WATAKAO KACHA JKT KUSHTAKIWA

Vijana wasiopungua 45,000 watakaomaliza kidato cha sita watajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na watakao kwepa mafunzo hayo ya miezi mitatu, watashtakiwa.

Mpango huo wa kupitisha JKT wahitimu wa kidato cha sita na vyuo, ambao ulifutwa mwanzoni mwa miaka ya 90 kutokana na matatizo ya kifedha na kurejeshwa bila mafanikio ya miaka ya hivi karibuni, ulilenga kujenga uzalendo kwa vijana na kuongeza ukakamavu.


Jana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk Hussein Mwinyi alisema utaratibu huo ni wa kisheria na si hiari, hivyo wahitimu wa kidato cha sita watambue kuwa ni kosa kukaidi wito wa kujiunga na JKT.Dk Mwinyi, aliyekuwa anawasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015,vijana watakaojiunga na jeshi watafanya hivyo kwa awamu tatu.


Alisema awamu ya kwanza itahusisha vijana 20,000 ambao wataingia katika mafunzo hayo Juni hadi Septemba 2014 na kufuatiwa na wa awamu ya pili itakayochukua vijana 14,450 kuanzia Oktoba hadi Januari 2015 wakati awamu ya tatu ya vijana 10,550 itaanza Januari hadi Aprili 2015.


Hata hivyo, kumekuwepo na mwingiliano wa muda wa kujiunga na jeshi hilo na wa kujiunga na masomo ya juu. Kati ya vijana 15,000 waliotakiwa kujiunga na jeshi hilo kati ya Oktoba 2013 na Januari 2014, waliojiunga walikuwa 1,002 tu.

Alipoulizwa kuhusu mwingiliano huo, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama alisema atatoa ufafanuzi huo leo.


Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Bulaya alitaka mafunzo ya JKT kwa wabunge yafanyike kwa miezi miwili hadi mitatu badala ya wiki mbili.

Bulaya, ambaye alipitia mafunzo hayo pamoja na wabunge wenzake wakati mpango huo uliporejeshwa mapema mwaka jana, alisema kuwa hali hiyo itawafanya wabunge hao kujifunza mambo mengi zaidi.


Bulaya aliwataja baadhi ya wabunge vijana wanaotakiwa kujiunga na mafunzo hayo kuwa ni John Mnyika (Chadema-Ubungo) na Catherine Magige (viti maalumu-CCM).


"Mheshimiwa Spika naomba uwaruhusu wabunge kwenda kwenye mafunzo kwa miezi miwili hadi mitatu," alisema na Bulaya na kuongeza:

"Katika kambi za JKT kuna tatizo la vifaa vya afya, hivyo wizara iliangalie hilo ili wanaokwenda katika mafunzo hayo wapate tiba sahihi na kwa wakati."


Wataka muda uongezwe

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kuhusu wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo, Vita Kawawa alipendekeza muda wa JKT uongezwe hadi miezi sita.


Kawawa alisema ingawa Serikali inasema kuongeza muda huo kunashindikana kutokana na mabadiliko ya mihula ya masomo vyuoni, bado wanasisitiza umuhimu wa kuongeza muda wa mafunzo.


Kamati hiyo imeshauri vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na JKT na wale ambao hawataripoti kwa mafunzo bila sababu za msingi, Serikali iwachukulie hatua za kisheria.


Bajeti ya Wizara Kuhusu bajeti, Dk Mwinyi alisema wizara yake itatumia Sh1.26 trilionikwa mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali, zikiwamo kununua ndege za kivita.


Dk Mwinyi aliliambia bunge kuwa kati ya Sh1.26 trilioni, Sh1.0 trilionizitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati kiasi cha Sh249 bilioni zitatumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa na wizara hiyo nipamoja na kununua vifaa na zana zakijeshi, ikiwamo vifaa vya uhandisi wa medani na ndege za kivita.


Pia,alisema wizara itaanza ujenzi wa gati katika Kamandi ya Jeshi la Wanamaji Kigamboni, kuboresha mifumo ya mawasiliano ya ndani na nje ya vikosi vya kambi za jeshi na kuendelea na ujenzi wa nyumba 6,064 za makazi ya wanajeshi.Dk Mwinyi alizitaja shughuli nyingine zitakazofanywa kuwa ni kukamilisha ujenzi wa shule ya mafunzo ya awali ya kijeshi (RTS), eneo la Kihangaiko, Pwani na Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC), Tengeru Arusha.


Pia,wizara itaanza ujenzi wa hospitali kuu ya jeshi eneo la Mataya mkoani Pwani, kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine duniani katika nyanja za kijeshi na pia kulipa madeni ya kimkataba.

Hata hivyo, Dk Mwinyi alisema kuwa pamoja na bunge kuidhinishia wizara hiyo Sh1.1 trilioni kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka huu, hadi Machi ilikuwa imepokea Sh 768.4 bilioni, sawa na asilimia 69.7.

DK. SHEIN AGOMA KUONGEZA POSHO BALAZA LA WAWAKILISHI

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amekataa maombiya kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000.Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.

Katibu wa BLW, Yahya Khamisi Hamad alithibitisha jana kuwa baraza hilo lilipeleka kwa Rais Shein maombi la kutaka posho ya vikao hivyo iangaliwe upya kutokana na sababu mbalimbali, lakini kulingana na mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa wakati huu imeshindikana kufanya hivyo.


Hamad alisema Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza kufikiriwa.

Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo alipokutana na Spika wa barazahilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya kumweleza uamuzi kuhusu suala hilo. "Rais amekataa maombi ya nyongeza ya posho za vikao vya wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya kiuchumi kutokuwa mazuri kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi hali ya mambo itakapotengamaa," alisema Hamad.

Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari imekwisha taarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.


Wajumbe hao wamekuwa wa kilipwa posho ya Sh 150,000 kwa siku mbali na mshahara na posho nyingine zinazokaribia Sh4,500,000 kwa mwezi.

Akizungumzia kikao cha bajeti kinachoanza leo mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao hicho kitalazimika kupunguzwa kwa siku ili kuwahi Bunge Maalumu la Katibaya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo lipo likizo na linatarajiwa kukutana Agosti 5.


Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao cha bajeti kinatarajia kutumiasiku 56, tofauti na miaka mingine ili kukimbizana na muda na kuwataka wajumbe kujadili bajeti ilikuokoa muda na kuwahi Bunge la Katiba.

Aidha, katibu huyo wa BLW alisemakikao hicho kitakuwa na maswali 90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa Sheria ya Fedha na ulewa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali mwaka 2014/2015.


Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee amesema SMZ katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1 bilioni, kati ya hizo, makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni na kiasi kingine cha Sh 305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo mbalimbali.

SERIKALI KUPUNGUZA BEI YA UMEME

SERIKALI imetangaza na kusisitiza mpango wake wa kupunguza bei yaumeme kwa wananchi, utakaoanza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alisema hayo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM).


Martha katika swali lake Mlata aliitaka Serikali kupunguza bei ya umeme, ili wananchi wa kawaida watumie nishati hiyo kupikia na kupunguza matumizi ya mkaa yanayochangia kuharibu mazingira nchini.

Akifafanua zaidi, Masele aliwataka Watanzania kuvuta subira kwa kuwa ujenzi wa bomba hilo kwa sasa umefikia kati ya asilimia 80 na90 kukamilika na ukikamilika, utawezesha kupungua kwa bei ya umeme.


Kwa mujibu wa Masele, kwa sasa Shirika la Umeme (Tanesco), linanunua umeme kutoka katika kampuni za ufuaji umeme wa mafuta kwa senti 38 na 55 za dola za Marekani kwa uniti moja, ili kuwauzia Watanzania.

Wakati kampuni hizo zikiuza umeme kwa bei hiyo, takwimu za Tanesco zinaonesha kuwa shirika hilo linalazimika kuuza umeme huo kwa kati ya senti 10 mpaka senti 19 za dola za Marekani kwa uniti moja kwa wananchi.


Takwimu hizo zinaonesha kuwa wateja wa majumbani uniti moja ya umeme wanauziwa kwa senti 19za dola za Marekani, wateja wa biashara senti 13, viwanda vya kati na vikubwa senti 10 na taa za barabarani senti 19.

Kwa takwimu hizo na kwa bei hizo, Tanesco katika kila uniti moja ya umeme inayouza imekuwa ikipata hasara ya senti 28 mpaka 36 za dola za Marekani.


Kushuka kwa bei Katika mpango wa Serikali, Masele alisema bomba hilo likianza kufanya kazi, umeme utaanza kununuliwa na Tanesco kutoka kwa wafanyabiashara kwa kati ya senti nane hadi tisa za dola za Marekani tofauti na sasa ambapo umeme unanunuliwa kwa kati ya Dola 38 na 55.


Alifafanua kwamba baada ya kuanza kununua umeme kwa bei nafuu, Serikali inapanga kupunguzabei ya umeme katika muda usiozidi miezi 12. Changamoto Masele alitangaza hayo bungeni huku kukiwa na taarifa kuwa wafanyabiashara wanaouzia umeme Tanesco, wamekuwa wakipambana bei hiyo isishuke.

Wafanyabiashara hao wenye mitambo ya kufua umeme wa mafuta na waagizaji wa mafuta, wanafanya jitihada kuhakikisha lengo hilo halifikiwi, kwa kuwa watapoteza karibu Sh bilioni nne wanazopata kila siku kutoka Tanesco.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa mkoani Mtwara kukagua ujenzi wa bomba la gesi hivi karibuni alisema kuwa wafanyabiashara hao wako katika mapambano kutaka malengo ya kushusha bei ya umeme yasifikiwe.

"Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na gharama hizi (za umeme) ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang'anywa tonge mdomoni, vita hii tunaijua; lakini sisi hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tuendelee mbele," alisema Pinda.


Pinda alisema mapambano hayo yalianza tangu wakati wa jaribio la kuzuia gesi isifike Dar es Salaam, kwa kuwa wafanyabiashara hao wanahofia kuwa mwisho wa biashara yao ya kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu, umefika.

Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta na kama wafanyabiashara hao wanataka kuendelea na biashara hiyo, ni vyema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na sio ya mafuta kama ilivyo sasa hivi.

WANAJESHI KUTOYUMBISHWA NA WANASIASA

WANAJESHI nchini, wamemwahidi Rais Jakaya Kikwete kuendelea kusimama imara, kupokea na kutii amri na maelekezo yake bila hila na kuhakikisha hawayumbishwi na kauli potovu za kisiasa.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kwa niaba ya wanajeshi wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15.


Dk Mwinyi ambaye wizara yake iliomba kuidhinishiwa Sh trilioni 1.3, aliwasilisha shukurani za wanajeshi kwa Rais Kikwete, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu kwa hiba yake ya uongozi, ushupavu, uvumilivu na maridhiano vitakumbukwa na kuenziwa na vizazi na vizazi hususani kwao.

"Ahadi yetu kwake ni kuwa tutaendelea kusimama imara kupokea na kutii amri na maelekezo yake bila hila yoyote nakutoyumbishwa na kauli potovu za kisiasa," alisema Dk Mwinyi na kushangiliwa bungeni.

Aidha katika hotuba hiyo ya Waziri, aliwasilisha salamu za pongezi za Rais Kikwete kwa wanajeshi wote kwa kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.


Katika salamu hizo, Rais Kikwete alisema kazi iliyofanywa na wanajeshi ni kubwa na waliifanikisha kwa weledi, utii, uhodari, ujasiri na kwa kishindo cha hali ya juu.

"Ushiriki wao umedhihirisha umma wa Watanzania na ulimwengu kwa ujumla kuwa jeshi letu ni imara, shupavu na lipo tayari kulinda, kutetea na kudumisha Muungano wetu…nami nikiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa natamka kuwa najivunia nao," alisema Dk Mwinyi.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, katika taarifa yake iliyosomwa na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, pia imepongeza wizara na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ya ulinzi na usalama wa nchi na hivyo kudumisha amani, utulivu na umoja wa nchi.


Pia ilipongeza majeshi yote kwa kufanikisha sherehe za Muungano ambazo kwa mujibu wa kamati, zilifana na kuhakikishia Watanzaniakuwa nchi iko salama.

Awali, akizungumzia bajeti ya Wizara yake, Dk Mwinyi alitaja changamoto za utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2013/14, alisema kulikuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wake kutokana na kuidhinishiwa kiwango kidogo cha bajeti ikilinganishwa na mahitaji halisi.


Alitoa mfano katika mwaka huo wafedha, wakati mahitaji halisi kwa kuzingatia vipaumbele vya Wizara yalikuwa ni Sh trilioni 1.74, bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa Sh trilioni 1.1 sawa na asilimia 63.3 ya mahitaji. Kamati ilizungumzia pia ufinyu wa bajeti na kushauri Serikali kutoa kwa wakati fedha zote zinazoidhinishwa na Bunge kila mwaka.


Wakichangia kwa nyakati tofauti, wabunge wengi walitetea wanajeshi na kutaka Serikali iendelee kuwajali wawapo kazini na wanapostaafu. Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) alisema ni lazima Jeshi liwezeshwe hususani vikosi vinavyotengeneza zana, Serikali ihakikishe inanunua vifaa hivyo badala ya kununua nje ya nchi.


"Wakati wa amani ndiyo wakati wa kutoa jasho jingi, ukitoa jasho wakati huu, ikija kutokezea damu itakuwa kidogo sana…Umoja wa Mataifa unapenda majeshi yetu," alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein (CUF) alitaka stahiki za wanajeshi ziangaliwe upya na kusema haipendezi kukuta mwanajeshi mstaafu akiwa katika hali mbaya.


Mbunge wa Manyoni, John Chiligati(CCM) alisema amani na utulivu vinavyoonekana, vinatokana na kuwepo Watanzania ambao usiku na mchana wanailinda nchi. Alisema kulinda amani ni aghali hivyo Serikali lazima iwekeze kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.


Alitaka vyombo hivyo visichukuliwe kama vyombo vya kawaida. Chiligati ambaye ni mwanajeshi mstaafu, alisema wastaafu mambo yao hayajakaa vizuri.


Alisema Kamati ilitembelea Bungela India ambalo miongoni mwa mambo waliyotaka kujifunza ilikuwa ni namna wanavyohudumia wanajeshi wastaafu. Chiligati alishauri askari hao waendelee kuundiwa mfumo wa kijeshi wawapo uraiani baada ya kustaafu.


Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid (CUF) ameshauri viongozi kuwa makini katika matamshi yao kuepuka kuchochea uvunjifu wa amani.

Alisema Jeshi linafanya kazi nzuri na kusisitiza kuwa watu wanaodhani vita ni kitu cha kawaida, wafuatilie nchi zilizokumbwa na machafuko.

CASTER SEMENYA AMPOSA MWANAMKE MWENZAKE

Habari zimeenea nchini Afrika kusini kwamba Mwanariadha maarufu wa kike nchini humo Caster Semenya amejipatia mchumba wa kike.

Taarifa katika vyombo vya habari nchini humo zinasema kuwa mahari au lobola kama inavyojulikana Afrika kusini imepelekwa kwa familia ya mchumba huyo iliyoko Polokwane jimbo la Limpopo na zikakubaliwa kwa mikono miwilina wazazi wa Violet Raseboya.


Caster Semenya

Kama unanijua vizuri basi unafahamu kuwa Caster hatangamani na vyombo vya habari. Nakutana na waandishi wahabari wakati wa mashindano tu! Na wala sitajishugulisha kujibu kama madai hayo ni kweli au la maanake ni swala ambalo limechapishwa magazetini siwezi kubadili lolote!"

Aidha Lobola yaani mahari ya rand elfu 25 sawa na dola 2500 za Marekani ilikubaliwa kwa mikono miwili.

Hata hivyo Semenya mwenyewe anavilaumu vyombo vya habari kwa kuingilia maisha yake ya kibinafsi.


Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya BBC nchini Afrika Kusini alipomtaka kuthibitisha kama taarifa hizo ni za ukweli, Semenya alisema hatapinga au kukubali Vyombo vya habari nchini A-Kusini tayari vimeripoti kuwa Caster Semenya (23 ) amekua na uhusiano wa kimapenzi kwa muda sasa na mwanariadha mwenzie wa kike Violet Raseboya.

Mwanariadha huyo aliyegonga vichwa vya habari kote duniani mwaka wa 2009 alipompiku Janeth Jepkosgey wa Kenya na kutwaa ubingwa wa dunia wa mbio za mita 800 za wanawake huko Berlin.


Wakenya walikata rufaa wakitilia shaka jinsia yake kutokana na maumbile yake yenye miraba minne.

Na matukio yaliyofwatia yalimlazimu Semenya kufanyiwa uchunguzi wa siha na jinsia na shirikisho la riadha duniani IAAF jambo lililompa fedheha sana bingwa huyo wa dunia.


Aliporejea nyumbani viongozi walioshabikia ushindi wake walimsifu kuwa binti wa Afrika Kusini na hata magazeti ya urembo ya kachapisha picha zake akiwa amejipodoa.

Mwaka wa 2006 wakati wa utawala wa Thabo Mbeki serikali ya Afrika Kusini ilipitisha sheria ya kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.

DAWA ZA MENO NA SABUNI HUSABABISHA KUPUNGUZA NGUVU ZA KIUME

Kemikali zinazopatikana katika baadhi ya bidhaa ambazo hutumiwa kila siku kama vile dawa ya kusugua meno, sabuni na mafuta ya kujikinga kutokana na miale hatari ya jua zinaweza kuharibu mbegu za uzazi za wanaume.

Kwa mara ya kwanza watafiti wanaonya kuwa bidhaa hizo zina uwezo wa kuanthiri uwezo wa mbegu za uzazi za wanaume kuzalisha mwanamke.

Wanasayansi hao wanasema kwamba bidhaa hizo zina kemikali ambazo zinachangia matatizo ya uzazi kwa wanaume katika nchi za magharibi.

Kemikali zinazopatikana katika dawa za kusugua meno zinasemekana kuharibu nguvu za mbegu za kiume kuweza kuzalisha.


Takriban mwanamume mmoja kati ya sita aliyeoa nchini Uingereza anakumbwa na tatizo la kuzalisha na tatizola utasa ndio kiini kikubwa cha hali hiyo.

Uchunguzi huu ulifanywa na watafiti kutoka Uingereza na Uholanzi na walifanyia uchunguzi kemikali 100 kila siku huku wakigundua kuwa thuluthi moja ya kemikali hizo ziliathiri uwezo wa Manii kufikia katika mayai ya mwanamke.


Utafiti huu uliandikwa katika jarida la afya la EMBO na watafiti wanasema nyingi ya kemikali hizo hatari zinapatikana katika mafuta yanayotumiwa kujizuia na miale hatari ya jua.

Kemikali nyingine inajulikana kama Triclosan, ambayo inapatikana katika sabuni na dawa ya kusugua meno.


Uchunguzi wa maabara ulionyesha kuwa kemikali hizo zinaathiri uwezo wa Manii ikitafuta mayai ya mwanamke kuweza kuizalisha.

Kadhalika kemikali hizo pia zinaharibu kabisa manii kiasi cha kukosa hisia kwa homoni za mwanamke.


Mabadiliko haya yanapotokea kwa mbegu za kiume, huifanya kuwa vigumukuweza kuzalisha.

Watafiti hao wanasema kuwa mchanganyiko wa kemikali hizo ni hatari zaidi kwa mbegu hizo.


Kemikali hizi hujulikana kama kemikali zinazoathiri jinsia kwa sababu ni sehemu ya kemikali zinazo athiri homoni za mwili wa mwanamume.

Mwaka jana shirika la afya duniani lilihusisha kemikali hizo na saratani ya matiti na pumu.

WACHIMBA MGODI 157 WAFA MGODINI

Mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe magharibi mwa Uturuki umesababisha vifo vya zaidi ya wachimbaji migodi 150 na kujeruhi wengine zaidi ya 70 kwa mujibu wa maafisa nchini humo.


Meya wa eneo la Manisa, Cengiz Ergun, ametoa tahadhari kwamba idadi ya watu waliokufa bado haijathibitishwa rasmi.

Inahofiwa kuwa wachimbaji mgodi wengine wengi bado wamefukiwa chini ya mgodi huo.


Inakadiriwa kuwa wakati mlipuko huo ulipotokea wafanyikazi 580 walikuwa ndani ya mgodi huo japo inaaminika wengi waliweza kukimbilia usalama wao.

Bado idadi ya walionaswa ndani ya mgodi huo haijabainika.


Mgodi huo uko katika mji wa Soma, mkoani Manisa , takriban kilomita 250 kusini mwa Istanbul.

Jamaa za wachimbaji migodi hao wamekusanyika katika makundi karibu na mgodi huoambao unamilikiwa na wawekezaji wa kibinafsi hukuwengi wao wakilia hadharani na kububujikwa na machozi.


Waziri wa nishati Taner Yildiz ameimabia televisheni ya Uturuki kuwa huenda wengi wamekufa kutokana na sumuya gesi aina ya carbon monoxide.

Amesema moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme.


Picha za televisheni zinaonyesha maafisa wa uokoaji wakiokoa wafanyikaziwa mgodi huo, huku nyuso zao zao zikiwa zimejaa vumbi.

Baadhi yao wanaweza kutembea na wengine wanabebwa na kupelekwa ndani ya magari ya kubebea wagonjwa yaliyoegezwa karibu na eneo la tukio.

GAVANA WA NAIROBI ATIMULIWA

Gavana wa mji mkuu wa Kenya Nairobi, Evans Kidero ametimuliwa mamlakani na mahakama ya rufaa.

Mahakama hiyo, imeamua kuwa Kidero na naibu wake Jonathan Mueke hawakuchaguliwa kihalali.


Uamuzi huo ulitolewa kufuatia ombi la waziri msaidizi wa zamani Ferdinand Waituti ambaye aliwania kiti hicho wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2012.


Gavana Kidero alisifika wakati mmoja kwa tukio la kumzaba kofi mwakilishi wa wanawake nchini Kenya Rachel Shebesh walipodai kuwa alivamia ofisi yake akiwa ameambatana na na wafanyakazi wa baraza la jiji waliokuwa wanadai kushughulikiwa kwa maslahi yao ya kikazi.

WAZIRI MKUU WA ISRAEL EHUD OLMERT JELA MIAKA SITA

Mahakama moja nchini Israel imempa kifungo cha miaka sita jela aliyekuwa waziri mkuu nchini Israel Ehud Olmert kwa kosa la kupokea hongo.

Bwana Olmert alipatikana na hatia mwezi machi katika kile kilichojulikana kama 'swala laeneo takatifu' ambapo hongo ilitolewa ili kuharakisha ujenziwa majumba ya kifahari mjini Jerusalem.

Kiongozi huyo alikuwa ameondolewa mashitaka katika kesi tofauti zilizokuwa zikimkabili.

Mashitaka yaliomkabili yalitekelezwa wakati Olmert alipokuwa meya wa mji wa Jerusalem na baadaye akiwa waziri wa serikali.


Ehud Olmert alimrithi Ariel Sharon kama waziri mkuu mnamo mwaka 2006 baada ya Sharon kuugua ugonjwa wa kiharusi.

Alijiuzulu mnamo mwaka 2008.

MAREKANI YATUMA NDEGE NIGERIA

Marekani imesema inapeleka vifaa vya uchunguzi nchini Nigeria kusaidia katika juhudiza kuwatafuta wasichana wanaozuiliwa na kundi la Boko Haram.

Wasichana hao walitekwa nyara kutoka shule moja Kusini mwa eneo la Borno mwezi mmoja uliopita.


Msemaji wa Rais Obama Jay Carney amesema kikosi cha maafisa 30 kiko nchini Nigeria tayari kushiriki juhudi hizo.


Amesema msaada huo wa Marekani kutoka wizara za mambo ya nje na ulinzi na piakutoka idara ya uchunguzi ya FBI.

Hatua hiyo imechukuliwa wakati baadhi ya Jamaa za wasichana waliotekwa nyara wakielezea majonzi baada yakutazama kanda ya video iliyotolewa na kundi hilo.


Baadhi wameiambia BBC kuwa kanda hiyo imewapa matumaini lakini wameshangaa kuona wasichana hao ambao wengi ni Wakristu wamevalia mavazi ya Kiislam.


Mzazi Nigeria

"Ni heri watuonyeshe maiti za wasichana wetu badala ya kuwazuilia vichakani. Hili ni swala la hisia za ubinadam. Sisi hatuwezi kwenda kuwaokoa, wanajeshi hawawezi kwenda huko. Ni heri kutumia nguvu. Tukiona maiti zao mioyo yetu itakua huru"

Akizungumza kwa uchungu nduguye mmoja wa wasicha waliotekwa ameiambia BBC ni heri kanda hiyo ingeonyesha maiti za wasichana hao kwa kuwa hiyo ingeondoa wasiwasi unaoendelea kukithiri na kuumiza mioyo ya wengi.


Kwenye kanda hiyo ya video kiongozi wa Boko Haram , Abubakar Shekau anasikika akiambia serikali ya Nigeria yuko tayari kubadilishana baadhi ya wasichana hao na wafuasi wake waliofungwa jela.

Hata hivyo wizara ya mambo ya ndani ya Nigeria imetupilia mbali pendekezo hilo.


Seneta Ali Ndume kutoka eneo ambapo wasichana hao walitekwa nyara anaisihi serikali kulegeza msimamo.

UKAWA WAANZA ZIARA YA SIKU 10 BARA

Wakati Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ukitarajiwa kuanza ziara ya siku 10 katika mikoa ya Tanzania Bara kesho, viongozi wa umoja huo wamemvaa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa kauli yake kuwa Katiba haina umuhimu.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema jana kwamba ameshangazwa na kauli ya Kinana kwa kuifananisha Tanzania na Uingereza ambayo haina Katiba.

"Kauli hii imenipa matatizo, naanza kutilia shaka kisomo cha hawa wenzetu..."

Hawana Katiba ya kuandika lakini wana sheria zao ambazo wanaziheshimu, ndiyo maana huwezi kuwahoji kuhusu Malkia Elizabeth wakakuelewa.


Mikutano ya Ukawa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema awamu ya kwanza ya ziara hiyo itaanza kesho hadi Mei 26, mwaka huu.

Alisema ili kufanikisha ziara hiyo, Ukawa imejigawa katika timu tatu ambazo zitakuwa zinafanya mikutano na maandamano ya amani.


Kundi la kwanza litaongozwa na Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Mosena Nyambabe, la pili litakuwa na Dk Slaa na la tatu litakuwa chini ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba.

TANZANIA YAPOTEZA SH 3 TRILION ZA KODI

Utafiti mpya umebaini kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya Sh3 trilioni kila mwaka kutokana na ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za uchimbaji madini na katika uingizaji bidhaa na kuuza nje.


Shirika la kiuchumi lenye makazi yake Marekani (GFI), lilitoa ripoti yake mwishoni mwa wiki iliyopita likieleza kuwa Tanzania inaongoza kwa kupoteza fedha nyingi zaidi kutokana na udanganyifu huo miongoni mwa nchi tano zilizofanyiwa utafiti za Kenya, Uganda, Ghana na Msumbiji.

Kiasi cha fedha kinachopotea kila mwaka, kingeweza kujenga zahanati 374 za kisasa kwa Sh8.1 bilioni kila moja.


Vilevile, utafiti huo umeonyesha kuwa kiasi hicho kinachopotea kingeweza kulisaidia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuzalisha nishati ya kiasi cha megawati 1,800, tatizo ambalo limekuwa sugu kwa miongo mingi.

Pia, kiasi hicho kingeliwezesha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kununua ndege 30 aina ya A320 ambayo hugharimu dola 60 milionikila moja.
Hivi karibuni Shirika la Ndege la Afrika Kusini lilinunua ndege hiyo.


Udanganyifu katika mauzo ulionekana zaidi katika uingizaji mafuta yenye msamaha wa kodi kwa kampuni za madini.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa huenda kampuni za madini hupandisha gharama za uingizaji wanishati hiyo ili kuhamisha fedha njeya nchi kwa njia haramu.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwangoambacho Tanzania hupoteza kila mwaka ni sawa na asilimia 16 ya bajeti ya sasa.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa kiasi kinachopotea ni mara tatu ya kile ambacho Serikali ilitangaza kukopa kupitia mashirika ya mikopo yenye masharti nafuu katika bajeti yake ya sasa.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania inafuatiwa na Kenya ambayo inapoteza Sh131 bilioni za Kenya (Sh2.489 trilioni), Ghana Dola za Marekani 1.44 bilioni (Sh2.304 trilioni) na Uganda Sh2.2 trilioni za Uganda (Sh1.4 trilioni) na Msumbiji iliyopoteza Dola za Marekani 585

WACHINA TISA WALAZWA KWA DENGUE DAR

Wakati raia tisa wa China wakibainika kuugua ugonjwa wa dengue na kulazwa hapa nchini, Rais Jakaya Kikwete amevunja ukimya na kuagiza wizara zake mbili kukabiliana na ugonjwa huo kwa dharura.


Ugonjwa huo uliingia nchini tangu mwaka 2010 lakini mlipuko wake mkubwa ulibainika Machi mwaka huu na hadi jana wagonjwa zaidi ya 400 walikuwa wameambukizwa, huku watatu wakiripotiwa kufariki dunia, akiwamo Daktari Bingwa wa magonjwa ya akili, Dk Gilbert Buberwa anayezikwa leo, Dar es Salaam.

Rais jana aliziagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na ile ya Fedha kushirikiana Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuchukua hatua za dharura kupambana nao kwa kuhakikisha vinapatikana vipimo vya kutosha na dawa.


*Wachina walazwa

Taarifa kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam zilieleza kuwa wagonjwa waliobainika kuugua homa hiyo hadi jana ni raia hao wa China na Watanzania wachache wenye historia ya kusafiri nje ya nchi hasa China, Ufilipino na Kusini mwa India.

Muuguzi katika kitengo cha magonjwa ya kuambukiza cha Aga Khan, Nyangee Lugoe alisema hospitali hiyo ilianza kupokea wagonjwa tangu Machi mwaka huu na kuanzia Aprili, raia wengi wa China wamegundulika kuwa na homa hiyo, ingawa baadhi walitibiwa na kuruhusiwa.


*Agizo la Rais Kikwete

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani huko Arusha, Rais Kikwete alisema: "Hili ni jambo la dharura la kitaifa lazima hatua muafaka zichukuliwe kudhibiti ugonjwa huu, ambao asili yake ni nchi za Asia na Bara la Amerika."


Alisema dalili za ugonjwa huo ambao unasababishwa na mbu ainaya Aedes Egyptie anayeuma mchana ni homa kali ya kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na kutoka damu puani na kwenye fizi na kupoteza fahamu.

"Napenda kutoa wito mtu yoyote ambaye atapata dalili za ugonjwa huu, aende mara moja hospitalini ili afanyiwe vipimo badala ya kunywa dawa," alisema.


Tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetangaza kuanza kuchukua hatua za dharura kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na uelimishaji na uhamasishaji wa jamii kuchukua tahadhari.


Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Charles Pallangyo alisema jana kuwa wizara yake imetoa hadhari ya ugonjwa huo kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilayakote nchini na itatoa mafunzo maalumu kwa watumishi wa afya ikiwajumuisha madaktari na mafundi maabara ili kuwajengea uwezo.


Aidha, wizara hiyo itaanzisha vituo maalumu vya ufuatiliaji wa ugonjwa huo katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke.


*Ugonjwa kutoka nje

Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue katika Hospitali ya Mwananyamala, Dk Mrisho Lupinda alisema upo uwezekano mkubwa kuwa virusi hivyo viliingia nchini kutokana na mwingiliano na urahisi wa watu kusafiri kati ya Tanzania na nchi za Mashariki ya Mbali.


"Namna watu wanavyopata nafasi ya kusafiri kwa haraka kwenda sehemu moja na kurudi kwa shughuli mbalimbali ikiwamo biashara ndivyo namna maambukizi yanavyoenea kwa urahisi. Hii inawezekana kabisa kwamba mwingiliano wa kibiashara umechangia kwa kiasi fulani," alisema.

Alisema ugonjwa huo ni wa kawaida katika maeneo ya kitropiki kwenye mabara yote, lakini umezoeleka zaidi kwenye nchi za Mashariki ya Mbali hasa bara la Asia.

Alisema mbu wanaoambukiza ugonjwa huo walikuwapo nchini kwa zaidi ya miaka 300 iliyopita lakini hawakuwa na virusi hivyo.


*Hakuna unyanyapaa

Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitaliya Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema licha ya ugonjwa huo unauana kuambukiza, wananchi hawapaswi kuwa na unyanyapaa kwa waliogua.

"Baada ya taarifa kuenea kwa kasi, kuna watu wameogopa na wanadhani wale waliopata hawapaswi kuguswa au kusogelewa lakini huu ni ugonjwa usioambukizwa kwa njia hizo kama ukoma," alisema.

Alisema mgonjwa wa dengue anahitaji tiba ya dalili zinazojitokeza na ili asiambukize atahitaji kulala kwenye chandarua hata kama ni mchana," alisema.

MAPACHA WAZALIWA WAKIWA WAMESHIKANA MIKONO

Mama mmoja nchini Marekani, amejifungua watoto pacha wakiwa wameshikana mikono.

Watoto hao pia walikuwa wanapumua bila usaidizi wowote walipotolewa kutoka katika mashine yenye hewa ya Oxygen.


Mama wa watoto hao, alisema kuwa watoto hao waliopewa majina ya Jillian na Jenna Thistlewaite walikuwa wameshikana katika kitovu na kutumia Kondo moja la nyuma , hali ambayo madaktari walisema ni nadra.

"Tayari wanaonekana kuwa marafiki ,'' alisema mama yaoSarah Thistlethwaite.


Walizaliwa Ijumaa katika jimbo la Ohio, wakiwa wameshikana mikono.

Inaarifiwa ni mama mmoja tukati ya akina mama elfu kumimwenye uwezo wa kujifungua watoto pacha wa aina hiyo.


Bi Thistlewaite, mwenye umri wa miaka 32, alilazimika kupumzika kwa wiki kadhaa kabla ya kujifungua kwani pacha wanaozaliwa wakiwa wameshikana mikoni ni hali nadra ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya watoto na mama kabla ya kuzaliwa.


Mama huyo alisema kupokea watoto wake ilikuwa zawadi tosha kwake wakati huu wa kusherehekea siku ya akina mama duniani.

MASHARTI YA BOKO HARAM KWA SERIKALI

Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekahu amesema kuwa atawaachilia huru wasichana waliotekwa nyara iwapo tu wapiganaji wakundi hilo wanaozuiliwa na serikali ya Nigeria wataachiliwa huru.

Katika kanda mpya iliyotolewa na kundi hilo, kiongozi huyo, amesema kuwa wasichana hao waliweza kusilimu katika kipindi cha wiki nne zilizopita tangu watekwe nyara.


Kanda hiyo inaonyesha zaidi ya wanawake miamoja wakiwa wamevalia hijabu na kuswali. Abubaka Shekau anasema kuwa wanawake hao ni wasichana waliotekwa nyara na kundi hilo.

Walitekwa nyara kutoka katika shule yao mjini Chibok, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo


Rais wa Ufaransa amejitolea kuwa mwenyeji wa mkutano utakaotafuta njia za kupambana na Boko Haram.

Wakati huohuo Waziri wa mambo ya ndani nchini Nigeria amesema serikali haitakubali masharti ya kundila Boko Haram kwamba kwanza liwaachilie wapiganaji wake kabla ya wasichana zaidi ya miambili waliotekwa nyara waachiliwe.


Waziri Abba Moro amsema nijambo la kipuuzi sana kwa kundi la kigaidi kujaribu kuweka masharti kama hayo.

Mwandishi wa BBC mjini Maiduguri John Simpson anasema kuwa masharti yaliyotolea na kundi hilo ni ishara kuwa liko tayari kufikia makubaliano na serikali


Wasichana watatu kati ya waliooyeshwa na kuongea katika kanda hiyo walikuwa wanavalia hijabu. Mmoja alisema kuwa amesilimu wakati mwingine akisema yeye tayari ni Muisilamu.

MCHWA WAVAMIA IKULU PARAGUAY

Mchwa wamevamia makaazi rasmi ya rais wa Paraguay na kutishia udhabiti wa jengo hilo.

Watalamu wa maswala ya ujenzi wameonya kwamba huenda Rais huyo akapoteza makaazi yake iwapo hatua zadharura hazitachukuliwa kuwaangamiza mchwa.

Kwa mujibu wa wanasayasi wa kibiolojia mchwa ni mdudu mwenye bidii sana na kamwe hachoki kutekeleza majukumu yake.

Na ni kutokana na hilo ndipo wahenga katika juhudi za kutoa motisha kwa yeyote yule anayetaka kufanikiwa maishani wakasema ''lazima awe na bidii ya mchwa''.


Msemo huu umedhihirika nchini Paraguay baada ya habari kwamba mchwa wamevamia makaazi rasmi ya Rais Horacio Cartes.

Wataalam wa maswala ya ujenzi wanasema mchwa haowameharibu sakafu na sehemu zilizojengwa kwa mbao.

Wahandisi hao wameonya kuwa huenda sehemu moja ya jengo hilo likaanguka iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.


Wamependekeza Rais huyo ahamishwe kutoka jengo hilo ili wataalam waweze kupambana na wadudu hao wenye bidii na ukarabati uweze kufanyiwa jengo hilo.

Ni dhahiri kuwa wageni hao waharibifu sasa wanatishia starehe na itifaki ya Rais Horacio Cartes.

DEREVA AFARIKI AKIWA KATIKA FOLENI

Dereva wa malori ya safari za masafa marefu Charles Mbungu (46), amefariki dunia akiwa ndani ya lori alipokuwa katika foleni ya ukaguzi wa magari kwenye Kituo cha Misugusugu, Kibaha, Pwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema dereva huyo aliyekuwa alikitoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), alikutwa na mauti hayo akiwa ndaniya gari aina ya Leyland Daf alilokuwa akiendesha kuelekea Dar es Salaam.

Kamanda Matei alisema kabla ya dereva huyo mwenyeji wa Mkoa waIringa kabla ya kufikwa na mauti, alikuwa akilalamika kuwa anajisikia vibaya walipokuwa njiani.


Akizungumzia tukio hilo utingo wa lori hilo, Said Hemed (22) alisema:

"Tulianza safari vyema, lakini tulipokaribia Chalinze, akaanza kulalamika kuwa hajisikii vizuri. Tuliendelea na safari, huku nampa moyo lakini alirudia maneno hayo tulipofika Mlandizi, lakini alikuwa akinieleza itambidi kwenda kupimapindi akifika tu Dar es Salaam."

Tukaendelea na safari na jamaa alikua safi tu akiendesha, lakini tulipokuwa kati ya Mlandizi na Kibaha alirudia kusema mwili wake kama haupo vizuri vile na tulipokuwa katikati ya safari kabla ya kufika Misugusugu aliniambia... 'Dogo hali siyo nzuri ninaumwa aisee'.


"Nikamuuliza sasa kuendesha utaweza kweli? Akaniambia Mungu ni mwema, nitajitahidi tufike Dar es Salaam ili nikafanye vipimo kabisa maana hali siyo nzuri. Tukajahadi hapa check point (kituo cha ukaguzi) sasa akawa ananieleza huku kalalia usukani. Mimi nikateremka kuangalia kinachoendelea, kwani ilikuwa foleni ndefu kiasi. Muda mfupi nikarudi kwenye gari, kufika nikamkuta 'bro' amefariki, yaani ni kama kaniambia hebu nipishe naondoka. Sikuamini lakini ndivyo ilivyotokea."

Kamanda Matei alisema kuwa mwiliwa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Tumbi kwa ajili ya kuhifadhiwa pamoja na kufanyiwa uchunguzi.


Ofisa Habari wa Hospitali ya Tumbi, Gerald Chami alisema vipimo vilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.

Hemed alisema baadaye kuwa baada ya tukio hilo alifanya utaratibu wa kuliingiza lori hilo katika yadi ya magari iliyopo eneo hilo na baadaye kufanya mawasiliano na tajiri yake kwa ajili ya utaratibu wa kuuhifadhi mwili pamoja na gari.

CAG AZIDI KUIBUA MADUDU SASA NI HESLB

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini madudu ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu yaJuu (HESLB) ambapo mikopo ilitolewa ni kwa wanafunzi waliofelimitihani.

Kiasi cha Sh 214.5 milioni kilitolewakama mkopo kwa wanafunzi walioshindwa mitihani na kutoendelea na chuo na wengine walioahirisha masomo katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.


Taarifa ya CAG, Ludovick Utouh aliyoiwasilisha Bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita, imebainisha wanafunzi walioacha masomo au kuahirisha masomo kuwa nao waliendelea kupatiwa mikopo hiyo.

CAG amebainisha kuwa kitendo hicho kilikuwa ni kinyume cha ibaraya pili, sehemu ya kwanza ya mwongozo wa ukopeshaji wa HESLB inayoelekeza vigezo vya wanaostahili kupata mikopo.


Moja ya vigezo hivyo ni ufaulu kwa wanafunzi kuelekea mwaka wa masomo unaofuata.

Hata hivyo CAG alibaini kwa mwaka 2012/2013, HESLB ilitoa mikopo ya Sh 214.5 milioni kwa wanafunzi waliofeli au kuahirisha masomo katika vyuo vikuu mbalimbali ndanina nje ya nchi.


Baadhi ya vyuo hivyo ni pamoja na vyuo vikuu katika nchi za Algeria na Cuba ambazo wanafunzi wake walipewa mikopo ya Sh131 milioni huku mikopo kwa wanafunzi Urusi ikiwa Sh9.6 milioni.

Nchini, wanafunzi waliopewa mikopo hiyo wanatoka Chuo kikuu Dodoma (UDOM) walilipwa Sh43.9 milioni na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) walilipwa Sh28.9 milioni.

TABORA WAMGOMEA SHEIKH MKUU

Kutokana na kuondolewa kwa Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Shaaban Salum na Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Issa bin Simba, baadhi ya Waislamu wamedai kitendo hicho hakivumiliki.

Sheikh Salum alivuliwa uongozi na kupewa barua iliyosainiwa na Sheikh Simba inayoeleza kuwa ameshindwa kutekeleza matakwa ya kufuta usajili wa Msikiti wa Ijumaa kutoka kwa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) baada ya kupewa miezi mitatu kufanya hivyo.

Akizungumza kwenye Msikiti wa Ijumaa baada ya Swala ya Alasiri, Sheikh Salum aliwaeleza waumini kuwa amevuliwa uongozi kutokana na mkakati wake wa kuwaendeleza Waislamu.

"Nimesimama kuwaeleza kuwa nimekumbwa na kadhia leo (jana), pengine nitabaki kuwa imamu kwani nimevuliwa uongozi siyo tena Sheikh wa Mkoa kutokana na mkakati na mpangokazi wangu wa maendeleo ambao umesababisha kuvuliwa madaraka," alisema Sheikh Salum.

Alisema alikuwa na mipango ya kujenga maduka kuzunguka msikiti na kwamba ana uhakika wameweza kupata Sh10 milioni ambazo zitatumika kwa manufaa ya Waislamu.


Sheikh Salum aliwalaumu watu wasiowatakia mema ambao alidai wamejaa husuda, huku akiwaita waongo na wanafiki duniani na ahera.

Akitoa msimamo wa Waislamu wanaoswali msikiti hapo, msemaji wa msikiti huo, Abuu Bakari alisema hawatambui kuvuliwa uongozi kwa Sheikh Salum na kwamba wanaendela kumtambua.


"Tunatoa taarifa kwa Mufti, Waislamu hususani wa Msikiti wa Ijumaa kuwa tunamtambua Sheikh Shaaban Salum kama Sheikh wa Mkoa. Tunamtambua hivyo na tunamwagiza mufti alete mtu atueleze sababu za kumtoa kwenyewadhifa wake," alisema.


Bakari aliitaka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Seleiman Kumchaya kutoa taarifa za kuvurugwa kwa waumini wa Kiislamu, vinginevyo yatakayotokea asije akalaumu watu wa Tabora.


Baadhi ya waumini waliunga mkono tamko hilo na kudai wataendelea kumtambua kama kiongozi wao na kwamba Simba amevunja Katiba ya Bakwata na kutaka aondolewe kwenye wadhifa wake huku wakisisitiza Sheikh Salum alichaguliwa na Waislamu ambao ndiyo wanaopaswa kuelezwa makosa aliyotenda ili wamhukumu siyo kuondolewa kinyemela.


"Kama mufti ameona Sheikh Salum amefanya makosa kwa nini hakuchagua mtu miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Ulamaa, badala yake amechagua mtu kutokanje ya baraza hilo?" alihoji Kansa Mbarouk.

BOKO HARAM WAONESHA PICHA ZA WASICHANA WALIOTEKWA

Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekahu amesema kuwa atawaachilia huru wasichana waliotekwa nyara iwapo tu wapiganaji wakundi hilo wanaozuiliwa na serikali ya Nigeria wataachiliwa huru.

Katika kanda mpya iliyotolewa na kundi hilo, kiongozi huyo, amesema kuwa wasichana hao waliweza kusilimu katika kipindi cha wiki nne zilizopita tangu watekwe nyara.

Kanda hiyo inaonyesha zaidi ya wanawake miamoja wakiwa wamevalia hijabu na kuswali.

Abubaka Shekau anasema kuwa wanawake hao ni wasichana waliotekwa nyara na kundi hilo.

ISRAEL YASAIDIA NIGERIA KUTAFUTA WASICHANA

Kikosi cha Israel cha kukabiliana na ugaidi kinatarajiwa kujiunga na juhudi za kuwatafuta zaidi ya wasichana 200 waliotekwa nyara nchini Nigeria na wanamgambo wa kundi la Boko Haram.


Kundi hilo litajiunga na wataalamu wa Marekani,Uingereza na ufaransa ambao tayari wako nchini Nigeria.

Rais Goodluck Jonathan amesema kuwa kujiunga kwa Israel katika operesheni hiyo ni wazi kwamba dunia nzima inaunga mkono usakaji wa wasichana hao.


Mwandishi wa BBC nchini Nigeria amesema kuwa uwepo wa wataalam wa Israel katika oparesheni hiyo huenda kukazua hisia za kisiasa nchini Nigeria ambapo wasiwasi kati ya wakristo wanaoshi kusini mwa taifa hilo na waislamu wanaoishi kazkazini huzua ghasia.

Awali Gavana wa jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa taifa hilo, eneo ambalo wasichana hao walitekwanyara alisema kuwa ana habari kuhusu kule walipo wasichana hao.

AJARI YA FUSO YAUA WATATU NA KUJERUHI

Watu watatu wamefariki dunia hapo hapo Wilaya Mpanda Mkoa wa Katavi baada ya gariRoli aina ya Fuso walilokuwa wakisafiria kupinduka na watu wengine wanne wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.

Ajari hiyo ilitokea hapo juzi majira ya saa kumi na moja jioni baada ya gari aina ya fuso lenye Nanba za usajiri T 168 APU lililokuwa likiendeshwa na Dreva Deus Lukas (28 )mkazi wa mtaa waKawajense Mjini hapa kupinduka katika mlima wa Sijonga Gari mali ya mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Ikola alifahamika kwa jina moja tuu (MAN) Katika ajari hiyo watu watatu walikufa hapo hapo ambao Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari aliwataja kuwai ni Agnes Martin(7) mwanafunzi wa shule ya Msingi Kashato katika Halmashauri ya mji wa Mpanda Elizabeti Mseveni (24) mkazi wa Mtaa wa Majengo mjini Mpanda ambae ni mama mdogo wa Agnes na Madanganya Rashid (53) mkazi wa kijiji chaIkola Tarafa ya Karema Wlaya ya Mpanda Kamanda wa Jeshi la Polisi waMkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari alisema ajari hiyo ilitokea katika eneo la Mlima wa Sijonga Katika Tarafa ya Kabungu Barabara inayotoka mjini Mpanda Kuelekea Tarafa ya Karema mwambao mwa Ziwa Tanganyika baada ya gari hilo kukatika propela shafuti likiwalikiwa kwenye mlima Kidavashari aliwataja watu wanne waliojeruhiwa ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kuwa niSaimoni Masafila (42)Mkazi wa Kijiji cha Mwamapuli Tarafa ya Mpimbwe Wilaya yaMlele Mwasiti Juma (19) Mwajuma Seif (19) na Nassir Salumu mtoto mdogo wa miezi minne wote wakazi wa mjini Mpanda


Alisema Dereva wa gari hilo Deus Lukas alikuwa akiendesha Fuso hilo huku akiwa amewapakia watu hao na mizigo mbalimbali ya bidhaa za wafanyabiashara huku akiwa anatokea mjini Mpanda akiwa anaelekea katika kijiji cha Ikola kilichoko mwambao mwa ziwa Tanganyika


Kidavashari alifafanua baadaya gari hilo kufika kwenye eneo la mlima wa Sijonga gari hilo lilikatika propela shafti na kusababisha roli hilo kupinduka na watu watatu walifariki Dunia hapo hapo na watu wanne walijeruhiwa nakulazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda wakiendelea kupatiwa matibabu huku hari zao zikiwa zinaendelea vizuri.

Alisema Dereva wa Gari hilo alikamatwa na anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi wakati taratibu za kumfikisha mahakamani zikiwa zinaendelea ili akajibu mashitaka ya kuhusiana na ajari hiyo.

Kidavashari alieleza mili ya marehemu wote watatu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa ajiri ya kufanyiwa uchunguzi wa Kidaktari na baada ya hapo watakabidhiwa ndugu kwa ajiri ya mazishi.

MBEYA CITY NDANI YA MASHINDANO YA NILE

Timu ya Mbeya City imeteuliwa kushiriki mashindano ya Shirikisho la Baraza la Vyama Vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yajulikanayo kama Kombe la Mto Nile (Cecafa Nile Basin) yatakayofanyika nchini Sudan kuanzia Mei 22 hadi Juni 4 mwaka huu.


Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye alitangaza uteuzi huo kwa waandishi wa habari jijini Mbeya mara baada ya kufanya kazi ya kukagua Uwanja wa Sokoine kama unafaa kuchezewa mechi za kimataifa, akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi.


Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mashindano hayo mapya hushirikisha timu zilizoshika nafasi ya pili katika ligi za nchi wanachama, ambapo kwa Tanzania, Yanga ndiyo ilitakiwa kushiriki michuano hiyo, lakini walisema hawapo tayari kushiriki.

Alisema kuwa hata walipoiteua timu ya Azam ambayo ndiyo mabingwa wa Ligi ya Tanzania Bara waligoma kushiriki wakidai kuwa wachezaji wao wapo likizo.


Alisema kuwa Cecafa kwa kushirikiana na TFF waliona ni vyema kuiteua Mbeya City ambayo imeshika nafasi ya tatu.

MALAWI, TANZANIA WASHIRIKIANA MSIBA WA BALOZI

MAOFISA wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wenzao wa Serikali ya Malawi, wameendelea namaandalizi msiba wa ghafla wa Balozi wa Malawi nchini, Flossie Chiyaonga.


Akizungumza jana na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, alisema misaya kumuaga Balozi Flossie itafanyikaleo katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Balozi Flossie alifariki Ijumaa iliyopita akiwa njiani wakati akipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu, baada ya kuugua akiwa nyumbani kwake.


Kwa mujibu wa Haule, Jumatatu iliyopita usiku, Balozi Flossie alijisikia vibaya na kupelekwa Aga Khan ambako alipatiwa matibabu nakuwekwa mapumziko kati ya saa sita usiku saa 12 asubuhi, ambapo alipatiwa dawa za kutumia nyumbani na kuruhusiwa.


Hata hivyo, Haule alisema Ijumaa iliyopita, hali ilibadilika mchana na kurejeshwa hospitalini, lakini alipofikishwa Aga Khan, madaktari walimfanyia vipimo na kubaini ameshafariki.


Sababu ya kifo Haule alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi jana, ambapo madaktari walibaini kuwa chanzo cha kifo chake ni kuvimba na kupasuka kwa mshipa mkubwa wa moyo, uliosababisha damu kujaa na kwenye mfuko wa moyo na kushindwa kufanya kazi.


Haule alisema wakati wa uhai wake,Balozi Flossie alifanya kazi zake kwa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi na kushirikiana vizuri na mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi zao Tanzania.


Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Leo utapelekwa ukumbi wa Mwalimu Nyerere kwa misa na kuaga kabla ya kusafirishwa kesho kwenda nyumbani kwao, Blantyre, Malawi kwa ajili ya maziko, yatakayofanyika Jumatano wiki hii.

MAPIGANO YAZUKA SUDAN KUSINI

Saa chache tu baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa usitishaji mapigano nchini Sudan kusini Malumbano yameibuka.


Sasa Serikali na wapiganaji wa Sudan Kusini wanalaumiana kila upande ukimshutumu mwenzake kuvunja makubaliano hayo yaliyosainiwa ijumaa.


Hata hivyo kiongozi wa waasi Riek Machar anasema bado ameazimia kutekeleza makubaliano hayo licha ya kwamba anasema serikali ya rais Salva Kiir inavunja mapatano hayo.


Machar amesema kuwa majeshi ya UPDF ya Uganda ambayo yamekuwa yakivamia maeneo inayoyadhibiti haijaafiki mkataba uliotiwa sahihi huko Adiss Ababa kati yake na RaisSalva Kiir.


Aidha msemaji wa jeshi la serikali, Kanali Philip Aguer, amesema waasi hao wameshambulia maeneo ya serikali katika mji wa Bentiu.

Upinzani umepinga madai hayo.


Machar ameiambia BBC kuwa angetaka mazungumzo zaidi na serikali kuhusu hilo, lakini amesema anafahamu kuwa Rais hana uwezo wa kudhibiti majeshi yote yanayopigana kwa upande mmoja na majeshi ya serikali kama vile majeshi ya Uganda na wapiganaji kutoka Darfur.


Serikali ya Sudan Kusini pia imelaumu upande wa waasi kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano saa chache tuu baada ya mkataba huo kutiwa saini.


Makubaliano ya kusitisha mapigano yalitiwa saini Ijumaa, na yalikusudiwa kumaliza vita vya miezi mitano ambavyo vimeuwa maelfu ya watu na kulazimisha zaidi ya milioni moja kuhama makwao.

MAHABUSU WAVUA NGUO NA KUKUMBATIA MLINGOTI WA BENDERA

MAHABUSU wawili kati ya sita wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji, wameleta kizaazaa baada ya kujaribu kutoroka na kukimbilia kwenye mlingoti wa Bendera ya Taifa nakuing'ang'ania kisha kuvua nguo na mmoja wao kubaki mtupu.


Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 4:00 asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, wakati mahabusu hao walipofikishwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi zao, lakini ghafla walipofika kwenye viwanja vya mahakama hiyo walitimua mbiyo kuelekea kwenye mlingoti wa Bendera hiyo ya Taifa na kuvua nguo.


Wananchi waliokuwa katika viwanja vya mahakamani hapo waliachwa midomo wazi na hali ya mshangao, mara baada ya mmoja kati ya hao wawili wakifanikiwa kuufikia mlingoti huo na kuvua nguo kisha kuanza kupiga kelele kwa kupaza sauti kudai haki itendeke.


Tukio hilo pia lilishuhudiwa na watumishi wa Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo, Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka ya jijini hapa (MWAUWASA), Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), na taasisi zingine zilizo jirani na majengo ya mahakamani hapo na wananchi waliokuwa wakisubilia kesi zao kutajwa.

Mahabusu hao sita waliojaribu kutoroka na kuishia kudhibitiwa vyombo vya dola, walitajwa kwa majina kuwa ni Thobiasi Warioba (35), aliyeamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu eneo la mlingoti wa Bendera ya Taifa, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji Na. 32/2012.

Watuhumiwa wengine waliojaribu kutoroka ni Hamis Ramadani (30), Anthony Petro (35), Marwa Mwita (38), na Chacha Wangwe (35), na mwingine ambaye hakufahamika majina yake mara moja, wote wanakabiliwa na kesi ya Jinai Na. 215/2013 na walikamatwa tangu mwaka 2011.


Wakiwa katika viwanja vya mahakama hiyo baada ya kudhibitiwa na askari polisi, mmoja wa mahabusu hao walisikika wakisema: "Haiwezekani, tangu mwaka 2011 tulipokamatwa hadi sasa kesi zetu hazijasikilizwa.


Wengine tumebambikiziwa kesi. "Tunaomba haki zetu, polisi mnatuonea, vyombo vya habari tunaomba mtusaidie tumekaa muda mrefu bila kusikilizwa na hatujui hatma yetu tangu 2011 tulipo kamatwa tumechoka kukaa mahabusu, tunaomba kesi zetu zisikilizwe".


Baada ya malalamiko yao, ndipo askari mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Inspekta Henry akiwa na wenzake sita waliokuwa wakiwadhibiti wasikimbie na kuwahoji kuhusiana na madai yao, huku askari hao wakiwataka kuondoka katika mlingoti huo na kumtaka Warioba avae nguo ili waweze kuingia mahakamani.


"Pamoja na maamuzi yenu haya, lakini mtambue mnavunja sheria na hili ni kosa jingine la jinai, hivyo ni vema mkaondoka kwenye mlingoti huu na kuingia mahakamani.

Malalamiko yenu tumeyasikia na yatashughulikiwa," alisema Inspekta Henry.


Mmoja wa maofisa waandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, ambaye alikataa kutajwa jina lake, alidai ushahidi wa kesi za watuhumiwa hao bado haujakamilika, na kwamba kesi zao haziwezi kusikilizwa na mahakama ya wilaya kwani haina uwezo na badala yake zitatajwa tu kisha kuhamishiwa Mahakama Kuu.

"Bado hiyo ni Criminal Case (kesi ya mauaji) au PI Case hivyo Mahakama Kuu haiwezi kuzungumzia hilo kwa sasa kwa kuwa utaratibu wa mahakama kuu ikisha kuwa tayari huitwa 'Criminary Session Case', ambapo sasa hupangiwa namba ya kesi na Jaji wa kuisikiliza," alisema.


Source:Matukio daima

ASILIMIA 48 YA WAKAZI WA MPANDA HUPATA MAJI SAFI

NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri, amesema ni asilimia 48 tu ya wakazi wa Wilaya ya Mpanda, ndio wanapata maji safi na salama.


Alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa MpandaVijijini, Moshi Kakoso (CCM) bungeni jana, aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la maji katika vijiji vya Kamsanga, Bugwe, Sibwesa, Mpemba, Kabage, Mwese na Bujombe.


Kutokana na hali hiyo, alisema bado ipo changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo ya maji kwa wakazi wa wilaya hiyo na ili kutatua tatizo la maji katika vijijihivyo, Serikali itatekeleza mradi wa maji wa kisima kifupi katika Kijiji cha Kamsanga na tayari upimaji wa eneo la kuchimba kisima kirefu umefanyika na kitachimbwa Juni mwaka huu.

Alisema Kijiji cha Bujombe katika mwaka 2013/14 kimetengewa Sh milioni 8 kwa ajili kuchimba kisimakifupi kimoja."


Katika Kijiji cha Mwese, Serikali kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki katika mwaka 2013/14, imepanga kutumia Sh milioni 65 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji mserereko utakaowahudumia wananchi wengi zaidi ukiwa na vituo vitano.

"Aidha, kijiji hiki pamoja na kijiji ya Mpemba vimeingizwa katika mpango wa kuleta Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambapo miradi yenye thamani ya Sh bilioni 1.4 inatarajiwa kujengwa ifikapo 2015/16,"alisema Mwanri.

Alisema hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imepokea Sh milioni 742 kwa mwaka wa fedha 2013/14, fedha ambazo zitatekeleza miradi yote ya maji.


Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufuatilia kwa karibu kiasi chote cha fedha kilichobaki, ilikipatikane kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2013/14.

AFARIKI BAADA YA KUZIDISHA KUNYWA VIROBA

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Michael Silanda (26 ) Mkazi wa Kijiji cha Ibindi Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi amefariki Dunia baadaya kunywa Pombe (VIROBA ) aina ya Zed kupita kiasi bila kula Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa Kamishina msaidizi mwandamizi Dhahiri Kidavashari tukio hilo lilitokea hapo mei tano mwaka huu majira ya saa sita usiku kijijini hapo.


Alisema siiku hiyo ya tukio marehemu baada ya kuamka asubuhi nyumbani kwake hapo majira ya saa tano asubuhi alielekea kwenye Bar ambayo ilikuwa ikiuza vinywaji vya aina mbalimbali vya pombe kali na vinywaji baridi.


Alifafanua kuwa baada ya kufika kwenye Bar hiyo aliwakuta baadhi ya wanakijiji wenzake wakiwa wanakunywa pombe za aina mbalimbali hari ambayo ilimfanya marehemu aweze kujumuika nao kwa kuagiza pombe (VIROBA ) aina ya Zed.


Alisema Michael aliendelea kunywa viroba kuanzia mudahuo kwenye bar hiyo bila kula kitu chochote hadi hapo majira ya saa sita usiku alipoamua kurudi nyumbani kwake huku akiwa amelewa pombe kupita kiasi.


Baada ya kufika nyumbani kwake aliingia ndani ya nyumba yake na kulala bila kula chakula chochote na siku iliyofuata majira ya saa mbili asubuhi ndipo walipomkuta Michael akiwa amefariki Dunia huku akiwa amelala kitandani kwake.


Kamanda Kidavashari alisema uchunguzi wa awali oliofanywa kuhusiana na kifo hicho umebaini kuwa kifo hicho kimesababishwa na marehemu kunywa pombe nyingi kupita kiasi bila kula chakula.


Alisema mwili wa marehemu Michae Silanda umehifadhiwa kwenye chumba cha kuifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa ajiri yakufanyiwa uchunguzi wa Kidaktari na baada ya uchunguzi huo watakabidhiwa ndugu wa marehemu kwa ajiri ya utaratibu wa mazishi.

CAG ABAINI KASORO VYAMA VYA SIASA

Ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), katika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu umebaini madudu ikiwamo vyama vinne kutokuwa na akaunti benki.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, CAG Ludovick Utouh alivitaja vyama ambavyo havina akaunti benki kuwa ni UMD, NLD, NRA na ADC.


"Katika hesabu walizotuletea kulikuwa hakuna ushahidi kwamba wanaendesha akaunti benki," alisema huku akibainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Vyama vya Siasa.


Halikadhalika katika ukaguzi huo, vyama vya siasa 11 kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu, havikuwasilisha taarifa za hesabu zamwaka kama Kifungu cha 14(1) cha sheria hiyo ya mwaka 1992 kinavyosema.

Alipoulizwa baadaye vyama hivyo, Utouh alivitaja CCK, UPDP, Tadea, Demokrasia Makini, Chausta, DP naAFP. Vyama vya Sauti ya Umma na Chauma viliwasilisha hesabu zao vikiwa vimechelewa.


Utouh alisema katika ukaguzi huo, taarifa za hesabu zilizowasilishwa na vyama 10 hazikufuata misingi yamfumo wa utoaji wa taarifa za fedha za kimataifa.


"Tulibaini kuwa hakuna chama cha siasa hadi sasa kilichowasilisha kwa msajili wa vyama vya siasa tamko lamali zote zinazomilikiwa na chama husika jambo ambalo ni kinyume cha sheria," alisema.


Utouh alitumia mkutano wake huo na wanahabari kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto kwa kusimama kidete kuhakikisha vyama vya siasa navyo vinakaguliwa na CAG kama sheria inavyoelekeza.


Kwa upande wake Zitto, naye alimpongeza CAG kwa kukagua vyama vya siasa akisema ni kati ya maeneo yaliyokuwa na matatizo.


"Kwa kitendo chako cha kuamua kukagua bila hata ya kupewa fedha ni kitendo ambacho kinaonyesha uzalendo wako wa hali ya juu," alisema Zitto na kuongeza:

"Kwa sababu tunachokitaka sisi ni kila senti ya mlipa kodi ikaguliwe na kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwa miaka minne vilikuwa vimepewa ruzuku ya Sh69 bilioni."


Zitto alihoji kama CAG anakwenda kukagua bodi za mazao nchini ni kwa nini vyama vya siasa visikaguliwe wakati ndivyo vinavyozalisha Serikali pale vinaposhinda uchaguzi?

EU YATOA SH.5 BILLION EAC

Jumuiya ya Ulaya (EU), jana ilitoa msaada wa Euro 2.3 milioni (Sh5.7 bilioni) kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kusadia vita dhidi ya maharamia na uhalifu wa majini Ukanda wa Kusini mwa Afrika.


Akizungumza kabla ya kutia saini makubaliano ya msaada huo jijini Arusha jana, Balozi wa EU nchini, ambaye pia ni Balozi wa Jumuiya hiyo kwenye Sekretarieti ya EAC, Filberto Sebregondi alisema wametoa fedha hizo kuimarisha usalama Ukanda wa Pwani wa EAC kutokana na umuhimu wake kibiashara.


"Licha ya kuhatarisha usalama, vitendo vya uharamia ni kikwazo cha maendeleo ya kibiashara kati ya Afrika na Ulaya, hatuna budi kuyakabili kwa pamoja," alisema Balozi Sebregondi


Msaada huo ni sehemu ya Euro 37.5 milioni kusaidia vita dhidi ya maharamia na uhalifu wa majini katika nchi za Ukanda wa EAC, COMESA, IGAD na IOC. Pamoja na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, fedha hizo pia zitatumika kuimarisha vyombo vya uamuzi.

WAGONJWA WA DENGUE WAFIKA 376

Homa ya dengue inaendelea kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari hadi juzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu 376 wamekwishagundulika kuugua ugonjwa huo.


Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa wizara hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema hadi jana watu wawili walikuwa wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema inaweza kuwa kubwa zaidi endapo upimaji utafanyika katika kila wilaya. "Pengine idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu wengi hawapimwi, Ijumaa (kesho) tutatoa,taarifa zaidi," alisema.


Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa wengi zaidi, ikifuatiwa naIlala na Temeke. Hata hivyo, alisema huenda wilaya zenye idadi ndogo ya wagonjwa hazijaweza kupima na kubaini watu wenye maradhi hayo ikilinganishwa na Kinondoni.


Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema hali nimbaya na wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.


Mtafiti wa malaria, tabia za mbu namazingira, wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Nicholas Govela alisema tayari wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa kina kuwajua mbu wanaoeneza homa yadengue nchini.

"Utafiti huu utasaidia kujua ni mbu kiasi gani wameathirika na virusi hivyo. Tukifanya hivyo tutajua ukubwa wa tatizo, tutajua wanapatikana wapi zaidi na virusi vyao vimetokea wapi," alisema.

Dk Govela alisema ni lazima utafiti huo ufanyike ili kudhibiti maambukizi zaidi ya homa hiyo akisema zipo sababu kadhaa zinazohisiwa kusababisha maradhi hayo, ikiwamo ya wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homahiyo na kuambukizwa kwa njia ya kuumwa na mbu."Ugonjwa huu umeenea zaidi nchi za Amerika ya Kusini na Kusini mwaBara la Asia.

Hapa kwetu mbu hawa walikuwapo lakini ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa kiasi hiki, ndiyo maana sababu zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji," alisema.


Alisema maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mtu mwenye ugonjwa huo kuumwa na mbu hao aina ya Aedes Egyptiae nambu hao wakichukua virusi, huvisambaza kwa watu wengine. "Inawezekana tatizo ni kubwa zaidi ya hivi inavyofikiriwa kwa sababu wanaokuja hospitali kupimwa na kugundulika ni wachache, wengi wasiofika hawawezi kujulikana," alisema.


Makazi duni hatarini zaidiDaktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue, Mrisho Rupinda alisema watu wanaoishi katika makazi duni wapo hatarini kuathiriwa zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa taka nyingi na madimbwi.


Alitoa mfano wa wagonjwa wa kwanza wilayani Kinondoni, akisema walitokea maeneo ya Kambangwa, Mwananyamala Komakoma ambako kulikuwa na madimbwi na bwawa la maji.


"Wagonjwa wengi huonekana zaidi kwenye makazi duni kwa sababu ya mpangilio mbovu na kuzagaa kwa taka. Lakini pia maeneo mengine ambayo watu huhifadhi maji kwenye matenki au ndoo kwa muda mrefu bila kuyafunika," alisema.

PUTIN HATAKI KURA YA MAONI

Katika hatua ambayo haikutarajiwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ametoa wito kwa makundi yanayotaka kujitenga wanaounga mkono Urusi Kusini Mashariki mwa Ukraine waahirishe kura ya maoni ya Jumapili juu ya kutaka kujitenga kama hatua muhimu kuimarisha mashauriano ya amani kati ya makundi yanayozozana nchini humo.

Rais Putin alisema kuwa hatua hiyo itaimarisha mazingira ya kufanya mashauriano kati ya Serikali ya Ukraine na wale nchini wanaopendelea Urusi wanaotaka maeneo yao kujitenga na kuungana na Urusi.

Amesema kuwa uchaguzi wa Urais uliopangwa kufanywa Mei 25, ni hatua inayofaa.

Siku chache zilizopita Bwana Putin alitaja uwezekano wa kuwa na uchaguzi huo wa Urais kama upuzi mtupu.

Lakini katika taarifa ya hivi sasa Bwana Putin amesema uchaguzi huo hautakuwa na maana iwapo raia wote wa Ukraine hawatahusishwa na kuwahakikishia jinsi haki zao zitakavyolindwa baada ya uchaguzi.


Vladmir Putin pia alidai kuwa Urusi imewaondoa wanajeshi wake kwenye mpaka wake na Ukraine.

Hata hivyo mataifa ya Magharibi yanatarajiwa kutoamini hakikisho hili hadi watakapo shuhudia kinachoendelea mpakani.


Mataifa hayo pia yanasubiri kuona iwapo taarifa ya Putin itapunguza uhasama miongoni mwa wananchi wa Ukraine.

BOKO HARAM WAFANYA SHAMBULIZI

Taarifa kutoka nchini Nigeria, zinasema kuwa mamia ya watu waliuawa katika shambulizi lililofanywa na kundi la wapiganaji wa Boko Haram katika mpaka wa nchi hiyo na Cameroon siku ya Jumanne.


Katika mahojiano na BBC kiongozi mmoja wa eneo hilo, Ahmed Zanna, alisema kuwa washukiwa walivamia mji wa Gamboru Ngala, katika jimbo la Borno, na kuwaua takriban watu 300.

Inaarifiwa wapiganaji hao waliwafyatulia risasi watu kiholela katika soko kuu la eneo hilo.


Mwandishi wa BBC nchini Nigeria anasema ilikuwa vigumu kupata taarifa hizo mapema kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano katika jimbo hilo hasa kwa sababu eneo hilo liko mbali sana.

Wakazi wa eneo hilo wanasema kuwa walipata zaidi ya maiti mia moja kutokana na shambulizi hilo

MVUA YA SAMAKI YANYESHA SRI LANKA

Wakaazi wa kijiji kimoja Magharibi mwa Sri Lanka wamesema kuwa wameshangazwa na pia kufurahishwa na tukio la 'kunyeshewa' na mvua ya Samaki wadogo.


Samaki hawa ambao walikuwa katika hali nzuri ya kuweza kulika wanaaminika kuwa walibebwa kutoka kwa mto kwa upepo mkali.

Wanakijiji hao wa wilaya ya Chilaw walisema kuwa walisikia kitu kizito kikianguka na wakapata samaki wengi wenye uzani wa kilo hamsini.

Hili si tukio la kwanza la aina hii kuwahi kutokea Sri Lanka- mwaka wa 2012, kulitokea kisa cha mvua ya viumbe vya baharini vijulikanavyo kama 'Kamba' ambavyo huliwa


Wanasayansi wamesema kuwa mvua ya Samaki hutokea wakati ambapo upepo mkali unazinga juu ya maji ya kina kifupi na hivyo kusababisha mzunguko wa maji unaovuta karibu kila kitu kilicho ndani ya maji ikiwa ni pamoja na samaki na hata Vyura.


Viumbe hawa wa majini wanaweza wakasafirishwa kwa masafa marefu kwa kushikiliwa na mawingu hata baada ya ule mzunguko wa maji kuisha.Wanakijiji wanasema kuwa mvua hiyo ya Samaki ilinyesha Jumatatu huku viumbe wale wakianguka kwenye mashamba, barabarana paa za kijiji hicho.


Baadhi ya samaki hao wenye urefu wa kati ya sentimita tano na nane, walikuwa bado wako hai na walitiwa kwenye ndoo za maji na wanakijiji waliowatumia kama kitoweo badaye.

Hii ni mara ya tatu kwa tukio kama hili kufanyika Sri Lanka, ingawa katika eneo tofauti.


Kando na ile mvua ya 'Prawn'ya mwaka wa 2012 kusini mwa Sri Lanka, mvua ya kimondo (meteors) nyekundu na manjano ilinyesha mwaka huo huo, tukio ambalo bado linachunguzwa na wanasayansi wa Marekani naUingereza.

Samaki wamadhamana kuu Sri Lanka.

YINGLUCK SHINAWATRA ATIMULIWA UWAZIRI MKUU

Mahakama ya kikatiba Nchini Thailand imeamuru Waziri mku wa Nchi hiyo Yingluck Shinawatra kuondoka madarakani baada ya kumkuta na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yake.


Alifikishwa mahakamani hapo jana Jumanne na akakanusha madai kwamba alimfuta kazi mkuu wa usalama wa taifa na mahala pake akamweka mwandani wa chama chake Thawil Pliensri mnamo mwaka wa 2011.

Mapema leo alirejeshwa tena mahakamani na ndipo uamuzi huo ukatolewa.


Katika uamuzi wake, mahakama imesema kuwa Bi Yingluck alikiuka katiba alipomhamisha afisa huyo mkuu wa serikali mwaka 2011.

Aidha mahakama pia imewaamuru baadhi ya mawaziri waliohusika katika uhamisho huo kujiuzulu nyadhifa zao.


Thailand imekuwa katika mikwaruzano ya kisiasa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Waandishi Habari wanasema kuwa hatua hiyo ya mahakama huenda ikafanya mambo kuwa mbaya zaidi.

HELENA COSTA KOCHA WA KWANZA WA KIKE KATIKA TIMU YA WANAUME

Klabu ya soka ya Ufaransa iliyo katika ligi ya daraja ya pili, Clermont, imemteua mwanamke raia wa Portugal Helena Costa kama kocha wake mkuu.

Uteuzi huu unamfanya mwanamke huyo kuwa wa kwanza kuwahi kushikilia wadhifa wa juu zaidi wa umeneja kama huu katika soka ya wanaume barani Ulaya.


Klabu hiyo kwa jina, Clermont, ilisema kuwa kocha mpya Helena Costa, aliyekuwa kocha wa timu za taifa za wanawake nchini Qatar na Iraq, ataanza kazi msimu ujao.

Costa pia aliwahi kuwa afisa wa klabu ya Celtic nchini Scotland ambaye kazi yake ilikuwa kuwatafuta wachezaji chipukizi wenye kipajii cha juukuchezea klabu hiyo.


Pia aliwahi kuwa kocha wa timu ya wanawake ya Iran tangu mwaka 2012.

Klabu ya Clermont imesema kuwa ina matumaini makubwa kwamba Helena atasaidia klabu kupiga hatua.


Atachukua nafasi ya Regis Brouard, ambaye mkataba wake unakamilika mwishoni mwa msimu.

Klabu hiyo inashikilia nafasi ya 14 katika ligi ya daraja ya pili.

AFRIKA KUSINI WAANZA KUPIGA KURA

Shughuli ya kupiga kura Nchini Afrika Kusini ilianza vyema mapema leo asubuhi huku idadi kubwa ya wapigaji kura ikijitokeza.

Zaidi ya watu million 25 nchini humo wanaendelea katika vituo vya upigaji kura kwa uchaguzi mkuu wa mara ya tano tangu kumalizika kwa utawala wa mtu mweupe.

Chama tawala cha African National Congress, ANC ndicho kilicho maarufu zaidi.

Lakini umaarufu wa chama hicho na rais Jacob Zuma umeathirika kutokana na tuhuma za rushwa na matatizo ya kijamii.

Licha ya kukumbwa na kashfaza ufisadi na utawala mbovu, duru zinasema kuwa chama cha ANC huenda kikanyakuwa ushindi.

Uchaguzi huo unasimamiwa na maafisa zaidi ya 200,000 wa tume ya uchaguzi watakao zunguka mikoa yote 9 iliyoko nchini.

Mwandishi wa BBC mjini Johannesburg anasema kuwa raia wengi wa Afrika Kusini bado wanakipenda chama cha ANC,kwa sababu kimeweza kuweka udhibiti na kujali masilahi ya wananchi masikini.

Anasema kuwa kifo cha Nelson Mandela huenda kimeipa ushaiwishi mkubwa chama hicho.

NDUGAI ANUSURIKA KIPIGO

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amenusurika kujeruhiwa na kundi la vijana waliokuwa wakipinga ongezeko la ushuru wa mazao na kuvamia ukumbi wa mkutano wa Kilimo uliopo Kibaigwa, wilayani Kongwa.

Katika vurugu hizo, ambazo zililazimisha polisi kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya waandamanaji, pia mali mbalimbali ziliharibiwa, likiwemo gari la Mbunge wa Tanga Mjini, Omary Nundu.

Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David Misime alisema vurugu hizo zilitokea juzi saa 7.30 mchana katika Mji mdogo wa Kibaigwa. Alisema jumla ya watu 34 wanashikiliwa wakihusishwa na vurugu hizo.


Misime alisema vijana wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 300, wakishirikiana na wabeba mizigo wa Soko Kuu la Mazao la Kibaigwa walifanya maandamano bila kibali na kung'oa bango la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.


Alisema bango lililong'olewa ni la tangazo la kuzuia wafanyabiashara kuingiza mazao sokoni bila kulipa ushuru uliowekwa kwa mujibu wa sheria.


Kamanda huyo alisema viwango vyaushuru vinavyotozwa vilipanda tangu Julai Mosi mwaka jana. Kwa mujibu wa viwango vipya, ushuru wa gunia la kilo 100 za karanga ulipanda kutoka Sh1,000 hadi Sh3,000, gunia la mahindi kutoka Sh500 hadi Sh1,000, dumu la mafuta ya alizeti lilianza kutozwa Sh500, gunia la mashudu Sh1,000 na gunia la alizeti Sh1,000. Viwangohivyo vinapingwa na wabeba mizigo.


"Vijana hao wabeba mizigo walifanya fujo kwa kufunga Barabara kuu ya Dodoma – Morogoro kwa mawe na kuchoma matairi, pia walivamia maduka na baa za jirani na kupora vinywaji na kuvunja majokofu na kusababisha uharibifu mkubwa," alisema Misime.

BOMU LALIPUKA KARIBU NA KANISA

BOMU limelipuka katika nyumba ya kulala wageni iliyopo katika eneo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Imani, jijini Mwanza na kujeruhi vibaya mtumishi wa kanisa hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Rogart Mollel, alimtaja aliyejeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Bernadetha Alfred, ambaye alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Akizungumza kwa masikitiko, Katibu huyo alisema bomu hilo lililipuka juzi saa 2 usiku na kusababisha taharuki kubwa kwa wageni waliokuwa kwenye nyumba hiyo na watu wanaoishi jirani na kanisa hilo.

Kutegwa

Akifafanua zaidi kuhusu bomu hilo, Mollel alisema lilifungwa katika kifurushi kilichopambwa na karatasi za zawadi na kuwekwa katika mfuko uliotelekezwa katika korido ya nyumba hiyo kwa takribani siku tatu.

Kwa mujibu wa Mollel, eneo hilo lakorido huwekwa kreti za soda na wageni wamekuwa wakiingia na kutoka kutumia njia hiyo, na wakati mwingine hupata chakula na chai katika eneo hilo, ndio maana watumishi hawakuhisi kwa haraka kama ni kitu cha hatari.

Kulipuka

"Jana (juzi) mhudumu huyo aliamua kufungua kifurushi hicho ili kuona ni nini na ndipo lilipomlipukia na kumjeruhi vibaya sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo usoni na miguuni na kukimbizwa Bugando kwa uchunguzi na tiba," alisema Mollel.

Lakini Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kikristo Mkoa wa Mwanza, Askofu ZenobiusIsaya, alielezea kwa undani kuwa Bernadetha aliamua kwenda kuchukua boksi hilo la zawadi juzi usiku, kwa kuwa lilikuwa limetelekezwa tangu Ijumaa iliyopita.

Kwa mujibu wa Askofu Isaya, nia yaBernadetha ilikuwa kufahamu ni lanani na kwa nini lipo kwenye korido hiyo kwa muda mrefu, ndiokufungua likamlipukia.

Alipoulizwa kuhusu ulinzi uliopo katika eneo hilo la Kanisa Kuu la KKKT, Mollel alisema ulinzi upo katika mageti yote mawili lakini upekuzi huwa haufanyiki kwa kina.

"Kwa kweli tukio hili limetuchanganya sana, tumekuwa tukisikia matukio hayo yakitokea maeneo mengine makanisani, kwetu limetokea kwenye nyumba ya kulala wageni, sina hakika waliofanya hivyo walilenga nini," alisema na kuongeza; " tunashukuru Mungu haijaleta madhara makubwa sana."

Mashuhuda

Baadhi ya watu waliohojiwa walidaiwaliposikia mlipuko huo, walidhanini transfoma ya Shirika la Umeme (Tanesco) kwa kuwa mara baada ya kulipuka, umeme ulikatika katika eneo hilo.

Mlinzi aliyekuwa zamu siku ya tukio, Charles Mathayo, alidai baada ya mlipuko huo alisikia kilio cha mhudumu Bernadetha akiomba msaada, na walipofika walimkuta akiwa amelala chini akilia huku damu zikimtiririka huku kukiwa na misumari midogo midogo katika eneo hilo.

Shuhuda ambaye kwa wakati huo alikuwa amekaa nje kwenye ngazi, Elina Emmanuel, alidai alisikia mlipuko mkubwa na kuona moshi huku waliokuwa vyumbani wakianza kutoka nje.

Elina ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha kompyuta alidai alikuwa kwenye nyumba hiyo na baada ya mlipuko huo wageni walihamishiwa kwenye nyumba nyingine ya kulala wageni.

Polisi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentine Mlowola, alithibitisha kutokea kwa mlipuko huo saa 2.20 usiku na kusema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Alisema uchunguzi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa unaendelea kubaini nani aliyefanya kitendo hicho na kwa sababu gani, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake ingawa mpaka jana hakukuwa na mtu aliyekuwa akishikiliwa kwa tuhuma hizo.

Kamanda Mlowola ametoa mwito kwa wananchi wanapoona vitu wasivyo na uhakika navyo na kuwa na wasiwasi navyo wasivishike, badala yake watoe taarifa Polisi.

Mganga Msaidizi wa Idara ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, aliyejulikana kwa jina moja la Baraka alisema kwa sasa waandishi hawaruhusiwi kumuona, kuongea wala kumpiga picha majeruhi kutokana na hali yake kuwa mbaya na kwa wakati huo hakukuwa na ndugu yake hata mmoja.

MAHABUSU WAGOMA WAVUA NGUO

Mahabusu wa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha, jana walizua tafrani katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini hapa, baada ya kuvua nguo na kugoma kushuka kwenye basi wakipinga kitendo cha watuhumiwa wawili wa dawa za kulevya kuachiwa kinyemela.

Watuhumiwa wanaolalamikiwa ambao mashtaka yao yalibadilishwa mara mbili ili wapewe dhamana ni Dharam Patel (26) na Nivan Patel (20) wanaodaiwa kukamatwa na kete 173 za heroini na misokoto 300 ya bangi, Aprili mwaka huu.


Mahabusu hao walikuwa wakipaza sauti kupinga madaraja kati ya wenye nacho na wasio nacho kwa wengine kuachiwa na wengine kubaki ndani kwa kisingizo cha 'upelelezi haujakamilika'.

Huku wakipaza sauti zao kwa nguvu, mahabusu hao wa kesi za mihadarati ikiwamo mirungi na bangi, wizi wa kutumia silaha na mauaji, walisema wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili, lakini hawajawahi hata kusomewa maelezo ya awali na kuendelea kuteseka gerezani.

Sauti ilisikika kutoka ndani ya basi:

"Wenzetu hata mwezi haujaisha wanafutiwa kesi, jamani sisi tumekosa nini? Tunataka haki itendeke kwa wote."


Mahabusu hao walionekana wakiwa wamesimama ndani ya basi hilo bila nguo, huku umati wa watu waliofika mahakamani hapo ukitazama.

Baada ya kuona umati wa watu unazidi kuongezeka kuwashangaa mahabusu hao, askari wa magereza waliondoa basi hilo eneo la Mahakama.


Kuachiwa watuhumiwa
Taarifa za kuachiwa kwa watuhumiwa hao wa dawa za kulevya waliokuwa na kesi mbele ya Hakimu Mkazi Arusha, Mwakuga Gwanta zilidaiwa kuwa zilitokana na Ofisi ya DPP Arusha, kubadilisha hati ya mashtaka.

Ilidaiwa kuwa badala ya kudaiwa kuwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya, iliandikwa kuwa walikutwa na dawa hizo mashtaka ambayo yana dhamana.


Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema jana kuwa ofisi yake haina taarifa za watuhumiwa hao kupewa dhamana lakini alisema kulikuwa na jaribio hilo.

"Ninachojua kesi hii ilipangwa kutajwa Aprili 29, mwaka huu, lakini ikasogezwa mbele hadi Mei 2 na kilichofanyika hati ya mashtaka ilibadilishwa na kuandikwa wamepatikana na dawa za kulevya".


Alisema kwa mujibu wa sheria, mtu ambaye anakamatwa na dawa za kulevya zenye thamani chini ya Sh10 milioni anaweza kupewa dhamana, lakini kiwango kikiwa zaidi ya hapo, hapati dhamana.

"Baada ya kubainika kuna njama za mashtaka kubadilishwa, tulipinga kwa kuwa kosa lipo wazi kwamba walikuwa wakisafirisha dawa hizo, sidhani kama wamepewa dhamana... sidhani kama inawezekana ila tunafuatilia kwa karibu tukio hili," alisema Nzowa.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kazi ya polisi ilikuwa ni kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani tu.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Wilibard Mashauri alisema hahusiki katika malalamiko hayo kwa kuwa si mpelelezi wa kesi.


"Lakini hawa mahabusu wanalalamikia kuachiwa kwa wale watuhumiwa wenye kesi ya dawa za kulevya, kesi ambayo haipo kwangu wala sijui wameachiwa kwa kifungu gani na inategemea na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DP) amewaachia kwa kifungu gani,"alisema.

POMBE HARAMU YAUA WATU ZAIDI YA 50

Watu zaidi ya hamsini na tano wamefariki katika maeneo mbali mbali nchini Kenya baada ya kunywa pombe 'haramu'.

Maeneo hayo yako katika mkoa wa kati na katika eneo la Mashariki mwa Kenya.


Vifo hivyo vilitokea kuanzia Jumapili siku ambayo watu zaidi ya mia moja walibugia pombe haramu inayosemekana ilikuwa imechanganywa na kemikali aina ya Methanol ambayo ni sumu kwa mwili.

Maeneo hayo ni pamoja na majimbo ya Kiambu ambako watu 15 wamefariki, Jimbo la Embu Mashariki mwa nchi ambako wengine zaidi ya 20 wamefariki. Katika majimbo ya Kitui na Makueni mashariki mwa Kenya watu 20 wameripotiwa kufariki.

Inaarifiwa wengine zaidi ya miamoja wamelazwa hospitalini baada ya kubugia pombe hiyo haramu siku ya Jumapili, baadhi wakiwa katika hali mahututi huku wengine wakiwa wamepoteza uwezo wao wa kuona.


Watu hao inashukiwa walikunywa mvinyo ambao ulikuwa umechanganywa na kemikali ya Methanol.
Mwanamume mmoja ambaye alienda ulevini na mkewe alisema kuwa mke wake alianza kwa kupoteza uwezo wake wa kuona na kisha kufariki muda mfupi baadaye.


Wengi waliofikishwa hospitalini walikuwa wanaumwa na tumbo, wanahisi kisunzi na kuumwa na kichwa.
Wengine walifikishwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi na kufariki wakipokea matibabu.

Shirika la kupambana na utumiaji wa pombe na madawa ya kulevya, NACADA limesema kuwa wale waliohusika katika uuzaji na usambaji wa pombe hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.


Vita dhidi ya pombe haramu nchini Kenya vimekuwa vigumu kushinda kwani watu wenye kipato cha chini huchagua kutumia pombe ya bei nafuu ambayo huwa sio pombe halali na kukabiliwa na hatari kama hizi.

MAREKANI KUSAIDIA NIGERIA KUTAFUTA MATEKA

Marekani imetangaza kwamba imetuma kikosi cha wataalamu nchini Nigeria kusaidia kuwatafuta wasichana takriban 200 wa shule waliotekwa nyara mwezi uliopita na wapiganaji wa kundi la Boko Haram.


Rais Barack Obama ameshutumu utekaji nyara wa wasichana hao na kusemakuwa mataifa yanapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kulikomesha Boko Haram."Tayari tumetuma kundi letu Nigeria.

Wamekubali msaada wetu ambao unashirikisha wanajeshi, wadumishaji wa sheria na mashirika mengine ambao wanajaribu kutambua waliko wasichana hawa ili wawape msaada," Rais Obama alisema.

Rais Obama amesema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kutumia utekeji wa kikatili wawasichana hao kama msingi wa kuungana na kuangamiza Boko Haram.


Nchini Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amekubalimsaada huo kama alivyosema msemaji wake, Daktari Reuben Abati.

"Msaada huo kutoka kwa Rais Obama uliwasilishwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni John Kerry kama saa tisa alasiri hivi," Daktari Abati alisema.

COCA-COLA KUONDOA KIUNGO TATANISHI KATIKA BIDHAA ZAKE

Kampuni kubwa zaidi ya vinywaji duniani Coca-Cola, inapanga kuondoa kiungo tatanishi katika baadhi ya vinywaji vyake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Hii ni kufuatia shinikizo kutoka kwa wateja wa vinywaji hivyo nchini Marekani waliotia saini ujumbe wa kusihinikiza kampuni hio kuondoa kiungo hicho kupitia kwenye matandao.


Kiungo hicho ni kemikali yenye mafuta ya kupikia iitwayo (Brominated vegetable oil au BVO) inayopatikana katika vinywaji kama Fanta na Powerade kinywaji cha kuongeza mwili nguvu.

Kampuni hasimu ya vinywaji Pepsi iliondoa viungo hivyo vya kemikali kutoka katika kinywaji chake kijulikanacho kama Gatorade mwaka jana.

Nchini Japan na katika muungano wa Ulaya kiungo cha BVO hakiruhusiwi kuongezwa katika vyakula au vinywaji.

Je nini umuhimu wa kiungo cha BVO?


Kampuni ya Coke hukitumia ili kuzuia viungo vingine vilivyo katika vinywaji hivyo kuachana.


Lakini watafiti wanasema kuwa kiungo hicho kinaweza kusababisha mtu kuwa msahaulifu ,kupata maradhi ya ngozi na matatizo ya Neva za mwili.

Hata hivyo msemaji wa kampuni ya Coke Josh Gold amesema kuwa hatua ya kuondoa kiungo hicho sio kutokana na tisho la kiafya kwani vinywaji vyake vyenye kiungo cha BVO viko salama na daima vimekuwa salama.

Kampuni hiyo imesema kuwa kiungo cha BVO hakitumiki sana katika nchi nyingi lakini kitaondolewa katika bidhaa zake zinazouzwa nchini Canada na Marekani ya Kusini.


Hatua ya Coke imetokana na shinikizo za watu na wadadisi wanasema kuwa ni funzo kwa kampuni nyingine kuanza kuhakikisha usalama wa bidhaa zao kiafya.


Kampeini hiyo ilianzishwa na kijana mmoja anayeishi katika jimbo la Mississippi, aliyehoji kwa nini Coke inatyumia kiungo hicho katika vinywaji vinavyotumiwa na wanariadha.

WASICHANA WENGINE 8 WATEKWA NIGERIA

Washukiwa wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu nchini Nigeria, Boko Haram, wamewateka nyara wasichana wengine 8 Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.


Tukio hili la hivi karibuni la utekaji nyara, lilifanyika Jumapili, katika kijiji cha Warabe katika jimbo la Borno.

Wasichana waliotekwa nyara wako kati ya umri wa miaka 12 na 15.

Mnamo siku ya Jumatatu, kiongozi wa kundi hilo alitishia kuwauza wanafunzi 230 waliotekwa nyara na kundi hilo katika shule ya Chibok tarehe 14 mwezi Aprili.

Kundi la Boko Haram limewaua maelfu tangu mwaka 2009. Lengo lake kuu ni kupinga elimu ya kimagharibi na kutaka utawala wa kiisilamu.

Kwa mujibu wa mhariri wa idhaa ya Hausa Mansur Liman, eneo la Warabe ambako wasichana wanane walitekwa nyara, ni ngome yakundi hilo la kiisilamu.

Wapiganaji waliwasili katika lori mbili huku wakiiba chakula na mifugo kutoka katika kijiji hicho.


Kuna tatizo la mawasiliano katika kijiji hicho sababu kuu ya kuchelewa kutolewa kwa taarifa hizo za utekaji nyara.


Waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano kuishinikiza serikali kuharakisha juhudi zake za kuwaokoa wasichana waliotekwa nyara tarehe 14 Aprili.

Kijiji hicho pia kiko akribu na msitu Sambisa ambako kikundi cha kwanza cha wanafunzi waliotekwa nyara walipelekwa.


Kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau, alitoa kanda ya video siku ya Jumatatu kudai kuwa kundi hilndilo liliwateka nyara wanafunzi hao na kwamba linapanga kuwauza.

MJAMZITO AUAWA KWA KIPIGO

MJAMZITO Agatha Isack (19) amekufa kwa kipigo kutoka kwa mumewe akisaidiwa na mwanamke anayeaminika kuwa hawara yake, akimtuhumu kuwa mvivu wa kulima shambani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alithibitisha kifo hicho na kuongeza kuwa mama huyo mjamzito ambayeni mkazi wa kijiji cha Manga, Kata yaKasokola wilayani Mlele alifikwa na umauti akikimbizwa katika zahanati kijijini hapo kwa matibabu na mumewe huyo Vitus Mlengo (23).

Akielezea mkasa huo unaodaiwa kutokea juzi saa sita mchana nyumbani kwa wanandoa hao kijijinihumo, Kamanda Kidavashari alisema awali baada ya kipigo mwanamke huyo alikwenda katika zahanati iliyopo kijijini humo kwa uchunguzi zaidi na matibabu.

Kabla ya kufika hospitalini alikwenda kwa mama yake mdogo aitwae Anastazia Charles na kumsimulia jinsi alivyopigwa na mumewe akishirikiana na Faustina Matheo (31) ambaye anadaiwa kuwana mahusiano ya kimapenzi na Mlengo.


"Baada ya kutibiwa Agatha alipitia nyumbani kwa bibi yake kijijini humo na kumweleza jinsi alivyopigwa na mumewe pia alimfahamisha bibi yake kuwa mumewe alimuonya asirudi nyumbani bila mboga hivyo bibi yake huyo alimpatia mboga naye akarejea kwake," alibainisha Kamanda Kidavashari.

Inadaiwa alipofika nyumbani kwa mumewe, Mlengo alimfukuza ndipo alirudi kwa bibi yake na kulazimika kulala huko hadi asubuhi alipofuatana na bibi yake ndipo mumewe akampokea.


Kidavashari alifafanua kuwa juzi, saa mbili usiku Agatha alishindwa kula chakula alichokipika mwenyewe ndipo mumewe alipoona hali yake imebadilika ndipo alilazimika kuomba msaada wa pikipiki kwa rafiki yake aitwae Alfred Kasonso na kumkimbiza katika zahanati kijijini humo kwa matibabu.

Kamanda alithibitisha kuwa mume wa marehemu huyo na Faustina wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.

MILIPUKO YA MABOMU YAUWA WAWILI NAIROBI

Watu wawili wameuawa na wengine 60 kujeruhiwa kufuatia milipuko miwili katika mji mkuu wa Kenya Nairobi ambayo imelenga mabasi mawili ya abiria.

Mabasi hayo yalilipuliwa katika eneo la barabara ya Thika karibu na mji mkuu.

Mlipuko mmoja umetoa katika basi la abiria ambalo lilikua likisafirisha abiria kutoka mjini Nairobi katika barabara ya Thika ambayo kawaida ina shughuli nyingi.


Basi la pili lililipuliwa karibu na hoteli moja iliyo umbali wadakika chache kutoka jengo kubwa zaidi la maduka katikakatika eneo hilo.

Shughuli za uokoaji zinaendelea na bado hakuna taarifa rasmi kuhusiana na watu waliouawa au kujeruhiwa kwa jumla. Picha za televisheni zinaonyesha mabasi hayo yakiwa yameharibiwa na madirisha kuvunjika.

Ni hapo jana tu ambapo watuwanne waliuawa na wengine wapatao ishirini kujeruhiwa katika shambulio lingine ambapo grunedi ilirushwa katika kituo cha mabasi ya abiria.


Shambulio la pili lilitokea karibu na mkahawa mmoja maarufu lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Mashambulio haya yanatokea mwezi mmoja tu baada ya serikali kuanzisha oparesheni ya usalama baada ya kukumbwa na mashambulio mengine hapo awali na pia kupata vitisho kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Alshabab waliodai kutekeleza shambulio la Westgate ambapo zaidi ya watu sitini waliuawa.

WACHEZAJI WATANO WA KIGENI RUKSA

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeamua msimu ujao klabu zinazoshiriki ligi hiyo kusajili wachezaji watano wa kigeni badala ya wachezaji watatu.

Awali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitaka kupunguza usajili wa wachezaji wa kimataifa kutoka watano hadi watatu ili kutoa nafasi kwa wachezaji wazawa kucheza zaidi.


Mabingwa wapya Azam tayari ina wachezaji watano ambao ni Brian Umony (Uganda), mapacha Kipre Tchetche na Kipre Balou (wote kutoka Ivory Coast) na hivi karibuniimesajili mshambuliaji kutoka Mali,Ismailla Diarra kwa mkataba wa miaka miwili na Didier Kavumbagu (Burundi) akichukua nafasi ya Mohamed Kone waliye mfungashia virago.

Taarifa za kubakisha wachezaji watano zitakuwa shangwe kwa Yanga, ambao walidai kupokwa Kavumbagu kwa vile sheria mpya ya TFF ya kutaka kubaki wachezaji watatu ndio iliyowabana na kusababisha kushindwa kuwapa mkataba kwa wakati Kavumbagu na Mbuyu Twite, ambaye usajili wake unasubiri maamuzi hayo.

Akizungumza kuwapo kwa taarifa za kubaki kwa kipengele hicho, mmoja kati ya viongozi wa TFF, ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwa kutokuwa msemaji, alisema Bodi ya Ligi imependekeza kuwa na wachezaji watano kwa misimu mitatu mfululizo.


"Azam wanashiriki Ligi ya Mabingwa mwakani, halafu Azam ni wadhamini wa Ligi Kuu Bara, kuna mambo mengi yameangaliwa ikiwamo ligi yetu kuwa bado changana wachezaji wa kigeni ndio wamekuwa wakitoa changamoto na kuleta ushindani kwa wachezaji wetu wa ndani na kuifanya ligi iwe angalau na mvuto," alisema.


Hata hivyo, licha Bodi ya Ligi kupitisha mapendekezo hayo, TFF ambao ndiyo wasimamizi wa mpira nchini watakutana na klabu za Ligi Kuu Mei 11 na kuwaeleza maazimioya Kamati ya Utendaji ya TFF ambayo ilikaa jana, pia watajadili mikataba mbalimbali ya ligi na kuangalia namna ya kuiboresha.

Pendekezo la kutumia wachezaji watatu katika ligi msimu ujao lilikuwa ni utekelezaji wa Azimio la a Bagamoyo ambalo limeonekana kuwa gumu kutekelezeka.


Mwaka 2007 TFF kwa ufadhili wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)iliandaa semina mjini Bagamoyo ikishirikisha viongozi wa klabu na wadau wa soka na kufikia makubaliano ya timu za Ligi Kuu kuwa na idadi ya wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu ili kuwapa nafasi wazawa.

Pendekezo la timu za Ligi Kuu kuwa na wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu lilipaswa kuanza kufanyiwa kazi msimu wa Ligi Kuu yaTanzania Bara uliomalizika hivi karibuni, lakini ilishindikana baada ya baadhi ya timu kuomba kuongezwa muda wa msimu mmoja kabla ya utekelezaji wake na hivyo lilitakiwa lianze kutumika msimu ujao, ambapo pia limegonga mwamba.


Akizungumzia suala hilo la usajili wa wachezaji watano wa kigeni, msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto

alisema: "Bado hatujapata mwongozo wowote kutoka TFF lichaya kuomba, hata hivyo Mei 11 kunakikao cha klabu za Ligi mambo yoteyataamuliwa huko."


Kwa upande wake, Meneja wa Azam FC, Jemedari Said, alisema: "Suala hilo ni kubwa kwangu, viongozi wa juu ndio wanahusika nalo zaidi, Jumatatu tuna kikao kule(TFF), ndio kila kitu kitajulikana."

Katibu wa Simba, Ezekiel Kamwaga hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.

WAETHIOPIA WADAKWA KICHAKANI

Waethiopia 55 wamekamatwa na wanakijiji cha Chekereni Pabliki kilichopo Himo, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakiwa wamejificha kichakani na mkazi mmoja wa kijiji hicho.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea tukio hilo nakwamba watu hao walikamatwa "Wanakijiji walitoa taarifa polisi baada ya kuwaona watu hao, na sisi tulifika mara moja kuwakamata wakiwa na mwenyeji wao," alisema Kamanda Boaz.

Aliongeza: "Kwa sasa hatuwezi kumtaja jina wenyeji wa watu hao kwa vile bado tunaendelea na uchunguzi zaidi."

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, watu hao baada ya kuhojiwa walidaikuwa walikuwa njiani kwenda nchiniAfrika Kusini kupitia Tanzania.

Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika wengine zaidi wa mtandao wa kusafirisha binadamu kabla ya kufikishwa mahakamani.

Aliwataka wananchi waishio mipakani kuendelea kuwa walinzi na kutoa taarifa polisi pindi wanapowaona watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.

ZAIDI YA WATU 2000 WAHOFIWA KUFA

Watu zaidi ya 2,500 wanahofiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na mmomonyoko wa ardhi Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo katika Jimbo la Badakhshan.

Taarifa nyingine zilizotolewa na Umoja wa Mataifa (UN), zinaeleza kwamba zaidi ya miili 350 imepatikana katika jimbo hilo.


Katika eneo hilo maelfu ya makazi ya watu yamefukiwa na matope baada ya mlima katika jimbo hilo kuporomoka kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Polisi wamekuwa wakiwapelekea mikate na maji raia walionusurika kwa kuwa usiku wa Ijumaa kuamkiajana, walishinda bila chakula. Mvua kubwa zimekuwa zikinyesha kwa wingi Kaskazini na Mashariki mwa Afghanistan na kusababisha madhara hayo.


"Idadi ya watu waliofariki dunia imefikia 350 na nyumba zaidi ya 1,000 zimearibiwa na mvua," taarifa ya UN ilieleza.

Taarifa ya UN ilieleza kwamba zaidiya nyumba nyingine 300, zimefukiwa baada mlima kwenye jimbo hilo kuporomoka.


Kamanda wa Polisi katika Jimbo la Badakhshan, Fazludeen Ayaz alisema katika Kijiji cha Hargu, nyumba za familia 215 zilifunikwa na udongo.

Ayaz alisema endapo kuna watu wamenusurika katika ajali hiyo itakuwa vigumu kuwaokoa kutokanana kufunikwa na matope.


Jimbo la Badakhshan linatajwa kuwa wanaishi watu wa kipato cha chini mpakani mwa Tajikistan, China na Pakistan.

MILIPUKO YA MABOMU YAUA WATU KENYA

Watu watatu wanaripotiwa kuuawa katika mlipuko uliotokea katika mji wa Mombasa nchini Kenya.


Kwa mujibu wa taarifa bomu la mkono lilitupwa kwenye basi katika kituo cha mabasi cha Mwembe Tayari ambao hupendwa kutembelewa na watalii na kusababisha vifo hivyo na wengine kujeruhiwa.

Mlipuko mwingine umetokea katika mtaa wa kifahari wa Nyali.


Kamishna mkuu wa polisi Mombasa, Nelson Marwa, amesema watu 6 wamejeruhiwa na kuwa watu waliotekeleza shambulizi hilo walitoroka kwa Pikipiki.

Kenya imekuwa ikikumbwa na matukio ya mashambulio yanayodaiwa kutekelezwa na kundi la kiislamu la Al shabaab la nchini Somalia.


Aidha nchi hiyo imekuwa katika tahadhari tangu mwezi Septemba mwaka jana ambapo wanamgambo wa Al shabaab walivamia kituo cha biashara cha Westgate kilichopo mji mkuu wa Nairobi na kuua watu wapatao 67.


Al Shabaab ni kundi ambalo lina uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda ambalo limeapa kulipiza kisasi kufuatia Kenya kutuma majeshi yake nchini Somalia mwaka 2011ambayo yameungana na yale ya Umoja wa Afrika AMISOM.

AJARI YAUA KIONGOZI WA KANISA KUELEKEA SHEREHE ZA KUSIMIKWA MKUU WA JIMBO MPANDA

Kwa habari zilizotufikia hivi punde ni kuwa father Kapufi na Katekista mmoja(jina halijafahamika) wamefariki dunia kutokana na ajari ya gari waliyopata wakitokea Inyonga kuja mpanda mjini kuhuzuria kusimikwa kwa mkuu wa jimbo katoliki la Mpanda askofu G. Nyaisonga.

Askofu Gervas Nyaisonga (48)anasimikwa kesho siku ya jumapili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda katika ibada inayotarajiwa kufanyika kuanzia saa nne asubuhi katika viwanja vya shule ya chekechea inayomilikiwa na Kanisa Katoliki jimbo la Mpanda.


Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda ibada ya kusimikwa Askofu Nyaisonga itahudhuriwa na Maaskofu wote wa Kanis hilo na mapadri watawa na walei wa kutoka majimbo mbalimbali ya kanisa hilo.


Askofu Nyaisonga anahamia jimbo Katoliki la Mpanda kabla ya hapo alikuwa ni Askofu wa Jimbo la Dodoma jimbo la Mpanda lilikuwa halina Askofu toka mwaka juzi kufuatia kufariki kwa aliyekuwa Askofu wa jimbo hilo Paskal Kikoti kufariki Dunia hapo mwaka juzi

Jimbo Katoliki la Mpanda lilianzishwa mwaka 2001 na Askofu wake wa kwanza wa Jimbo hilo alikuwa ni marehemu Paskali Kikoti hinyo Askofu Gervas Nyaisonga atakuwa ni Askofu wa PILI tangia jimbo katoliki laMpanda lilipoanzishwa.


Katika ibada hiyo ya kusimikwa kwa Askofu Nyaisonga Serikari itawakilishwa na Waziri wa Nchi ofisi ya waziri Mkuu uwekezaji na uwezeshaji MeryNangu ambae atatowa salamu za Serikali kwenye ibada hiyo.


Miongoni wa watakao hudhuria ibada hiyo hapo kesho ni Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda na viongozi mbalimbali wa Serikali wa Mkoa wa Katavi na Viongozi wa mikoa ya jirani ya Rukwa Tabora na Kigoma.

UKAWA WAANZA MIVUTANO

WAKATI viongozi wa kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanaonesha kushikamana hadharani, habari za ndani ya Umoja huo zinasema kuwamivutano imeanza kuzuka huku baadhi ya viongozi wake wakitaka kurejea Bunge Maalum la Katiba.


Habari kutoka ndani ya Umoja huo zinasema kuwa angalau viongozi wawili wa vyama vinavyounda UKAWA wanataka kurejea bungeni na kushiriki mchakato wa kutunga Katiba mpya wakati Bunge hilo litakapoanza tena Agosti mwaka huu.


Habari zinasema kuwa viongozi hao wawili, wanataka kurejea tena bungeni kwa sababu wameanza kubaini kuwa kuna ujanja mwingi ndani ya UKAWA na kuwa baadhi ya vyama vinavidanganya na kuvitumiavingine, bila kuonekana kwa faida yoyote dhahiri.

"Tulisusa Bunge kwa pamoja, lakini sasa inaanza kuonekana kuwa wapo wenzetu ambao wana maslahi binafsi na kuonekana kututumia sisikwa manufaa yao ya kisiasa na hata kifedha," anasema mmoja wa viongozi wa UKAWA, ambaye anahisi baadhi ya wenzao wanapata maslahi zaidi kuliko wengine.


Kuna madai kuwa UKAWA wamepatiwa fedha, tena nyingi na mfadhili ama wafadhili wa nje ya Tanzania, lakini fedha hizo zinaishia mifukoni mwa kiongozi mmoja amawawili wa umoja huo, usiosajiliwa na unaoendesha shughuli zake za kisiasa, bila hati zozote za kuuhalalisha kuendesha shughuli za kisiasa.

Viongozi wa vyama CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vidogo vidogo walisusa Bunge Maalumu la Katiba mwezi uliopita, wakiazimia kuendesha kampeni ya kutafuta Katiba mpya nje ya Bunge, kupitia mikutano ya hadhara ya wananchi. UKAWA walifanya mkutano wao wa kwanza mjini Zanzibar juzi.


Pamoja na kwamba ni dhahiri kuwa Umoja huo na shughuli zake haziungwi mkono na wananchi wa Tanzania walio wengi, lakini viongozi wake wameendelea kushikilia kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.


Wachunguzi wa masuala ya kisiasa, wanasema kuwa UKAWA wamechagua kuanzia mikutano yao Zanzibar, kwa sababu huko ndiko wana uhakika wa kupata watu wa kuhudhuria mikutano yao, kwa sababu ya wanachama wa CUF.

"Wamekimbia Zanzibar kwa sababu huko Bara watampata nani wa kwenda kupoteza muda wake kusikiliza hoja zisizokuwa na mashiko," amesema mchunguzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro.

CHUNGA USIWE MUATHIRIWA WA MAPENZI MTANDAONI

Polisi nchini Ufilipino, wamesema kuwa wamewakamata washukiwa wa uhalifu katika mitandao ambao ni sehemu ya kikundi cha watu wanaowahadaa watu kwenye mitandao ya kijamii kote duniani.


Washukiwa hao huwashawishi watumiaji wa Internet au walengwa wao katika nchi za kigeni kujipiga picha wakiwa uchi na wakiwa katika vitendo vya mapenzi na kujirekodi kisha kuwatumia.


Wahalifu hao baadaye hudai kiasi Fulani cha pesa kutoka kwa walengwa la sivyo huwatishia kuwa watawatumia jamaa wao picha na video hizo.

Polisi wamefanikiwa kuwakamata washukiwa 58 katika operesheini hiyo iliyohusisha polisi wa kimataifa Interpol.


"Lengo la washukiwa hawa ni kutengeza akaunti kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kuwatafuta wateja wao hasa wazee katika nchi za kigeni,'' alisema afisa mmoja wa polisi.


"Katika akaunti zao hizo wao hujidai kuwa ni wasichana wenye asili ya Asia wanaotafuta wapenzi katika nchi za kigeni.''


"Baada ya kujuana vyema na watumiaji wa mitandao wasiojua kuwa wanahadaiwa, wao huwakaribisha kuwa marafiki zao kwenye mitandao , kuwasiliana nao kwa njia ya video kwenye mitandao hiyo hiyo na kisha kufanya nao vitendo vya mapenzi kupitia kwa kompiuta huku wakirekodi kila kinachofanyika. ''Kanda hizo sasa hutumiwa kama njia ya kupata pesa kutoka kwa waathiriwa kwa kutumia vitisho kuwa watasambaza kanda hizo kwawatu wa karibu wa waathiriwa la sivyo walipwe kati ya dola 500 na 2,000. Pia hutishia kusambaza kanda hizo kwenye mitandao ya kijamii.


Afisa mkuu wa Interpol amesema kuwa uhalifu huo umeenea sana kwenye mitandao. Uhalifu wa aina hii hauna mipaka umeenea kote, sio Ufilipino peke yake.


Kijana mmoja kutoka Scotland, alijiua baada ya kujikuta katika hali ya kuhadaiwa kwenye mitandao kwa njia hii.

JK, MKAPA NA SHEIN WAONYA MCHAKATO WA KATIBA

VIONGOZI wa kitaifa wameonya kuhusu muelekeo wa mchakato wakupata Katiba mpya, kwamba usiachiwe kuvuruga amani, upendona mshikamano wa kitaifa, huku Rais Jakaya Kikwete akihadharisha kuwa isipopatikana, Katiba hiyo, itatafutwa tena miaka ijayo.

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akikabidhi nyumba 30 za watumishi wa afya wa Mkoa wa Singida, zilizojengwa kwa ufadhili wa Global Fund Round9 na kusimamiwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa juzi, aliwataka Watanzania kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unaoendelea hivi sasa, hauvurugi amani, upendo na utulivu uliopo nchini.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, akihutubia katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi janaBwawani Zanzibar, alisema zipo dalili kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kuutumia mchakato wa Katiba mpya vibaya, kwa kuanza kujenga uhasama wa kisiasa ambaohatma yake ni nchi kuingia katika machafuko.

Mkapa alisema amani na utulivu uliopo nchini kwa miaka mingi havina budi kudumishwa na kukuzwa, ili kuenzi waasisi wa Taifaletu.“

Vyovyote utakapoishia mchakato huu wa Katiba…amani, upendo na utulivu lazima vihimili maisha yetu,” alisema Mkapa na kuongeza:

“Tuhitilafianeni lakini bila kupigana.”

Tahadhari Zanzibar

Dk Shein kwa upande wake kutokana na dalili alizozibaini, amewatahadharisha wananchi na wanasiasa, kwamba mchakato wa kupata Katiba mpya usiwe chanzo cha kuvuruga amani na utulivu uliopo na kujenga uhasama.

Alisema kwa muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa ikipata mafanikio makubwa, ikiwemo kuimarika kwa amani na utulivu ambao umewafanya wananchi kuishi vizuri kwa maelewano na kuzika tofauti za itikadi za kisiasa.

“Wananchi wa Zanzibar nawaasa kwamba Bunge Maalumu la Katiba lipo kwa mujibu wa Sheria na wananchi kamwe wasijenge chuki na uhasama utakao sababisha nchi yetu kurudi katika siasa za chuki nauhasama,” alisema.

Miaka ijayo Rais Kikwete akizungumza katika Sikukuu ya Wafanyakazi Dar es Salaam jana, aliwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kutumia ipasavyo nyongeza ya siku 60 watakayopatiwa kwa kuja na uamuzi wenye manufaa kwa Watanzania, vinginevyo ikishindikana, Katiba hiyo, itatafutwa tena miaka ijayo.

“Mimi Rais kazi yangu nimemaliza ya kuteua wajumbe, sasa yanayoendelea mle ndani ni ya kwao…kwa kweli nasikitishwa na kilichokuwa kikijiri ndani ya Bunge lile na kuniacha na maswali kuwa hivi tusi ni hoja?” alihoji Kikwete.

Alisema kuteuliwa kwa wajumbe hao kutoka taasisi, itikadi na maeneo tofauti, ilikuwa ni moja yambinu ya kuibua mijadala mbalimbali ambayo ingewezesha kupatikana kwa Katiba nzuri yenye manufaa kwa Watanzania.

“Hata wazungu wanasema acha mawazo 100 yagongane ili kupatikane wazo moja la msingi, lakini naamini kuwa wajumbe hawa hawataishia pale, watakaa na kutumia likizo waliyonayo na kuja na mawazo mazuri na kutuletea Katiba mpya,” alisisitiza.

Aliwataka Watanzania kuwatumia wajumbe wanaowawakilisha katika Bunge hilo, kuwasilisha mawazo yao badala ya kuwaachia watoe mawazo yao jambo ambalo ni rahisi kwao kutekwa na mawazo ya wengine.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, Nicholaus Mgaya, alisema shirikisho hilo, limesikitishwa na mwenendo wa Bunge hilo la Katiba, ambao umesababisha wananchi kupoteza imani nalo na kushauri wajumbe wote waliohusika na makosa yaliyojitokeza kujirekebisha katika Bunge lijalo.