kuwa Makone aliitwa na serikali ili kueleza alichomaanisha Rais Zuma.

Balozi huyo alifanya mkutano na afisaa mkuu katika wizara ya mambo ya nje George Mkondiwa ingawa Kalichero inaarifiwa alikataa kutoa maelezo ya mkutano.

Mnamo siku ya Jumatatu, Zuma alizua utata alipokuwa anawashawishi madereva wa nchi hiyo kukubali kutozwa kodi za barabarani mjini Johannesburg.

''Tuko mjini Johannesburg, na hii ni Johannesburg. Sio kama barabara ovyo ya kitaifa nchini Malawi,'' alinukuliwa akisema Zuma.

Hata hivyo msemaji wa Zuma Mac Maharaj alisema kuwa taarifa hiyo ilitafsiriwa visivyo.

Aliongeza kuwa Zuma alikuwa tu anasisitiza kuhusu mfumo mzuri wabarabara Afrika Kusini ikilinganishwa na nchi zengine katika kanda ya Afrika Kusini.

Hata hivyo, Maharaj aliomba radhi kwa matamshi hayo akisema kuwa watu wengi wameghadhabishwa nchini Malawi.

MABAKI YA MOBUTU SESEKO KUZIKWA DR CONGO

Serikali ya Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo, imesema itahamisha mabaki ya mwili wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko kufuatia makubaliano na familia yake. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya rais wa nchi hiyo, President Joseph Kabila.

Hayati Mobutu alizikwa nchini Morocco, alikofariki mnamo mwaka 1997 baada ya kuondolewa mamlakani kutokana na uasi ulioongozwa na baba yake Rais Joseph Kabila.

Alikuwa mtu aliyechukiwa sana na wengi nchini Congo, lakini nchi hiyo imekumbwa na migogoro tangu alipong'olewa mamlakani.

Hatua ya Kabila inaonekana na wengi kama mpango wake wa kuwapatisha watu wa nchi hiyo.

Kabila alishinda uchaguzi wa mwaka 2007 bila ya pingamizi na anakabiliana na uasi Mashariki mwa nchi.

Rais Kabila ametoa tangazo hilo la kipekee katika hotuba yake kwa bunge ambapo aliahidi kuunda serikali ya pamoja.

''Serikali hii itajumuisha wanachamawa chama tawala na wale wa upinzani pamoja na viongozi kutoka mashirika ya kijamii,'' alisema katikahotuba yake.

Mtaalamu wa maswala ya Afrika Ibrahima Diane anasema kuwa huenda Kabila alishauriana na mwanawe Mobutu, Nzanga Mobutu, kabla ya kutangaza kuwa mabaki ya hayati Mobutu yatazikwa nchini Congo.

Mobutu Sese Seko angali anawakumbuka wengi hasa wafuasi wake wanaoamini kuwa moja ya mambo mazuri aliyoyafanya ni kuunganisha nchi hiyo.

Nzanga Mobutu ni mbunge ambaye sasa ni mshirika wa karibu wa Rais Kabila.

Mobutu Sese Seko alitoroka DR Congo wakati waasi walioongozwa na Laurent Kabila, kuzingira mji mkuu Kinshasa, mnamo mwaka 1997.

Wakosoaji wake wanamtuhumu kwakuwa mkatili na kiongozi mfisadi aliyekandamiza upinzani na kuponda maliasili ya DR Congo.

Pia alitumia mamilioni ya dola kuijengea kasri yake ya Gbadolite, iliyo ndani ya misitu ya DRC ambayo ilifanyiwa msako mkubwa alipotoroka DR Congo.

Aliingia mamlakani kupitia kwa mapinduzi na kuitawala DR Congo, iliyokuwa inajulikana kama Zaire, kwa zaidi ya miaka 30.

Hata hivyo alifariki akiwa na miaka 66 miezi michache tu baada ya kuikimbia nchi yake.

MOSHI WA KIWANDA CHA OK PLASTIC WAZUA TAHARUKI

Moto uliowaka eneo la kiwanda cha OK Plast Ltd wasababisha hali ya taharuki.

Moto uliowaka katika eneo la Jalala la kiwanda cha OK Plast Ltd kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam umesababisha hali ya taharuki ikiwemo watu kukimbia ovyo na kuacha ofisi na mali zao kwa kuhofia maisha yao baada ya Moshi mzito uliotokana na moto huo kutanda angani.

Tukio la moto huo umetokea katika eneo la wazi la kiwanda cha OK Plast Ltd inayohusika na utengenezaji wa vitu mbalimbali ikiwemo viatu aina ya kandambili pamoja na mikeka, ambapo kwa mujibu wa wenyweji wa eneo hilo wamedai kiwanda hicho cha OK Plast Ltd walikuwa wakitumia eneo hilo kutunzia mabaki ya mali gafi yao ambapo ghafla kijana mmoja amedaiwa kwenda katika eneo hilo na kuwasha moto ikisemekana alikuwa akitafuta asali kutokana na kuwepo kwa nyuki waliokuwa wakiishi kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Moto huo ulisababisha moshi mzito kutanda angani huku vikosi vya zimamoto na baadhi ya wafanyakazi wa makampuni ya jirani na eneo la tukio wakijitahidi moto kuenea katika viwanda na makampuni mengine ambayo kwa wakati huo tayari yalikuwa yapo tupu baada ya watu kutimua mbio kuokoa maisha yao ambapo mkurugenzi wa Pb Investment bwana Mushtack Fazar aliyethibitisha kununua eneo hilo kutoka kwa kiwanda cha Ok Plast Ltd anaeeleza tukio ilivyokuwa.

Licha ya tukio hilo la moto kutokea katika eneo hilo lakini wakazi wa maeneo wamesema kiwanda hicho kinaongoza kwa kuchafua mazingira na kwamba tukio kama hilo si la kwanza ambapo afisa utawala wa kiwanda cha OK Plast Ltd bwana Martin Msamba alipofuatwa kujibu malalamiko hayo amesema ni tukio la kwanza na kwamba kijana aliyehusika kuwasha moto ameshikiliwa na polisi tayari.

KAMPUNI YA SIGARA KOREA YADAIWA KUFANYA UBAGUZI WA RANGI

Kampuni kubwa ya Tumbako nchini Korea Kusini, imeahidi kubadilisha tangazo lake la kibiashara ambalo limekosolewa kwa kuonekana kuwa la kibaguzi.

Mabango yenye tangazo hilo la aina mpya ya sigara ya kiafrika, yalikuwa na picha za Tumbili waliovalia kama waandishi wa habari wakitangaza kuwa ''Afrika inakuja!" Sigara hizo ni bidhaa mpya ya kampuni ya 'This Africa line'.

Aidha kampuni hiyo inasema kuwa sigara hizo zimetengezwa kwa Tumbako ya kiafrika na ambayo imekaushwa kwa njia za kitamaduni.

Paketi za Sigara zina picha zinazoonyesha Tumbili wakichoma tumbako hiyo.

Kejeli kwa Afrika

"tumeudhiwa sana na picha hii ya kejeli iliyotumiwa na kampuni hiyo ikionyesha Tumbili na kuwahusisha na Afrika,'' alisema, ilisema taarifa ya baraza kwa kudhibiti biashara ya Tumbako ya Afrika ikisema kuwa sharti tangazo hilo liondolewe haraka iwezekanavyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, ''kukejeli Afrika ili kuongeza mauzo ya bidhaa ambazo husababiha vifo na maradhi sio jambo linalokubalikana wala hatutakubali. ''Tangazo hilo la biashara limewekwa katika maeneo ya maduka kote nchini humo.

Hata hivyo msemaji wa kampuni hiyo ameelezea kuwa tangazo hilo litaondolewa madukani mwezi ujao.

Amesema kuwa kampuni imejutia utata uliosababishwa na tangazo hilo na kusema kuwa kampuni hiyo ingependa kuondoa wasiwasi wowowte ulioibuka kutokana na tangazo hilo kuhusu ubaguzi wa rangi Alisema hawakuwa na nia yoyote yakuwa kejeli waafrika na kuwa walichagua kutumia tumbili kwa sababu ni wanyama wazuri wanaowakumbusha watu kuhusu Afrika.

Kampuni hiyo inasema kuwa kwa sababu bidhaa hii ina majani ya tumbako kutoka Afrika, nia ya kampuni ilikuwa tu kufananisha bidhaa hiyo na Afrika.

DIWANI ACHEZEA KICHAPO HUKU MTU MMOJA AKIUWAWA KWA RISASI MKOANI KATAVI

Diwani wa Kata ya Majimoto Tarafa ya Mamba Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi Nyasongwe (45) amejeruhiwa vibaya na kulazwa hospitalini baada ya kupigwa na askari wanaofanya oparesheni kimbunga katika Mkoa wa Katavi wakati akiwa msibani kwa mwanakijiji aliye uwawa kwa kupigwa risasi na Askari wanaofanya oparesheni kimbunga baadaya kutokea vurugu baina yao na wanakijiji cha Luchima kata ya Majimoto Wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Akiongea kwa taabu na waandishi wa habari Diwani huyo wa Kata ya Majimoto ambae amelazwa katika wodi namba moja huku akiwa chini ya ulinzi wa Polisi katika wodi namba moja katika hospitali ya wilaya ya Mpanda ambako amelazwa Alisema tukio hilo na kupigwa na kujeruhiwa lilitokea hapo oktoba 13 mwaka huu majira ya saa sita mchana wakati akiwa msibani kijijini hapo alipokuwa amekwenda kwenye msiba wa mwanakijiji ambae alikuwa ameuwa muda mfupi kwa kupigwa risasi na askari wanaofanya opuresheni Kimbunga.

Alieleza kuwa siku hiyo ya tukio yeye wakiwa na Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mamba Lyoba Juma Shomari walipata taarifa kuwa kumetokea vurugu baina ya wanakijiji cha Luchima na Askari wanaofanya opuresheni Kimbunga na kusababisha kifo cha mwanakijiji mmoja na kushambuliwa na kujeruhiwa kwa mkuu wa kituo cha kutuliza ghasia wa Mkoa wa Katavi ASP Mafie Diwani huyo ambae ameumia vibaya sehemu yamatako.

Alisema ndipo walipokubaliana na afisa tarafa huyo na kuelekea kwenye eneo la tukio ambapo walikuta wanakijiji wakiwa wameweka tayari msiba wa mwanakijii mwenzao ambae alikuwa ameuwawa kwa kupigwa risasi Alifafanua kuwa kifo cha mwanajijiji huyo kilitokana na vurugu zilizotokana na wanakijiji hicho kutoridhishwa kuona mwenzao mmoja nyumba yake ikipekuliwa na kikosi cha opareshen kimbunga ndipo walipoamua kumshambulia kwa fimbo ASP Mafie na kujeruhi kichwani na kumfanya kupoteza fahamu.

Pia wanakijiji hao walilishambulia kwa mawe gari la polisi lenye namba PT 0985 na kulivunja kioo ndipo askari hao wa opuresheni kimbunga walipo amua kufyatua risasi ambayo ilimuuwa mwanakijiji huyo na kumjeruhi mguuni mwakakijiji mwingine ambae amepelekwa Katika hospitali ya Sumbawanga mkoani Rukwa kwa ajiri ya matibabu Serengeti alieleza kuwa wakati wakiwa bado wako hapo msibani ghafla lilitokea kundi la askari wa opuresheni kimbunga na kuanza kuwashambulia waombolezaji wote waliokuwepo hapo bila kujali jinsia ingawa yeye na afisa Tarafa hiyo waliweza kujitambulisha lakini waliendelea kupokea kipigo bila huruma kutoka kwa askari hao.

Alieleza kuwa kisha walipakiwa kwenye roli la jeshi wakiwa na kundi la watu waliokuwa wanaomboleza msibani hapo kwa kudaiwa kumshambulia mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia wa Mkoa wa Katavi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari alipotakiwa kutowa ufafanuzi kuhusiana na tukio hili alisema kuwa opuresheni hiyo Kimbunga mhusika ambae anatakiwa kutowa taarifa za tukio hili ni mkuu wa Hifadhi ya wanyama pori ya Katavi Kwa upande wake mkuu wa Hifadhi ya Katavi Ignasi Gara alishindwa kutowa kabisa ushirikiano kwa waandishi wa habari na kuatupia jeshi la wananchi kuwa wao ndio wasemaji wakuu.


Chanzo:Katavi Yetu blog

MADIWANI WAGOMA KUJADILI TAARIFA YA KAMATI YA FEDHA

Mpanda Katavi

Madiwani wa Halimashauri ya Mji wa Mpanda Mkoa wa Katavi wamekataa kujadili taarifa ya kamati ya fedha na mipango ya Halmashauri hiyo iliyo wasilishwa kwenye kakao cha Baraza la madiwani kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Mkoa wa Katavi.

Baraza hilo la madiwani lilikataa kupitisha taarifa hiyo kufuatia hoja mbalimbali zilizotolewa na Madiwani ambao walidai kuwa taarifa hiyo iliyoletwa mbele ya kikao hicho haikuwa imejitosheleza.

Miongoni mwa kasoro zilizodaiwa kuwemo kwenye taarifa hiyo ni kutokuwemo kwa viambata vinavyo onyesha namna ya mapato yandani yalivyo kusanywa na sehemu yaliko tokaDiwani wa kwanza kipinga taarifa hiyo kwenye kikao hicho cha Baraza la madiwani kilicho kuwa kinaongozwa na makamu mwenyekiti wa Halimashauri ya mji wa Mpanda Yusuph Ngasa.

Alikuwa ni Diwani wa Kata ya Shanwe Abel Kapini Diwani Kapini alidai kuwa taarifa hiyo inamapungufu ambayo yatawafanya madiwani kama wataamua kuijadili washindwe kuijadili kitaalamu kwani haina mchanganuo ambao utawawezesha madiwani kuhoji taarifa hiyo ya kamatiya fedha na mipango Kwa upande wake diwani wa Kata ya Ilembo Wensilaus Kaputa alilieleza Baraza hilo kuwa taarifa hiyo haiko wazi kwani inaonekana taarifa zake zimefichwa kwa hari hiyo ni vizuri irudishwe ikaandaliwe upya.

Mwenyekiti wa kikao cha baraza la madiwani baada ya kutolewa hoja hizo aliwashauri madiwani wapige kura ili kujua ni madiwani wangapi wanao unga mkono hoja hiyo ya kuikataa taarifa hiyo.

Kufuatia uamuzi wa mwenyekiti madiwani walipiga kura ambapo kulikuwa na madiwani kumi kwenye kikao hicho na madiwani wanane waliunga mkono kuikataa taarifa hiyo na madiwani wawili waliikubali Nae Mkugenzi wa Halimashauri ya Mji wa Mpanda Selamani Lukanga alihaidi kuwa kikao kijacho cha Baraza hilo watasomewa taarifa ikiwa na viambatanisho na mchanganuo kama ambavyo walivyo hitaji madiwani.


Source:Katavi Yetu

RENAMO YAFANYA SHAMBULIO HUKO MSUMBIJI

Ripoti kutoka Musumbiji zinaarifu kuwa wanaharakati waliojihami kutoka kundi la upinzani la Renamo, wameshambulia kituo kimoja cha polisi katika mji wa kati wa Maringue.

Kisa hicho kinajiri siku moja baada ya Renamo kusema kuwa inajiondoa katika mazungumzo ya amani ya mwaka 1992 yaliosababisha kusitishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Renamo ilikaidi makubaliano hayo baada ya vikosi vya serikali kushambulia kambi iliokuwa na kiongozi wake Afonso Dhlakana na kumlazimu kutoroka.

Hali ya wasiwasi kati ya serikali na Renamo imeongezeka katika siku za hivi karibuni huku mapigano yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali.

Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni moja waliuawa katika vita hivyo vya miaka 16 vilivyo sababisha mazungumzo ya amani huku Renamo ikibadilika kutoka kundi la wanamgambo hadi chama cha kisiasa.

SIMBA, YANGA WAINGIZA SH. MILIONI 500

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya watani wa jadi Simba na Yangailiyochezwa jana (Oktoba 20 mwakahuu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar esSalaam na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 imeingiza sh. 500,727,000.Washabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 63kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000na sh. 30,000.Ni tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B namoja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayondiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo.

Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko laThamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.


Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.18,766,611.51 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.14,596,253.39.

WASHAMBULIWA WAKATI WAKITOKA KANISANI

Waumini walishambuliwa wakiwa wanatoka kanisaniWatu watatu akiwemo msichana mdogo mwenye umri wa miaka 8 aliuawa wakati watu waliokuwa wamejihami wakiwa kwenye pikipikikushambulia sherehe za ndoa nje ya kanisa la Kikopti mjini Cairo.

Takriban wengine 9 walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo mjini Giza.

Hata hivyo hakuna taarifa zozote kuhusu nani aliyehusika na shambulizi hilo.

Jamii ya wakristo wa kikopti wamekuwa wakishambuliwa na baadhi ya waisilamu wanaotuhumu kanisa kwa kuunga mkono jeshi katika kumpindua aliyekuwa Rais Mohammed Morsi mwezi Julai.

Washambuliaji hao ambao hawakutambuliwa, waliwafyatulia risasi kiholela watu waliokuwa wanaondoka kanisani.

Mwanamume mmoja na mtoto huyo waliuawa nje ya kanisa hilo wakati mwanamke mmoja akifariki akipelekwa hospitalini. "Tulisikia mlio mkubwa sana mfano wa kitu kilichokuwa kinaanguka,'' alisema shahidi mmoja.

"Nilimkuta mwanamke mmoja akiwa ameketi kwenye kiti chake, akiwa amejeruhiwa kwa risasi. Watuwengi walikuwa wameanguka kandoyake akiwemo mtoto mdogo.

''Kasisi wa kanisa hilo Thomas Daoud Ibrahim alisema kuwa alikuwa ndani ya kanisa hilo, wakati, milio ya risasi ilikuwa inasikika.

"Kilichofanyika ni kitu kibaya sana na sio waksristio wakopti waliolengwa pekee yao , tunaharibunchi yetu,'' alisema kasisi huyo.Kasisi mwingine aliambia vyombo vya habari kuwa kanisa hilo liliachwa bila polisi wala mlinzi tangu mwishoni mwa mwezi Juni.

Kanisa hilo ni moja ya makaisa ya zamani ya kikristo iliyoanzishwa mjini Alexandria mapema miaka ya 50 AD.

Idadi ya wakristo nchini Misri ni asilimia 10 ikiwa waumini milioni 80, na wamekuwa wakiishi kwa amani na waisilamu wa kisunni kwa miaka mingi.

Hata hivyo, kuondolewa mamlakani kwa Morsi kijeshi, kumefuatiwa na mashambulizi mabaya dhidi ya makanisa na rasilimali za waumini hao kwa miaka mingi.

Wakati mkuu wa majeshi Generali, Abdul Fattah al-Sisi, alitangaza kwenye televisheni kuwa rais Morsi aliondolewa mamlakani baada ya maandamano makubwa yakimtaka ajiuzulu aliandamana na papa Tewadros.

Tewadros alisema kuwa mkakati uliofikiwa na Al-asisi ulitokana na mawazo ya viongozi waheshimiwa ingawa hakuwataja.

WANAJESHI WA KENYA WALIENDA KUPORA AU KUOKOA WESTGATE?

Picha za wanajeshi wa Kenya waliokwenda katika jumba la Westgate katika juhudi za uokozi na kisha baadaye kuonekena kwenye kamera za CCTV wakiondoka na mifuko ya plasitiki yenye bidhaa za madukani, bila shaka zimewashangaza wengi.

Picha hizo mwanzo zimeonyesha wanajeshi wakiingia ndani ya jengo hilo wakiwa wamebeba silaha kukabiliana na wanamgambo walioshambulia jengo hilo wiki nne zilizopita na baadaye wakitoka wakiwa wamebeba mifuko hiyo wakiwa na silaha zao kwa wakati mmoja.

Hata hivyo haijulikani walichokuwa wamekibeba kwenye mifuko hiyo.

Pamoja na picha za wanajeshi wakiwa wamebeba mifuko, pia kulikuwa na picha zengine zilizoonyesha mashine ya pesa zikiwa zimeporwa ndani ya mikahawa huku picha za alama za risasi kwenye maeneo ya kuhifadhiapesa, pia zikionekana.

Inaarifiwa ilikuwa jaribio ya kufungua hifadhi hizo ambalo halikufanikiwa.

Madai haya ya wanajeshi kufanya uporaji wa maduka katika jingo hilo, yalikanushwa vikali na jeshi la Kenya kiasi cha kutaka hatua kuchukuliwa dhidi ya waliokuwa wanatoa madai hayo, lakini haijulikani jibu lao litakuwa nini hasa kwa picha hizo za CCTV zilizoonyesha wanajeshi hao wakifanya uporaji.

Wamiliki wa maduka waliorejea kwenye maduka yao baada ya shambulizi , walidai kuwa maduka yao yaliporwa ingawa jeshi lilikanusha madai hayo baadhi ya taarifa zikisema kuwa ilikuwa njamaya wafanyabiashara kudai fidia kwa mali zao zilizoharibika.

Sio wanajeshi pekee waliotuhumiwakwa uporaji, kwani polisi mmoja naye alifikishwa mahakamani kwa kosa la uporaji baada ya kupatikana na pochi la mtu liliokuwa na damu.

Wangambao wa Al Shabaab walitekanyara jengo la Westgate kwa siku nne na kusababisha vifo vya watu 60 pamoja na kuwajeruhi zaidi ya watu miamoja.

WAKAMATWA NA SHEHENA YA BUNDUKI NA NYARA ZA SERIKALI

WAKAZI tisa Wilaya ya Handeni na Kilindi mkoani Tanga wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka kwa kosa la kukutwa na bunduki zaidi ya 25 na nyara nyingine za Serikali kinyume cha sheria.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, Nzagalila Kikwelele mbele yaHakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Handeni, Patrick Maligana kuwa, Oktoba 11, mwaka huu katika nyakati tofauti wilayani Handeni na Kilindi, Jeshi la Polisi, maofisa wanyamapori na misitu walifanya msako wa kutafuta wawindaji haramu katika maeneo hayo na kufanikiwa kuwakama watu hao.

Alidai kuwa, katika msako huo watu tisa walikamatwa wakiwa na nyara mbalimbali za Serikali ikiwemo ngozi za pongo, tandala na nyati, pembe za nyati, meno matano ya ngiri na vifaa vya kutengenezea magobore, pia walikamata magobore zaidi ya 25 yakiwa katika makazi yao.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa, hadi sasa upelelezi kuhusu watu hao umekamilika na kwamba, mahakama inaweza kuendelea na mchakato wa usikilizaji wa shtaka hilo.

Akitoa hukumu kwa mtuhumiwa wa kwanza, Iddi Abdalah (51), Hakimu wa mahakama hiyo, Patrick Maligana alidai kuwa, anamtia hatiani kwa kosa la kukutwa na ngozi tatu za tandala zenye thamaniya zaidi sh. milioni 25 na bunduki aina ya gobore ambazo ni nyara za Serikali.

Alipotakiwa kujitetea kabla ya kupewa hukumu, mtuhumiwa alidaikuwa, anaomba kupunguziwa adhabu kwani ana watoto watano wadogo na kwamba, hawana mlezi.

Baada ya utetezi huo, hakimu alisema anamhukumu kwenda jela miaka 20 ama alipe faini ya zaidi ya sh. milioni 125, ambapo mtuhumiwa alisema hana fedha hizo. Wengine waliohukumiwa ni Muya Kidundo (63), ambaye amehukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la kukutwa na meno matano ya ngiri na ngozi ya swala.

Mwingine ni mkazi wa Negero, Bakari Mwikalo (50), ambaye alihukumiwa miaka saba jela kwa kosa la kukutwa na silaha bila kuwa na kibali. Pia, alimhukumu Selemani Mzimba (45), kwenda jela miaka sita kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.


HakimuMaligana alimuachia Hamza Msami (70), kutokana mazingira ya kosa lake kuwa dogo na umri wake mkubwa, kwani hakuisumbua mahakama katika kujua ukweli wa kesi yake na kwamba, watuhumiwa wengine wapo nje dhamana.

Watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika operesheni okoa maliasili inayoendeshwa nchini koteambapo katika Wilaya ya Handeni na Kilindi, watu tisa walikamatwa.


Chanzo:Jambo leo

P-NESTA KUKIMBIZA SAN NSIRO

Yule star wa Jini kisirani na raha mustarehe kutoka Mpanda Katavi na kundi zima la Katavi for Real anakumua show yake siku ya jumapili tarehe 20 Oktoba kuanzia saa saba mchana, kiingilio ni bure.

Njoo utoe support yako kwa P-Nesta wakati akishambulia jukwaa, Na timu nzima ya Clouds fm katika shindano la Fiesta Super Nyota ni pale pale San Nsiro Sinza Jijini Dar es salaam.

Wote mnakaribishwa, Utamcheki akikamua Jini kisirani aliyoshirikiana na Sabria kutoka Mjomba Band, Raha Mustarehe aliyopiga na marehemu Ngwair na Nyingine kibao, atasindikizwa na wasanii kadhaa ya ndani ya Dar

KATI YA VIJANA 10, 6 WANAPIGA PICHA AU VIDEO YA NGONO NA KUISAMBAZA

Sita kati ya vijana 10 wanasema kuwa wameombwa picha au video za kingono. Hii ni kwa mujibu wa utafiti a kitengo kuhusu maslahi ya watoto Uingereza ambao BBC iliweza kuuona

Kati ya waliohojiwa , asilimia arobaini walisema kuwa walijipiga picha au kunasa video wakiwa katika vitendo vya ngono na karibu robo yao walimtumia mtu picha hizo kwanjia ya SMS au ujumbe mfupi.

Mkuu wa kitengo hicho, Peter Wanless, alisema kuwa "sexting" au jambo la vijana kutuma ujumbe wenye mada ya ngono limekuwa la kawaida miongoni mwa vijana Uingereza.

Matokoe haya yanaonyesha kuwa tabia hii inafanyika sana miongoni mwa vijana na ni moja ya mambo ambayo vijana hufanya katika mahusiano yao.

Katika utafiti huu vijana 450 walihojiwa kuhusu tabia hiyo kote nchini.

Miongoni mwa wale waliohojiwa kuhusu kutuma picha zao za ngono au video kwa njia ya simu asilimia hamsini walisema kuwa waliituma picha hiyo kwa wapenzi wao wanaume au marafiki zao wa kike, lakini thuluthi moja wakasema kuwa walimtumia mtu wasiyemjua kwenye mtandao wa internet.

Lakini wataalamu wanasema kuwa watu wanawadhalilisha vijana kwa kuwataka wawatumie picha zao kwa kutumia vitisho.

Miongoni mwa wale waliosema kuwa walimtumia mtu picha yao, , asilimia 20 walisema kuwa waligundua watu walichangia picha zao wakati wengine wakisema hawajui zilikokwenda picha zao.

Kulingana na sheria za Uingereza ni halali kujihusisha na ngono ukiwa na umri wa miaka 16 lakini ni kinyume na sheria kupiga picha za ngono au kuchangia picha za ngono za kijana walio chini ya umri wa miaka 18.

Hata hivyo, ilisemekana kuwa vijana hawawezi kuchukuliwa hatua kwa kutuma picha zenye mada ya ngono miongoni mwao.

MAMA YAKE UFOO SARO ALIPIGWA RISASI TANO

TAARIFA zaidi za kusikitisha kuhusumauaji ya kinyama, yaliyofanyika katika familia ya Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, UfooSaro zimeendelea kutolewa, ambapo imebainika mama mzazi wa mtangazaji huyo, Anastazia Saro(58), aliuawa kwa kupigwa risasi tano.

Msemaji wa familia hiyo, Idd Lemaalisema hayo jana wakati wa ibada ya kumuaga Anastazia, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibwegere, Dar es Salaam.

Awali, taarifa zilizokuwepo, zilidai Anastazia alipigwa risasi mbili kifuani, lakini Lema alisema baada ya uchunguzi wa mwili huo uliofanywa na Polisi, ilibainika kuwa alipigwa risasi tano na si mbili.

Akizungumza wakati wa ibada ya kumuaga Anastazia, ambayo mwanawe wa pekee Ufoo hakuweza kuhudhuria, Mwinjilisti wa Kanisa hilo, Margaret Shekoloa alisema Anastazia atakumbukwa kwa mambo mengi, aliyoyafanya katika Kanisa hilo katika nafasi mbalimbali alizokuwa nazo ukiachaya muumini.

Alisema siku moja kabla ya kifo chake, Anastazia alikwenda kanisani na kupanda maua katika bustani ya kanisa na kupamba madhabahu.

"Alipomaliza kupamba madhabau pamoja na kupanda maua katika bustani, aliniaga na kuniambia mchungaji tutaonana katika ibada ya kesho bila kujua kuwa siku hiyo hataiona," alisema Mwinjilisti Shekoloa.

Alisema matukio ya ukatili, kwa sasa yamezidi kuongezeka nchini na chanzo chake ni watu kutokuwa karibu na Mungu wao. Alisema matukio hayo, yanayowagusa watu wengi wasio na hatia, pia yamekuwa yakichangia uvunjifu waamani.

"Anastazia alikuwa na malengo makubwa na Kanisa hili, aliwaunganisha wanawake wote kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali," alisema Shekoloa.

Alisema hata pale alipohitajika na kanisa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana, aliitikia mwito bila tatizo lolote.

Ibada ya kuaga mwili huo ilimalizika saa 11.30 jioni na mwili huo kusafirishwa kwenda kijiji cha Shali, Machame mkoani Kilimanjaro.

WARUHUSIWA KULA PAKA NA MBWA

Wengi wamenaswa katika vitongoji vinavyokumbwa na vita na kukosa chakula kwa muda mrefuKikundi cha viongozi wa dini nchini Syria kimetoa Fatwa inayowaruhusuwatu wanaoishi katika vitongoji vya mji mkuu Damscus vinavyokumbwana vita kula nyama ambayo kwa kawaida huwa imeharamishwaKwenye kanda ya video, viongozi hao walisema kuwa watu wanaokumbwa na njaa wanaweza kula nyama ya Paka,Mbwa na Punda.

Fatwa hiyo imetolewa huku kukiwa na ripoti za watu kukumbwa na njaa katika kitongoji cha Muadhamiya mjini Damsacus moja ya vitongoji vilivyotekwa na waasi Mashirika ya misaada yameitaka serikali kuruhusu misaada ya kibinadamu kupelekwa katika eneo hilo , ambako wenyeji wamekwama.

Mamia ya raia , hata hivyo walifanikiwa kutoroka maeneo hayomwishoni mwa wiki baada ya vita kusitishwa kwa muda.

Katika ujumbe wao wakati wa sherehe za Eid al-Adha viongozi wa kidini waliwashauri wenyeji wa eneo la Ghouta kula nyama ambazokwa kaiwada huwa haziliwi katika dini ya kiisilamu.

Viongozi hao walisema huu ni wito kwa dunia nzima na kuongeza kuwa ikiwa hali itaendelea ilivyo, watu wanalio hai watalazimika kula wafu.Sio mara ya kwa fatwa kama hii kutolewa kwenye mzozo wa Syria.

Fatwa sawa na hii iliwahi kutolewa mjini Homs na Aleppo wakati mapigano yalikuwa mabaya zaidi katika miji hiyo.Mashirika ya misaada ambayo yamekuwa yakitoa msaada wa chakula katika maeneo ya vita yamesema kuwa lazima jambo hilo liwe muhimu kama ilivyo kuharibu silaha za kemikali za Syria.

WIZARA YA AFYA YATANGAZA UWEPO WA HOMA YA UTI WA MGONGO MKOANI RUKWA

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa Ugonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo mkoani Rukwa. Ugonjwa umedhibitika kuwepo baada ya Vipimo vya Maabara kuonyesha uwepo wa vijidudu vya homa ya uti wa mgongo kwenye sampuli za wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa Sumbawanga. Hadi kufikia tarehe 08/10/2013 jumla ya wagonjwa 21 wameripotiwa katika hospitali ya Mkoa na kati yao wanne (4) wamefariki dunia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote yaTanzania hususani mikoa iliyo mpakani na mkoa wa Rukwa na vilevile wasafiri wanaotarajiwa kwendamkoani Rukwa.

Homa ya Uti wa Mgongo

Homa ya Uti wa Mgongo inasababishwa na bakteria aitwaye Neisseria meningitidis. Bakteria huyu ndiye anayeleta milipuko mikubwa ya Homa ya Uti wa mgongo.

Ugonjwa huu hatari unaathiri zaidi meninji na husababisha athari kubwa kwa ubongo. Ugonjwa huu unapatikana kwa binadamu tu. Asilimia 50 za wagonjwa hupoteza maisha iwapo matibabu hayataanzishwa mapema.

Dalili kuu ni Kukakamaa kwa shingo, Homa kali, Kutokupenda mwanga mkali, Kuchanganyikiwa, Kichwa kuuma pamoja na Kutapika.

Ugonjwa huu unaweza kuathiri ubongo na kupelekea kupoteza uwezo wa kusikia au kupoteza kabisa uwezo wa kuelewa na kunyambulisha vitu mbalimbali. Iwapo ugonjwa huu utaathiri ubongo na meninje kwa kiasi kikubwa, umauti hutokea.

Dalili za ugonjwa ni kati ya siku 2 hadi 10 baada ya kupata maambukizi.

Ugonjwa huu unaenezwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu kwa njia ya hewa au kwakugusa majimaji/mate kutoka kwa mtu ambaye tayari ni mgonjwa. Ugonjwa huu unaenea kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine kwa urahisi na kwa kasi sana iwapo mtuatakuwa karibu na mgonjwa mwenye maambukizi kwa muda mrefu. Uambukizo unaweza kutokana iwapo mgonjwa atapiga chafya au mate ya mgonjwa huyu kuguswa. Aidha kasi ya maambukizi pia inatokea iwapo mtu ataishi kwa karibu ndani ya nyumba moja na mgonjwa na kushirikiana naye kwa kula chakula kwenye chombo kimoja.

Ugonjwa huu unatibika iwapo mgonjwa atawahi hospitalini na kupewa dawa.

Hatua zinazochukuliwana WizaraKutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara hususan mikoa inayopakana na Rukwa.

Aidha taarifa hii pia imewakumbusha waganga wakuu warejee miongozo yao ya kudhibiti Ugonjwa wa Homaya Uti wa Mgongo yaani namna ya utambuzi wa mgongwa na, uchukuaji wa sampuliKuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani.

Kutuma Timu ya Taifa ya Maafa ambayo imeenda kuungana na timu za Mkoa na Wilaya za Rukwa katika kukabilana na ugonjwa huu.

Aidha timu hiyo imeondoka tarehe 10.10.2013.

Kutuma chanjo pamoja na dawa na vifaa Kinga kwa mkoa wa Rukwa ili kuweza kukabilana na ugonjwa huu Elimu ya Afya inaendelea kutolewa katika maeneo ambayo yamekumbwa na mlipuko na pia mashuleni, vyuoni, magerezani, nakwenye mikusanyiko na msongamano wa watu.

Aidha wananchi wanashauriwa kujenga nyumba bora zenye madirisha yanayoingiza hewa na mwanga wa kutosha.

Kufungua kambi maalamu mkoani Rukwa kwa ajili ya wagonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo.

Wananchi wanashauriwa kutoa taarifa pindi kutoa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Wadau wengine wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha ugonjwa huu unathibiwa mkoani Rukwa na kwa mikoa mengine.