RAGE, TAMBWE WAPATA AJALI

WABUNGE Wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba kupata ajali.

Wabunge hao ni Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage na Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe. Majeruhi wengine katika ajali hiyo ni Issa Chimwaga (31), Mwanahamisi Ramadhani (34), John Hoya (32) ambaye ni dereva ambapo pia hakuumia katika ajali hiyo.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya alisema jana mchana walipokea majeruhi wannewa ajali hiyo wakiwemo Wabunge Rage na Munde.

Alisema majeruhi hao walitokana na ajali waliyoipata katika eneo la Chigongwe Manispaa ya Dodoma walipokuwa wakisafiri kwenda Dodoma kwa gari binafsi.

Dk Mpuya alisema vipimo vimeonesha Munde pamoja na kupata majeraha usoni na kichwanipia amevunjika mkono wakati Rageameteguka bega la kushoto. Hata hivyo, alisema hali zao zinaendelea vizuri na wanaendelea na matibabu.

Hata hivyo, Rage na Munde wamelazwa katika Wodi namba 18 Grade One chumba namba moja na mbili wakiwa na majeraha mbalimbali mwilini. Akizungumza akiwa wodini Rage alisema amepata majeraha katika bega la kushoto na eneo la nyuma ya mgongo.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada yadereva wa gari lao anataka kulipita lori lakini ghafla dereva wa lori hilo akaingia katikati ya barabara.

Alisema dereva wao alipoona hivyo badala ya kuligonga lori aliamua kwenda pembeni ndipo gari lao likaruka na kuingia kwenyekorongo na kupinduka.

Alisema kilichowasaidia walikuwa wamefunga mikanda jambo ambalo. Kwa upande wake Tambwe alikuwa akilalamikia maumivu katika sehemu za kichwani na mkono.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma, Peter Sima alipotakiwa kuzungumzia ajali hiyo alisema bado anakusanya taarifa na kuahidi kutoa taarifa baadaye.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa familia za wabunge hao iliyopatikana baadaye jana, ilisema wabunge hao walichukuliwa kwa ndege maalumu jana jioni kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar kwa matibabu zaidi.

DAKTARI AAMBUKIZWA EBOLA NIGERIA

Daktari mmoja jiji Lagos Nigeria amepatikana ameambukizwa na maradhi ya homa ya Ebola.

Daktari huyo ambaye alimtibu mfanyikazi wa wizara ya hazina nchini Liberia aliyepatikana na homa hiyo ya Ebola na kuwa mtu wa kwanza kuaga dunia nchini Nigeria sasa amedhibitishwa kuambukizwa.

Waziri wa afya nchini humo Onyebuchi Chukwu amesema kuwa daktari huyo pamoja na watu wengine 70 waliokutana na marehemu wametengwa kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Patrick Sawyer alitua nchini Nigeria Julai tarehe 20 na akafa tarehe 25 katika hospitali moja mjini Lagos.

Mlipuko huu wa ugonjwa wa ebola katika ukanda wa magharibi mwa Afrika umesababisha vifo vya watu zaidi ya 826 katika mataifa ya Guinea, Liberia na Sierra Leone.

MAHASIMU WA SUDAN KUSINI KUKUTANA TENA

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi yameanza tena katika nchi jirani ya Ethiopia.

Mazungumzo hayo, yalikuwa yameahirishwa kwa wiki kadhaa Vita vimeendelea nchini Sudan Kusini licha ya makubaliano ya kusitisha vita kufikiwa kati ya pande husika.

Zaidi ya watu milioni moja unusu, wameachwa bila makazi kutokana na vita hivyo.

Umoja wa Mataifa na mataifa mengine ya Magharibi yameonya kua Sudan Kusini inakabiliwa na tisho la kukumbwa na njaa.

Maafisa wa baraza la usalama la Umoja huo, wanatarajiwa kuzuru nchi hio wiki ijayo.

Katika mazungumzo hayo, serikali na waasi wanatarajiwa kuzungumzia swala la kubuni serikali ya mpito pamoja na muundo wake Makataa ya makubaliano hayo ni chini ya wiki moja na huenda muda huo usifikiwe.

DAKTARI FEKI ADAKWA MANYARA

Jopo la madaktari katika hospitali ya rufaa ya mkoani Manyara kwa kushirikiana na polisi wamefanikiwa kumnasa mkazi wa jijini Dar-es-salaam Bw Godlove Sozigwa akituhumiwa kuomba kufanya mazoezi ya kutibu kwa muda kama daktari wa magonjwa ya moyo na figo kwa kutumia vyeti bandia wakati akitambua kuwa yeye si mtaalam wa tiba.
Bw Godlove Sozigwa kabla ya kukamatwa kwake asubuhi kufuatia jopo hilo la madaktari kubaini kuwa vyeti alivyoviwasilisha katika hospitali hivyo julai 31 ni bandia na hata hivyo alipoitwa na kufanyiwa mahojiano amedai huku akionyesha ukomavu wa kujieleza taaluma hiyo aliipatia katika chuo cha sayansi, tiba na utafiti cha Muhimbili na kufuzu hata hivyo alibahatika serikali kumpeleka nchini India kwa mafunzo zaidi kusomea dawa zaidi.

Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoani Manyara Dr Peter Mshali akizungumza na ITV baada ya kukabidhiwa kwa polisi ili kufanyiwa upelelezi amesema katika mahojiano na jopo la madaktari walibaini vyeti hivyo ni bandia aidha pia mtuhumiwa Dr huyo Godlove Sozigwa si mtaalam kulingana na maelezo yake bali ni tapeli na hatari endapo angebahatika kupata nafasi hiyo.

Nae kamanda wa polisi mkoani hapa afande Deusdedit Nsimeki amekiri na katika mahojiano amesema polisi imebaini baada ya kumfanyia mahojiano na upekuzi kumkuta na kompyute mpakato(laptop) muhuri wa kuchonga wa hospitali ya rufaa ya Muhimbili, koti na vyeti mbalimbali,lakini wanafanya upelelezi zaidi kabla ya kumfikisha mahakamani.

Tangu awali ITV iliyoshughudia mtego huo mapema asubuhi na baada ya mtuhumiwa Godlove Sozigwa kufikishwa polisi amekiri kuwa yeye si daktari aliyesoma chuo hicho cha Muhimbili bali anafanya hivyo kutokana na mazingira magumu, hasa kwa kuipenda taaluma ya udaktari baada ya kujifunza katika kituo cha tiba cha Neptune cha matabibu ya kichina kilichopo Ubungo Plaza jijini Dar-es-salaam na kupata uzoefu.

Chanzo: ITV

RAIS KIKWETE AKANUSHA KUMUOKOA RIDHIWANI CHINA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Sina muda kujadili upuuzi huu kuhusu Ridhiwani–Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni mkusanyiko wa upuuzi mtupu madai kuwa yeye Rais alishiriki kumwokoa mtoto wake, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ambaye alikuwa amekamatwa na madawa ya kulevya nje ya nchi.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Urais ni taasisi kubwa sana nchini na hivyo yeye akiwa Rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya watu wanamsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.


"This is nonsense–ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,"amesema Rais Kikwete usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi katika Marekani kwenye Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington D.C.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa katika Marekani alitoa majibu hayo baada ya kuwa ameulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi, 2012 na Katibu Mkuu wa Chama cha CHADEMA, Wilbroad Slaa, madai hayo yamempeleka mahakamani.
Amesema Rais Kikwete:"

Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga.

Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.'

Amesisitiza Rais Kikwete:
"Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa."


Kuhusu swali jingine aliloulizwa kuhusu suala hilo, kuwa Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete amesema:

"Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani. Haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania."


Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu–Dar es Salaam.
04 Agosti, 2014

JK, OBAMA KUKUTANA NA MARAIS WA AFRIKA

RAIS Jakaya Kikwete yuko Marekani kwa ziara ya siku tisa nchini humo ambako miongoni mwa mambo mengine, atahudhuria Mkutano waKwanza wa Kihistoria wa Viongozi wa Bara la Afrika na Marekani ulioitishwa na Rais Barack Obama.

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika kuanzia leo ukianza na mkutano wa biashara kati ya Afrikana Marekani. Unafuatiwa na mkutano wenyewe wa Marekani naAfrika utakaofanyika kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles mjini Washington, Rais Kikwete alipokewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Kwenye ziara hiyo, Rais Kikwete ameongozana na mkewe, Mama Salma Kikwete ambaye naye atakuwa na programu tofauti wakati wa ziara hiyo, kama watakavyokuwa wake wa viongozi wengine wa Afrika wanaohudhuria mkutano huo.

Mkutano huo wa kwanza wa aina yake kati ya kiongozi wa Marekani na viongozi wa Afrika umepangwa kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi 47 ambazo zote zimealikwa naRais Obama kushiriki mkutano huo.

Mbali na shughuli zake nyingi za mjini Washington, Rais Kikwete atasafiri kwenda Dallas, Jimbo la Texas, ambako atakutana na Rais wa 43 wa Marekani, George W. Bush, kabla ya kuendelea na safari katika mji mwingine mkubwa wa jimbo hilo wa Houston.

Mjini Houston, Rais Kikwete atafanya mkutano wa kimkakati wakibiashara na wafanyabiashara maarufu mbalimbali hasa wa sektaya gesi na mafuta kabla ya kumaliza ziara yake.

Miongoni mwa shughuli zake, Mama Salma Kikwete atahudhuria mkutano wa wake wa marais wa Afrika na mke wa Rais wa Marekani, Michelle Obama utakaofanyika kwenye Kituo cha John F Kennedy.

Mkutano huo utahudhuriwa pia na mke wa Rais George W. Bush, Mama Laura Bush.

''UKAWA WAMEPOTOSHA'' JK

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, waliojiundia kundi la Umojawa Katiba ya Wananchi (UKAWA), warudi katika Bunge hilo, watumie mifumo maalumu waliyojiwekea na kanuni walizojitungia wenyewe, kutafuta maridhiano.

Ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hotuba yakealiyoitoa kwa Taifa katika utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na wananchi kila mwisho wa mwezi.


Rais Kikwete amewataka wajumbe hao, watafute maridhiano kwa kutumia mifumo hiyo rasmi, na yeye yupo tayari kusaidia pale watakapohitaji msaada wake kuhusu suala hilo, ili Watanzania wapate Katiba bora wanayoihitaji.Ameonya kuwa ikiwa maridhiano wanatafuta nje ya mifumo hiyo, watakuwa wakitumia mitandao tu isiyokuwa na faida kwao wala jamii.

Mbali na kuwapa onyo hilo, pia aliwakumbusha kuwa Bunge Maalumu la Katiba lina mamlaka ya kutunga Katiba, na kama isingekuwa hivyo kusingekuwa na haja ya kuwa na siku 70 za awali nayeye kupewa mamlaka ya kuongeza siku 60 kujadili.

Alionesha kuwashangaa wajumbe hao kwamba, kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba waliitunga wenyewe na sasa katika utekelezajiwa sheria hiyo, wanasusia vikao jambo alilosema si haki kwa ummawa Watanzania.

Kikwete alisema yeye si Mwanasheria hivyo anakiri kwamba anaweza kuwa na upungufu katika kuelewa maana yabaadhi ya maneno ya kisheria, lakini akasema hakumbuki kuwepokwa kifungu chochote katika Sheria, kinachosema kuwa Bunge Maalumu la Katiba halina mamlakahayo.

"Tangu tuliposikia maneno hayo yakisemwa (kwa Bunge Maalumu haliwezi kubadilisha rasimu ya Katiba), nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa madai hayo lakini bado sijaambiwa vinginevyo. Kama ukweli huo upo naomba wanisaidie," alisema Rais Kikwete.

Alisema badala yake ameambiwa kuwa maneno yaliyotumika katika Sheria, hayaakisi dhana inayotolewa kuwa kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kubariki Rasimu na si kufanya vinginevyo."Nimeambiwa kuwa sheria inasema Tume itaandaa Rasimu ya Katiba na Bunge Maalumu la Katibalitatunga Katiba iliyopendekezwa," alifafanua Kikwete.

Akielezea hatua iliyofikiwa kabla yakuahirishwa kwa Bunge hilo Aprili 25 mwaka huu kupisha Bunge la Bajeti na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Rais Kikwete alisema wakati baadhi ya wajumbe wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, wakisusia vikao Aprili 16, kazi kubwa ilikuwa imefanyika."Tayari kamati zote 12 za Bunge hilo zilikuwa zimekamilisha kujadiliSura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume. Sura hizo zinazungumzia utambulisho wa nchi na muundo wa Muungano.

"Kamati zote zilipiga kura ya kupitisha uamuzi wao kuhusu sura hizo mbili. Kamati kadhaa ziliweza kupata theluthi mbili ya kura kwa wajumbe wa pande zote mbili za Muungano, jambo lililoonesha dalili njema kwamba Katiba mpya inaweza kupatikana," alisisitiza Kikwete.Alisema kazi iliyobaki baada ya taarifa ya kila Kamati kuwasilishwa kwenye Bunge zima, ni Kamati ya Uandishi kukamilisha taarifa yake na kuiwasilisha kwenye Bunge zima kwa ajili ya kujadiliwa.

Alisema ikijadiliwa wajumbe watapiga kura kuamua kuhusu Sura hizo mbili kwa kutumia theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano.

Kuhusu Ukawa kususia vikao vya Bunge hilo, Rais Kikwete alisema sababu walizotoa zimekuwa zikiongezeka na kubadilika kadri siku zinavyosonga mbele na upepowa kisiasa unavyokwenda.

"Hivi sasa wanazungumzia mambo mawili. Kwanza, kwamba Bunge Maalumu halina mamlaka ya kuifanyia mabadiliko yoyote Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa naTume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa maoni yao, kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu ya Katiba ya Tume na siyo kubadili chochote.
Pili, wametoa sharti la wao kurudi bungeni ni kuhakikishiwa kwamba, kitakachojadiliwa bungeni ni Rasimu ya Tume. Bila ya sharti hilokukubaliwa, wamesisitiza kutorudi bungeni," alieleza Kikwete.

Akifafanua suala hilo, Kikwete ambaye alihusika kubuni wazo la kuwa na mchakato wa kuandika Katiba mpya, na katika maandalizi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ya kuongoza na kuendesha mchakato huo, alisema hakuna popote katika vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba walipozungumzia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuwa haiwezi kufanyiwa marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.

Alisema ndio maana suala hilo limewekwa kisheria kwa uwakilishi mpana kupitia ngazi nne muhimu za mchakato wa kutunga Katiba hiyo ikiwamo wananchi kutoa maoni, Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na Mabaraza ya Kitaasisi kutoa maoni yao kuhusu Rasimu yakwanza ya Katiba iliyotayarishwa naTume.

Bunge Maalumu na Kura ya Maoni itakayoshirikisha wananchi wote ambao ndio wenye kauli ya mwisho kuhusu Katiba wanayoitaka.

Alisema mamlaka ya kutunga Katiba kwa mila na desturi za mabaraza ya kutunga sheria, ni uwezo wa kurekebisha, kubadili, kufuta na hata kuongeza kilichopendekezwa. Alisema kama ingekuwa kilichokusudiwa ni kubariki tu, kusingekuwa na haja yaneno "kutunga Katiba" wala kura inayohitaji theluthi mbili.

Kikwete alisema anapata shida kuelewa mkanganyiko unatokea wapi kutokana na ukweli kwamba wale wanaoongoza kuhoji mamlakaya Bunge Maalumu, ni wale wale waliotunga Sheria ya Mabadiliko yaKatiba tena hatua kwa hatua.

Alisema siku zote za mjadala kilichokuwa kikijadiliwa ni Sura ya Kwanza na Sura ya Sita hivyo haiingii akilini kudai kuwa kinachojadiliwa bungeni humo si Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.

Aliwataka Ukawa kuwa wakweli kwaWatanzania na kueleza kabla huenda katika Kamati kumefanyikamarekebisho kwenye Rasimu ambayo hayakuwapendeza kuliko kusema mambo yasiyowakilisha ukweli halisi wa Rasimu inayojadiliwa na kuwafanya watu waamini kinachojadiliwa si rasimu hiyo ya Jaji Warioba na kwamba ni matakwa ya CCM.

Kikwete alisema kama Ukawa hawakuridhishwa na yaliofanyika, walipaswa kutumia mifumo waliyojitengenezea wenyewe kwenye Kanuni kumaliza tofauti zao.

"Kanuni zinaelekeza kuwa mambo wasiyoridhika nayo yajadiliwe kwenye Kamati ya Mashauriano na Maridhiano. Ukiacha mifumo ya maridhiano ndani ya Bunge ukaenda nje kwa wananchi au vyombo vya habari na mitandao si jawabu la tatizo," alisema Kikwete.Aliwasihi Ukawa warejee bungeni na watumie mifumo maalumu ya Bunge iliyowekwa na Kanuni kutafuta maridhiano na wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama vingine vya siasa na hasa CCM kutafuta maelewano.

"Mimi niko tayari kusaidia pale watakapoona inafaa kufanya hivyo kama ambavyo nimekuwa nikifanya siku za nyuma," alisema Kikwete.Alisisitiza kuwa ili kupata Katiba mpya inayohitajika, maelewano baina ya wadau wakuu wa kisiasa nijambo lisilokuwa na badala yake. Vinginevyo kupata theluthi mbili kwa pande zote mbili za Muunganohaitawezekana.Alimpongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa uamuzi wa kuvikutanisha vyama vinne vikuu vya siasa kujadili suala hilo.

"Ombi langu kwa viongozi wa vyama hivyo ni kuitumia vyema fursa ya majadiliano kuukwamua mchakato kwa maslahi ya nchi yetuna watu wake," alisisitiza Kikwete na kumpongeza Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kwa juhudi za kusaka maridhiano ingawa wajumbe waliosusia vikao hawakushiriki, alimtaka asikate tamaa.Kikwete alisema amesikia madai kwamba hotuba yake ya ufunguzi ndio iliharibu mchakato na kwamba ameikana Rasimu ya Katiba ambayo na yeye ni mmoja wa watu waliotia saini.

Nadhani ndugu zetu wanaotoa madai haya wameitafsiri isivyo, saini yangu katika Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema katika kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza ajitambulishe kuwa yeye ni nani na atie saini yake. Kwa kufanya hivyo, hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila kinachopendekezwa na Tume.Jambo lingine linalofanana na hilo ni yale madai kwamba nilikuwa napata taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume mara kwamara, iweje leo nitoe maoni tofauti kama niliyoyatoa katika hotuba yangu kwenye Bunge Maalumu.

Ni kweli kabisa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, Makamu wake, Mheshimiwa Jaji Agustino Ramadhani na Mheshimiwa Dk Salim Ahmed Salim wamekutana na mimi kwa nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato. Lakini, hayakuwa mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo ya Tume, alieleza Kikwete.

Alisema Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza alipokabidhiwa rasmi, tena kwa uwazi na kwamba watu wasijenge dhana kuwa alipewa Rasimu na kuisoma kabla ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni yake Tume hii ilikuwa huru na niliiacha iwe hivyo.

Sikuiingilia kwanamna yoyote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo. Kuthibitisha dhamira yangu ya kutaka Tume iwe huru katika kufanya kazi zao hata pale waliponitaka nitoe maoni niliwaomba tusifanye hivyo ili nisiwakwaze katika kufanya kazi zao, wakapata taabu ya kuwianisha wanayofikiria na mawazo yangu, alisema Kikwete. Kuhusu hotuba yake kuvuruga mchakato, Kikwete alisema madai hayana ukweli wo wote wala msingi kwani hakuna chaajabu alichofanya siku alipohutubiaBunge hilo.

Ukweli ni kwamba nilisema yale yale ambayo Tume yenyewe imeyasema katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume.

Niliyoyasema kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano na uzuri na changamotoza miundo ya serikali mbili na serikali tatu ni yale yale yaliyomo kwenye taarifa za Tume.

Nimetumia takwimu zile zile za Tume.

Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiri taarifa hizo na mapendekezo ya Tume, alisema Kikwete.Alisema haoni kosa lake kutoa maoni kuhusu baadhi ya vipengele vya Rasimu hususan uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo kwa kuwa ilitolewa hadharani ili ijadiliwe.

Lakini, pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo dhamana ya uongozi na ulezi wa taifa letu. Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatma ya nchi yetu nilinyamazie kimya. Watanzania wangeshangaa na wangekuwa na haki ya kuhoji Rais wao ana maoni gani. Bahati nzuri nilitoa maoni yangu mahali penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye Bunge Maalumu la Katiba.Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kuwa namna nilivyotoa maoni yangu sikuwa natoa maagizo wala kushurutisha, ndiyo maana kila wakati niliwakumbusha Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao.

Yangu yalikuwa maoni tu wanahiariya kuyakubali au kuyakataa, alisema Kikwete.Kuhusu muundo wa serikali tatu, nilieleza wazi kuwa sina tatizo nao kama ndiyo matakwa ya Watanzania. Lakini, nilieleza hofu yangu kuhusu mapendekezo ya Tume na kuwataka Wajumbe wafanye kazi ya ziada kuondosha udhaifu iwapo wataukubali muundo unaopendekezwa.

Nilieleza nia yangu ya kutaka tuwe na Serikali ya Muungano yenye ukuu unaoonekana, yenye nguvu ya kuweza kusimama yenyewe, inayoweza kuwa tegemeo kwa nchiwashirika, Serikali isiyokuwa tegemezi wala egemezi kwa nchi washirika na ambayo inavyo vyanzo vya uhakika vya mapato.

Hivi kwa kutoa ushauri huo kwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba inageuka kuwa nongwa. Kwakweli sielewi lawama ni ya nini, alibainisha Rais. Alisema anachoamini hastahili lawama bali pongezi kwa kuwa muwazi na kutoaushauri wa msingi ambao utasaidianchi kupata Katiba nzuri inayojali maslahi ya watu wa nchi yetu na yanchi zetu mbili zilizoungana miaka 50 iliyopita.

Rais alitaka mgogoro uliopo sasa katika mchakato wa Katiba usiendelee kwani malalamiko ya wajumbe wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi yanaweza kushughulikiwa kwa ukamilifu katika mifumo ya Bunge hilo. Nawasihi waitumie. Hali kadhalika, kwa kupitia mazungumzo wanayofanya na wenzao wa CCM wanaweza kutengeneza nguvu ya pamoja kutatua changamoto za sasa na zitakazojitokeza baadaye.

Kilicho muhimu ni kwa pande zote kuwa na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tulipo sasa. Kama utashi wa kisiasa upo kwa kila mmoja wetu, hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Narudia kuahidi utayari wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele, alihitimisha Rais Kikwete.

MVIETNAM ADAKWA NA KUCHA NA MENO YA SIMBA

RAIA wa Vietnam, Dong Van (47) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa na meno 65 na kucha 447 za simba zote zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 189.

Kamanda wa Polisi Makao Makuu ya Viwanja vya Ndege, Hamisi Seleman alisema Van alikamatwa juzi saa 10 jioni akijiandaa kusafiri kwa ndege ya Shirika la Qatar kwenda Vietnam.

Alisema Polisi ilimkamata raia huyo wa nje mwenye hati ya kusafiria No.B 9306216 iliyotolewaVietnam, akiwa katika eneo la kuondokea abiria.

Baada ya kupekuliwa, inadaiwa alikutwa akiwa amehifadhi nyara hizo kwenye pakiti saba za kahawa na moja ya mchele aina ya 'Pure Basmati'.

Inadaiwa alichanganya na pakiti zingine 15 za vyakula mbalimbali.

"Baada ya kupekuliwa raia huyo alipatikana na meno 65 na kucha 447 za simba akiwa amevihifadhi katika hali ya umaridadi katika begilake la nguo ambapo ndani yake pia kulikutwa suruali mbili," alisema Selemani.

Aidha alisema uchunguzi wa suala hilo unaendelea ukihusisha vyombo mbalimbali vya usalama pamoja na watu kutoka Idara ya Maliasili kubaini mahali alipotoa nyara hizo.

Kulingana na tathmini iliyofanywa, inaonesha simba 21 wameuawa. Kwa mujibu wa Kamanda, mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuandaa mashitaka kabla ya kuwasilisha jalada la kesi yake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DPP).

"Tunawaomba Watanzania kuwa makini katika suala zima la ulinzi wa maliasili kwa kuwa sasa inaonekana ujangili haufanyiki kwa tembo peke yake bali hata kwa wanyama wakali kama simba ambao hapo awali hatukuwahi kuusikia," alisisitiza Selemani.

Pi alitaka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa pamoja waweze kuzuia uhalifu unaofanywa kupitia maeneo mbalimbali ya mipaka.

WATUHUMIWA ULIPUAJI MABOMU ARUSHA WATAJWA

WATUHUMIWA 19 wa ulipuaji mabomu mkoani Arusha, majina yao yamewekwa hadharani jana na leo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Watuhumiwa hao ni pamoja wanaodaiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika viwanja vya Soweto, wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa Chama cha Demokrasiana Maendeleo (Chadema) uliofanyika Juni 15, 2013.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema askari Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa watuhumiwa wengine akiwemo mtuhumiwa Yahaya Hella, ambaye anatafutwa sana na polisi akihusishwa na matukio mbalimbali ya ulipuaji mabomu.

Alifafanua kwamba mahojiano kati ya polisi na watuhumiwa hao, ndiyo yaliyotoa mwanga wa kukamatwa kwa watuhumiwa wengine na kuunganishwa katika kesi mbalimbali ambazo tayari zilishapelekwa mahakamani.

Mbali na mashitaka ya kulipua mabomu, Kamanda Sabas alisema watuhumiwa hao leo watakabiliwa pia na mashitaka ya kumwagia watu tindikali na kuhamasisha vitendo vya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, baadhi ya watuhumiwa walishiriki katika tukio zaidi ya moja hali inayoonesha ulikuwa mtandao.

Hata hivyo tofauti na ilivyotarajiwa, Chadema iliposhirikishwa katika kuwapata watuhumiwa, kutokana na madai kwamba ina ushahidi wa aliyetupa bomu katika viwanja vya Soweto, viongozi wa chama hicho walishindwa kutoa ushahidi.

Akizungumza jana katika utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na Taifa kila mwisho wa mwezi, Rais Jakaya Kikwete, alisema watuhumiwa waliokamatwa safari hii, wanaelekea kutoa sura nzuri zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili jijini Arusha na kwingineko nchini. Alipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri ya kukamata watuhumiwa wa mashambulio ya mabomu.

"Kila lilipotokea shambulizi uchunguzi ulifanyika na watuhumiwa kukamatwa. Lakini, watuhumiwa waliokamatwa safari hii wanaelekea kutoa sura nzuri zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili pale Arusha na kwingineko nchini," alisema Rais Kikwete.

Alisema watu 38 wameishafikishwa Mahakamani, wengine watafikishwa mahakamani kesho na uchunguzi na msako unaendelea kote nchini kuwapata watuhumiwa wengine.

Ameomba vyombo hivyo viongeze bidii, maarifa na ushirikiano mpaka wote waliohusika wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Aidha Rais Kikwete alishukuru wananchi waliotoa taarifa zilizowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa.

"Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wananchi wenye taarifa kuhusu wanaotafutwa au yeyote anayejihusisha na vitendo hivi viovu watoe taarifa kwenye vyombo vya usalama ili hatua zipasazo zichukuliwe," alisema Rais Kikwete.

Tukio la kwanza ni la mlipuko wa bomu uliotokea nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo, Oktoba 25 mwaka 2012, ambapo watuhumiwa wanne walikamatwa.

Watuhumiwa hao ni Yusuph Huta (30), mkazi wa Ngusero, Kassim Ramadhan (34), mkazi wa Kaloleni na Shekhe wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa na Abdul-Aziz Mohamed (49), ambaye ni mkazi wa Faya ambaye pia alikuwa ni Imamu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa.

Tukio la pili ni la mlipuko wa bomuuliotokea katika Kanisa Katoliki la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti Mei 5 mwaka jana ambapo watuhumiwa 12 wanadaiwa kuhusika.

Watuhumiwa hao ni Huta (30), ambaye anadaiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo na Ramadhan Waziri (28) ambaye ni mkazi wa Kwa mrombo.

Wengine ni Abdul Humud (30) ambaye ni wakala wa mabasi ya Mohamed Trans ambaye pia aliwahi kufikishwa mahakamani akishitakiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama.

Pia yupo Jafar Lema (38) aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Quba, ambaye pia alifikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na tukio la bomu katika mgahawa wa Vama, Said Ramadhan (34) ambayeni mwendesha bodaboda Standi Kuu Arusha na Kassim Ramadhan (34) ambaye ni dereva wa bodaboda eneo la Friends Corner, Arusha.

Watuhumiwa wengine ni Abashar Omar (24) ambaye ni dereva wa bodaboda Stendi Kuu Arusha, Abdulrahaman Hassan (41), mfanyakazi wa Benki ya Stanbic Arusha na Morris Muzi (44) mkazi wa Kilinzi mkoani Kigoma.

Pia yupo Niganya Niganya (28) mkazi wa Businde Ujiji mkoani Kigoma, Baraka Bilango (40), ambaye ni mkazi wa Kalinzi mkoani Kigoma na Hassan Omar (40) mkazi wa Ilongero mkoani Singida.

Tukio la tatu ni la mlipuko wa bomu Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema Juni 15 mwaka jana, ambalo viongozi wa kitaifa wa chama hicho walidai kuwa na ushahidi wa mhusika wa bomu hilo.

Watuhumiwa waliokamatwa na Polisi, baada ya Chadema kukataa kutoa ushirikiano ni Huta (30) mkazi wa Ngusero, ambaye pia anadaiwa kushiriki katika ulipuaji wa bomu nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo na katika Kanisa la St Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Mwingine ni Humud (30) ambaye ni wakala wa mabasi ya Mohamed Trans, ambaye pia aliwahi kufikishwa mahakamani akishitakiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama, na pia anadaiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Wengine ni Jafar Lema (38) mkazi wa Ngulelo, Arusha, Said Temba (42), ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Kilombero, Morogoro ambaye pia alifikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama.

Pia yupo Kassim (34) mbaye ni dereva wa bodaboda eneo la Friends Corner na anatuhumiwa pia kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti na Ramadhan Omar (24), mkazi wa Arusha.

Wengine ni Hassan (41) ambaye ni mfanyakazi wa Benki ya Stanbic na Muzi (44), Niganya (28) na Bilango (40) wanaotokea Mkoa wa Kigoma na Omar (40) anayetokea Singida, ambao pia wanadaiwa kushiriki ulipuaji bomu katika Kanisa Katoliki la St, Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Tukio la nne ni la kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Said Makamba, lililotokea katika Msikiti wa Kwamrombo Julai 11/2013. Watuhumiwa wapo wanne ambao ni Huta (30) anayedaiwa kushiriki katika mlipuko wa bomu uliotokea nyumbani kwa Shekhe Abdulkarim Jonjo, mlipuko wa bomu uliotokea katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti na mlipuko wa bomu katika viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema.

Mwingine ni Waziri (28) anayedaiwa pia kushiriki katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti.

Mtuhumiwa mwingine ni Kassim (34) mbaye ni dereva wa bodabodaeneo la Friends Corner na anatuhumiwa kuhusika katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti na mlipuko wa bomu katika viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema na Jafar Lema (38)Tukio la tano ni la kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Mustapha Kiago wa Msikiti Mkuu Februari 28 mwaka huu, ambapo watuhiwa wanne wametajwa ambao ni Huta (30), Kassim Ramadhan (34), Jafar Lema (38) na Hassan Mfinanga (57).

Tukio la sita ni la bomu Arusha Night Park lililotokea Aprili 13 mwaka huu, ambapo watuhumiwa wawili ambao ni Jafar Lema (38) naIbrahim Lenard maarufu kwa jina la Shekhe Abuu Ismail (37) mkazi wa mabatini Mwanza watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.

Katika tukio la sita ni bomu nyumbani kwa Shekhe Sudi Ally Sudi, lililotokea Julai 3 mwaka huu,ambapo watuhumiwa nane watafikishwa mahakamani akiwepo Yahaya Twahir (37) ambaye ni mfanyabiashara mtaa wa Bondeni na Idd Yusuph (23), mkazi wa mtaa wa Jaluo.

Wengine ni Said Temba (42), ambaye ni mfanyabiashara katika Soko la Kilombero, Morogoro ambaye pia alifikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama na pia ametajwa katika tukio la bomu Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema.

Mwingine ni Anwar Hayael (29) ambaye ni mfanyabiashara, Jafar Lema (38), Hassan Mfinanga (57) ambaye pia ametajwa katika tukio la kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Mustapha Kiago wa Msikiti Mkuu.

Wengine ni Yusuph Ramadhan (23) mkazi wa Ngusero na Omar (24) ambaye ametajwa pia katika tukio la mlipuko wa bomu Viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa Chadema.

Kukutwa na mabomu Tukio la nne ni la kupatikana kwa mabomu Julai 21 mwaka huu, ambapo watuhumiwa 10 watafikishwa mahakamani wakiwemo mume na mke.

Watuhumiwa hao ni Huta (30) ambaye anatajwa katika matukio mengi na mkewe Sumaiya Ally (19)wakazi wa Ngusero na Waziri (28) anayedaiwa pia kushiriki katika ulipuaji wa bomu katika Kanisa Katoliki la St Joseph Mfanyakazi Olasiti na kumwagiwa tindikali kwa Shekhe Said Makamba.

Pia yupo Mfinanga (57) na Omar (24), Muzi (44) na Niganya (28) ambao wametajwa katika matukio kadhaa, Kimoro Mchana (25) mkaziwa Itolwa Kondoa, Hassan Omar (40) mkazi wa Mkoa wa Singida na Baraka Ntembo (40) mkazi wa Arusha.

Kosa la tisa ni la kuhamasisha vitendo vya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii, ambalo watakaotakiwa kujibu mashitaka yake ni Lenard (37), anayetajwa katika tukio la bomu la Arusha Night Park, Hayel (29) anayetajwa katika tukio la bomu nyumbani kwa Shekhe Sudi na Yasin Shaban (20), mkazi wa Arusha.

Kamanda Sabas alisema operesheni ya kukamata watuhumiwa wengine bado inaendelea nchi nzima, na tayari wanayo majina ya watuhumiwa kadha ambao wametoweka Arusha kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

ISRAEL: HATUONDOKI GAZA MPAKA TUYAHARIBU MAHANDAKI

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema kuwa Israel imeamua kuyaharibu kabisa mahandaki na njia za chini yaardhi zilizojengwa na wapiganaji wa Palestina-Hamas, katika mipaka yake huko Gaza.

Amesema uharibifu huo utatekelezwa na majeshi ya Israeli kukiwa au kutokuwa na muafaka wa kusitisha mapigano.

Netanyahu amesema hayo huku Serikali ya Israel ikishikia kani kuwa kuwa itaendeleza mashambulizi katika eneo la Gaza licha ya shutma za kimataifa kufuatia shambulizi la shule moja ya umoja wa mataifa ambapo takriban watu 15 walipoteza maisha yao.

Msemaji wa serikali ya Israel amesema kuwa wataomba msamaha iwapo watabaini kwamba shambulizi hilo, lilitekelezwa kimakosa na wanajeshi wa Israel.

Umoja wa mataifa umesema kuwa ni wazi kwamba ni jeshila israel ndilo lililorusha kombora hilo katika shule hiyo ambapo zaidi ya raia elfu tatu wa Palestina walikuwa wameomba hifadhi.

Licha ya malalamiko kutoka kote duniani kuhusiana na idadi kubwa ya vifo vyaNjia za chini kwa chini za Hamas ambazo Israeli inalenga kuharibu

Mashambulizi ya Israel kutoka angani na nchi kavu yamerindima kwa milipuko ya mizinga na ndege za kivita.

Na sasa Israel inajiandaa kwavita zaidi baada ya kuwaamuru wanajeshi wa akiba kujiunga na jeshi la taifa. Katika ukanda wa ngazani kilio na majonzi makubwa...

AJALI YAUA 19

JUMLA ya watu 19 wamekufa katika ajali mbili tofauti zilizotokeamkoa wa Dodoma na Arusha jana.

Ajali hizo mbili zimesababisha majeruhi zaidi ya 70.

Ajali ya kwanza mbaya ilihusisha basi la abiria na lori ambapo watu 17 walikufa na wengine 56 kujeruhiwa. Katika ajali hiyo basi laabiria na lori yaligongana uso kwa uso.

Aidha, katika ajali ya Arusha, madereva wa magari mawili yaliyogongana maeneo ya Sadeki wilayani Arumeru, walikufa na wakati huo huo watu 14 wamejeruhiwa.

Basi Morobest

Ajali ya mkoani Dodoma ilihusisha basi la Morobest lililokuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam, na ilitokea eneo la Pandambili, Wilaya ya Kongwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi jana. Kati ya 17 waliopoteza maisha, wanaume ni 12.

Basi hilo lenye namba za usajili T258 AHV likiendeshwa na Said Lusogo, liligongana na lori namba T820CKU/ T390CKT likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, likiendeshwa na Gilbert Nemanya. Madereva wote wawili wamekufa.

Kwa mujibu wa Kamanda Misime, kufikia jana mchana miili 11 ilikwishatambuliwa. Majina ya waliokufa Waliotambuliwa ni dereva wa lori hilo, Nemanya pamoja na utingo wake, Mikidadi Zuberi. Wengine ni dereva wa basi la Morobest, Lusogo na kondakta wake, Omary Mkubwa.

Marehemu wengine waliotambuliwa ni Merina Malikeli,Nasib Machenje, Wilson Suda, Gabriel Mejachiwipe, Justine Makasi na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina moja la Christina.

Kwa mujibu wa Misime, watu 56 wamepata majeraha mbalimbali na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kutokuwa na hadhari kwa magari yaliyokuwa yanakuja mbele yake wakati anapita gari lingine.

Majeruhi

Majeruhi 23 wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Majina yao ni Frank Raymond, Patricia Ngamwai, Amos Chiwaga, Mary Mateo, Safari Jonas, Suzan Charles, Gasper Shao,Felician Rite, Felister Mathias, Amos Jonas, Edina Lwande, Seleman Kaseni, Nazareth Kasua, Saimon Msoloka, Juma Mtezi na Swalehe Bakari.

Wengine ni Naseria John, Getruba Kombo, George Njelewa, Manase Makuja, Chibago Mchiwa, Nicholous Roger na Michael Chibwela.

Ajali Arusha

Kwa upande wa ajali ya mkoani Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ilitokea juzi saa 3 usiku maeneo ya Sadeki kwa Fundi.

Alisema gari aina ya Subaru lenye namba za usajili T842 CCP lililokuwa likiendeshwa na David Natal (35) liligongana na gari ya Nissan Mini Bus lenye namba za usajili T355 CGA lililokuwa likiendeshwa na aliyetambuliwa kwa jina moja la Joshua.

Alisema ajali hiyo ilitokea wakati Natal aliyekuwa anatoka Arusha mjini kwenda Makumira, alipojaribu kupita gari lililokuwa mbele yake ndipo lilipogongana nagari lililokuwa linatoka Usa River kwenda Arusha mjini.

Mbali na vifo vya madereva hao, ajali hiyo ilisababisha majeruhi 14 waliokuwa kwenye gari aina ya Nissan Mini Bus.

Majeruhi hao ni Frida Joseph (18), Elisante Mungure (45), Lilian Mathias (29), Juma Mohamed (42), Silvia Kelvin (26), Charles Massawe (40), Kelvin Charles (29), Emmanuel Adedia (29), Zainabu Issa (40), Regard Joseph (30), Elirehema Abrod (29), Alfred Lucas(21), Gipson Tackson (3) na Salma Abdallah (44).

Kamanda alisema majeruhi hao wanatibiwa katika Hospitali ya Tengeru na Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

AJINYONGA BAADA YA MKEWE KUMUACHA

MKAZI wa Kijiji cha Vikonge, Kata ya Mpandandogo wilayani Mpanda,Joseph Lukato (52) amejinyonga kwa kujitundika mtini akitumia mtandio wa mkewe baada ya kughadhabika na kuachwa naye.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Focas Malengo, alisema tukio hilo lilitokea Julai 27,mwaka huu saa mbili asubuhi kijijini hapo ambapo alijinyonga katika shamba la jirani yake.

Kamanda huyo alisema Lukato alikuwa na ugomvi wa muda mrefuna mkewe Mary Joseph (42) aliyekuwa akimtuhumu kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanaume mwingine kijijini hapo.

Alisema siku ya Julai 19, mwaka huu, Lukato alirejea nyumbani kwake saa nane mchana akitokea shambani na kula chakula ambapo alimlalamikia mkewe kuwa kilikuwa kibichi.

Alisema hatua hiyo ilizua ugomvi baina ya wanandoa hao ambapo Lukato alimwambia mkewe kwamba amempikia chakula kibichi kwa kuwa alichelewa kurudi nyumbani kutoka mwanaume huyo mwenye uhusiano naye wa kimapenzi.

Kamanda Malengo alisema mke waLukato alijitahidi kujijitetea kwa mumewe kuwa hakuwa ametoka nyumbani kwake siku hiyo na kumhakikishia mumewe kuwa chakula kilikuwa kimeiva.

Inadaiwa Lukato hakukubaliana na utetezi wa mkewe na aliendelea kumshutumu na baadaye akaanza kumpiga katika ugomvi uliochukua muda mrefu hatua iliyomfanya mke wa Lukato kurudi nyumbani kwa wazazi wake kwa kuhofia usalama wa maisha yake.

"Lukato alijitahidi kufanya jitihada za mara kwa mara za kumshawishi mkewe arudi nyumbani kwake ili wakaendelee kuishi kama walivyokuwa wakiishi awali lakini mkewe alikataa kurejea, hatua iliyomfanya Lukato kujinyonga," alisema Kamanda.

Alisema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Chanzo: Habari leo

AJIRA ZA UHAMIAJI ZAFUTWA

Imeelezwa kuwa kufutwa kwa ajira hizo kunatokana na madai ya kuwa kuna upendeleo ulifanyika.

MASHAMBULIZI YAANZA TENA GAZA

Ndege za kivita za Israel zimeshambulia maeneo matatu tafauti kwenye Ukanda wa Gaza, kwa kile jeshi la nchi hiyo linachosema ni kujibu kombora moja lililorushwa na Hamas na kuangukia kwenye mji wa pwani wa Ashkelon, kusini mwa Israel hivi leo.

Majibizano ya risasi yalisikika kati ya pande hizo mbili, licha ya kutajwa kwamba zimesitisha mapigano kwa muda kupisha siku tatu za Sikukuu ya Eid al-Fitr zilizoanza leo, baada ya kukamilika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Juhudi za kimataifa zimeongezeka kusitisha mapigano hayo ya wiki tatu kwenye Ukanda wa Gaza. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano hayo mara moja na bila ya masharti yoyote.

"Baraza la Usalama linaunga mkono kikamilifu wito wa washirika wa kimataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa mapigano mara moja na bila masharti yoyote ili kuruhusu uwasilishwaji wa bidhaa zinazohitajika haraka kwenye kipindi hiki cha Eid al-Fitr na hata baada ya hapo," amesema Eugene-Richard Gasana, ambaye ni balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa na rais wa sasa Baraza la Usalama.

Jioni ya jana, Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kumueleza wasiwasi wake juu ya idadi kubwa ya Wapalestina waliouwa na kujeruhiwa. Tayari Wapalestina 1,030 na Waisraili 43 wameshauawa hadi sasa.

USALAMA WAZIDI KUZOROTA LIBYA

Kiasi ya watu 150 wameuawa katika ghasia ambazo zimezuka upya katika miji ya Benghazi na Tripoli katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kufuatia makabiliano makali kati ya wanajeshi na makundi hasimu ya wanamgambo.
Wizara ya afya ya Libya imesema tangu makabiliano hayo kuzuka wiki mbili zilizopita, kiasi ya watu 94 wameuawa katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na zaidi ya wengine 400 wamejeruhiwa wakati wa mapambano kati ya wanajeshi na wanamgambo wanaong'angania kuudhibiti mji huo.
Kiasi ya wengine 55,wengi wao raia wameuawa katika mji wa Benghazi mwishoni mwa juma katika makabaliano mengine kati ya jeshi na makundi ya wanamgambo wa kiislamu.

Maroketi yalenga mapipa ya mafuta
Shirika la taifa la mafuta limesema maroketi yaliyokuwa yakirushwa, yalilenga matangi ya kuhifadhia mafuta karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli hapo jana na kusababisha moto mkubwa ambao wazima moto wameshindwa kuuzima. Matangi hayo yalikuwa yanahifadhi kiasi cha lita milioni sita za petroli na yako karibu na mengine yanayohifadhi gesi na diesel.
Abiria wakisubiri kusafiri katika uwanja wa ndege wa Miitiga
Abiria wakisubiri kusafiri katika uwanja wa ndege wa Miitiga
Wizara ya mafuta na nishati imewaonya raia wanaoishi karibu na maeneo ya matangi hayo kuondoka mara moja kuepusha majanga ya kibinadamu na kimazingira kufuatia kuzuka kwa moto huo mkubwa.
Mapigano hayo ya wiki mbili ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu kung'olewa na baadaye kuuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa tafa hilo Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Marekani,Umoja wa Mataifa na Uturuki zimewaondoa wafanyakazi wa balozi zao kutoka taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Marekani iliwahamishia wafanyakazi hao katika nchi jirani ya Tunisia siku ya Jumamosi chini ya ulinzi mkali baada ya mapigano kupamba moto karibu na ubalozi wake mjini Tripoli.
Msafara wa magari yaliyokuwa yamewabeba maafisa wa Uingereza ulishambuliwa jana katika jaribio la utekaji nyara nje ya mji wa Tripoli ulipokuwa ukielekea Tunisia na ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika kisa hicho, magari yaliharibiwa.
Wajumbe maalumu wa jumuiya ya nchi za kiarabu kuhusu Libya,Marekani na umoja wa Ulaya wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali inavyozidi kuzorota nchini Libya na kusema hali hiyo imefikia hatua ngumu na kutaka mapigano kusitishwa mara moja.

Nchi za magharibi zawataka raia wake kuondoka

Ujerumani, Uingereza ,Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Misri na Uturuki nimiongoni mwa nchi nyingine ambazo zimewataka raia wao walioko Libya kuondoka nchini humo mara moja kwa sababu ya kudorora kwa hali ya usalama.
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Misrata
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Misrata

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema raia wa Ujerumani walioko Libya wako katika hatari kubwa ya kutekwa nyara na kuuawa kwa sababu sio rahisi kutabiri hali nchini humo itachukua mkondo gani.
Bunge jipya la Libya lililochaguliwa mwezi Juni mwaka huu linatarajiwa na nchi za magharibi kuwa litaweza kumaliza mzozo huo kwa kufikiana makubaliano ya kisiasa wakati wabunge watakapokutana kwa kikao cha kwanza mwezi ujao.
Miaka mitatu baada ya kung'olewa kwa Gaddafi,ndoto ya Libya kuifikia demokrasia imezongwa na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe ya kisiasa na mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi hasimu ya waasi waliosaidia kumuondoa Gadafi madarakani ambayo yanataka kuidhibiti miji mikuu na viwanda vya mafuta.

MAREKANI WAFUNGA UBALOZI LIBYA

Marekani imefunga ubalozi wake wa Libya kwa muda na wafanyakazi wake wote wamehamishiwa nchi jirani, Tunisia.Walipelekwa huko kwa magari huku wakilindwa na ndege za Marekani.

Wizara ya mashauri ya nchi za nje ya Marekani piya imewasihi raia wote wa Marekani waondoke nchini humo.

Jengo la ubalozi wa Marekani mjini Tripoli liko katika eneo ambalo limeathirika na mapambano kati ya makundi ya wapiganaji yanayozozana, ambayo yamekuwa yakigombania kudhibiti uwanja wa ndege wa kimataifa wa Libya.

Waziri wa mashauri ya nchi za nje, John Kerry, alisema kulikuwa na hatari hasa ikiwakabili wafanyakazi wa ubalozi huo, lakini alisisitiza kuwa shughuli za ubalozi zinasimamishwa kwa muda tu.

Miaka miwili iliyopita balozi wa Marekani aliuwawa pale ofisi ndogo ya ubalozi wa Marekani katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya, iliposhambuliwa na wapiganaji Waislamu.

MUUZA BANGI AKWEPA JELA, ALIPA FAINI

MUUZA JI wa bangi, Ferdinand Makundi (40) amenusurika kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada kulipa faini ya Sh 100,000 kwa kosa la kukutwa na kilo mbili za bangi.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama yaWilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, Ramadhani Rugemalira alimhukumu mkazi huyo wa kijiji cha Mkole wilayani humo kutumikia kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh 100,000 baada ya kukiri kosa.

Awali Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi, Hamimu Gwelo alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Mei 14 mwaka huu saa 7:00 mchana akiwa nyumbani kwake kijijini Mkole.

Alipotakiwa kujitetea, mshitakiwa aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kuwa ana watoto kumi na mke wanaomtegemea.


Chanzo: Habari Leo

WATALII 17 WAPORWA NA MAJAMBAZI

Kundi la watu wanaoaminika ni majambazi wakiwa na bunduki wamevamia Hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge iliyopo wilayani Hai na kuwapora watalii fedha na vitu vingine.

Majambazi hao walipora Sh5.4 milioni, Dola 3,200 za Marekani sawa na Sh5 milioni na Pauni za Uingereza 110 sawa na Sh300,000.


Pia walipora kamera moja yenye thamani ya Sh1.5 milioni, kamera ya video yenye thamani ya Dola 3,000 sawa na Sh4.8 milioni na kamera nyingine sita za kisasa.

Taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz zilisema watalii 17 kutoka mataifa mbalimbali waliporwa huku watalii wanne wakijeruhiwa katika tukio hilo.

"Ni kweli hilo tukio lipo na tumeanzisha msako mkali wa kuwatafuta watu hao pamoja na vitu walivyoiba na tunaomba yeyote mwenye taarifa sahihi za majambazi hao watusaidie," ma Boaz.


Tukio hilo lilitokea juzi saa 9:30 alfajiri baada ya majambazi hao kufanikiwa kuingia katika hoteli hiyo na kuwakusanya watalii wote waliokuwa wamelala na kuwaweka katika hema moja.

Baada ya kuwakusanya katika tenti hilo, majambazi walirudi katika mahema ambayo watalii hao walikuwa wamefikia na kuanza kupora kila kitu zikiwamo saa na simu za mkononi.

Wakati majambazi hao wakiendeleana uporaji, walijitokeza watalii wanne ambao walikuwa wanawahi ndege Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kutibua harakati hizo.


"Hao watalii waliokuwa wanakwenda KIA wao walikuwa wamelala vyumbani kwa hiyo walipopanda kwenye gari na lilipowashwa tu wale majambazi wakataharuki," ilidokezwa.

Chanzo kimoja katika hoteli hiyo kimedokeza kuwa, baada ya gari hilo kuwashwa, majambazi hao waliokuwa na bunduki na mapanga waliliendea gari hilo na kuvunja kioo cha gari hilo.


Baada ya kuvunja kioo hicho, majambazi hao walianza kuwapora watalii hao lakini sauti za kuvunjika kwa kioo cha gari ndiko kunakodaiwa "kuwashtua" walinzi wa hoteli hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, Novatus Makunga aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili watu hao waweze kukamatwa.

SERIKALI YAIFUNGIA HOSPITALI YA IMTU

Serikali imeifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), baada ya kuifanyia ukaguzi na kubaini kasoro kadhaa za uendeshaji wake.


Ukaguzi huo ulifanywa jana na jopo la wataalamu kutoka Manispaa ya Kinondoni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya IMTU kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ukaguzi huo ulifanywa jana na jopo la wataalamu kutoka Manispaa ya Kinondoni, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya IMTU kukumbwa na kashfa ya utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Hospitali hiyo imefungiwa wakati Kamati ya Watu 15, iliyoundwa na Serikali ikiendelea kuchunguza kashfa hiyo.


Hata hivyo, wakati taarifa za kufungiwa zikitolewa habari za ndani zinaonyesha kuwa hapakuwa na mgonjwa yeyote hospitalini hapo, ikielezwa kuwa wagonjwa wote waliondoka baada ya kuibuka kwa kashfa ya viungo IMTU ikihusishwa.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Bunini Kamba alisema kuwa wameamua kuifungia hospitali hiyo kwa muda usiojulikana, baada ya kukuta upungufu mbalimbali katika maeneo ya kutolea huduma, jambo linalohatarisha usalama wa wagonjwa.

"Maabara tumekuta dawa ambazo muda wake wa kutumika umepita na hazikuwa katika mpangilio maalumu. Wodini hakuna usimamizi maalumu, hasa kwa wagonjwa wenye majeraha," alisema Dk Bunini.


Aliongeza: "Hakuna wauguzi wa kutosha na mashine ya kuchoma taka ngumu haifanyi kazi vilivyo. Tumeona kuwa hospitali hii haistahili kuendelea kutoa huduma kwa jamii."

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Yasin Mgonda alisema: "Tumesikia uamuzi huo uliotolewa baada ya kufanyika ukaguzi. Tutajirekebisha na tutakapokamilisha tutawaita kuja kutukagua tena."

Alisema kuwa pamoja na sababu nyingine, hospitali yake imefungiwa baada ya kubainika kuwa bomba la maabara limeharibika na halitoi maji.


Nyingine ni kutojaza vitabu vya wagonjwa kwa mujibu wa taratibu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pia duka lake la dawa kuwa halijasajiliwa lakini akasema sababuhiyo imewashangaza kwani wanachojua wao duka hilo limesajiliwa.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia aliliambia gazeti hili kwamba anaipongeza Serikali kwa uamuzi huo akisema utanusuru maisha ya wananchi waliokuwa wakipata huduma hospitalini hapo.

"Tunaipongeza Serikali, ila tunaiomba iwatafutie wanafunzi wachuo hicho maeneo mengine ya kujifunzia," alisema Dk Saidia.

Juzi, Dk Saidia alisema kuwa wote waliohusika na kashfa ya utupaji mabaki ya viungo vya binadamu wanastahili kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kitendo hicho kimekiuka sheria, taratibu, haki za binadamu, maadili ya ufundishaji na taaluma ya udaktari.


"Kama ni taasisi ya utafiti imepoteza sifa ya kufanya utafiti nakama ni ya mafunzo basi imepoteza sifa ya kutoa mafunzo ya tiba.
Kama ni hospitali itakuwa imepoteza sifa za kutoa tiba kwa binadamu," alisema Dk Saidia.

Naye spika wa serikali ya wanafunziwa chuo hicho (IMTUSO), William Mapunga alisema kuwa kufungiwa kwa hospitali hiyo kutawaathiri, kwani watakosa sehemu ya kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo, akiiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwa mapana.


Chanzo: Mwananchi

MABAKI YA NDEGE YA ALGERIA YAONEKANA

Mabaki ya ndege iliyopotea ikiwa na watu 116 njiani kutoka Burkanafaso kwenda Algers yamepatikana nchini Mali.

Maafisa wa Jeshi wa Burkina faso wamesema ndege hiyo iliyokuwa chini ya shirika la ndege la Algeria imeanguka karibia kilomita 50 kutoka mpaka wa Burkanafaso.


Waongoza ndege walipoteza mawasilino na ndege hiyo muda mfupi baada ya kupata taarifa kutoka kwa Rubani kuwa alikuwa kwenye eneo lenye hali mbaya ya hewa.

Utafutaji wa ndege hiyo umeanzia katika eneo la Gao mpaka Tessalit. Kumekuwepo na hali mbaya ya hewa kwa zaidi ya saa 24. Waziri wa mambo ya nje wa ufaransa, Laurent Fabius amesema inaonekana ndege ilihamishwa mwelekeo kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.

„Walikuwa wameelekezwa kubadili njia ya kawaida kutoka na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ndege ilikuwa ikipaa juu ya eneo la Malian. Pamoja na juhudi kubwa , mapaka sasa hakuna dalili za kupatika na kwa ndege hiyo.


Pengine ndege imeangua"Ameongeza kuwa waziri wa ulinzi wa ufaransa alikuwa akisaidia katika utafutaji wa ndege hiyo. "Waziri wa ulinzi wameviruhusu vyombo vyao kwenda kwenye eneo kuitafuta ndege. Majeshi ya Algeria na Umoja wa mataifa wanafanya hivyo pia. Ndege mbili za jeshi la ufaransa zilizopiga kambi Niyame hivi sasa na tangu asubuhi zimekua zikiitafuta ndege hiyo.

Majeshi yetu katika eneo hilo ikiwamo vifaa vya matibabu vyote viko tayari

"Hapo awali, waziri mkuu wa Algeria Abdelmalek Sellal alitoa ufafanuzi wa tukio la kuanguka kwa ndege hiyo."


Usiku wa jana kama saa 9 ndege ya Hispania iliyokodiwa na Shirika la Ndege la Algeria ilikuwa katika safari yake kati ya Ouagadougou na Algiers.

Ilipoteza mawasiliano na Rada muda huo wa saa tisa usiku dakika 10 tu baada ya kupaa.

Mawasiliano ya mwisho ilikuwa na mnara wa kuongozea ndege ulioko Niger na ndege ilikuwa juu ya Gao, kama kilomita 500 kutoka kwenye mpaka wa Algeria. Kulikuwa na abiria 119 wakiwamo wafanyakazi wake.

Utafutaji bado unaendelea na tunawasilianana mamlaka zinazohusika. Waliokuwa kwenye ndege ni raia wa Algeria pamoja na mataifa mengine"Mamlaka zinazohusika nchini Burkina Faso ambako ndiko ndege ilitokea wameamua kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wanafamilia wa wale waliokuwa katika ndege. Baadhi ya ndugu wamefika katika uwanja wa ndege wa Ouagadougou kufuatilia taarifa kuhusu ndugu zao.


Baadhi walikuwa na malalamiko "Tuwanataka watuambie kama ndege hiyo imeanguka, kuna walionusurika, au wote wamekufa. Hayo ndio tunayotaka kujua. Tupo kwenye wakati mgumu. Watatu miongoni mwetu, tulitaka kusafiri na dada yetu lakini tuliamua kuahirisha safari katika dakika za mwisho. Hata hivyo dada yetu yeye aliondoka usiku jana." Mwaume mwingine aliyekuwepo kwenye uwanjahuo wa ndege alisema.

ISIS YAAGIZA WANAWAKE WAKEKETWE

ISIS yaagiza wanawake wote kuanzia umri wa miaka 11-46 kukeketwa.


Umoja wa Mataifa umeelezea ghadhabu kutokana na Fatwa iliyotolewa na Kundi la wapiganaji wa Kiislamu wa ISIS ya kuwataka wanawake wote waliozidi umri wa miaka 11 kukeketwa.
Afisa wa shirika la umoja wa mataifa nchini Iraq ,Jacqueline Badcock ameonya kuwa agizo hilo la kidini ama Fatwa itawaathiri zaidi ya wanawake milioni nne kati ya umri wa miaka 11-46.
Kundi hilo la wapiganaji wa Kiislamu ndilo linaongoza mashambulizi katika maeneo ya Kaskazini mwa Iraq na wao ndio wanaotawala mji wa Mosul.
Kundi hilo linalosheheni wapiganaji wa dhehebu la Sunni ndilo linaloendeleza wimbi la mashambulizi katika taifa hilo linalotishia kusambaratika katika ya maeneo yanayotawaliwa na madhehebu.
Ukeketaji sio kawaida nchini Iraq.
Mapema juma hili, Isisi iliwalazimisha Wakriso katika mji wa Mosul kuondoka na kuandika herufi N kwenye nyumba zao, hatua ambayo imetambuliwa kama kutaifisha mali za Wakristo katika eneo hilo.
Kulingana na amri hiyo mpya iliyotolewa chini ya Sharia, , wanawake wote kati ya umri wa miaka 11 na 46 wanapaswa kukeketwa.
ISIS yaagiza wanawake wote kuanzia umri wa miaka 11-46 kukeketwa.


Bi Badcock alisema kuwa utamaduni huo ni jambo geni sana nchini Iraq na ni swala linalopaswa kujadiliwa.
Alisema hayo alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari kupitia simu ya video katika mji mkuu wa Mkoa wa Kurdi wa Ibril.
Zoezi hilo la kuwapasha tohara wanawake limeenea sana katika mataifa mengi ya Afrika mashariki ya kati na jamii kadhaa barani Asia.
Baraza la Umoja wa mataifa lilipitisha mswada mnamo mwaka wa 2012 ya kuharamisha tamaduni hiyo ya upashwaji tohara kwa wanawake.
Isis ilitwaa mji wa Mosul mnamo mwezi wa Juni miongoni mwa miji mingine midogo midogo kuelekea mji mkuu wa Baghdad.

AJALI YA NDEGE YAUA ZAIDI YA WATU 40





Ndege ya Abiria ya Kampuni ya Trans Asia ya Taiwan imedondoka wakati ikijaribu kutua kwa dharura na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40.
Waziri wa usafiri wa Taiwan Yeh Kuang-Shih amesema watu 47 wamefariki na 11 kujeruhiwa katika ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 54 na wafanyakazi wa ndege wanne.

ATR 72 iliondoka Kaohsiung lakini ikapoteza mawasiliano baada ya mwendo wa saa moja ndipo ikaanguka na na kunawaka moto katika kijiji cha xixi kisiwani Penghu.
Meneja Mkuu wa TransAsia Hsu Yi-Tsung huku akilia, ameomba msamaha kwa ajali hiyo na akaahidi kuongeza juhudi za uokoaji na pia kuwasafirisha ndugu wa waliopoteza maisha kwenda kwenye eneo la tukio.

Siku za hivi karibuni Taiwan imepigwa na upepo mkali uliombatana na Mvua zilizoletwa na kimbunga Matmo, hata hivyo wanaosimamia anga katika eneo hilo wamesema hali ya hewa iliyokuwepo muda huo haikuwa inazidi kiwango kinachoweza kuzuia ndege kutua.

Habari za kuanguka kwa ndege hii kunakuja wakati visanduku viwili vya kutunzia kumbukumbu ya ndege ya malaysia iliyoangua nchini Ukraine tarehe 17 mwezi huu vikiwa vimefika mikononi mwa wataalamu wa masuala ya anga ili kuchunguza ni ni kitu gani kiliisibu ndege hiyo.

ALIYEBADILI DINI SUDAN KUSINI AKUTANA NA PAPA

Aliyebadili dini Sudan akutana na Papa Francis 


Mwanamke raia wa Sudan aliyesamehewa adhabu ya kifo baada ya kubadili dini amesafirishwa hadi nchini Italia baada ya kuwa kwenye ubalozi wa Marekani mjini Khartoum kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Meriam Yahia Ibrahim Ishag na familia yake waliondoka na ndege ya serikali ya Italia wakiongozana na Waziri wa nchini Italia Lapo Pistelli.
Baba wa Meriam ni muislamu na kwa Misingi ya sheria ya dini hiyo nchini Sudan Meriam pia ni muislamu na hawezi kubadili dini.
Meriam mwenyewe alilelewa na mama yake ambaye ni mkristo na kusema kuwa hajawahi kuwa muislamu.
Aliyebadili dini Sudan akutana na Papa Francis 


Pistelli Naibu waziri wa mambo ya nje wa Italia, aliweka picha yake na Meriam kwenye ukurasa wake wa facebook akisema kuwa wanaelekea kutua mjini Roma.
Mume wa Meriam Daniel Wani, ni mkristo,ana asili ya Sudani kusini na ana uraia wa Marekani.
Mtoto wa Meriam, Maya alizaliwa gerezani mwezi May, muda mfupi baada ya kuhukumiwa kunyongwa hatua iliyosababisha ghadhabu dunia nzima.
Aliachwa huru mwezi Juni baada ya kuwepo kwa mashinikizo.

NDEGE YA ALGERIA YATOWEKA NA WATU 116

Ndege ya Air Algerie imetoweka ikiwa na abiria 116


Shirika la ndege la Algeria , Air Algerie, limesema kuwa limepoteza mawasiliano na moja ya ndege zake ilipokuwa ikitoka mji mkuu wa Burkina Faso Ouagadougou.
Afisa huyo anasema kuwa ndege hiyoya Air Algerie ilikuwa imepaa dakika 50 katika anga ya Sahara mara ya mwisho mawasiliano yao.
Ndege hiyo iliokuwa inaeelekea mji mkuu wa Algiers, ilikuwa na watu mia na kumi na wahudumu sita .
Oparesheni ya dharura ya kuitafuta ndege hiyo ieanzishwa,
Ndege hiyo nambari AH 5017 inamilikiwa na shirika la ndege la kihispania la Swiftair.
Mwandishi wa BBC Alex Duval Smith aliyeko katika mji mkuu wa Mali Bamako anasema kuwa kuna habari kuwa ndege hiyo huenda ilianguka katika eneo la janga la sahara kati ya
mji wa Gao and Tessalit .
Mwandishi huyo wa BBC ananukuu ripoti kutoka kwa wanajeshi wa kulinda amani walioko huko Mali na duru za shirika la habari la AFP.
Brigadia mkuu wa majeshi ya kulinda amani nchini Mali Koko Essien, amesema kuwa maeneo hayo ya jangwani yana idadi ndogo sana ya wakaazi kwa hivyo ni vigumu kupata habari kutoka huko na inawabidi kutafuta ilikoanguka ndege hiyo.
Ndege ya Air Algerie imetoweka ikiwa na abiria 116


Aidha Brig Essien anasema kuwa eneo hilo linamilikiwa na wapiganaji waasi .
Wamiliki wa ndege hiyo Swiftair wamesema kuwa ndege hiyo aina ya MD83 ilikuwa imeomba kubadili uelekeo wake kutokana na hali mbaya ya anga na ukungu mkubwa karibu na mpaka wa Algiers.
Ndege namba AH 5017 husafiri kupitia njia ya Ouagadougou-Algiers mara nne kwa wiki,AFP imeripoti.
Raia wa Algeria ni miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya Ndege hiyo,Gazeti moja la Algeria limeripoti.
Mwezi Februari ndege ya kijeshi ya Algeria ilianguka na kuuwa watu 77 waliokuwemo.
Tukio hili la hivi punde Linaloongeza wasiwasi kuwa njia inayotumiwa na misafara ya ndege ziendazo sehemu hiyo inapitia eneo lenye utata la anga ya Mali.

KIJANA ANG'OLEWA MENO 232

Madaktari nchini India wametumia saa 7 kufanikisha upasuaji wa kinywa cha kijana Ashik Gavai mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa akipata maumivu ndani ya kinywani.

Dr Sunanda Dhiware, mkuu wa Kitengo cha tiba ya meno katika hospitali ya JJ mjini Mumbai ameiambia BBC kuwa wamefanikiwa kuyang'oa meno 232 kinywani mwa Ashik aliyeletwa hospitalini hapo akiwa amevimba taya huku akilalamika kwa maumivu makali.

Madaktari wamesema wamelazimika kutumia nyundo na tindo kuyatoa meno hayo na wakadai kwamba hilo ni tukio la ajabu na linaingia katika rekodi ya dunia.
Hata hivyo Upasuaji huo umehusisha jopo la madaktari wanne.

Dr Dhiware anasema katika uzoefu wake wa miaka 30 ya udaktari wa kinywa na meno hajawahi kukutana na tukio lanamna hiyo.

Ameongeza pia kuwa kulingana na vitabu vilivyopo vinasema hali kamahiyo inaweza kujitokeza katika taya la juu na meno yaliyowahi kung'olewa katika hali hiyo yalikuwa 37 lakini cha kushangaza ni kuwa tukiola Ashik Gavai limetokea katika taya ya chini na ameng'olewa meno 232 idadi ambayo ni kubwa huku akisalia na 28 kwa matumizi yake ya kawaida wakati kitaalamu mtu mzima anapaswa kuwa na meno 32.

Baba mzazi wa kijana Ashik, Suresh Gavai amenukuliwa akisema mtoto wake alikuwa akilalamika kwa miezi kadhaa juu ya maumivu na kwamba walidhani inaweza kuwa ni matatizo ya saratani na ndipo wakamleta Mumbai




MBUNGE MWANAMUZIKI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI

Mwanamuziki mashuhuri ambaye pia mbunge katika bunge la Somalia Saado Ali Warsame ameuawa kwa kupigwa risasi.


Msemaji wa kundi la wanamgambo wa kiislamu al-Shabab Abdulaziz Abu Musab aliiambia BBC kuwa mbunge huyo aliauawa kutokana na siasa zake wala sio muziki.

Mwandishi wa bbc mjini Mogadishi Mohammed Moalimu anasema kuwa mbunge huyo ni wa nne kuawa mwaka huu.


Bi Warsame alipata umaarufuwakati wa uongozi wa rais Siad Barre ambaye alipinduliwa mwaka 1991 kupitia nyimbo zake zilizokuwa zikiiushutumu uongozi wake.

Mbunge huyo aliishi kwa kipindi kirefu nchini Marekani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kabla ya kurejea nyumbani mwaka 2012 ili kuwakilisha ukoo wake kwenye bunge jipya nchini Somalia.

Mapema mwezi huu mbunge mwengine Ahmed Mohamud Hayd aliuawa baada ya kutoka hotelini ambapo katika tukio hilo, mlinzi wake pia aliuawa na katibu wa Bunge pia alijeruhiwa.


Kundi la Al-Shabab, ambalo lina uhusiano na al-Qaeda, limeapa kuendelea na mashambulizi zaidi katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Wanamgambo hao walipoteza ngome yao mjini Mogadishu na kuchukuliwa na Vikosi vya Umoja wa Afrika mwaka 2011,lakini wameendelea kutekeleza mashambulizi ya mabomu namauaji mjini humo.


Msemaji wa kundi hilo Abdulaziz Abu Musab amesema kuwa kundi lake limetekeleza mauaji kama ilivyopangwa na kuwa wataendelea kuwafuatilia Wabunge wengine ikiwa hawataachana na Bunge.

Al-Shabab imekua ikipigania kuunda taifa la kiislamu nchini Somalia.

MKE WA ASKARI AKUTWA AMEKUFA CHUMBANI KWA DEREVA BODABODA

Jeshi la Polisi linamshikilia dereva mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa dereva huyo.

Tukio hilo ambalo limezua gumzo kubwa wilayani humo lilitokea juzi saa 12:00 jioni katika eneo la New Mwanga wilayani humo na mtuhumiwa akidaiwa kukutwa akiwa amelewa chakari.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.


"Hilo tukio lina ukweli na bahati mbaya sana mumewe ndiyo kwanza amehamishiwa Geita na alikuwa akaripoti halafu aje kuchukua familia yake," alisema Ndemanga.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa haijafahamika nini kilitokea na kwamba hilo ni moja kati ya mambo ambayo polisi inachunguza.


"Hayo yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo kijana, nini sababu za kifo yatajulikana kadiri upelelezi unavyoendelea," alisema.

Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.


"Mpaka sasa hivi haijajulikana nini hasa kilitokea huko chumbani na ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo dereva," alisema mmoja wa watu waliokuwapo katika eneo la tukio ambaye hata hivyo, hakutaka kutaja jina lake na kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi.


Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda alinyongwa.

Habari nyingine zinadai kuwa siku ya tukio, mwanamke huyo alikuwa ameaga kuwa anakwenda kanisani lakini baadaye simu yake ilipopigwa ilikuwa ikipokewa na mwanamume.


Ilidaiwa kuwa mume wa marehemu alipojaribu kupiga simuya mkewe, ilikuwa ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wakupindukia hali iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki zake wa karibu ili wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa ulikuwapo uhusiano kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda. Ilidaiwa kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dereva huyo wa bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa na walipoingia ndani walimkuta shemeji yao akiwa ameshafariki dunia."


Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.

ANYONGA KICHANGA NA KUTUPA KISIMANI

POLISI mkoani hapa inamshikilia msichana wa miaka 18, aliyetajwa kwa jina la Rhoda Idetemya kwa tuhuma ya kumyonga mtoto wake wa miezi miwili.


Ilidaiwa kuwa, Idetemya baada ya kumnyonga mtoto huyo aliyetajwa kwa jina moja la Elizabeth, mwili aliutumbukiza katika kisima cha maji ya kunywa katika Kijiji na Kataya Nyasubi wilayani Kahama.


Ilielezwa kuwa mwili wa mtoto huyo uligundulika katika kisima hicho saa moja jioni wakati mkazi wa eneo hilo Ada Patrick (25) alipokuwa akichota maji.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilona alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliozuka kati ya msichana huyo na baba wa mtoto kukataa kutoa fedha za matumizi ya mtoto.

Chanzo:Habari Leo

KAMBI YA JESHI YAVAMIWA DRC

Kumetokea ufyatulianaji mkali wa risasi katika kambi ya kijeshi katika mji mkuu wa Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa zinasema kuwa raia wameondolewa katika eneo hilo na haijafahamika makabiliano hayo yaliyotokea katika kambi ya wanajeshi wakumlinda rais yametokana nanini.


Wadadisi wa mambo wanahisi kwamba kisa hiki huenda kikazusha utata tena kati ya Congo Kinshasa na Congo Brazzaville kwa vile shambulio lilitokea karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili.


Taarifa kutoka kwa serikali zinasema kuwa wavamizi walijaribu kupenyeza katika kambi ya kijeshi ya Camp Tshatshi na makabiliano yalizuka kwa zaidi ya dakika 30 hivi.

Jamhuri hiyo ya Kidemokrasia ya Congo imesakamwa na vita kwa kipindi kirefu sasa nahata rais aliyepo madarakani kwa sasa Joseph Kabila alichukua mamlaka baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila mwaka wa , 2001.

Duru zinasema kuwa wavamizi takriban 20 walijaribu kuingia ndani ya kambi hiyo lakini shambulizi likazimwa.


Raiya walihamishwa kutoka maeneo yaliyoko karibu na uwanja wa ndege ulifungwa wakati wa shambulizi hilo.

Serikali bado haijamtaja nani aliyeishambulia.


Hii sio mara ya kwanza kwa Camp Tshatshi kushambuliwa mwaka uliyopita kami hiyo ilishambuliwa tena na wakati huo wafuasi wa dini ya ya kikristo ya dhehebu linaloongozwa na Paul Joseph Mukungubila walilaumiwa.

GENGE LA ULIPUAJI MABOMU LANASWA ARUSHA

JESHI la Polisi jijini Arusha limewakamata watu 16 akiwemo Imam wa Msikiti wa Al Quba uliopo mkoani Arusha, Jafar Lema na mfanyabiashara 1 wote wakihusishwa na matukio ya ulipuaji wa mabomu jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai nchini (DCI), Issaya Mungulu, katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Jumanne Julai 22, 2014 imedaiwa kuwa Julai 21, 2014 saa 20.00 usiku katika maeneo ya Sombetini, Jeshi hilo limewakamata Yusufu Ally (30) na mkewe Sumaiya Juma (19) wakiwa nyumbani kwao baada ya kupekuliwa walikutwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono Saba (7), risasi sita za bunduki aina ya shortgun, mapanga mawili, unga wa baruti unaokadiriwa kufika nusu kilo na bisibisi moja.

Mungulu amenukuliwa akisema kuwa Yusufu ni miongini mwa watuhumiwa waliokuwa wanatafutwa kwa ulipuaji wa mabomu maeneo yote jijini Arusha na kuwa mahojiano juu ya mtuhumiwa bado yanaendelea dhidi yake.
Aidha, amesema uchunguzi wa shauri hilo pamoja na matukio mengine ya milipuko yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuwahoji watuhumiwa walioko mikononi mwa polisi na kuwakamata watakaobainika kuhusika na matukio hayo.


Mtuhumiwa mwingine wa milipuko nchini asakwa na Polisi

Hata hivyo, Jeshi hilo limesema linamtafuta, Yahya Hella (33) mkazi wa Mianzini mkoani humo, mwenyeji wa Chemchemu, Kondoa–Dodoma kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya ulipuaji mabomu nchini.

"Zawadi nono itatolewa kwa yeyote atakaye toa taarifa zitakazowezesha ukamatwaji wa mhalifu huyu na pia nipende kuwashukuru sana wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa jeshi letu hapa nchini"alisema Mungulu.


Watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani

Amesema kufuatia tukio la mlipuko wa bomu Julai 7, 2014 saa 22.15 usiku katika mgahawa wa VAMA, eneo la Uzunguni Jijini Arusha, ambapo watu wanane walijeruhiwa vibaya, Jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 25 kwa uchunguzi na kuwa kati yao watu sita watafikishwa Mahakamani mapema iwezakanavyo.


Amewataja watuhumiwa watakaofikishwa Mahakamani kwa tukio hilo kuwa ni pamoja na Shaaban Mmasa (26) ambaye ni mlinzi aliyekuwa zamu siku hiyo kwenye mgahawa huo, Athuman Mmasa (38) na Mohamed Nuru (30), wote walinzi katika Mgahawa wa Chinese uliopo eneo la Gymkhana jirani na eneo la tukio.


Wengine ni Sheikh Jaffar Lema (38) ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Olturmet katika wilaya ya Arumeru, pia alikuwa Imam wa Msikiti wa AL-QUBA mjini Arusha ambaye ametambuliwa kama mmoja wa viongozi walioratibu matukio ya milipuko ya mabomu maeneo balimbali nchini, Abdul Salim (31), wakala wa Mabasi Stendi Arusha, na Said Temba (42), mfanyabiashara wa Arusha.

Kwa mujibu wa Mtandao wa JamiiForums, inadaiwa kuwa kuna vijana wamekuwa wakisafirishwa kwenda Somalia kujifunza ugaidi na Alshabab lakini wananchi wanalilalamikia Jeshi la Polisi kwa kutochukua hatua mapema.


Chanzo: FikraPevu

OBAMA MATATANI, TANZANIA YALAUMIWA

SERIKALI ya Rais wa Marekani, Barrack Obama imeingia lawamani kutokana na kufumbia macho mapigano yanayofanywa nchini Palestina na mamia ya watu wakiangamia, huku wengine wengi wakikosa makazi.

Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa kukaa kimya katika suala hilo, tofuti na enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alionesha msimamo usioyumba katika kupigania haki za Wapalestina.

Akizungumza Dar es Salaam jana,Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Nasri Jaish alisema kinachoendelea Palestina kwa sasa ni mauaji ya halaiki au kimbari(genocide), lakini anashangwa na ukimya wa jumuia ya kimataifa."

Mauaji yanayoendelea Palestina kwa sasa hukuna namna nyingine ya kuyaelezea zaidi ya kusema niya kimbari,kwa kipindi kifupi watu 400 wameuawa,300 kujeruhiwa na nyumba za ibada zimevunjwa.

"Jumuia ya kimataifa, akiwemo Rais Obama anasubiri nini kitokee Palestina ndipo wazungumze, kimsingi inasikitisha. Jumuia ya kimataifa ni lazima ivunje ukimya na kuiambia Israel unyama wanaofanya kwa Wapalestina umetosha,"alisema Balozi Jaish.

Kwa upande wake, Profesa Sheriff Rwizi alisema Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kusemea watu wanao kandamizwa, wakiwemo Palestina, lakini anashangazwa na ukimya uliopo hivi sasa.

Akimwelezea Mwalimu Nyerere kuhusu msimamo wake kwa Palestina wakati huo, Profesa Rwizi alifafanua kuwa Mwalimu alisema: "Israel ni lazima iachie maeneo iliyonyakua kutoka kwa Palestina, hakuna anayeweza kuangalia unyonyaji wa aina hiyo ukiendelea," huku akimnukuu Nelson Mandela aliyewahi kusema;

"Ubaguzi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu,Israel imewaondoa mamilioni ya watu katika makazi yao, huu ni ukandamizaji mkubwa ambao hauvumiliki."

Kwa sababu hiyo, alihoji iko wapinguvu ya Tanzania leo katika kuwatetea waPalestina.

WATU NANE WASHIKILIWA NA POLISI WAHUSIKA WA UTUPWAJI MABAKI YA BINADAMU

JESHI la Polisi Kanda ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji watu wanane kwa kutupa viungo vya binadamu katika bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaan Suleiman Kova amesema hayo leo Ofisi kwake wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Amesema kuwa watu hao wakimemo madaktari wa International Medical and Technological University (IMTU) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukiri kuhusika na tukio la utupaji wa viungo vya binadamu katika eneo hilo.

Kamishna Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji na kufanya uchunguzikuona kama wahusika wamefanya kosa linalohitaji kuchukuliwa hatua za kisheria au hawana kosa.

Ameongeza kuwa kufuatia tukio hilo tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeshafungua jarada la uchunguzi kubaini ikiwa wahusika wametenda kosa linalohitaji kufikishwa kwenye vyombo vya sharia kwa hatua zaidi.

Kamishna huyo amesema kuwa katika kutekeleza jambo hilo tayari jopo la wachunguzi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jaffar Mohamed linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha watu hao kutupa viungo hivyo katika eneo hilo na idadi ya watu kulingana na viungo vilivyotupwa.

Aidha Kamishna Kova amewasihi wananchi wasiwe na wasiwasi kwani viungo vilivyookotwa havina uhusianona mauaji ya watu wengi na wala havihusiki na masuala ya ushirikina.

Amewaahidi wananchi kutoa taarifa kamili mara tu upepelezi utakapokamilika.

Viungo vya binadamu vikiwemo mikono, miguu, vichwa , mapafu na mioyo viligundulika jana (21.7.2014) jioni vikiwa vimehifadhiwa katika mifuko ya plastiki 85 na kutupa katika bonde la MbweniMpiji eneo la Bunju wilayani Kinondoni.

Mara baada ya kugunduliwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni walivichukua na kuvipeleka katika Hospitali ya Taifa kwa uchunguzi zaidi.

MAFUTA BEI CHINI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza mchakato wa kutafuta namna ya kupunguza gharama za uingizaji wa mafuta nchini. Hatua hiyo itawezesha pia bei ya nishati hiyo nchini kushuka.


Chini ya mchakato huo, Ewura inataka kushusha gharama za uagizaji wa mafuta, kwa kuchagiza ushindani wa upatikanaji wa mitaji ya fedha za uagizaji nishati hiyo.

Inataka katika ushindanishaji wa watoaji wa fedha ambao ni benki, hatimaye kuwe na ulinganifu wa upatikanaji fedha hizo miongoni mwa kampuni za mafuta.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema jijini Dar es Salaam jana, baada ya kufanikiwa katika utaratibu wa uingizaji mafuta wa pamoja, sasa wameamua kukutana na wadau kujadili namna ya kushusha zaidi gharama za nishati hiyo muhimu.

Mkutano huo wa wadau ulikutanisha washiriki mbalimbali, ikiwemo Benki Kuu (BoT), kampuniza mafuta, benki za biashara.

Ngamlagosi alisema uingizaji wa pamoja wa mafuta, umesaidia kuokoa muda na gharama kubwa za fedha zilizokuwa zikilipwa kutokana na meli kukaa muda mrefu. Mjadala huo umelenga mambo mawili makuu, yatakayowezesha kushuka kwa nishati hiyo.


Ushindani wa benki

Mkurugenzi huyo mkuu wa Ewura alisema kwanza wanaangalia namna ya kuweka ushindani wa benki katika ulipaji wa huduma za mikopo ya kampuni, ambazo zinaingia mkataba kwa ajili ya ununuzi wa mafuta.

"Kwa mfano, kwa sasa ni asilimia moja ambayo inalipwa na mlaji, lakini bado tunataka tuangalie iweze kushuka zaidi ya hapa. Kwa mfano nchi ya Msumbiji, kampuni zinalipa kati ya asilimia 0.3 mpaka 0.4 kwa hiyo na sisi tufike huko," alisema Ngamlagosi.


Alisema jambo lingine ni kurekebisha barua za benki kwa ajili ya kuruhusu upakuaji wa mafuta. Alisema katika uagizaji wa pamoja wa mafuta, meli moja inakuwa na mafuta ya kampuni nne au tano na ikitokea mmoja akashindwa kuwasilisha barua husika, hukwamisha ushushaji wa mafuta.

"Hapa ikitokea mmoja akashindwa kuleta 'letter of credit' (barua) kutokana na kushindwa kuelewana na benki, anakwamisha mzigo wa watu wote, kwa hiyo hata hii tutaangalia namna ya kurekebisha," alisema.


Mafuta bei chini

Kwa mujibu wake, kwa sasa suala hili wamelileta kwa ajili ya majadiliano na kupata mawazo ya wadau wa sekta hiyo. Mpango huo utakapofanikiwa, utatoa unafuu kwa mtumiaji wa mwisho ambaye ni mlaji.


Aidha, utaratibu wa uingizaji wa mafuta kwa pamoja umebainika kupunguza gharama kubwa na hivyo kuwa nafuu kwa walaji na uchumi wa nchi. Taarifa ya mamlaka inasema utaratibu huo umeokoa takribani Sh bilioni 126 ambazo hutumika.

"Hata gharama zimepungua sana. Zamani meli moja ilikuwa inakaa karibu siku 40 hadi 60 na kwa siku zinakaa meli tano mpaka sita, ambazo zote ilikuwa lazima uzilipiedola za Marekani 20,000 kwa hiyo ilikuwa gharama kubwa sana," alisema.

JWTZ WAONYA JUU YA WANAOVAA SARE ZAKE

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeonya juu ya matumizi ya sare na vifaa vingine vya majeshi kwa watu wasiohusika.Limetangaza kuwa hatua kali za kisheria, zitachukuliwa dhidi ya watu hao.

Limehadharisha juu ya uvaaji, uingizaji nguo nchini ikiwemo mitumba, kwamba kama itatokea, zinafanana kwa aina yoyote ile na ikadhaniwa ni za jeshi hilo, mtu anayehusika atafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi zilizopo.

"Msisitizo uliwekwa hapa katika vifungu vya sheria ni kwamba sio lazima ukutwe na sare ambazo zinatumiwa na JWTZ. Hasha!. Hapa sheria inasema hata kama tu nguo hiyo itaelekea kufanana kwa namna yoyote ile na sare za JWTZ, ni kosa la kisheria kuitumia," ilisema taarifa ya Jeshi kwa vyombo vya habari.


Taarifa hiyo ilitolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano, Makao Makuu ya Jeshi, jijini Dar es Salaam, jana. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu yeyote yule asiyena ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare za jeshi, atakuwa ametenda kosa, hivyo atafikishwa mahakamani.

Tamko hilo la jeshi linasema kwa muda mrefu sasa katika miji mikubwa, hasa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma na mikoa mingine, kumekuwa na ongezeko la matukio ya wizi na uhalifu wa kutumia silaha.


"Imeonekana kuwa wanaohusika navitendo hivyo, baadhi yao huonekana wamevaa sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na zimekuwa zikitumika katika matukio yenye sura ile ile," ilisema.

Taarifa hiyo ilisema, "Hivi karibuni vichwa vya habari vimetawala sana kwenye vyombo mbalimbali vya habari sehemu mbalimbali hapa nchini, mara utasikia 'Mwanajeshi feki mbaroni Tanga' au AliyejifanyaOfisa wa JWTZ akamatwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na mengine mengi."

Ilisema pia kumejitokeza mtindo wa baadhi ya wasanii hasa wanamuziki wa kufokafoka maarufu bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare zajeshi, kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.

Kulingana na taarifa hiyo, mitaani nako kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi, hasa vijana, wanaovaa sare za jeshi, ambao wakiulizwa wanakozitoa, hudai wamenunua kwenye mitumba au kwenye maduka ya nguo.


"Ukipita kwa wauza mitumba nao utakuta wanauza nguo za jeshi, ingawa wao hufanya biashara hiyo kwa kificho, kwani huziweka sare hizo kwa nyuma ndani kwenye maghala yao na kuziuza kwa kifichona usiri mkubwa kwani wanafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi kuuza sare hizo, ingawa wapo baadhi yao ambao huziuza hadharani wakidai kuwa ni mitumba," ilisema.

Taarifa hiyo ilisema inawezekana kuwa kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo, hawafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi, kukutwa na sare yoyote ile ya kijeshi, lakini kutokujua sheria, siyo utetezi mbele ya mahakama.

SHEHENA YA MABAKI YA BINADAMU YAKAMATWA BUNJU


Shehena yenye viungo vya binadamu vikiwa vimekaushwa na kuwekwa kwenye mifuko ya plastiki zaidi ya 85,imekutwa imetupwa katika dampo lisilo rasmi la Bunju"A"bonde la mto mpiji, mpakani mwa jiji la Dar-es-salaam na Bagamoyo mkoani Pwani,hali iliyozua taharuki,simanzi na mshangao kwa wakazi wa eneo hilo la Bunju.
Katika eneo hilo maarufu kama bonde la mto mpiji na kukumbana na umati wa watu wakienda kushuhudia tukio hilo ambalo wananchi hao walikuwa wakishangaa kutokea katika eneo lao,huku jeshi la polisi kituo cha polisi bunju na wale wa wazo hill,wakijaribu kuzuia umati wa watu wasisogelee katika eneo la tukio.

Nao mashuuda wa tukio hilo Bwana Ruta na Bwana Huseni wamesema kuwa mama mmoja aliyekuwa akiponda kokoto katika eneo hilo ambalo si halali kwa shuhguli za machimbo na dampo, aliona gari likija na kumwaga mifuko hiyo,ambapo mara baada ya kuondoka wamwagaji hao alikwenda kutafuta chohote kitu na ndipo alipokumbana na kadhia hiyo na kukimbia na kuomba msaada.

katika kituo kidogo cha polisi Bunju, jeshi la polisi chini ya kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni kamishan msaidizi wa polisi Camilius Wambura. Walilazimika kuongeza ulinzi ili kudhibiti wananchi hasa bodaboda waliokuwa wamefurika katika kituo hicho ili kujua hatma ya tukio hili mara baada ya kuwepo kwa tetesi za gari dogo maarufu kama kiyoliyoli kufikishwa kituoni hapo huku ndani ya gari hilo likitoa majimaji yaliyoashiria uwepo wa mizigo waliyotilia shaka.

Katika eneo la tukio wananchi wakishirikiana na askari wa jeshi la polisi walivalia kiraia, walichukua shehena hiyo na kwenda kuiihifadhi sehemu salama, ambapo licha ya zoezi hilo kufanyika karahisi kwa kuvalia gloves bila ya maski za puani, huku baabdhi ya wadadisi wa mambo wakisema huwenda zoezi hilo likawa na madhara kwa wahusika kwani viungo hivyo havikujulikana mara moja vilikaushwa kwa dawa gani.

kamandaa wa polisi mkoa wa kipolisi kinondoni Acp Camilius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa bado jeshi linaendelea na upelelezi ili kujua hiyo mifuko zaidi ya 85 yenye viungo vya binadamu vikiwa vimekaushwa kwa ustadi vimetoka wapi na pindi uchunguzi utakapo kamilika watatoa majibu.

WANAKIJIJI WAFANYA UHARIBIFU MALI KWA KUMTUHUMU UCHAWI MWANAFAMILIA

Wakazi wa kijiji cha Nguruka wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wamechoma nyumba nne za familia moja yenye zaidi ya watu ishirini na kuteketeza vyakula na mali nyingine zenye zaidi ya shilingi milioni mia moja baada ya kumtuhumu mmoja wa wanafamilia kwa ushirikina.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mkoronga katika kijiji cha Nguruka Matei Charle ambaye alimuokoa mtuhumiwa wa uchawi aliyetambulika kwa jina la Siyajui Ahmad, amesema mama huyo alianza kushambuliwa akiwa katika msiba wa kijana Masoud Vyombo ambaye alifariki ghafla ambapo wakazi wa kijiji hicho waliomtuhumu kumuua kwa njia ya ushirikina walianza kumshambulia kabla ya kuokolewa ambapo mamia ya wananchi waliamua kuteketeza nyumba yake pamoja na nyumba tatu za kaka zake na wazazi wake, huku Siyajui Ahmad aliyetuhumiwa akieleza kuwa familia hiyo imepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni mia moja na kwamba alilazimika kutoroka ili kuokoa maisha yake.

Kamanda wa polisi mkoani Kigoma Frasser Kashai amesema jumala ya watu kumi na watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo huku kwa upande wake katibu mwenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Uvinza Majaliwa Zuberi akitoa wito kwa wananchi kutochukua sheria mkononi na akiitaka kamati ya maafa ya wilaya kuzisaidia familia nne zilizoathirika ambazo kwa sasa zinalala nje na hazina chakula, mavazi na mahitaji mengine ya msingi.

MAPIGANO YAENDELEA UWANJA WA NDEGE TRIPOLI

Mapigano yamezuka tena kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Libya, siku mbili baada ya wapiganaji kukubaliana kusitisha mapambano.

Ripoti zinasema kuwa vifaru vinatumiwa katika mapambano makali katika uwanja wa ndege wa Tripoli, ambao umeshambuliwa kwa makombora na mizinga.

Uwanja huo ulianza kushambuliwa juma lilopita na ikalazimika kuufunga.

Wakuu wa Libya wameonya kuwa kazi ya kukarabati uwanja huo itachukua miezi na kugharimu mamilioni ya dola.

AL SHABAAB WASHAMBULIA TENA LAMU

Kundi la Al shabaab limekiri kutekeleza shambulizi katika basi moja la abiria katika pwani ya Kenya hapo jana usiku.

Shirika la msalaba mwekundu limesema kuwa watu saba walipigwa risasi na kufariki huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Shambulizi hilo lilitokea katika mji wa Witu katika Kaunty ya Lamu.

Watu kadhaa wameuawa katika Pwani ya Kenya katika kipindi cha miezi kadhaa iliopita.

Kundi la Alshabaab limekiri kutekeleza mauaji hayo.

Linasema kuwa linalipiza kisasi kuwepo kwa majeshi yaKenya nchini Somali.

Ghasia hizo zimeathiri pakubwa sekta ya utalii nchiniKenya.

409 WAKAMATWA KWA UJANGILI KATAVI

WATU 409 wanaosadikiwa kuwa majangili sugu wamekamatwa wakifanya ujangili katika Hifadhi yaTaifa ya Katavi wilayani Mlele mkoa wa Katavi katika kipindi kilichoanzia Juni 2013 hadi Juni mwaka huu.


Katika kipindi hicho, silaha kadhaa zimekamatwa ndani ya hifadhi hiyoya Taifa zikiwemo bunduki nzito aina ya SMG zipatazo tano, riffle G3 zipatazo nane pamoja na risasi zipatazo 357 za SMG.

Silaha nyingine zilizokamatwa katika kipindi hicho ni pamoja na bunduki aina ya shotgun zipatazo 21, bunduki zilizotengenezwa kienyeji "magobori" yapatayo 138.

Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Hifadhiya Taifa ya Katavi, Mhifadhi Davis Mushi wakati akitoa taarifa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mpanda (DDC) iliyoketi mjini hapa.


Alibainisha kuwa kuwepo kwa makazi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mlele na Mishamo wilayani Mpanda karibu na Hifadhi ya Taifa ya Katavi kumesababisha wakimbizi wa makazi hayo kujihusisha ujangili kama njia ya kupatia kipato chao.

Akifafanua alibainisha kuwa mtandao wa watu kupitia mkoa wa jirani wa Kigoma na wakibadilishana na majangili na meno ya tembo.

WAKAMATWA KWA WIZI WA KILO 40 ZA TANZANITE

WAFANYAKAZI saba wa kampuni yaTanzanite One, wakiwemo viongozi wakuu wa idara ya ulinzi ya kampuni hiyo wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za wizi wa madini aina ya tanzanite yenye uzito wa kilo 40 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 10.


Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimeki alisema wizi huo ulitokea majira yasaa 8 usiku juzi, ikielezwa wafanyakazi hao walishirikiana na wafanyakazi wa Shirika la Madini laTaifa (STAMICO) kupanga wizi huo.

Nsimeki alisema uchunguzi wa awali umebaini mpango mzima wa viashiria vya upangaji wizi huo umefanywa na wafanyakazi hao na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ambao bado hawajakamatwa mpaka sasa, lakini polisi iko katika msako mkali dhidi yao.

Alisema kiutaratibu madini yote yanayotoka mgodini kwenda kwenda chumba maalumu cha kuhifadhi madini, husafirishwa na gari maalumu lisiloruhusu risasi kupenya.


Nsimeki alisema cha kushangaza siku ya tukio hilo, shehena hiyo ya madini ilisafirishwa kwa gari ya kawaida aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 256 APQ, mali ya kampuni hiyo hatua ambayo ilihisiwa wafanyakazi hao pamoja na viongozi wa idara ya ulinzi walikuwa wanajua kikamilifu kilichokuwa kikiendelea.

Kamanda huyo alisema mara baada ya madini kupakiwa kwenye gari hilo la kupangwa kuelekea katika chumba cha kuhifadhia madini, ghafla walisikia risasi zikilia na moja ya risasi iligonga mlango wa gari hiyo na nyingine kwenye chesisi ya gari.


Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya walinzi na dereva wa Kampuni ya Tanzanite One kuona hali hiyo nao walitimua mbio bila ya hata ya kujitetea pamoja na kwamba walinzi hao walikuwa na silaha za moto na za kisasa za ulinzi.

''Lakini cha kushangaza muda mfupiwalinzi hao walirejea katika gari nakukuta mifuko miwili ya kilo 15 na 25 imeshachukuliwa na majambazihao na kutoweka nayo,'' alisema.


Hata hivyo, mfuko mmoja wenye uzito wa kilo 25 umepatikana ndani ya gari ya kampuni hiyo, kwani majambazi walishindwa kubeba kwa kuwa ulikuwa mzito nakuchukuliwa na kuhifadhiwa katika ofisi za Tanzanite One.

Nsimeki aliwataja wanaoshikiliwa na polisi ni pamoja na viongozi wakuu wa idara ya ulinzi ambao ni George Odeku Kisambe (38), mkaziwa Arusha ambaye ni meneja wa kitengo cha kamera (CCTV) na pia ni mkuu wa idara ya ulinzi na Jonathan Nyange (52), mkazi wa Kilimanjaro na pia ni dereva wa gari hilo.


Wengine ni Hussein Ng'ombo (64), mkuu wa zamu siku hiyo, Sunday Nzogora (35) mkaguzi wa Madini, Rodney Ngowi (48), na Samwel Kajumu (29) ambao ni mafundi mitambo, wote wakazi wa Mkoa waKigoma na Erick Briygy (44) raia waAfrika Kusini ambaye ni mdhibiti wa madini wa Tanzanite One.

Hii ni mara ya pili kufanyika kwa wizi huo, kwani mara ya mwisho ilikuwa mwaka juzi ambapo watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivamia chumba maalumu na kuiba shehena kubwa ya madini yenye thamani ya mabilioni na kutokomea nayo kusikojulikana.